Katembea Na Mume Wa Rafiki Yake, Kaomba Msamaha

SWALI:

 

Salaam aleykum, nimelala na mme wa mtu nikaona vibaya nikaomba samahani kwa mkewe akanisamehe yakaisha, baadae mme wa yule dada akanifata tena na mimi na mapenzi nae tukaendelea kufanya hivyo vitendo tena sio mara moja nimemwambia tuoane anababaisha lakini kuzini na mimi ndo kazi yake, ni aibu wala sioni sifa kwa sababu namuogopa mwenyezi mungu nasali sala tano ila hapo tu kwenye zinaa na huyo mme wa mtu ndo nashindwa ila Alhamdulillah nimeamua kuacha sema tatizo lipo hapa natamani kumuomba mkewe samahani lakini nashindwa kwa sababu mwanzo aliumia sasa wenyewe wanapatana naogopa kuwagombanisha tena sielewi tamuomba vp samahani, NIMEPATA MCHUMBA NAOGOPA ASIJE AKAONA NAMUACHISHA YY ME LABDA TAOLEWA, nifanyeje? Nijibu haraka jamani nipo kwenye wakati mgumu sitaki kuolewa bila kumuomba samahani nikisubiri je huyo atakaekua mume wangu akisikia, naombeni ushauri jamani.

 


 

 

JIBU:

 

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kutembea na mume wa mtu.

Hakika ni kuwa zinaa ni katika madhambi makubwa ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Ameliwekea adhabu kali sana kwa mwenye kuiendea. Pia inatakiwa utahadhari sana na hata ‘Ibaadah yako ya Swalah, kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anatufahamisha kinaganaga kazi ya Swalah pale Aliposema: “Soma uliyofunuliwa katika Kitabu, na usimamishe Swalah. Hakika Swalah inazuilia mambo machafu na maovu” (al-‘Ankaabuut 29: 45).

Kazi ya Swalah ni kukuzuilia wewe ‘Faahishah’ ambayo ni zinaa na maovu yote. Vipi utakuwa unaswali kisha unatembea na mume wa watu na unazini naye.

 

Kama Muislamu, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatulezea kuwa,

Muislamu haumwi na nyoka kwenye tundu moja mara mbili”. Itakuaje wewe uwe utazini mara ya kwanza na usamehewe mbali na kuwa jambo hilo ni gumu sana kwa mume au mke pia kulikubali. Kukubali kwa mkewe ni kuonyesha kuwa anakutakia wewe kheri lakini wewe ukaenda nyuma yake ukarudia tena kosa hilo.

 

Tufahamu kuwa masharti ya kukubaliwa toba ni manne inapoingia haki ya mwanadamu katika suala lako hilo. Nayo ni kama yafuatayo:

 

1.     Kujiondoa katika maasiya.

2.     Kujuta kwa kufanya dhambi hilo.

3.     Kuazimia kutorudia tena kosa hilo.

4.     Kuomba msamaha kwa uliyemkosea.

 

Katika kosa hilo inaonyesha hujatekeleza sharti namba nne. Hivyo, inatakiwa wewe ufanye bidii kutekeleza hilo sharti, kwani unapokufa huenda akakudai haki siku ya Qiyaamah siku ambayo utamlipa thawabu zako na ikiwa huna basi madhambi yake utapatiwa wewe. Fanya bidii uombe msamaha kabla hujaaga dunia. Na ni ajabu ya kuwa mwanaume ambaye anadai anakupenda kisha akakataa kukuoa lakini anataka kustarehe nawe, nawe ukawa ni mwenye kukubali bila ya kusita kabisa. Je, kwa ishara hukufahamu kuwa huyo mwanaume anataka kukuchezea na kukupeleka motoni pamoja naye. Fanya bidii ukaombe msamaha kabla ya kuaga dunia na hatujui kila mmoja wetu ataondoka lini hapa duniani.

 

Ufahamu kuwa malipo mara nyingine ni hapahapa ulimwenguni, kama ulivyomfanyia mwenzio mke wa mtu ukalipwa kwa mumeo kufanywa anazurura na wanawake wengine usipate raha ya ndoa. Kisha jambo ambalo ni muhimu ni kuweza kutazama kama una mimba ya yule mwanamme uliyezini naye. Ikiwa utakuwa umebeba mimba itakuwa kwako haifai kuolewa mpaka uzae na uwe tayari umetubu na kuonekana mabadiliko yako ya kimaadili ndio utapata idhini kishari’ah ya kuolewa. Pia ufahamu kuwa ikiwa mume anayetaka kukuoa anataka mwanamke bikra utakuja adhirika usiku wa mwanzo kwani akiona si bikira basi kutakuwa na ugomvi na pengine kuachana. Kwa hivyo, ikiwa atauliza kama wewe ni bikira ni lazima useme ukweli kwani kusema uongo ni dhulma nyingine mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).

 

Ushauri wetu nenda tena ukaombe msamaha kwa mke wa mume kama inawezekana na hakutotokea madhara yoyote yale kwa kufanya hivyo, basi ni bora kufanya. Lakini ukiwa atahofia kutokea matatizo au shari kwa kufanya hivyo, ni bora uepuke na uombe Istighfaar sana na umuombee du'aa njema huyo aliyemfanyia ubaya na kumfanyia wema ukiweza.


Na Allaah Anajua zaidi

 

Share