Skip navigation.
Home kabah

Fadhila Za Swawm

                                                                                  Imeandikwa na: Ukht Muznah  Faraj

Ndugu katika iymaan

 

Sifa njema zote Anastahiki Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) Mola wa viumbe wote mwingi wa rehma na mwingi wa kusamehe na rehma na amani zimfikie kipenzi chake Allah Mtume wetu Muhammad (swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Jamaa na Sahaba wake wote.

 

Amma Baad:

Ndugu yangu Muislamu ama kwa hakika umetufikia mwezi ulio mtukufu na wenye fadhila kubwa na mavuno kwa wenye mazingatio kwa hayo, nao ni mwezi wa Ramadhan ambao Allah Ameufaradhisha kwa Waislam kwa kauli yake Jalla wa ‘Alaa Aliposema:

 

Enyi mlioamini mmefaradhishiwa (mmelazimishwa) kufunga (Swawm mwezi wa Ramadhaan) kama walivyofaradhishiwa kabla yenu ili mpate kumcha Allah. Qur-aan 2-183

 

Na hili la kumcha Allah ndio lengo kubwa la ibada hii ya funga kwani ni ibada ya siri baina yako na Mola wako. Na wengi wanaliona gumu jambo hili la kufunga wakati lina fadhila kubwa kabisa wengi wanapitwa na fadhila za kufunga kwa kupenda kula na kunywa. Majuto yatawajia pale watakapokutana na Mola wao hali hawana kitu.

Na ni siku maalum, siku chache katika mwaka mzima zilizowekwa watu hawamuonei hayaa Mwenyeezi Mungu kwa kula mchana bila ya udhuru wowote wa kisheria.  Allah Anatwambia katika kitabu Chake kitukufu: 

"Siku chache tu (kufunga huko) Na atakae kuwa mgonjwa katika nyinyi au katika safari (akafungua baadhi ya siku), basi (atimize) hisabu katika siku nyingine" Qur-aan 2-184

 

Ama kwa hakika tumeona umuhimu na wajibu wa kufunga. hivyo basi napenda kuchukua fursa hii adhimu kuwafahamisha ndugu zangu katika imaan fadhila za kufunga namuomba Allah Aniwezeshe.

 

Miongoni mwa fadhila hizo ni:

1- Funga inamuokoa mtu kutokana na moto:

Kama ilvyopokewa na imam Ahmad katika Hadiyth sahihi.

Kutoka kwa Jaabir (radhiya Allahu ‘anhu) hakika ya Mtume (swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: " Swawm ni kinga itamukoa mja kutokana na moto (siku ya Qiyaamah)

(imepokewa na At-Twabaraaniy kutoka kwa ‘Uthmaan bin Abil ‘Aas)

Na katika Hadiyth iliyopokewa na ambayo ni muttafaqun ‘alayhi, inasema:

Kutoka kwa Abu Sa’iyd Al Khudhriyy (radhiya Allahu ‘anhu) hakika Mtume (swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Mwenye kufunga siku kwa ajili ya Allah Mwenyeezi Mungu Atamuokoa uso wake kutokana na moto kwa umbali wa miaka sabini"

Ndugu yangu Muislam ikiwa unafunga siku moja na Allah Anakuokoa na moto wa Jahannam je, Ukifunga Ramadhaan yote! Hakika hii ni fadhila kubwa.

Na fadhila hizi zinaingia katika funga za lazima na funga za Sunnah.

 

2- Swawm ni kinga kutokana na matamanio:

Imekuja katika Hadiyth

Kutoka kwa Ibn Mas’uud (radhiya Allahu ‘anhu) amesema Mtume (swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Enyi kundi la vijana miongoni mwenu atakae kuwa na uwezo wa kuoa basi na aoe, (kufanya hivyo) kutampelekea kuinamisha macho yake na kuhifadhi tupu yake. Ikiwa hana uwezo wa kuoa basi na afunge kwani hiyo ni kinga kwake. (hadiythun muttafaqun alayhi)

 

Hakika vijana wengi wanashtakia kutokana na matamanio khasa katika zama zetu hizi za wanawake wanaotembea wazi katika masoko, waliowekwa picha zao tupu kwenye magazeti, wanajitoa katika matangazo ya televisheni, hii ndio sababu kubwa inayoleta athari ya uchafu na ufisadi mkubwa katika ardhi. Allah Atuhifadhi! Na kwa sababu hiyo Mtume (swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawanasihi vijana ikiwa mtu hana uwezo wa kuoa basi na afunge.

 

3- Swawm ni njia ya kumpelekea mtu peponi:

Kutoka kwa Abu Umamah (radhiya Allahu ‘anhu) amesema kumwambia Mtume (swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), “Ewe Mtume wa Allah Niamrishe mimi jambo litakalonifaa mbele ya Allah”. Akasema Mtume (swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), “Ni juu yako kufunga kwa hakika hakuna mfano wake" (Sunanu An-Nasaaiy)

Akabainisha ‘alayhi sswalaatu wa ssalaam kuwa hakuna kitu kitakacho mkurubisha mja kwa Allah, na kumuweka mbali na adhabu kama kufunga.

Bali ametupa khabari Mtume (swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika pepo kuna mlango khasa wa wenye kufunga.

Kutoka kwa Sahal bin Sa'ad (radhiya Allahu ‘anhu) hakika Mtume (swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Hakika katika pepo kuna mlango unaitwa Rayyaan,wataingia humo siku ya Qiyaamah wenye kufunga tu, hatoingia yeyote mwingine, utasema wako wapi wenye kufunga? Watasimama kuingia hatoingia yeyote mwingine, wakisha kuingia utafungwa, basi hatoingia mwengine" (imepokewa na Al-Bukhaariy)

Na umepewa jina hilo kunasibiana na sifa ya Swawm ambayo inampata mtu kiu kutokana na athari ya kufunga. mara nyingi mtu anapofunga  hatamani chakula kama anavyotamani maji.

 

4- Funga itamuombea mtu siku ya Qiyaamah:

Kutoka kwa Abdullah bin ‘Amru bin Al-‘Aas (radhiya Allahu ‘anhuma) amesema Mtume (swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) " Funga na Qur-aan zitamuombea mja siku ya Qiyaamah, itasema funga ewe Mola amejizuilia kutokana na chakula chake na matamanio yake wakati wa mchana, basi nnamuombea msamaha, na itasema Qur-aan amejizuilia kutokana na usingizi wake wakati wa usiku ninamuombea msamaha. Akasema wamesamehewa. (imepokewa na Ahmad na Al-Haakim)

 

5- Swawm ni kafara na msamaha kutokana na madhambi:

Kwa hakika mema huondosha maovu na Swawm ni katika jambo jema sana.

Na Amesema Allah (Subhaanahu wa Ta'ala): "Hakika ya mema huyaondosha maovu"  Qur-aan 11-114

 

Na katika Hadiyth iliyopokewa na maimamu sita.

Kutoka kwa Hudhayfah (radhiya Allahu ‘anhu) amesema Mtume (swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) " Fitna ya mtu kwa mke wake, mali yake na jirani yake itamfidiya kutokana na Swalah, funga na sadaqa"

Mara nyingi kunakua na upungufu ima katika haki za mkeo kwa njia ya maneno au kuudhi na upungufu mdogodogo na katika makosa ya haki za jirani iwe kwa matendo au qauli na katika kuitakasa mali, vyote hivyo hutakaswa na Swalah, funga na sadaqa. Iwapo mtu atajilazimisha na haya basi atasamehewa madhambi yake madogo.

 

Na kutoka kwa Abu Hurayrah (radhiya Allahu ‘anhu) hakika Mtume (swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema "mwenye kufunga Ramadhaan kwa imani na akatarajia malipo atasamehewa madhambi yake aliyoyatanguliza"

Imaani ni kumuamini Allah na funga ukamkusudia Allah Aliyetukuka na ukataraji malipo ambayo Allah Ameyatolea ahadi kwa wenye kufunga.

Kwani kuna baadhi ya watu bado wanamshirikisha Mwenyeezi Mungu katika ibada zake. Wafunga, waswali kwa ajili ya majini, n.k. nayo ni makosa makubwa sana.

 

Na katika Hadiyth nyingine:

Kutoka kwa  Abu Hurayrah (radhiya Allahu ‘anhu) amesema Mtume (swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): "Swalah tano, na ijumaa mpaka ijumaa, na Ramadhaan mpaka Ramadhaan, zitamfidia baina yake madamu atakua ni mwenye kujiepusha na madhambi makubwa" (imepokewa na Muslim)

Kufunga mwezi wa Ramadhaan ni sababu ya kusamehewa madhambi ambayo umeyatanguliza katika kipindi cha mwaka mzima uliopita lakini basi imewekewa sharti ni kwamba ujiepushe na madhambi makubwa kwani madhambi makubwa hayafutiki mpaka ulete tawbah, na hili wamekubaliana wanavyuoni wote. Na vilevile Allah Amesema katika Kitabu Chake kitukufu:

“Ikiwa mtajiepusha hizo  na (madhambi) Makubwa yaliyo katazwa Atakufutieni (Mwenyeezi Mungu) maovu yenu na Atakuingizeni katika maingizo matukufu”  Qur-aan 4-31.

 

6- Swawm ni sababu ya kupata furaha ya nyumba mbili:

Kama ilivyokuja katika hadiyth.

Kutoka kwa Abu Hurayrah (radhiya Allahu ‘anhu) amesema Mtume (swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Mwenye kufunga ana furaha mbili; furaha ya kwanza anapofungua na furaha ya pili atakapokutana na Mola wake". Al-Bukhaariy na Muslim

Amma kwa hakika  katika furaha ya kwanza ni pale Allah Alipotuhalalishia wakati wa jioni kula na kunywa kwani ni vitu ambavyo tunavipenda kwa hivyo tukamuabudu Mwenyeezi Mungu kwa kujizuilia kula, kunywa na matamanio wakati wa mchana.

Amma furaha ya pili ni pale Allah Alipotuwafiqisha kuitimiza Swawm hadi jioni kwani mara nyingine unakuwa taabani mpaka ikifika jioni unamshukuru Allah, ‘Alhamdulillahi nimeifikisha Swawm hadi jioni na nimeikamilisha ibada’

 

7- Harufu ya mdomo wa mwenye kufunga mbele ya Allah ni nzuri kuliko harufu ya miski: 

Harufu ya mdomo ambayo inatoka ni kutokana na kutokula chakula. Nayo ni harufu iwachukizayo watu lakini mbele ya Allah ni yenye kupendeza:

Amesema Mtume (swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):  "Naapa kwa yule ambaye nafsi ya Muhammad iko mikononi Mwake; harufu ya mdomo wa mfungaji ni nzuri mbele ya Allah kuliko harufu ya miski". Al-Bukhaariy na Muslim