Swawm Katika Mwezi Wa Rajab - Kufunga Mwezi Mzima Au Siku Maalumu Ni Sunnah?

SWALI:

Kwajina la mwenyezimungu mwingi wa rehema, napenda kuuliza maswali yangu ambayo kidogo yananitatiza.

 Jee kuna suna ya kufunga swaumu katika mwezi wa Rajabu?

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka, Mola wa walimwengu wote, Swalah na salaam zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Kwanza kabisa tujue kuwa mwezi wa Rajab hakika ni katika miezi mitukufu minne Aliyotuwekea Allaah سبحانه وتعالى kama Alivyosema: 

{{إِنَّ عِدَّةَ الشُّهُورِ عِندَ اللّهِ اثْنَا عَشَرَ شَهْرًا فِي كِتَابِ اللّهِ يَوْمَ خَلَقَ السَّمَاوَات وَالأَرْضَ مِنْهَا أَرْبَعَةٌ حُرُمٌ ذَلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ فَلاَ تَظْلِمُواْ فِيهِنَّ أَنفُسَكُمْ}}

{{Hakika idadi ya miezi kwa Allaah ni miezi kumi na mbili katika hukumu ya Allaah tangu Alipoumba mbingu na ardhi. Katika hiyo iko minne mitakatifu. Hiyo ndiyo Dini iliyo sawa. Basi msidhulumu nafsi zenu humo}} [At-Tawbah: 36]

 

 

 

Vilevile tumethibitishiwa na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  kuwa mojawapo ya miezi hiyo minne ni mwezi huu wa Rajab kama katika Hadithi hii ifuatayo:

((عن أبي بكرة - رضي الله عنه - أن النبي صلى الله عليه وسلم خطب في حجة الوداع وقال في خطبته إن الزمان قد استدار كهيئة يوم خلق السماوات والأرض السنة اثنا عشر شهرا منها أربعة حرم ثلاث متواليات ذو القَعدة وذو الحجة والمحرم ورجب مضر الذي بين جمادى وشعبان ))  رواه البخاري

((Kutoka kwa Abu Bakrah رضي الله عنه kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alitoa Khutba yake ya mwisho akasema: "Wakati umemaliza mzunguko wake kama vile siku Allaah سبحانه وتعالى Alipoumba mbingu na ardhi. Mwaka ni miezi kumi na mbili, ambayo ndani yake kuna minne ni mitukufu, mitatu inafuatana, Dhul-Qaadah, Dhul-Hijjah na Muharram na Rajab upo baina ya Jumaada na Sha'abaan)) [Al-Bukhaariy] 

 {{يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ لاَ تُحِلُّواْ شَعَآئِرَ اللّهِ وَلاَ الشَّهْرَ الْحَرَام}}

{{Enyi mlioamini! Msivunje hishima ya alama ya Dini ya Allaah wala mwezi mtakatifu}} [Al-Maaidah: 2]

 

Kwa hivyo kuitukuza miezi hii mitukufu ni wajibu wetu kwa kutokufanya aina yoyote ya maasi, na kumcha Mungu zaidi.  Lakini katika kumcha Allaah, hakuna uthibitisho kwamba tunatakiwa tufunge siku maalumu au mwezi mzima (ila kwa dalili kama ilivyo funga ya mwezi wa Ramadhaan) kama wanavyofanya baadhi ya watu, kwani Mtume صلى الله عليه وآله وسلم hakufanya hivyo na sisi inatupasa tumfuate kutenda yale yale aliyoyafanya na kuacha yale asiyoyafanya.

Ikiwa atapenda mtu kumcha Allaah katika mwezi huu kwa kufunga saumu ambayo ni mojawapo ya 'ibaadah nzuri kabisa, basi hakuna neno kama atafunga Jumatatu na Alkhamiys na siku za 'Ayyaamul-Biydh' (Tarehe 13, 14 na 15 ) kama alivyokuwa akifunga Mtume صلى الله عليه وآله وسلم katika miezi yote. Au funga Swawm ya Nabii Dawuud ya kufunga siku moja na kuacha nyingine.

 

Ama kufunga mwezi mzima wa Rajab au siku maalumu kama siku ambayo wengi wamechukulia bila ya kupatikana na ushahidi kuwa ni siku ya Israa wal-Mi'iraaj, hakuna uthibitisho wowote kuwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم au Maswahaba wake walifunga mwezi mzima au siku hiyo abadan.

 Kwa maelezo zaidi ili upate kufahamu maudhuu hii tafadhali soma makala katika tovuti hii ya AL HIDAAYA, ambayo yapo katika kiungo hiki hapa chini:

 

Mwezi Wa Rajab: Fadhila Zake Na Yaliyozuliwa Ndani Yake

 

Wa Allaahu A'lam.

 

 

   
Share