Rajab: Uzushi Wa Kuomba Maghfirah Katika Mwezi Wa Rajab

 

Uzushi Wa Kuomba Maghfirah Katika Mwezi Wa Rajab

 

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

Assalam aleikum warahma tullahi wabarakatu  Kutoka katika hadith Qudsi Allah amesema, Mtu yeyote atakaye sema: Astagh'firullah dhul jalali wal- ikramu min jamii dhunubi wal-aatham" mara 1000 katika mwezi wa Rajab basi sitomuadhibu mtu huyo katika kaburi wala siku ya kiama  watumie Waislam wengine.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Hakuna dalili ya fadhila hizo. Baada ya utafiti tumetambua kwamba uzushi wa du’aa na adhkaar kama hizo zimejaa katika vitabu na mitandao ya Kishia.

 

Uzushi huo unasambazwa katika mitandao ya jamiii na la kusikitisha ni kuona jinsi Waislamu wanavyoharakisha kuwatumia watu bila ya kufanya utafiti, kwa kutekeleza amri ya mzushi huyo katika hilo swali hapo juu kuwa ‘watumie Waislam wengine’. 

 

Tena uzushi huo umeendelezwa na wengine kwa kauli zao kuwa: “Atakayeomba maghfirah mara mia, akakhitimisha kwa  Swadaqah, Allaah Atamkhtimisha  kwa rahmah na maghfirah na atakayesema mara mia nne Allaah Atamuandikia ujira wa mashahidi mia, na atakapokutana na Allaah Siku ya qiyaamah Atasema Nimethibitishia ufalme wangu basi tamani unachokitaka mpaka nikupe kwani hakuna mweza ghairi Yangu” [Inapatikana katika kitabu cha Kishia kiitwacho, Wasaail Ash-Shiy’ah (10/484).

 

Waislamu tahadharini na fitnah za mitandao ambayo zama hizi imekuwa fitna kubwa ya kusambazwa uzushi humo. Atambue Muislamu kwamba pindi inapomfikia kauli kuwa ni ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) basi imeshakuwa ni jukumu lake kufanya utafiti au kuulizia kwa Ahlul-‘Ilm (wenye ilmu) apate uhakika wa kauli hizo, au sivyo atakuwa ni katika wanaomuongopea Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye ametahadharisha:

 

 عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عَمْرٍو العَاص (رضي الله عنهما) أَنَّ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((…ومن كَذَبَ عَلَيَّ مُتَعَمِّدًا فَلْيَتَبَوَّأْ مَقْعَدَهُ مِنْ النَّارِ)) البخاري

Imepokelewa kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amr Al-‘Aasw (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) kwamba  Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:  ((…Na mwenye kunizulia uongo kwa makusudi, basi ajiandalie makazi yake motoni)). [Al-Bukhaariy]

 

'Ulamaa wa Salaf wametahadharisha mno kuhusu uzushi mwingi unaozuliwa katika mwezi wa Rajab na wakaandaa nukuu kadhaa na wakajibu fataawa mbali mbali. Miongoni mwao ni Al-Haafidhw bin Hajar (Rahimahu Allaah) katika kitabu chake: “Kubainisha Ajabu Katika Yaliyokuja Kuhusiana Na Fadhila Za Rajab” akasema: “Hakuna kilichothibiti katika fadhila za mwezi wa Rajab wala katika Swiyaam (funga) zake wala katika Swiyaam khaswa humo wala Qiyaamul-Layl (kuswali usiku) makhsusi ndani yake chochote katika Hadiyth Swahiyh." [Tabyiyn Al-'Ajab, uk. 11]

 

Kwanini Waislamu wasifuate na kutekeleza du’aa au adhkaar zilizothibiti ambazo zimejaa tele na dalili zake? Kwanini wawe na hima ya kufuata uzushi unaosambazwa na kila msambazaji?

 

Basi na tukomeke Waislamu na yale yaliyothibiti katika Qur-aan na Sunnah na tuilinde Dini yetu na uzushi na wazushi.

 

 

Na Allaah Ndiye Anajua Zaidi

 

 

 

Share