Ufafanuzi Wa Aayah Za Kutunza Mali Ya Yatima Na Kuhusiana Kuoa Wake Wanne

SWALI:

 

ASSALAAM ALAYKUM

 

NAOMBA NISAIDIE KUPATA MAANA YA KINA YA AYA ZILE ZA MWANZO (AYA 1- 4) WA SURAN NISAA. HABARI ZA KUTUNZA VEMA MALI ZA YATIMA, ALLAAH (SUBHANAHU WA TA'ALA) AMEZIUNGANISHA MOJA KWA MOJA NA KUOA WAKE 2, 3, NA 4. MIMI NAONA ELIMU YA AYA HII NI MUHIMU KUIELEWA.

 

WA BILLAH TAUFIQ.


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu ufafanuzi wa Aayah nne za mwanzo za Suratun Nisaa’. Ni muhimu kufahamu tafsiri ya Aayah hizo kabla hatujaingia katika ufafanuzi wenyewe.

 

Tafsiri ni kama ifuatayo:

 

1. Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi Aliyekuumbeni kutokana na nafsi moja, na Akamuumba mkewe kutoka nafsi ile ile. Na Akaeneza kutokana na wawili hao wanaume na wanawake wengi. Na tahadharini na Allaah ambaye kwaye mnaombana, na jamaa zenu. Hakika Allaah ni Mwenye kuwaangalieni.

 

2. Na wapeni mayatima maliyao. Wala msibadilishe kibaya kwa kizuri. Wala msile mali zao pamoja na mali zenu. Hakika yote hayo ni jukumu kubwa.

 

3. Na ikiwa mnaogopa kuwa hamtowafanyia mayatima uadilifu, basi oeni mnao wapenda katika wanawake, wawili au watatu au wanne. Na mkiogopa kuwa hamwezi kufanya uadilifu, basi mmoja tu, au wale ambao mikono yenu ya kulia imewamiliki. Kufanya hivi ndiko kutapelekea kutofanya jeuri.

 

4. Na wapeni wanawake mahari yao hali ya kuwa ni kipawa. Lakini wakikutunukieni kitu katika mahari, kwa radhi yao, basi kileni kiwashuke kwa raha.

 

Tukitazama kwa makini Aayah ya kwanza utaona kuwa inatuelezea kuhusu amri ya kuwa na Taqwa (uchaji Mngu), tanbihi kuhusu kuumbwa kwa mwanaadamu na kuwatendea wema jamaa.

 

Ama Aayah ya pili hadi ya nne inatuelezea kuhusu ulinzi wa mali ya mayatima. Katika hayo ni kule kuamriwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kuwa mayatima wakabidhiwe mali zao zote wanapofikia baleghe. Hapo hapo Ameharamisha kuitumia au kupora sehemu yake. Hivyo Amesema: “Wala msibadilishe kibaya kwa kizuri”. As-Suddiy amesema: “Mmoja wao (mdhamini wa mayatima) angechukua kondoo mnono kutoka kwa mali ya yatima na badala yake akamweka kondoo mkondefu, huku akisema: ‘Kondoo kwa kondoo’. Aidha akachukua dirham halisi na kuibadili kwa dirham bandia, akisema: ‘Dirham kwa dirham’”.

Na kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala): “Wala msile mali zao pamoja na mali zenu”. Hiyo ina maana msichanganye ili msile na mali zao, kama Mujaahid, Sa‘iyd bin Jubayr, Muqaatil bin Hayyaan, as-Suddiy na Sufyaan Husayn walivyoelezea, yaani msichanganye mkala wote. Na Allaah Amesema: “Hakika yote hayo ni jukumu kubwa”, kufanya hivyo ni dhambi kubwa kulingana na Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma). Haya yamepokewa pia kutoka kwa Mujaahid, ‘Ikrimah, Sa‘iyd bin Jubayr, al-Hasan, Ibn Siriyn, Qataadah, Muqaatil bin Hayyaan, adhw-Dhwahhaak, Abu Maalik, Zayd bin Aslam na Abu Sinaan. Maana iliyotajwa hapo juu ni kuwa kuchanganya mali yako na yao ni dhambi kubwa na kosa kubwa, hivyo jiepushe nayo.

 

Aayah ya tatu hasa inaharamisha kuwaoa mayatima bila ya kuwapa mahari, kwani kufanya hivyo ni kujitoa katika nidhamu ya Kiislamu iliyo njema kuwa kila mmoja apewe haki yake kwa wakati wake. Ama sehemu ya Aayah: “Na ikiwa mnaogopa kuwa hamtowafanyia mayatima uadilifu, basi oeni mnao wapenda katika wanawake, wawili”. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anaamuru hapa kuwa mmoja wenu anayemlea yatima wa kike na anachelea kuwa asingeweza kumpa mahari yenye hadhi yake, basi analazimika kumuoa mwanamke mwengine – ambao hao wanawake - wako wengi na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) hakumkwaza kwa hilo. Imaam al-Bukhaariy alipokea kutoka kwa ‘Urwah bin az-Zubayr (Radhiya Allaahu ‘anhuma), alisema kuwa alimuuliza Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) kuhusu maana ya kauli ya Allaah isemayo: “Na ikiwa mnaogopa kuwa hamtowafanyia mayatima uadilifu’. Akasema: ‘Ewe mpwa wangu! Kauli hii inamhusu yatima wa kike anayesihi na mlezi anayetumia mali yake. Mali yake na uzuri vinaweza kumshawishi kumuoa bila ya kumpa mahari ya kutosha ambayo angepewa na mchumba mwengine. Hivyo, walezi wa aina hiyo wamezuiwa kuwaoa mayatima wa aina hiyo mpaka wawafanyie uadilifu na kuwapa mahari iliyostahili yao; vinginevyo wameamrishwa kuoa wanawake wengine”. Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) aliongeza kusema: “Baada ya kushuka Aayah hiyo, watu waliendelea kumuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya kuoa mayatima. Allaah Alishusha Aayah ifuatayo:Wanakuuliza nini sharia’ah ya wanawake’ (an-Nisaa’ [4]: 127). Akasema, kauli ya Allaah katika Aayah hii.Na mnapenda kuwaoa’. Inamhusu mlezi ambaye hakusudii kumuoa yatima anayemlea kwa sababu ama hana mali au si mzuri. Walezi walizuiwa kuwaoa mayatima jamali na wenye mali bila kuwatendea uadilifu kama walivyo jiwekea baidi kuwaoa (waliokuwa na mali na jamali)”.

 

Kisha Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Ametoa rukhsa kwa wanaume kuoa wanawake wengi mpaka wanne: “Wawili au watatu au wanne”, yaani oeni wanawake wengi kama mtakavyo minghairi ya msichana yatima, wawili, watatu au wanne. Na iwapo mmoja wenu anachelea kutofanya uadilifu basi aoe mke mmoja peke yake: “Na mkiogopa kuwa hamwezi kufanya uadilifu, basi mmoja tu, au wale ambao mikono yenu ya kulia imewamiliki”. Kwa hiyo, kuoa wake wengi kumewekewa sharti na shari’ah ya kuwafanyia insafu na uadilifu na kushindwa kufanya uadilifu inabidi utosheke na mke mmoja tu. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Amesema: “Kufanya hivi ndiko kutapelekea kutofanya jeuri”. Muradi wake ni kutofanya udhalimu. Na wanachuoni wengine wengi wanasema maana yake ni kukengeuka (kwenye haki) kwa mahali ni lazima.

 

Ama Aayah ya nne inatuonyesha sisi uwajibu wa kutoa mahari kuwapa wanawake wanaoolewa. Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) amesema, Nihlah katika kauli ya Allaah (Aayah ya 4) inakusudiwa mahari. Na Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) akasema maana yake imeshurutishwa, na Ibn Zayd akasema: “Katika lugha ya Kiarabu, Nihlah ina maana kitu kilicho lazima”. Hivyo Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anatuamrisha msioe mpaka muwape wake zenu haki zao. Baada ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hapana mtu mwengine aliyeruhusiwa kuoa mwanamke mpaka kwa kutoa mahari wala si kwa kutoa ahadi za uongo kuhusu mahari iliyokusudiwa. Kwa hiyo, mwanamme anafaa kumpa mahari mkewe kwa moyo safikama ampavyo zawadi. Hata hivyo, endao mke atampa sehemu au mahari yote kwa hiyari yake bila kulazimishwa, mume anaruhusiwa kuipokea na ni halali kwake katika mazingira haya kuitumia kwa kuifanyia lolote kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala): “Lakini wakikutunukieni kitu katika mahari, kwa radhi yao, basi kileni kiwashuke kwa raha”.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share