Nataka Kuchukua Mkopo Katika Shirika Nifanyalo Kazi Ila Wameniwekea Masharti Kutumia Gari Langu – Inafaa Kuchukua Mkopo Wao?

SWALI:

 

Asalam alaykum Warahmatullahi Taala Wabarakatu. Kwanza kabisa na mshukuru Alla (Subhanna Wataala) kwa kunipa fursa hii ya kuweza kutafuta elimu ya dini yetu ya Kiislamu. Pili na waombea kwa Allah (Subhana Wataala) awalipe kwa kila kilicho jema nyie wenzetu mlio jitolea muda wenu na fikra zenu kwa kutoa maoni na elimu iliyo nasaha.

 

Swali langu ni kama ifuatavyo: Ninahitaji mkopo kutoka kwenye Kampuni ninayo fanya kazi, lakini masharti yake ni kwamba nitawalipa hela niliyokopa na ni lazima nitumie gari kwa faida ya kampuni, na kampuni itachangia gharama ya matengenezo. Nilichokuwa nikishauriana nao ni kwamba maadam nawalipa chote nilichokopa si haki kwa wao kunilazimisha kutumia gari yangu kwa madai kua watachangia gharama ya matengenezo. Nikikataa masharti hayo wanasema sinto pata mkopo kwani kampuni ikotiyari kumkopesha mfanyakazi kwa makubaliano hayo. Ningeomba fatwa yenu kuhusu, mkopo huo kama unafaa kuchukuliwa ama haufai? Nawatakia kila lakheri kwenye kazi yenu.


 

 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuchukua mkopo kutoka katika shirika ufanyalo kazi.

 

Hakika ni kuwa ndugu yetu umetueleza mengi kuhusu mapatano na usaidizi wa kuchukua mkopo na utakiwayo kufanya lakini hukutueleza kuhusu aina ya mkopo wenyewe. Ibara hiyo ya awali inamaanisha kuwa je, mkopo wenyewe ni wa ribaa au utapatiwa bila ya kulipa ribaa? Ikiwa mkopo wenyewe ni wa kutoa ribaa unapolipa utakuwa hufai kuchukua mkopo kama huo.

 

Ama ikiwa mkopo wenyewe ni bila ya ribaa inatakiwa utazame maslahi utakayopata katika kutekeleza masharti na hasara yake. Kwa mfano, katika masharti labda waliyotaka ni kuwa gari hilo ambalo ni lako waweza kukutaka umpatie mtu mwengine ili afanye kazi ya shirika hapo itakuwa ni kama si lako. Kwa hiyo, kitu ambacho ni muhimu kwako ni kupata masharti ya mkataba wenu kabla yetu sisi kuweza kukusaidia katika kukupatia mwelekeo wa Kidini. Na mara nyingi utaweza hata kuamua kwa kuona mkataba wenyewe kwani mambo mengine ni ya kutumia mantiki na akili.

 

Nadhani itakuwa tumefahamika vizuri sana.  

 

Na Allaah Anajua

 

Share