Je, Unampenda Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Ipasavyo Ili Upate Mapenzi ya Allaah?

Je, Unampenda Nabiy  (صلى الله عليه وآله وسلم) Ipasavyo Ili Upate Mapenzi ya Allaah?   

 

Alhidaaya.com

 

 

Hakuna Muislamu asiyekiri kuwa Anamependa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwani hakuna mapenzi yaliyo muhimu kabisa kama mapenzi ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ambaye tunamtegemea na kumhitaji kwa mambo yetu yote.

 

 

Jambo la kukupeleka kupata mapenzi ya Allaah Amelithibitisha Mwenyewe Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika kauli Yake:

         

قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللَّـهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللَّـهُ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ ۗ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ﴿٣١﴾

Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Mkiwa mnampenda Allaah, basi nifuateni mimi, Atakupendeni Allaah na Atakughufurieni dhambi zenu. Na Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu” [Aal-‘Imraan 3: 31].

 

Swali kwa kila Muislamu ni: “Je, unamfuata kikweli Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)?” Kwa maana; kufuata aliyoyaamrisha na kuachana na aliyoyakataza?

 

Jibu la Swali hili ni moja tu hakuna la pili yake. Nalo ni: Kumfuata kikweli kwa kutii aliyoyaleta (aliyotuamirisha) na kuyaacha aliyotukataza; yakiwemo mafundisho yake yote na nyendo za Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) kama alivyoamuru pale alipotueleza kwamba kutatokea ikhtilaaf nyingi kama zinavyodhihirika zama hizi:

 

أُوصِيكُمْ بِتَقْوى اللَّه، وَالسَّمْعِ وَالطَّاعَةِ وإِنْ تَأَمَّر عَلَيْكُمْ عَبْدٌ حبشيٌ، وَأَنَّهُ مَنْ يَعِشْ مِنْكُمْ فَسَيرى اخْتِلافاً كثِيرا, فَعَلَيْكُمْ بسُنَّتي وَسُنَّةِ الْخُلُفَاءِ الرَّاشِدِينَ الْمَهْدِيِّينَ، عضُّوا عَلَيْهَا بالنَّواجِذِ، وإِيَّاكُمْ ومُحْدثَاتِ الأُمُورِ فَإِنَّ كُلَّ بِدْعَةٍ ضلالَةٌ   رواه أبو داود ، والترمذِي وقال حديث حسن صحيح

((Nakuusieni kumcha Allaah, usikivu na twaa hata ikiwa kiongozi wenu (Au atakayekuamrisheni) ni Mtumwa Mhabashi. Mtakaoishi miongoni mwenu mtaona ikhtilaaf nyingi. Kwa hiyo shikamaneni na Sunnah zangu na Sunnah za Makhalifa waliongoka baada yangu. Ziumeni kwa magego (zikamateni kwa nguvu wala msiziache). Na tahadharini na mambo ya uzushi kwani kila bid'ah ni upotofu)) [Abu Daawuwd, At-Tirmidhiy kasema Hadiyth Hasan Swahiyh].

 

Faida nyingine inayopatikana pindi utakapothibitisha kumfuta Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama ilivyotajwa katika Aayah hiyo tukufu ni kughufuriwa madhambi.

 

Hakika ni faida mbili kuu anazozihitaji Muislamu kila wakati katika maisha yake.

 

Na katika makemeo na makatazo yake ni kuacha mambo yote ya uzushi; nayo ni kama haya tuyaonayo leo ya sherehe za Mawlid ambayo yalianzishwa na Mashia maadui wakubwa wa hii Dini. Muislamu mzuri ni yule anayemfuata Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumtii na si mwenye kufuata Mashia na kuwaona ni bora wa kuwaundia nidhamu na mfumo wa mambo ya Dini yao. Huku ni kumdharau Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumuona pia yeye kafanya khiyana ya kutowaletea au kuwafundisha haya ambayo wamefundishwa na Mashia na hali amekiri kuwa keshakamilisha ujumbe aliotumwa na Allaah (‘Azza wa Jalla) pale aliposema:

 

 والذي نفسي بيده ما تركت شيئا يقربكم من الجنة ويباعدكم عن النار إلا أمرتكم به، وما تركت شيئا يقربكم من النار، ويباعدكم عن الجنة إلا نهيتكم عنه      

 ((Naapa Kwa Yule Ambaye nafsi yangu iko katika mikono Yake, sikuacha jambo la kukukurubisheni na Jannah na la kukuwekeni mbali na moto ila nimekwisha kukuamrisheni nalo. Wala sikuacha jambo la kukukurubisheni na moto na kukuwekeni mbali na Jannah ila nimekwisha kukukatazeni nalo)) [Silsilatul-Ahaadiyth Swahiyhah]

 

Hao Mashia  ni maadui wakubwa wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwani wanamtukania Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wake zake, wanamtukania vipenzi vyake, wanamtukania ummah wake mzima. Huku si kumpenda Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) bali ni kumuasi na kuwapenda maadui wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na hiili ni dhahiri kwa kuonekana mashirikiano yao ya wazi na Mashia na namna wanavyoungana pamoja katika kusherehekea hizi sherehe za uzushi na kuungana katika miunganiko mingine ya uzushi kama ya mwaka mpya na Husayniyyaat (Hussein Day) katika mwezi wa Al-Muharram ambamo ndani yake kuna maombolezo ya uzushi na uongo na vilevile kutukanwa ndani yake Swahaba (Radhiwya Allaahu ‘anhum) watukufu. Bila shaka huku kunaonyesha dalili za wazi kuwa wanaofuata mwendo huo si wapenzi wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na si wapenzi wa Allaah. Kwani kwa kumuasi na kumkhalifu mafunzo yake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), hapana shaka wamemkhalifu na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), na kwa hali hiyo, kama Aayah juu inavyofahamisha, hawatopendwa na Allaah.

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atujaalie ni wenye kumpenda Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wetu mapenzi ya kweli kweli ya dhati kwa kufuata maamrisho yake na Sunnah zake zote na kuwa mbali na bid’ah na kila aina ya uzushi na njia zozote zitakazotupeleka kumkhalifu yeye.

 

 

 

 

Share