Kuna Ubaya Gani Mashia Kuwatukuza Maimaam Na Hali Sunni Wanawatukuza Maswahaba, Na Vipi Kuswali Nao?

SWALI:

 

Asalamun alaykum

Poleni kwa kazi, niliona majibu yenu lakini nashangazwa sana kwni kuhusu hao mashia ni kuna ubaya gani wao kuwapenda watu wa mtume? Kwani sio watu wa mbali na ni wakaribu sana kwa mtume wetu muhammad na wao maisha yao ni vigezo kwetu sisi kwani ndio waliokua na mtume bega kwa bega kama tukisoma tarekh na ikiwa wao wao wanasifu sna watu wa mtume na kuwatukuza watu wa mtume na ikiangalia hao watu wa mtume sio wa mbali ni mtoto wa mtume na wajukuu wa mtume. sasa na sisi tutawakjibu nini ikiwa watawambia kua nanyi mnawapenda sna maswahaba na kuliko watu wa mtume na vile vile hao mtume hakuwachagua kua viongozi mutawajibu nini? Na jengine mm nilikua nauliza kusali na mshia mthnasharia vibaya au laa? Na kama vibaya kwa nini?

Salamun alaykum.

Kwanza poleni kwa kazi na jengine niliuliza kipindi kidogo suali langu lakini nashangaa mbona hamkunijibu? Na suali langu nilitatanishwa pale kuhusu yule mtu aliyeuliza je kusali au kuwatolea salam mashia inafaa au haifai? Kwani muliongea kuwa wao hawawapendi maswahaba na wanapenda sna watu wa mtume. Yaani bibi fatma na watoto wake. Sasa mm hapa nilikua nauliza kwani kuna ubaya kuwapenda watu wa mtume? Na vile vile kama wao wanawapenda watu wa mtume hata nasi pia tunawapenda hao masahaba na ukiangalia hasa watu wa mtume ndio waliokua karibu zaidi kuliko hata mtu yoyote yule. Basi ikiwa mutafahamu na mnalo suala langu basi naomba mnijibu kwa haraka sana.


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuwapenda Maswahaba na familia ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Hakika ni kuwa haiwezekani kama unavyotaka kuwa swali lako lijibiwe haraka sana kwani katika alhidaaya kuna nidhamu ya kujibu maswali. Ikiwa kila mmoja wetu atataka hivyo basi hatutaweza kujibu swali lolote. Maswali yanajibiwa yanavyokuja, la mwanzo kujibiwa mwanzo na yanayokuja baadaye kujibiwa kwa utaratibu huo. Kwa kuwa tumelipata swali lako na kumekuja wakati wa kulijibu twalijibu bila ya upendeleo wala kwenda kinyume na nidhamu hiyo.

 

Kisha twashangazwa na ibara yako, hata nasi pia tunawapenda hao masahaba. Hilo neno ‘hao’ linaonyesha kuwa ni kama kujitoa kuwa wewe huwapendi. Ni itikadi ya Muislamu iliyo sahihi kuwapenda Maswahaba wote bila kubagua (Radhiya Allaahu ‘anhum) na pia jamaa ‘Aali Bayt’ za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Allaah Aliyetukuka Mwenyewe Ametutaka tuwapende na kuwaheshimu Maswahaba kwani Yeye Alikuwa radhi nao na ndivyo alivyotuagizia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Allaah Aliyetukuka Amesema: “Na wale waliotangulia, wa kwanza, katika Muhaajiruun na Answaar, na waliowafuata kwa wema, Allaah Ameridhika nao, na wao wameridhika Naye; na Amewaandalia Bustani zipitazo mito kati yake, wadumu humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa” (at-Tawbah [9]: 100).

 

Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema kuhusu Answaar: “Hawapendi Ma-Answaar isipokuwa Muumini na hawachukii wao isipokuwa mnafiki” (al-Bukhaariy na Muslim). Zipo Hadiyth za kuonyesha fadhila za Maswahaba na kuhitajika sisi kuwapenda. Wale waliokuwa msitari wa mbele zaidi Makhalifa waongofu (Abu Bakr, ‘Umar, ‘Uthmaan na ‘Aliy) ambao tunahitajika kufuata Sunnah zao bila kusita. Baadaye wapo wale kumi waliobashiriwa Pepo na Maswahaba wanaume na wanawake waliopatiwa sifa moja au nyingine. ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikubali ubora wa Abu Bakr na ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma). Kwa hiyo, Muislamu anafaa awapende Maswahaba, hata hivyo asiwatukuze kupita mipaka ya kidini, Uislamu.

 

Ama familia ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Muislamu wa kweli anatakiwa awapende kwa dhati, hasa wake zake watukufu na wale waliojulikana kwa wema, kama ‘Aliy, Faatwimah, Zaynab, Ummu Kulthuum, Ruqayyah, al-‘Abbaas, Hasan na Husayn na wengineo waliojulikana. Inafaa wao pia tuwapende kwa mipaka iliyowekwa na Uislamu sio zaidi ya hapo. Na ndio kwa kuwapenda kwetu huwa tunawaombea kila tunapomswalia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Hata hivyo, Mashia mbali na kusema wanawapenda Ahlul Bayt, lakini wanafanya mambo ya ajabu na kuwapatia sifa za ajabu wale ambao wanawaita ni Maimamu. Wamewapatia sifa za uungu wanaadamu. Kwa mfano mwanachuoni wao mmoja kwa jina Tabatabai amesema kuwa hawa Maimamu wao 12 wanapata Wahyi, kumaanisha kuwa walikuwa Mitume. Ilhali twafahamu kuwa Allaah Aliyetukuka Amesema:

Muhammad si baba wa yeyote katika wanaume wenu, bali ni Mtume wa Allaah na Mwisho wa Manabii, na Allaah ni Mjuzi wa kila kitu” (Al-Ahzaab [33]: 40).

 

Sisi twatakiwa tumfuate katika mwisho wa utume Allaah Aliyetukuka au Tabatabai au Kulayniy aliyesema kuwa ‘Hao Maimamu wao wanajua Ghaibu na wanajua siku yao ya kufa na wanachagua kifo wanachotaka wafe!!’ Ilhali Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametufahamisha kuwa yeye ni Mtume wa mwisho hakuna mwengine atakayekuja baada yake, na yeyote atakayedai utume ni Dajjaal (mwongo).

 

Pia Mashia wanasema kuwa Maimamu wao wanajua yote yaliyotokea hapo mwanzoni na yatakayotokea mpaka mwisho wa dunia. Je, hii ni sifa ya mwanaadam au ya Allaah Aliyetukuka? Katika miaka ya themanini, Bilaal Muslim Mission, taasisi ya Kishia Kenya iliiandikia Wizara ya Elimu kuwa masomo ya Kiislamu yanayosomeshwa mashuleni yanakwenda kinyume na itikadi yao kwa hivyo kuwe na syllabus yao ya Kishia. Kwani wao na Masunni wanatofautiana katika misingi hasa ya Dini. Hiyo ni kumaanisha Dini yao ni tofauti kabisa na tuliyonayo sisi. Allaah Aliyetukuka Atuepushe na hayo ya maajabu.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share