Kuitikia Salaam Au Kumuamkia Asiye Muislam

SWALI:

 

Asalaam Aleykoum Warahmatullah Wabarakatu.

 

Natumai kwa uwezo wa Allah mko katika kheri zake Inshaalah. Swali langu naomba mnifahamishe vipi kuitikia salam ya mtu ambaye si Muislam na vipi jinsi ya kumwamkia yeye katika sheria.

 

Wabilahi Tawfiq.

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu kwa swali lako kuhusu kuitikia salaam au kumuamkia asiye Muislamu.

Ama kuhusu salaam ambazo Muislamu anatolewa na asiye Muislamu ikiwa ni katika yale maamkuzi ya Kiislamu, yaani asiye Muislamu akikuamkia kwa Assalaamu ‘Alaykum, basi wewe unawajibika kumjibu kwa kusema Wa ‘Alaykum (Imepokewa na al-Bukhaariy na Muslim). Ama ikiwa ni habari yako au habari ya asubuhi basi utamjibu kuwa ni nzuri au ni njema.

 

Ama kuanza kumuamkia asiye Muislamu kwa Assalaamu ‘Alaykum haifai kabisa (Imepokewa na Muslim), kwani hiyo ni salaam ya Muislamu kwa mwenziwe. Lakini ikiwa ni zile habari za kawaida habari ya jioni au habari za asubuhi hakuna shida yoyote ile.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share