Mwenye Kuzini Kisha Akatoa Mimba Nini Hukmu Yake?

SWALI:

 

Assalam alaykum.

Nauliza  hivi, nini  hukmu  ya  binti  aliyezini, kisha  akapata  uja uzito  na  kuutoa?

Na   pia  vipi  ataleta  tauba  ya  kikweli  ili  Allah  Amsamehe?Nitashukuru nikijibiwa kwa haraka na kwenye e-mail address hii. Shukran jaziila.



JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allahu 'anhum jamiy'an) na watangu wema mpaka Siku ya Qiyaamah.

Hili lilikuwa si tatizo katika jamii yetu, lakini kwa athari inayoonekana kwa kuiga ustaarabu wa Kimagharibu na utanda wazi katika kueneza uasherati na utovu wa maadili. Kwa sasa ubaya unaonekana kuwa mzuri na jambo zuri linaonekana baya.  Sasa tatizo hili la uzinzi limekuwa kubwa sana katika jamii yetu. Ni jambo la kusikitisha sana kuona ndugu zetu wanapotea kiasi hiki cha kuingia katika maasi ya uzinifu bila ya khofu.. 

Zinaa ni kosa kubwa katika Uislamu ndio Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Akatuusia tusikarie kabisa:

 ((وَلاَ تَقْرَبُواْ الزِّنَى إِنَّهُ كَانَ فَاحِشَةً وَسَاء سَبِيلاً))

((Wala msikaribie uzinzi. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya)) [Al-Israa:32]

 Na pia mzinzi ambaye hajaoa au kuolewa anafaa apigwe mijeledi mia moja hadharani

((الزَّانِيَةُ وَالزَّانِي فَاجْلِدُوا كُلَّ وَاحِدٍ مِّنْهُمَا مِئَةَ جَلْدَةٍ وَلَا تَأْخُذْكُم بِهِمَا رَأْفَةٌ فِي دِينِ اللَّهِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ وَلْيَشْهَدْ عَذَابَهُمَا طَائِفَةٌ مِّنَ الْمُؤْمِنِينَ))

((Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume, mtandikeni kila mmoja katika wao bakora mia. Wala isikushikeni huruma kwa ajili yao katika hukumu ya Allah, ikiwa nyinyi mnamuamini Allah na Siku ya Mwisho. Na lishuhudie adhabu yao kundi la Waumini)) [An-Nuur: 2]

Na ikiwa ameoa au ameolewa basi wanafaa wapigwe mawe hadi kufa kama ilivyothibiti katika Hadiyth ifuatayo:

فِي الصَّحِيحَيْنِ مِنْ رِوَايَة الزُّهْرِيّ عَنْ عُبَيْد اللَّه بْن عَبْد اللَّه بْن عُتْبَة بْن مَسْعُود عَنْ أَبِي هُرَيْرَة وَزَيْد بْن خَالِد الْجُهَنِيّ فِي الْأَعْرَابِيَّيْنِ اللَّذَيْنِ أَتَيَا رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَقَالَ أَحَدهمَا : يَا رَسُول اللَّه إِنَّ اِبْنِي هَذَا كَانَ عَسِيفًا - يَعْنِي أَجِيرًا - عَلَى هَذَا فَزَنَى بِامْرَأَتِهِ فَافْتَدَيْت اِبْنِي مِنْهُ بِمِائَةِ شَاة وَوَلِيدَة فَسَأَلْت أَهْل الْعِلْم فَأَخْبَرُونِي أَنَّ عَلَى اِبْنِي جَلْد مِائَة وَتَغْرِيب عَام وَأَنَّ عَلَى اِمْرَأَة هَذَا : الرَّجْم فَقَالَ رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ :  ((وَاَلَّذِي نَفْسِي بِيَدِهِ لَأَقْضِيَنَّ بَيْنكُمَا بِكِتَابِ اللَّه تَعَالَى الْوَلِيدَة وَالْغَنَم رَدّ عَلَيْك وَعَلَى اِبْنك مِائَة جَلْدَة وَتَغْرِيب عَام . وَاغْدُ يَا أُنَيْس - لِرَجُلٍ مِنْ أَسْلَم - إِلَى اِمْرَأَة هَذَا فَإِنْ اِعْتَرَفَتْ فَارْجُمْهَا))  فَغَدَا عَلَيْهَا فَاعْتَرَفَتْ فَرَجَمَهَا     البخاري و مسلم

Katika Swahihayn kutoka kwa Abu Hurayrah na Zayd bin Khaalid Al-Juhani (Radhiya Allahu 'anhum) katika kisa cha Mabedui wawili waliokuja kwa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).  Mmoja alisema: "Ewe Mjume wa Allaah, mwanangu (wa kiume) aliajiriwa na bwana huyu kisha akafanya zinaa na mke wake. Nimemlipa fidia kwa ajili ya mwanangu kwa kumpa kondoo mia moja na mtumwa mwanamke. Lakini nilipowauliza watu wenye elimu, wamesema kwamba mwanangu apigwe mijeledi mia na ahamishwe mji kwa muda wa mwaka na mke wa huyu bwana apigwe mawe hadi afariki".  Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Naapa kwa Yule Ambaye nafsi yangu imo Mikononi Mwake, nitahukumu baina yenu wawili kutokana na kitabu cha Allaah. Rudisha mtumwa mwanamke na kondoo  na mwanao apigwe bakora mia kisha mwanao ahamishwe mbali kwa muda wa mwaka. Nenda Ewe Unays! )) Alimwambia mtu katika kabila la Aslam, ((Nenda kwa mke wa huyu bwana na akikiri makosa yake, basi mpige mawe hadi mauti [yamfike])) Unays akamuendea na akakiri makosa yake, kwa hiyo akampiga mawe hadi mauti. [Al-Bukhaariy na Muslim]

Dhambi la uzinzi hivyo si dogo mbele ya Allah (Subhaanahu wa Ta'ala). Inafaa sisi Waislamu tuviondoshe vishawishi vyote ambavyo vinaweza kutupeleka karibu na zinaa. Hili ni kosa la kwanza kwa dada yetu.

Mbali na kosa hilo akatoa mimba ambayo inahesabiwa kuwa ni kuua nafsi. Kuua nafsi ambayo Allah Ameharamisha ni miongoni madhambi makubwa kwa kauli ya Mtume Muhammad (Swalla Llaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

عَنْ أَبِي هُرَيْرَة  رضي الله عنه أَنَّ رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ   ((اِجْتَنِبُوا السَّبْع الْمُوبِقَات))   قِيلَ يَا رَسُول اللَّه وَمَا هُنَّ ؟ قَالَ   ((الشِّرْك بِاَللَّهِ وَقَتْل النَّفْس الَّتِي حَرَّمَ اللَّه إِلَّا بِالْحَقِّ وَالسِّحْر وَأَكْل الرِّبَا وَأَكْل مَال الْيَتِيم وَالتَّوَلِّي يَوْم الزَّحْف وَقَذْف الْمُحْصَنَات الْمُؤْمِنَات الْغَافِلَات)) البخاري و مسلم  

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allahu 'anhu) ambaye amesema: Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Jiepusheni na dhambi saba kubwa zinazoangamiza)).  Wakauliza, ewe Mjumbe wa Allah! Yepi hayo? Akasema: ((Kumshirikisha Allah, kuua nafsi ambayo imeharamishwa na Allah ila kwa haki, uchawi, kula riba, kula mali ya yatima, kukimbia adui siku ya vita na kuwatuhumu wanawake wema ambao hata hawafikirii jambo la kuharibu utawa na ni Waumini  wema)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

Hivyo kuitoa mimba ni dhambi kubwa sana katika Dini yetu. Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amesema kuwa mwenye kuua nafsi pasi na nafsi nyengine au ufisadi katika ardhi ni kama kwamba ameua watu wote:

((مِنْ أَجْلِ ذَلِكَ كَتَبْنَا عَلَى بَنِي إِسْرَائِيلَ أَنَّهُ مَن قَتَلَ نَفْسًا بِغَيْرِ نَفْسٍ أَوْ فَسَادٍ فِي الأَرْضِ فَكَأَنَّمَا قَتَلَ النَّاسَ جَمِيعًا وَمَنْ أَحْيَاهَا فَكَأَنَّمَا أَحْيَا النَّاسَ جَمِيعًا))

((Kwa sababu ya hayo Tuliwaandikia Wana wa Israili ya kwamba aliyemuua mtu bila ya yeye kuua, au kufanya uchafuzi katika nchi, basi ni kama amewaua watu wote. Na mwenye kumuokoa mtu na mauti ni kama amewaokoa watu wote)) [Al-Maaidah:32]

Na pia Amekataza kuua watoto kwa sababu kwa kuogopa umasikini, kwani kuwaua ni dhambi kubwa :

((وَلاَ تَقْتُلُواْ أَوْلادَكُمْ خَشْيَةَ إِمْلاقٍ نَّحْنُ نَرْزُقُهُمْ وَإِيَّاكُم إنَّ قَتْلَهُمْ كَانَ خِطْءًا كَبِيرًا))

((Wala msiwauwe wana wenu kwa kuogopa umasikini. Sisi Tunawaruzuku wao na nyinyi. Hakika kuwaua hao ni khatia kubwa.)) [Al-Israa:31]

Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ameyataja madhambi yote haya mawili ambayo lau mtu atakufa nayo basi atapata adhabu maradufu.

((وَالَّذِينَ لَا يَدْعُونَ مَعَ اللَّهِ إِلَهًا آخَرَ وَلَا يَقْتُلُونَ النَّفْسَ الَّتِي حَرَّمَ اللَّهُ إِلَّا بِالْحَقِّ وَلَا يَزْنُونَ وَمَن يَفْعَلْ ذَلِكَ يَلْقَ أَثَامًا))

   ((يُضَاعَفْ لَهُ الْعَذَابُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَيَخْلُدْ فِيهِ مُهَانًا))

((Na wale wasiomuomba mungu mwengine pamoja na Allah, wala hawaui nafsi Aliyoiharimisha Allah isipokuwa kwa haki, wala hawazini - na atakaye fanya hayo atapata madhara))

((Atazidishiwa adhabu Siku ya Kiyama, na atadumu humo kwa kufedheheka)) [Al-Furqaan:68-69]

Baada tu ya Ayah hizi Allah Anasema, isipokuwa kwa mwenye kutubia, akaamini, akafanya matendo mema, hao Allah Atawabadilishia maovu yao yawe mema na hakika Allah ni Mwingi wa kusamehe na Mwenye kurehemu. Pia mwenye kutubia na akafanya amali nzuri, hakika yeye amerudi kwa Allah kwa toba ya kweli

 

 

((إِلَّا مَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ عَمَلًا صَالِحًا فَأُوْلَئِكَ يُبَدِّلُ اللَّهُ سَيِّئَاتِهِمْ حَسَنَاتٍ وَكَانَ اللَّهُ غَفُورًا رَّحِيمًا))

 

 

 

))   وَمَن تَابَ وَعَمِلَ صَالِحًا فَإِنَّهُ يَتُوبُ إِلَى اللَّهِ مَتَابًا)) 

 

 

((Isipokuwa atakayetubu, na akaamini, na akatenda vitendo vyema. Basi hao Allah Atayabadilisha maovu yao yawe mema. Na Allah ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu))

 

 ((Na aliyetubu na akafanya mema, basi hakika huyo ametubu kweli kweli kwa Allah) [Al-Furqaan:70-71].

Toba inafaa iletwe kwa madhambi yote anayofanya mja, na mlango wa toba uko maadamu jua halijachomoza kutoka magharibi na mtu hajafikia katika hali ya kukata roho. Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema kuwa Yeye Anasamehe madhambi yote

((قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَى أَنفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِن رَّحْمَةِ اللَّهِ إِنَّ اللَّهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ))

((Sema: Enyi waja wangu waliojidhulumu nafsi zao! Msikate tamaa na Rehma ya Allah. Hakika Allah Husamehe dhambi zote. Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu)) [Az-Zumar: 53]

Toba ina masharti yake ambayo yanafaa yatimizwe ili mja asamehewe madhambi na makosa yake. Ikiwa dhambi alilolifanya mja ni baina mja na Allah Aliyetukuka haliingiliani na haki ya binadamu, litakuwa na sharti tatu:

Ya kwanza: Kuacha maasiya.

Ya pili: Kujuta kwa kufanya hayo maasiya.

Ya tatu: Kuazimia kutorudia tena kosa lile milele. Likikosekana sharti moja katika hizi tatu basi toba haitosihi.

Na ikiwa dhambi lililofanywa lina mafungamano na mwanadamu sharti za kupata toba znakuwa ni nne: “Sharti hizi tatu zilizotajwa hapa juu na ya nne ni kuirudishia haki ya yule mtu, ikiwa ni mali au kitu chengine chochote umrudishie. Ni wajibu kwa Muislamu kutubu (kuomba msamaha) kwa madhambi yote. Ikiwa atatubia baadhi ya dhambi husihi toba yake kwa dhambi ile na zinabaki zile zilizobakia. Zimedhihiri dalili katika Kitabu na Sunnah na Ijma’ ya Ummah katika uwajibu wa toba 

Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:

((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا تُوبُوا إِلَى اللَّهِ تَوْبَةً نَّصُوحًا عَسَى رَبُّكُمْ أَن يُكَفِّرَ عَنكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ وَيُدْخِلَكُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ))

))Enyi mlioamini! Tubuni kwa Allah toba iliyo ya kweli! Asaa Mola wenu Mlezi Akakufutieni maovu yenu na Akakuingizeni katika Pepo zipitazo mito kati yak(e[At-Tahriym: 8]

Fanya mema mengi, kwani mema hufuta maovu kama alivyosema Allah katika Qur-aan na Hadithi za Mtume (Swalla Llaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 Tunamuombea dada yetu Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amsamehe madhambi yake na ampatie hima ya kuweza kubaki katika Imani, ‘Ibadah na amfishe akiwa Muislamu,  pamoja na Waislamu wengine wote.

 

Na Allah Anajua zaidi

 

Share