Ushindi Katika Ramadhwaan

 

Imekusanywa Na: Muhammad Al-Ma'awy

 

 

UTANGULIZI

 

Mwezi wa Ramadhaan ni mwezi uliojaa juhudi na fadhila tele na nyingi ambazo lau zitatiliwa maanani, Ummah huu utanyanyuka kutoka daraja moja hadi nyengine. Huu ni mwezi wa Qur-aan, kwa kuwa iliteremshwa kwayo. Hivyo ni juu yetu kuisoma kwa kuzingatia na kufanyia kazi amri zilizotolewa ndani yake. Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Anasema: “Ramadhaan ni mwezi ambao Qur-aan imeteremshwa ili iwe uongozi kwa watu, na hoja zilizo wazi wa uongozi na upambanuzi (wa baina ya haki na batili)” (2: 185).

 

Huu ni mwezi wa Usiku wa Qadari (wenye Nguvu – Laylatul Qadr), ambao usiku huo ni bora kuliko miezi elfu moja. Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Anasema: “Laylatul Qadr ni bora kuliko miezi elfu moja” (97: 3).

 

Huu ndio mwezi wa Funga ya Faradhi, kwani Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Anasema: “Enyi Mlioamini! Mmelazimishwa kufunga kama walivyolazimishwa kufunga waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Allaah” (2: 183).

 

Huu pia ndio mwezi wa Sadaka, ‘Umrah, Du’aa, Subira na Jihadi. Hii haimanishi miezi mingine huwa hivi vitu havifai kufanywa. Laa hasha! Maana yake ni kuwa katika mwezi wa Ramadhaan Muislamu anatakiwa aongeze amali hizi. Tufahamu ya kuwa huu sio mwezi wa kulala kupindukia au kula sana bali ni mwezi ambao tunafaa tuongeze ‘Ibadah zetu kwa kiasi kikubwa zaidi.

 

 

 

MASHARTI YA USHINDI

 

Ushindi hauteremki kutoka katika ombwe wala haiji bila kutarajiwa. Ushindi na kushindwa zipo na kutawaliwa na kanuni na njia, ambazo zimenukuliwa na Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) katika Qur-aan ili Waumini waweze kuzijua kwa yakini, elimu ya uhakika na kwa upeo mkubwa zaidi. Kanuni hizi hazibadiliki kwa kiasi kikubwa. Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Anasema yafuatayo kuhusu kanuni hizi: “Kabla yenu zimepita nyendo nyingi; basi tembeeni katika ulimwengu muangalie vipi ulikuwa mwisho wa wanaokanusha” (3: 137).

Na pia, “Hii ni ada ya Allaah iliyokuwa kwa wale waliopita zamani. Wala hutapata mabadiliko katika ada ya Allaah” (33: 62).

Na Anasema tena Aliyetukuka: “Huo ndio mwendo wa Allaah uliokwishapita zamani, wala hutapata mabadiliko katika mwendo wa Allaah” (48: 23).

 

Shida kubwa ya Ummah huu ambao unakumbana nao leo ni kuwa wafuasi wake (Waislam) wameleweshwa na kasumba za Kimagharibi na za kigeni, zilizopotoka kutoka katika njia nyoofu na wamesahau ujumbe wao. Tumeshindwa kutofautisha baina ya adui na rafiki na hatujui mikakati na njama dhidi yake na yetu). Hivyo, kwa Umma wowote kuweza kushinda dhidi ya adui yake masharti fulani ni lazima yapatikane. Ikiwa kipote kimoja au chochote kimeweza kutekeleza masharti hayo, ushindi utakuwa wao. Nyakati za ushindi na kushindwa zinabadilishana mikono kutegemea kanuni fulani. Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Anasema: “Kama yamekupateni majaraha, basi na hao watu wengine yamewapata majaraha mfano wa haya. Na siku za namna hii tunaweletea watu kwa zamu, ili Allaah Awapambanue walioamini na awateuwe miongoni mwenu mashahidi. Na Allaah hawapendi madhalimu” (3: 140).

 

Masharti yenyewe yameelezwa hapa chini:

 

 

1.    IMANI YENYE NGUVU

 

Imani ni sharti kwetu sisi kuweza kuwashinda makafiri. Ikiwa Waislam ni wakweli na Waumini wa kihakika basi wataweza kuwashinda maadui zao kila wakati na lau hatutaweza kuwa juu yao itakuwa sisi ndio wenye shida kubwa sana. Waumini ndio walengwa wa kupata ushindi, na kuhusu suala hilo Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Anamzungumzia Mtume Wake (swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama ifuatavyo: “Na wakitaka kukukhadaa basi Allaah atakutosheleza. Kwani Yeye Ndiye Aliyekuunga mkono kwa nusura yake na kwa Waumini. Na Akaziunga nyoyo zao. Na lau wewe ungelitoa vyote viliomo duniani usingeliweza kuziunga nyoyo zao, lakini Allaah Ndiye Aliyewaunganisha” (8: 62 – 63).

Wakati mwengine Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Anawatumia Malaika ili wawasaidie Waumini kama Alivyosema: “Mola wako Mlezi Alipowafunulia Malaika: Hakika Mimi ni pamoja nanyi, basi watieni nguvu walioamini. Nitatia woga katika nyoyo za waliokufuru” (8: 12).

Yeye (Subhaanahu Wa Ta’ala) Anasema tena: “Kisha Allaah Akateremsha utulivu wake juu ya Mtume wake na juu ya Waumini. Na Akateremsha majeshi ambayo hamkuyaona, na Akawaadhibu wale waliokufuru. Na hayo ndiyo malipo ya makafiri” (9: 26).

 

Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Anatumia njia nyengine yoyote Anayopenda kuwasaidia Waumini katika vita dhidi ya mushirikina kama kwa mfano Alipotumia kimbunga kuwasambaratisha katika Vita vya Handaki, “Enyi mlioamini! Zikumbukeni neema za Allaah zilio juu yenu. Pale yalipokufikilieni majeshi, Nasi Tukayapelekea upepo, na majeshi msiyoyaona. Na Allaah Anayaona mnayoyatenda” (33: 9). Au kutuma mvua kama rehema kwa Waislam katika Vita vya Badr, “Alipokufunikeni kwa usingizi uwe ni uaminisho kutoka kwake, na Akakuteremshieni maji kutoka mbinguni ili kukusafisheni kwayo na kukuondoleeni uchafu wa Shetani, na kuzipa nguvu nyoyo zenu, na kuitia imara miguu yenu” (8: 11). Au Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) wakati mwengine Anatumia jeshi la adui lenyewe kuuana wenyewe kwa wenyewe kama ilivyotokea kwa kabila la Kiyahudi la Nadhiir lililokuwa likiishi katika mji wa Madinah, “Yeye ndiye aliyewatoa waliokufuru miongoni mwa Watu wa Kitabu katika nyumba zao wakati wa uhamisho wa kwanza. Hamkudhani kuwa watatoka, nao walidhani kuwa ngome zao zitawalinda na Allaah. Lakini Allaah Aliwafikia kwa mahali wasipopatazamia, na akatia woga katika nyoyo zao. Wakawa wanazibomoa nyumba zao kwa mikono yao na mikono ya Waumini. Basi zingatieni enyi wenye macho!” (59: 2).

 

Sharti kubwa ya kushinda maadui ni kuwepo kwa pote la “Waumini”. Na lau Waumini watasimama imara basi Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Atawafanya wao waweze kuitawala ardhi hii, ikitokea kinyume na hilo basi watakuwa ni wenye kutawaliwa. Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Anasema: “Allaah Amewaahidi wale walioamini miongoni mwenu na wakatenda mema, ya kwamba Atawafanya makhalifa katika ardhi kama Alivyowafanya makhalifa wa kabla yao, na kwa yakini atawasimamishia Dini yao aliyowapendelea, na Atawabadilishia amani baada ya khofu yao. Wawe wananiabudu Mimi, wala wasinishirikishe na chochote. Na wataokufuru baada ya hayo, basi hao ndio wapotovu” (24: 55).

 

Waumini wanatakiwa kuwa na ufahamu na utambuzi na mas-ala kadhaa ya Uislamu. kwa huu ufahamu ina maana kuwa hata fikra zetu ziwe kwa ukamilifu wake zinakwenda sambamba na mambo yanayohusiana na maisha katika dunia hii. Katika haya Muumini anafaa afahamu mas-ala yafuatayo ambayo ni muhimu sana:

 

·         Tawhidi iliyo safi na ya asili isiyokuwa na mawaa (madoa) aina yoyote wala kuchanganyika na ushirikina aina yoyote ile kama Shriki Kubwa, Ndogo au Khafiy (isiyoonekana/ iliyofichikamana). Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Anasema: “Basi jua ya kwamba hapana muabudiwa wa haki ila Allaah, na omba maghfira kwa dhambi zako na za Waumini wanaume na Waumini wanawake” (47: 19).

·         Kujua misingi na mambo muhimu ya Uislamu na kushikamana barabara na Qur-aan na Sunnah za kipenzi chetu Mtume Muhammad (swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) anasema: “Enyi mlioamini! Mtiini Allaah, na mtiini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi. Na mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume, ikiwa mnamuamini Allaah na Siku ya Mwisho. Hayo ndiyo bora zaidi na ndiyo yenye mwisho mwema” (4: 59).

·         Uoni (kuona mbali) na uangalifu katika kazi na shughuli za Da‘wah. Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Anasema: “Sema: Hii ndiyo Njia yangu - ninalingania kwa Allaah kwa kujua - mimi na wanaonifuata. Na ametakasika Allaah! Wala mimi si katika washirikina” (12: 108).

·         Kuwa na maadili madhubuti yenye kuigwa na wengine kwa sababu wewe umefuata kielelezo na ruwaza njema katika shakhsiya ya Mtume Muhammad (swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Tukiiga Akhlaaq za Mtume (swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) basi hatutapotea bali tutakuwa na ufanisi wa hapa duniani na pia Kesho akhera. Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Anatuambia: “Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Allaah kwa anaye mtaraji Allaah na Siku ya Mwisho, na akamkumbuka Allaah sana” (33: 21). Na pia, “Na hakika wewe una tabia tukufu” (68: 4). Na pia kumfuata yeye ni kupendwa na Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) kama alivyosema Aliyetukuka: “Sema: Ikiwa nyinyi mnampenda Allaah basi nifuateni mimi, Allaah atakupendeni na atakufutieni madhambi yenu. Na Allaah ni Mwenye kufuta madhambi na Mwenye kurehemu” (3: 31). Na Mtume (swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakika mimi sikutumwa ila kukamilisha maadili mema” (Maalik, al-Bayhaqiy).

·         Kutafuta elimu yote yenye manufaa kwa Ummah huu wa Kiislamu na kushindaa katika hilo. Sababu ni kuwa kushindana katika wema ni thawabu kubwa elimu ikiwa ni mmoja wapo. Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Anasema: “Na katika watu, na wanyama, na mifugo, pia rangi zao zinakhitalifiana. Kwa hakika wanao mcha Allaah miongoni mwa waja wake ni wanazuoni. Hakika Allaah ni Mwenye nguvu, Mwenye kusamehe” (35: 28).

·         Kuweza kufuatilia habari za yanayojiri kila leo pamoja na kujua habari za Waislam katika nchi nyengine.

 

2. UKIMSAIDIA Allaah, ATAKUSAIDIA

 

Hakika ni kuwa ushindi unakuja kutoka kwa Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala). Yeyote anayesaidiwa na Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) hakuna hata mmoja wa kumshinda na kumpiku, japokuwa huenda wakawa wao ni wengi na wenye silaha kali na kubwa za kisasa. Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Anasema: “Akikunusuruni Allaah hapana wa kukushindeni, na Akikutupeni ni nani, basi, baada yake Yeye atayekunusuruni? Na Waumini wamtegemee Allaah tu” (3: 160).

 

Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Anawasaidia Waumini japokuwa watakuwa kidogo kama vile jeshi la Twaalut, kama Anavyosema Aliyetukuka: “Alipovuka mto yeye na wale walioamini pamoja naye, walisema: Leo hatumwezi Jaluti na majeshi yake. Wakasema wale wenye yakini ya kukutana na Allaah: Makundi mangapi madogo yameshinda makundi makubwa kwa idhini ya Allaah. Na Allaah yu pamoja na wenye kusubiri. Na walipotoka kupambana na Jaluti na majeshi yake walisema: Mola wetu Mlezi! Tumiminie subira, na isimamishe imara miguu yetu, na utusaidie tuwashinde watu Makafiri. Kwa idhini ya Allaah waliwatimua, na Daawuud akamuuwa Jaluti, na Allaah akampa Daawuud ufalme na hikima” (2: 249 - 251). Pia Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Alimpatia ushindi Mtume Muhammad (swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake walipokuwa wachache kama katika Vita vya Badr, Khandaq, Taabuk, Mu’ta na vita vyenginezo. Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) wakati mwengine humsaidia mtu au watu japokuwa hana (hawana) silaha wala jeshi. Mfano wa hili ni usaidizi aliopata Mtume (swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Abu Bakr (Radhiya Llahu ‘Anhu) walipokuwa pangoni wakati wa kuhama kwao kutoka Makkah kuelekea Madinah. Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Anasema: “Ikiwa nyinyi hamtamnusuru Mtume, basi Allaah Alikwisha mnusuru walipomtoa waliokufuru, naye ni wa pili katika wawili walipokuwa katika pango, naye akamwambia sahibu yake: Usihuzunike. Hakika Allaah yu pamoja nasi. Allaah akamteremshia utulivu wake, na akamuunga mkono kwa majeshi msiyoyaona” (9: 40).

 

Hivyo ni kuwa yeyote mwenye kumsaidia Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala), Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Ametoa ahadi ya kumsaidia kwa msingi wa sharti hili. Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Anasema: “Enyi mlioamini! Mkimnusuru Allaah naye Atakunusuruni na Ataithibitisha miguu yenu” (47: 7).

 

 

 

3.    KUSHIKAMANA VILIVYO NA UISLAMU

 

Kushikamana kikweli na kwa ikhlasi na Uislamu ni sharti katika kufaulu na kupata ushindi. Lau watu watapotoka kutoka kwa mafundisho ya Qur-aan na Sunnah basi wakati huo tutakumbwa na matatizo na shida aina zote mpaka tutakaporudi katika mafundisho ya Dini yetu, sahihi na safi.

 

Utii kwa Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) na Mtume Wake (swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni muhimu sana. Hebu tutazame mfano wa Vita vya Uhud (3H/ 625 Miladi) wakati ambapo Maswahaba 50 (radhiya Allaahu ‘anhum) waliowekwa katika kijinjia kwenye mlima na maagizo makali wasiwe ni wenye kuondoka sehemu hiyo waliyowekwa kwa hali yoyote ile. Lakini pindi walipoondoka ule ushindi waliokuwa nao ukageuka na kuwa ni majuto na hasara. Takriban Maswahaba 70 (radhiya Allaahu ‘anhum) walikuwa ni wenye kupata shahada wakiwemo Hamzah ibn ‘Abdul-Mutallib, Musw‘ab ibn ‘Umayr, Julaybib, Anas ibn an-Nadhr (radhiya Allaahu ‘anhum) na wengineo. Ikiwa kuacha agizo moja maafa yake ni hayo jee kuacha maagizo chungu mzima, itakuwaje?

 

Sayyidna ‘Umar ibn al-Khatwtwaab (eadhiya Allaahu ‘anhu) amesema: “Sisi ni watu tuliopatiwa utukufu na nguvu na Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) kwa Uislamu, pindi tu tukapokengeuka (na kupotoka) na Uislamu basi hapo Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Atatudhoofisha na kututweza”.

 

 

 

4.    UONGOZI WENYE IKHLASI

 

Wakati ambapo tulikuwa na uongozi wenye ikhlasi na uchaji Mngu, Waislam waliendelea kuwashinda maadui zao kwa usahali sana. Mfano ni katika kipindi cha Mtume (swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), makhalifa Waongofu (radhiya Allaahu ‘anhum), watawala wa awali baada yao (watawala wa Banu Umayyah na Banu ‘Abbaas). Pia wale watawala wema waliokuja muda mrefu baada yao waliweza kurudisha nguvu na utukufu wa Uislamu kama wakati wa Swalaah ud Diyn Hasan al-Ayyubiy, Nuur ud Diyn Zinkiy, Nuur ud Diyn Mahmuud, Qitz Mudhaffar Mahmuud na kadhalika. Kiongozi wa Kiislamu anatakiwa awe ni mfano mzuri na ruwaza njema kwa wafuasi ili nao wapate kielelezo hai cha aliyejipamba kwa sifa kemkemu za Kiislamu. Miongoni mwa sifa ambazo kiongozi anafaa kuwa nazo ni Taqwa, uadilifu, elimu, utiifu kwa Qur-aan na Sunnah, maadili mema (ukweli, uaminifu, kutekeleza ahadi, upole na ulaini, na kadhalika), Istiqaamah, awe ni mwenye kuwataka washauri wenziwe, ujasiri na kutoogopa, na kadhalika.

 

 

 

VITA WAKATI WA RAMADHAAN

 

Katika mwezi mtukufu wa Ramadhaan, Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Aliwasaidia Waislam sana, ambao nao walikuwa msitari wa mbele katika kumridhisha Mola wao Mlezi. Walipata ushindi mmoja baada ya mwengine na hivyo kuweza kuutawala ulimwengu bila ya shida aia yoyote. Lakini pindi tu Ummah ulipo asi na kurudi nyuma kutoka kwa uimara wao katika malengo, kupotoka katika njia ya sawa ilinyooka, wakapuuza na kusahau ‘Ibadah, udhaifu mkubwa uliingia kati yao. Hivyo kwa wakati huu wanaonekana ni kama watumishi waliotiwa minyonyoro na Ummah mwengine. Katika udhaifu huu, Ummah umepata waumini washupavu waliosimama imara katika kuutetea Uislamu na hivyo kwa sasa kuweza kunyanyua kichwa tena.

 

Baadhi ya matukio ya kivita yaliyo muhimu ambayo yalitokea katika mwezi huu wa Ramadhaan wakati ambao Waislam waliweza kupata ushindi ni:

 

 

1.    Vita vya Badr, vilivyopiganwa tarehe 17 Ramadhaan 2 H (624 Miladi): Waislam walikuwa 313 dhidi ya makafiri 1000. Mbali na idadi ndogo na maandalizi duni, waliweza kuwashinda mahasimu wao. Hivi ndivyo vilivyokuwa vita vya kwanza, ambavyo viliwafungulia Waislam silsila ya ushindi.

 

2.    Maandalizi ya Vita vya Khandaq vilianza Ramadhaan ya mwaka wa 5 H (627 M). Matayarisho yalikuwa ni kufukuliwa kwa handaki katika pande tatu za mji wa Madinah ili kuwa ni kizuizi kwa makafiri waliojiandaa na kushirikiana.

 

3.    Kufunguliwa kwa mji wa Makkah ambao ndio uliokuwa ushindi na ufanisi mkubwa wa Mtume (swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) dhidi ya mushirikina wa Makkah. Ushindi huu wa kuingia Makkah bila ya kumwagwa damu ulitokea 20 Ramadhaan 8 H (630 M).

 

4.    Safari ya kuelekea Taabuk kwa Mtume (swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na jeshi lake ili kupambana na dola kuu ya wakati huo, Warumi wakati uliokuwa mzito wa joto kali na msimu wa mazao na masafa marefu. Kurudi kwa jeshi hilo ilisibu kuwa ni mwezi wa Ramadhaan 9 H (631 M).

 

5.    Kufunguliwa na kutawaliwa kwa Maghrib al-Awswat (Morocco ya Kati) na Waislam ilitokea tarehe 2 Ramadhaan 82 H (701M).

 

6.    Ufuo wa Pwani wa Andalus (Spain) ulitekwa na jemadari jeshi wa Kiislamu, Twaariq ibn Ziyaad mnamo 28 Ramadhaan 92 H (711 M).

 

7.    Amuriah ilitekwa tarehe 6 Ramadhaan 222 H.

 

8.    Mujaahid Nuur ud Diyn Zinkiy aliwashinda Wakristo wa msalaba na kuurudisha mji Harem mnamo 9 Ramadhaan 559 H.

 

9.    Sultan wa Misri wakati huo wake, Qitz Mahmuud Mudhaffar akiongoza jeshi waliokuwemo wanazuoni, vijana, wazee na hata wanawake, mkewe akiwemo ndani yake walipambana na Matatari ambao walikuwa wanatisha na kuogopewa. Hawa watu walivamia na kuiteka miji mingi katika dola ya Kiislamu pamoja na kumuua Khalifah wa Banu ‘Abbaas, mwaka 1258 M. Baghdad ambao ulikuwa ni mji mkuu wa dola hiyo ulivunjwa kabisa. Kwa hofu waliokuwa nayo Waislam walikuwa na msemo: “Ukisikia Matatari wameshindwa basi usisadiki”. Lakini walitokea waliowashinda watu hao majabari. Sultan Qitz na mujahidina wake walipambana na Matatari katika Vita vya ‘Ayn Jaalut huko Palestina tarehe 25 Ramadhaan 658 H (1260 M) miaka miwili pekee baada ya kuuliwa kwa Khalifa. Qitz alinyanyua hima na hamasa ya mujahidina wake. Chini ya uongozi wake, Waislam walishikanishwa juu ya Imani, umoja, zana za kivita za chuma ili kupambana na adui. Matokeo yake yalikuwa ni ushindi wa wazi kabisa katika wakati wa udhaifu na unyonge. Hata leo tunaweza kupata ushindi na aina hiyo ya uongozi. Kadhiya ya Afghanistan iko hai machoni petu walipoondoa tofauti zao na kupigania kwa sababu ya Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala), Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Aliwasaidia na kuweza kuishinda dola iliyokuwa kuu ya USSR (Urusi).

 

10.           Ndugu zetu huko Afghanistan walipigana na Warusi kwa Ramadhaan 10 mfululizo (1979 – 1988) bila kupumua.

 

11.           Ukinzani na mapigano dhidi ya maadui wa Uislamu bado yanaendelea kwa miongo kadhaa katika nchi kama Palestina, Kashmir, Phillipine, Bosnia, Chechniya na kadhalika.

 

12.           Vita vya Ramadhaan 1973 baina ya majeshi ya Kiarabu na Waisraeli imeonyesha kuwa lau nchi za Mashariki ya Kati zitashikana mikono na kuungana kwa ikhlasi na kupigana dhidi ya adui kwa ajili ya Allaah basi adui atatoka mwenyewe katika eneno hilo.

 

Lakini wakati masharti ya kupata ushindi yalikosekana Waislam walishindwa katika mwezi huo mtukufu wa Ramadhaan. Mojawapo ya kushindwa vibaya sana Waislam ilikuwa ni katika Vita vya Balata Shuhadaa, pale Waislam waliposhindwa na Wakristo katika eneo la milima huko Ufaransa mnamo tarehe 1 Ramadhaan 114 H. Katika enzi zetu hizi mauaji ya Waislam ndani ya Msikiti wa Ibraahimiy huko Khaliil (Hebron), Palestina ni ya kuzingatiwa. Waislam walikuwa wakiswali Swalah yao ya Alfairi mnamo tarehe 15 Ramadhaan 1414 H (25 Februari 1994) pale Mzeyuni mwenye siyasa kali, Dkt. Bharuch Goldstein alipoingia ndani ya Msikiti huo huku nje jeshi la Israeli likimlinda na kufyatua risasi. Kwa dakika chache aliwaua muswalina 30 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 75.

 

 

HITIMISHO

 

Kwetu sisi kutoka katika janga hili la balaa inafaa tuwe na suluhisho, la sivyo shida na matatizo yatazidi. Kwa mtazamo wa haraka ni kuwa mustakabali katika hii dunia ni kwa Uislamu hata wakichukia makafiri, lakini majukumu ni lazima yabebwe na kila mmoja wetu. Kila mmoja wetu anafaa kucheza dauru yake ili kuweza kufikia malengo yetu. Hili ni lazima lichukuliwe kama timu ambapo kila mmoja ana jezi na namba. Je, mimi na wewe tutacheza namba gani katika timu hiyo?

 

Mabadiliko ni lazima yaanze sana kwani kesho kesho haifiki na ngoja ngoja huumiza matumbo. Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Anatueleza:

Hakika Allaah Habadili yaliyoko kwa watu mpaka wabadili wao yaliyomo nafsini mwao” (13: 11). Njia ya sisi kwenda mbele ni kufuatilia muongozo ufuatao:

 

 

1. Mazoezi ya Kimwili: Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Anatueleza kwamba: “Basi waandalieni nguvu kama muwezavyo, na kwa farasi waliofungwa tayari-tayari, ili kuwatishia maadui wa Allaah na maadui zenu, na wengineo ambao hamuwajui, lakini Allaah Anawajua. Na mkitoa chochote katika Njia ya Allaah mtarudishiwa, na wala nyinyi hamtadhulumiwa” (8: 60).

Na Mtume wa Allaah (swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatuambia: “Muumini aliye na nguvu ni bora na anapendwa zaidi na Allaah kuliko Muumini aliye dhaifu” (Muslim). Hata wanawake hawakuachwa nyuma katika mas-ala haya ya kujiweka katika hali ya maandalizi na mazoezi. Wakati mmoja ‘Aaishah (radhiya Allaahu ‘anha) alishindana mbio na Mtume (swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) naye akashinda (Ahmad na Abu Daawuud). Hivyo, ni muhimu sana kwetu kuwa na matayarisho hayo.

 

2. Mazoezi ya Kiroho: Ni muhimu kwa Waislam kujitolea mhanga kwa ajili ya kuzisafisha nyoyo zao kwa kusoma, kujua maana na kuzingatia maamrisho yaliyomo ndani ya Qur-aan pamoja na kushikamana barabara na Sunnah. Ni lazima walime na kupalilia ndani ya nafsi zao hisia ya kutekeleza ‘Ibadah kwa mfano Swalah, Funga, Dhikr na aina nyengine za ‘Ibadah ambazo zitatuleta sisi karibu na Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) za faradhi na za Sunnah. Hii itaitakasa na kuisafisha roho zetu. Jambo hili linatakiwa lipatiwe umuhimu mkubwa kabisa.

 

3. Mazoezi ya Kiakili: Ikiwa ni katika Misikiti au katika vyuo vya masomo Waislam wanatakiwa wajengwe kiakili. Akili zao zinatakiwa zifunguliwe na masikio yao yatolewe taka na uchafu. Hili litawaimarisha na wao kuweza kutathmini mambo yanavyoendelea kwa muono wa Kiislamu. Ni muhimu kuwa na programu na duruus ambazo zitamlenga Muislamu pamoja na changa moto aina zote zinazomkumba katika ulimwengu huu wa utandawazi. Hizi halawaat za taalimu zitawaimarisha Waislam katika dini yao pamoja akili zao. Vitabu tofauti vinaweza kuchaguliwa ili mradi baada ya miaka kama 2 – 3 tunaweza kukaa na kutathmini faida pamoja na kuangalia udhaifu uliopo. Masomo ambayo yanaweza kuwepo ni kama Tajwiyd. Tafsiri ya Qur-aan, Hadiyth, Siyrah, ‘Aqiydah, Fiqhi, mambo yanavyojiri wakati huu, kutazama dini na madhehebu nyengine pamoja na kuangalia zile itikadi na harakati zilizo dhidi pamoja na kuwa na uadui mkubwa na Uislamu, na kadhalika.

 

Wabillahi at-Tawfiyq

 

 

Share