Fadhila Za Kusuluhisha Waliokhasimiana -1

 Anasema Allaah سبحانه وتعالى:

 

 ((لاَّ خَيْرَ فِي كَثِيرٍ مِّن نَّجْوَاهُمْ إِلاَّ مَنْ أَمَرَ بِصَدَقَةٍ أَوْ مَعْرُوفٍ أَوْ إِصْلاَحٍ بَيْنَ النَّاسِ وَمَن يَفْعَلْ ذَلِكَ ابْتَغَاء مَرْضَاتِ اللّهِ فَسَوْفَ نُؤْتِيهِ أَجْرًا عَظِيمً ))

 

((Hakuna kheri katika mengi ya wanayoshauriana kwa siri, isipokuwa kwa yule anayeamrisha kutoa sadaka, au kutenda mema, au kupatanisha baina ya watu. Na mwenye kufanya hayo kwa kutaka radhi ya Allaah basi Tutakuja mpa ujira mkubwa)) [An-Nisaa: 114]

 

Na kasema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم

 

((ألا أخبركم بأفضل من درجة الصيام والصلاة والصدقة ؟ إصلاح ذات البين وفساد ذات البين هي الحالقة))  رواه أحمد وأبو داود والترمذي صحيح الجامع

 

((Je, nikujulisheni lililo na daraja bora kuliko Swawm na Swalah na Sadaqah? Ni kusuluhisha baina ya watu. Na ama kuharibu uhusiano (baina ya watu) ni uharibifu [Ahmad na Abu Daawuud na At-Tirmidhy katika Swahiyhul-Jaami'i]

 

Katika mambo ya kheri Aliyoyataja Allaah سبحانه وتعالى watu wanapozungumza kwa siri ni kuamrishana kutoa sadaka au kutenda mema. Kisha Ametaja kuhusu kupatanisha watu, jambo ambalo mara kwa mara hutokea katika jamii na khaswa jamii yetu. Na bila ya shaka ugomvi na ikhtilaaf ni katika silaha ya hatari kabisa anayopenda kuitumia Shaytwaan kufarikisha watu watengane na kuchukiana baada ya kuwa ni ndugu au marafiki au majirani au baina ya mume na mke. Lakini Uislamu haukuacha kutilia hima jambo la kusuluhisha ugomvi kwa kutukumbusha fadhila zake kubwa katika Qur-aan na Sunnah kama tunavyoona katika Aayah na Hadiyth hapo juu.

 

Lakini inasikitisha kuona kwamba jambo hili la kusuluhisha halikutiliwa mkazo sana katika jamii yetu, kwani wangapi tunasikia miongoni mwetu kuwa 'fulani kagombana na fulani na hawasemeshani', kisha zikapita siku na miezi na miaka hawa watu wako katika hali hii jambo ambalo Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amekataza kabisa zisipite zaidi ya siku tatu ndugu wa Kiislamu kuwa katika hali kama hiyo:

 

 

 عن أبي أيوب الأنصاري رضي الله عنه قال : قال النبي صلى الله عليه وسلم : (( لا يَحِلُّ لِمُسْلِمٍ أَنْ يَهْجُرَ أَخَاهُ فَوْقَ ثَلَاثِ لَيَالٍ ، يَلْتَقِيَانِ فَيُعْرِضُ هَذَا وَيُعْرِضُ هَذَا ، وَخَيْرُهُمَا الَّذِي يَبْدَأُ بِالسَّلامِ  .(( رواه البخاري ومسلم و في رواية أبو داود بإسناد على شرط البخاري ومسلم

((فَمَنْ هَجَرَ فَوْقَ ثَلاَثٍ فَمَاتَ دَخَلَ النَارَ ))   

Imetoka kwa Abu Ayyuub Al-Answariy رضي الله عنه ambaye alisema: Kasema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم: ((Haimpasi Muislamu amhame ndugu yake zaidi ya siku tatu hata wanapokutana huyu anamgeuzia (uso) huyu na huyu anamgeuzia (uso) huyu. Na aliye mbora wao ni yule anayeanza kutoa salaam)) [Al-Bukhariy na Muslim  na katika Riwayaah ya Abu Daawuud

((Atakayemhama (mwenzake) zaidi ya siku tatu akafariki basi ataingia  motoni))

 

Na huenda ikawa kila mmoja anataka kupatana na mwenziwe lakini Shaytwaan amewatia ari kuwa vipi aanze yeye? Na pia pengine huenda wakawa ni ndugu, au jamaa au jirani lakini hakuna mmoja wetu anayekimbilia kusuluhisha, sababu ni kwamba kila mmoja ameshughulika na kazi zake na maisha yake. Kwa hiyo tulichukulie hima jambo hili bila ya kuchelewesha kila inapotokea ugomvi baina ya ndugu wa Kiislamu na kufanya hivyo ni kumcha Allaah سبحانه وتعالى, kumtii Allaah سبحانه وتعالى na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم na ndio sifa ya Waumini kama Anavyosema Allaah سبحانه وتعالى:

 

  ((فَاتَّقُواْ اللّهَ وَأَصْلِحُواْ ذَاتَ بِيْنِكُمْ وَأَطِيعُواْ اللّهَ وَرَسُولَهُ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ))

 

((Basi mcheni Allaah na suluhisheni mambo baina yenu, na mtiini Allaah na Mtume Wake ikiwa nyinyi ni Waumini))  [Al-Anfaal:1]

 

Itaendelea sehemu ya pili in Shaa Allaah...

 

 

************

 

 

 

Share