Kuswali Rakaa Mbili Baada Ya Kutawadha Ni Sunnah? Nini Fadhila Zake?

Kuswali Rakaa Mbili Baada Ya Kutawadha Ni Sunnah Na Nini Fadhila Zake?

 www.alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Asalam Aleikum

 

Ninapomaliza kutawadha huwa na sali rakaa mbili kwanza kabla ya sala ya fardhi hii suna una inuwia vipi?

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Tufahamu kuwa Niyyah ya ‘Ibaadah yoyote ile ipo moyoni. Baada ya kutawadha ikiwa upo nyumbani Niyyah yake ni ya Sunnah ya kutawadha. Ama ikiwa upo Msikitini ndio umetawadha kisha ukaingia ndani au ulikuwa na wudhuu Niyyah kwa Swalaah hiyo itakuwa ni Tahiyyatul-Masjid.

 

Kwa maelezo zaidi bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi:

 

 Vipi kutia Niyyah Swalaah za Sunnah?

 

Vipi Kutia Niyyah Ya Ibaadah?

 

 Vipi Kutia Niyya Swalaah Za Qiyaamul-Layl?

 

 Swalaah Ya Witr Inaswaliwa Vipi Na Vipi Kutia Niyyah?

 

Vipi Kutia Niyyah Ya ‘Ibaadah Kama Swawm?

 

 

Fadhila ya Kuswali Sunnah ya Wudhuu (yaani baada ya kuchukua wudhuu) ni kubwa sana.  ‘Uqbah bin ‘Aamir (Radhiwya Allaahu ‘anhu) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

Mmoja akichukua Wudhuu vizuri kabisa na kuswali rakaa mbili kwa moyo wake wote na uso (ukiwa katika Swalaah kwa ukamilkifu), Jannah itakuwa yake” [Muslim, Abu Daawuwd, Ibn Maajah na Ibn Khuzaymah].

 

Na katika Hadiyth nyingine, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:  “Yeyote atakayechukua Wudhuu hivi (kwa ukamilifu wake na kama alivyofundisha) na baadaye akaswali rakaa mbili bila ya kuwa na mawazo yoyote akilini mwake, atasamehewa madhambi yake yote yaliyopita” [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

Na katika Hadiyth, siku moja Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alimuuliza Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu): "Nielezee juu ya ‘amali njema kabisa unayoitenda, kwani nimesikia sauti ya viatu vyako vikiwa mbele yangu Jannah (Peponi)?"

Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) Akajibu: "Ee Rasuli wa Allaah, sijafanya ‘amali yoyote niliyoiona kuwa ni bora kwangu isipokuwa kawaida yangu mimi kila nikitawadha huswali kadiri ninavyojaaliwa kuswali.” Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: “Hilo ndilo lililokufikisha”.  Al-Bukhaariy

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share