008 - Al-Anfaal

 

الأَنْفَال

 

008-Al-Anfaal

 

 008-Al-Anfaal: Utangulizi Wa Suwrah

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيم

 

 

يَسْأَلُونَكَ عَنِ الْأَنفَالِ ۖ قُلِ الْأَنفَالُ لِلَّـهِ وَالرَّسُولِ ۖ فَاتَّقُوا اللَّـهَ وَأَصْلِحُوا ذَاتَ بَيْنِكُمْ ۖ وَأَطِيعُوا اللَّـهَ وَرَسُولَهُ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ﴿١﴾

1. Wanakuuliza (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kuhusu Anfaal (mali inayopatikana katika vita). Sema: Mali inayopatikana katika vita ni ya Allaah na Rasuli. Basi mcheni Allaah na suluhisheni yaliyo baina yenu. Na mtiini Allaah na Rasuli Wake mkiwa ni Waumini.

 

 

 

 

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ اللَّـهُ وَجِلَتْ قُلُوبُهُمْ وَإِذَا تُلِيَتْ عَلَيْهِمْ آيَاتُهُ زَادَتْهُمْ إِيمَانًا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ﴿٢﴾

2. Hakika Waumini ni wale ambao Anapotajwa Allaah, nyoyo zao zinajaa khofu na wanaposomewa Aayaat Zake huwazidishia imaan, na kwa Rabb wao wanatawakali.

 

 

 

الَّذِينَ يُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ﴿٣﴾

3. Ambao wanasimamisha Swalaah na katika yale Tuliyowaruzuku hutoa.

 

 

 

 

أُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُؤْمِنُونَ حَقًّا ۚ لَّهُمْ دَرَجَاتٌ عِندَ رَبِّهِمْ وَمَغْفِرَةٌ وَرِزْقٌ كَرِيمٌ﴿٤﴾

4. Hao ndio Waumini wa kweli!  Wana daraja (za Jannah) kwa Rabb wao na maghfira na riziki karimu.

 

 

 

 

كَمَا أَخْرَجَكَ رَبُّكَ مِن بَيْتِكَ بِالْحَقِّ وَإِنَّ فَرِيقًا مِّنَ الْمُؤْمِنِينَ لَكَارِهُونَ﴿٥﴾

5. Kama Alivyokutoa Rabb wako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kutoka nyumbani kwako kwa haki (kwa ajili ya Vita vya Badr[1]) na hakika kundi miongoni mwa Waumini linachukia.

 

 

 

 

 

يُجَادِلُونَكَ فِي الْحَقِّ بَعْدَ مَا تَبَيَّنَ كَأَنَّمَا يُسَاقُونَ إِلَى الْمَوْتِ وَهُمْ يَنظُرُونَ﴿٦﴾

6. Wanajadiliana nawe katika haki baada ya kubainika, kama kwamba wanasukumwa kwenda katika mauti nao huku wanatazama.

 

 

 

 

وَإِذْ يَعِدُكُمُ اللَّـهُ إِحْدَى الطَّائِفَتَيْنِ أَنَّهَا لَكُمْ وَتَوَدُّونَ أَنَّ غَيْرَ ذَاتِ الشَّوْكَةِ تَكُونُ لَكُمْ وَيُرِيدُ اللَّـهُ أَن يُحِقَّ الْحَقَّ بِكَلِمَاتِهِ وَيَقْطَعَ دَابِرَ الْكَافِرِينَ﴿٧﴾

7. Na pale Allaah Alipokuahidini moja kati ya makundi mawili (la msafara au la jeshi) kwamba ni lenu, nanyi mkatamani kwamba lisilo na silaha liwe lenu, na Allaah Anataka Athibitishe haki kwa Maneno Yake, na Akate mizizi ya makafiri.

 

 

 

 

لِيُحِقَّ الْحَقَّ وَيُبْطِلَ الْبَاطِلَ وَلَوْ كَرِهَ الْمُجْرِمُونَ﴿٨﴾

8. Ili Athibitishe haki na Abatilishe ubatilifu japokuwa wahalifu wamekirihika.

 

 

 

 

 

إِذْ تَسْتَغِيثُونَ رَبَّكُمْ فَاسْتَجَابَ لَكُمْ أَنِّي مُمِدُّكُم بِأَلْفٍ مِّنَ الْمَلَائِكَةِ مُرْدِفِينَ﴿٩﴾

9. Na pale mlipomuomba uokovu[2] Rabb wenu Naye Akakuitikieni kuwa: Hakika Mimi Nitakusaidieni kwa Malaika elfu wafuatanao mfululizo.

 

 

 

 

وَمَا جَعَلَهُ اللَّـهُ إِلَّا بُشْرَىٰ وَلِتَطْمَئِنَّ بِهِ قُلُوبُكُمْ ۚ وَمَا النَّصْرُ إِلَّا مِنْ عِندِ اللَّـهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ﴿١٠﴾

10. Na Allaah Hakujaalia haya isipokuwa ni bishara na ili zitumainike nyoyo zenu kwayo. Na hakuna nusura isipokuwa kutoka kwa Allaah. Hakika Allaah Ni Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote.

 

 

 

 

إِذْ يُغَشِّيكُمُ النُّعَاسَ أَمَنَةً مِّنْهُ وَيُنَزِّلُ عَلَيْكُم مِّنَ السَّمَاءِ مَاءً لِّيُطَهِّرَكُم بِهِ وَيُذْهِبَ عَنكُمْ رِجْزَ الشَّيْطَانِ وَلِيَرْبِطَ عَلَىٰ قُلُوبِكُمْ وَيُثَبِّتَ بِهِ الْأَقْدَامَ﴿١١﴾

11. Pindi Alipokufunikeni kwa usingizi kuwa ni amani kutoka Kwake, na Akakuteremshieni maji kutoka mbinguni, ili Akutwaharisheni kwayo, na Akuondosheeni wasiwasi na rai ovu za shaytwaan, na ili Atie nguvu nyoyo zenu, na Aisimamishe kwayo imara miguu.

 

 

 

 

 

إِذْ يُوحِي رَبُّكَ إِلَى الْمَلَائِكَةِ أَنِّي مَعَكُمْ فَثَبِّتُوا الَّذِينَ آمَنُوا ۚ سَأُلْقِي فِي قُلُوبِ الَّذِينَ كَفَرُوا الرُّعْبَ فَاضْرِبُوا فَوْقَ الْأَعْنَاقِ وَاضْرِبُوا مِنْهُمْ كُلَّ بَنَانٍ﴿١٢﴾

12. Pindi Rabb wako Alipowatia ilhamu Malaika (kuwaambia): Hakika Mimi Niko pamoja nanyi, basi wathibitisheni wale walioamini. Nitatia kizaazaa katika nyoyo za waliokufuru. Basi wapigeni juu ya shingo na wapigeni kila kiungo (au ncha za vidole).

 

 

 

 

 

ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ شَاقُّوا اللَّـهَ وَرَسُولَهُ ۚ وَمَن يُشَاقِقِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَإِنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ﴿١٣﴾

13. Hivyo kwa kuwa wao wamempinga Allaah na Rasuli Wake. Na yeyote ampingae Allaah na Rasuli Wake basi hakika Allaah Ni Mkali wa Kuakibu.[3]

 

 

 

 

 

ذَٰلِكُمْ فَذُوقُوهُ وَأَنَّ لِلْكَافِرِينَ عَذَابَ النَّارِ﴿١٤﴾

14. Hayo yaliyokupateni, basi yaonjeni (nyie makafiri). Na jueni (enyi Waumini) kwamba makafiri wana adhabu ya moto.

 

 

 

 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا لَقِيتُمُ الَّذِينَ كَفَرُوا زَحْفًا فَلَا تُوَلُّوهُمُ الْأَدْبَارَ﴿١٥﴾

15. Enyi walioamini! Mtapokutana na wale waliokufuru vitani, basi msiwageuzie migongo (kukimbia).[4]

 

 

 

 

وَمَن يُوَلِّهِمْ يَوْمَئِذٍ دُبُرَهُ إِلَّا مُتَحَرِّفًا لِّقِتَالٍ أَوْ مُتَحَيِّزًا إِلَىٰ فِئَةٍ فَقَدْ بَاءَ بِغَضَبٍ مِّنَ اللَّـهِ وَمَأْوَاهُ جَهَنَّمُ ۖ وَبِئْسَ الْمَصِيرُ﴿١٦﴾

16. Na yeyote atakayewageuzia mgongo wake siku hiyo - isipokuwa akigeuka kama mbinu ya kupigana au kujiunga na kikosi kingine - basi amestahiki Ghadhabu ya Allaah, na makazi yake ni Jahannam, na ni pabaya palioje mahali pa kuishia.[5]

 

 

 

 

 

فَلَمْ تَقْتُلُوهُمْ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ قَتَلَهُمْ ۚ وَمَا رَمَيْتَ إِذْ رَمَيْتَ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ رَمَىٰ ۚ وَلِيُبْلِيَ الْمُؤْمِنِينَ مِنْهُ بَلَاءً حَسَنًا ۚ إِنَّ اللَّـهَ سَمِيعٌ عَلِيمٌ﴿١٧﴾

17. Hamkuwaua nyinyi, lakini Allaah Ndiye Aliyewaua. Na wala hukurusha (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم  mchanga) pale uliporusha lakini Allaah Ndiye Aliyerusha, na ili Awajaribu Waumini jaribio zuri kutoka Kwake. Hakika Allaah Ni Mwenye Kusikia yote, Mjuzi wa yote.

 

 

 

 

 

ذَٰلِكُمْ وَأَنَّ اللَّـهَ مُوهِنُ كَيْدِ الْكَافِرِينَ﴿١٨﴾

18. Ndio hivyo! Na hakika Allaah Ni Mwenye Kudhoofisha mbinu za makafiri.

 

 

 

 

 

إِن تَسْتَفْتِحُوا فَقَدْ جَاءَكُمُ الْفَتْحُ ۖ وَإِن تَنتَهُوا فَهُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ ۖ وَإِن تَعُودُوا نَعُدْ وَلَن تُغْنِيَ عَنكُمْ فِئَتُكُمْ شَيْئًا وَلَوْ كَثُرَتْ وَأَنَّ اللَّـهَ مَعَ الْمُؤْمِنِينَ﴿١٩﴾

19. Mkitafuta hukmu (enyi makafiri), basi imeshakujieni hukmu. Na mkikoma (uhalifu) basi hivyo ni kheri kwenu. Na mkirudia (kuhujumu) Nasi Tutarudia, na wala kundi lenu halitokufaeni kitu chochote japo likikithiri. Na Hakika Allaah Yu Pamoja na Waumini.

 

 

 

 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَلَا تَوَلَّوْا عَنْهُ وَأَنتُمْ تَسْمَعُونَ﴿٢٠﴾

20. Enyi walioamini! Mtiini Allaah na Rasuli Wake, na wala msijiepushe nazo (amri za Rasuli) na hali nyinyi mnasikia. 

 

 

 

 

 

وَلَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ قَالُوا سَمِعْنَا وَهُمْ لَا يَسْمَعُونَ﴿٢١﴾

21. Na wala msiwe kama wale waliosema: Tumesikia na hali wao hawasikii.

 

 

 

 

 

إِنَّ شَرَّ الدَّوَابِّ عِندَ اللَّـهِ الصُّمُّ الْبُكْمُ الَّذِينَ لَا يَعْقِلُونَ﴿٢٢﴾

22. Hakika viumbe viovu kabisa mbele ya Allaah ni viziwi, mabubu ambao hawatumii akili.

 

 

 

 

 

وَلَوْ عَلِمَ اللَّـهُ فِيهِمْ خَيْرًا لَّأَسْمَعَهُمْ ۖ وَلَوْ أَسْمَعَهُمْ لَتَوَلَّوا وَّهُم مُّعْرِضُونَ﴿٢٣﴾

23. Na kama Allaah Angelijua kuwa wana kheri yoyote ile, basi Angeliwasikilizisha. Na kama Angeliwasikilizisha, wangeligeuka nao huku wakipuuza.

 

 

 

 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اسْتَجِيبُوا لِلَّـهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُمْ لِمَا يُحْيِيكُمْ ۖ وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ يَحُولُ بَيْنَ الْمَرْءِ وَقَلْبِهِ وَأَنَّهُ إِلَيْهِ تُحْشَرُونَ﴿٢٤﴾

24. Enyi walioamini! Muitikieni Allaah na Rasuli Anapokuiteni kwenye yale yenye kukupeni uhai mwema (wa dunia na Aakhirah). na jueni kwamba Allaah Anaingilia kati baina ya mtu na moyo wake, na kwamba Kwake mtakusanywa.

 

 

 

 

 

وَاتَّقُوا فِتْنَةً لَّا تُصِيبَنَّ الَّذِينَ ظَلَمُوا مِنكُمْ خَاصَّةً ۖ وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ﴿٢٥﴾

25. Na ogopeni mitihani ambayo haitowasibu pekee wale waliodhulumu miongoni mwenu. Na jueni kwamba Allaah Ni Mkali wa Kuakibu.

 

 

 

 

 

 

 

وَاذْكُرُوا إِذْ أَنتُمْ قَلِيلٌ مُّسْتَضْعَفُونَ فِي الْأَرْضِ تَخَافُونَ أَن يَتَخَطَّفَكُمُ النَّاسُ فَآوَاكُمْ وَأَيَّدَكُم بِنَصْرِهِ وَرَزَقَكُم مِّنَ الطَّيِّبَاتِ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ﴿٢٦﴾

26. Na kumbukeni pale mlipokuwa wachache, mkikandamizwa ardhini, mnakhofu watu wasikunyakueni. (Allaah) Akakupeni makazi na Akakutieni nguvu kwa Nusra Yake, na Akakuruzukuni katika vizuri mpate kushukuru.

 

 

 

 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَخُونُوا اللَّـهَ وَالرَّسُولَ وَتَخُونُوا أَمَانَاتِكُمْ وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ﴿٢٧﴾

27. Enyi walioamini! Msimfanyie khiyana Allaah na Rasuli na wala msikhini amana zenu na hali nyinyi mnajua. 

 

 

 

 

 

وَاعْلَمُوا أَنَّمَا أَمْوَالُكُمْ وَأَوْلَادُكُمْ فِتْنَةٌ وَأَنَّ اللَّـهَ عِندَهُ أَجْرٌ عَظِيمٌ﴿٢٨﴾

28.  Na jueni kwamba mali zenu na watoto wenu ni jaribio, na kwamba kwa Allaah uko ujira mkubwa mno. 

 

 

 

 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِن تَتَّقُوا اللَّـهَ يَجْعَل لَّكُمْ فُرْقَانًا وَيُكَفِّرْ عَنكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ۗ وَاللَّـهُ ذُو الْفَضْلِ الْعَظِيمِ﴿٢٩﴾

29. Enyi walioamini! Mkimcha Allaah Atakupeni upambanuzi na Atakufutieni maovu yenu, na Atakughufurieni. Na Allaah Ni Mwenye Fadhila kubwa mno.

 

 

 

 

 

وَإِذْ يَمْكُرُ بِكَ الَّذِينَ كَفَرُوا لِيُثْبِتُوكَ أَوْ يَقْتُلُوكَ أَوْ يُخْرِجُوكَ ۚ وَيَمْكُرُونَ وَيَمْكُرُ اللَّـهُ ۖ وَاللَّـهُ خَيْرُ الْمَاكِرِينَ﴿٣٠﴾

30. Na pindi (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) walipokupangia makri wale waliokufuru ili wakufunge, au wakuue, au wakutoe (Makkah). Na wanapanga makri, na Allaah Anapanga makri[6] (kupindua njama zao), na Allaah Ni Mbora wa kupanga makri kuliko wote.

 

 

 

 

 

وَإِذَا تُتْلَىٰ عَلَيْهِمْ آيَاتُنَا قَالُوا قَدْ سَمِعْنَا لَوْ نَشَاءُ لَقُلْنَا مِثْلَ هَـٰذَا ۙ إِنْ هَـٰذَا إِلَّا أَسَاطِيرُ الْأَوَّلِينَ﴿٣١﴾

31. Na wanaposomewa Aayaat Zetu, husema: Tumekwishasikia. Lau tungelitaka tungelisema kama haya. Haya si chochote isipokuwa ni hekaya za watu wa kale.

 

 

 

 

 

وَإِذْ قَالُوا اللَّـهُمَّ إِن كَانَ هَـٰذَا هُوَ الْحَقَّ مِنْ عِندِكَ فَأَمْطِرْ عَلَيْنَا حِجَارَةً مِّنَ السَّمَاءِ أَوِ ائْتِنَا بِعَذَابٍ أَلِيمٍ﴿٣٢﴾

32. Na pindi waliposema: Ee Allaah! Kama haya ni haki kutoka Kwako, basi Tunyeshee mvua ya mawe kutoka mbinguni au Tuletee adhabu iumizayo.[7]

 

 

 

 

 

وَمَا كَانَ اللَّـهُ لِيُعَذِّبَهُمْ وَأَنتَ فِيهِمْ ۚ وَمَا كَانَ اللَّـهُ مُعَذِّبَهُمْ وَهُمْ يَسْتَغْفِرُونَ﴿٣٣﴾

33. Na Allaah Hakuwa wa kuwaadhibu na hali wewe (Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) uko nao. Na Allaah Hakuwa wa kuwaadhibu hali wao wanaomba maghfirah.[8]

 

 

 

 

 

 

وَمَا لَهُمْ أَلَّا يُعَذِّبَهُمُ اللَّـهُ وَهُمْ يَصُدُّونَ عَنِ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ وَمَا كَانُوا أَوْلِيَاءَهُ ۚ إِنْ أَوْلِيَاؤُهُ إِلَّا الْمُتَّقُونَ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لَا يَعْلَمُونَ﴿٣٤﴾

34. Na wana nini hata Allaah Asiwaadhibu na hali wao wanazuia (watu) na Al-Masjidil-Haraam, na hawakuwa walinzi wake (Msikiti huo). Hawakuwa Rafiki Wake walinzi isipokuwa wenye taqwa, lakini wengi wao hawajui.

 

 

 

 

 

وَمَا كَانَ صَلَاتُهُمْ عِندَ الْبَيْتِ إِلَّا مُكَاءً وَتَصْدِيَةً ۚ فَذُوقُوا الْعَذَابَ بِمَا كُنتُمْ تَكْفُرُونَ﴿٣٥﴾

35. Na haikuwa Swalaah zao (makafiri) kwenye Nyumba (Al-Ka’bah) isipokuwa ni miruzi na kupiga makofi. Basi onjeni adhabu kwa sababu ya kufru yenu.  

 

 

 

 

 

إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا يُنفِقُونَ أَمْوَالَهُمْ لِيَصُدُّوا عَن سَبِيلِ اللَّـهِ ۚ فَسَيُنفِقُونَهَا ثُمَّ تَكُونُ عَلَيْهِمْ حَسْرَةً ثُمَّ يُغْلَبُونَ ۗ وَالَّذِينَ كَفَرُوا إِلَىٰ جَهَنَّمَ يُحْشَرُونَ﴿٣٦﴾

36. Hakika wale waliokufuru wanatoa mali zao ili wazuie Njia ya Allaah. Basi watazitoa, kisha zitakuwa ni majuto juu yao, kisha watashindwa. Na wale waliokufuru watakusanywa kwenye Jahannam.

 

 

 

 

 

لِيَمِيزَ اللَّـهُ الْخَبِيثَ مِنَ الطَّيِّبِ وَيَجْعَلَ الْخَبِيثَ بَعْضَهُ عَلَىٰ بَعْضٍ فَيَرْكُمَهُ جَمِيعًا فَيَجْعَلَهُ فِي جَهَنَّمَ ۚ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ﴿٣٧﴾

37. Ili Allaah Apambanue waovu na wema, kisha Awaweke waovu juu ya waovu wengine, halafu Awarundike pamoja Awatie katika Jahannam. Hao ndio waliokhasirika.

 

 

 

 

قُل لِّلَّذِينَ كَفَرُوا إِن يَنتَهُوا يُغْفَرْ لَهُم مَّا قَدْ سَلَفَ وَإِن يَعُودُوا فَقَدْ مَضَتْ سُنَّتُ الْأَوَّلِينَ﴿٣٨﴾

38. Waambie waliokufuru kwamba wakikoma wataghufuriwa yaliyopita, lakini wakirudia, basi imekwishapita desturi[9] (ya Allaah) ya watu wa awali.

 

 

 

 

 

 

وَقَاتِلُوهُمْ حَتَّىٰ لَا تَكُونَ فِتْنَةٌ وَيَكُونَ الدِّينُ كُلُّهُ لِلَّـهِ ۚ فَإِنِ انتَهَوْا فَإِنَّ اللَّـهَ بِمَا يَعْمَلُونَ بَصِيرٌ﴿٣٩﴾

39. Na piganeni nao mpaka kusiweko fitnah, na Dini yote iwe kwa ajili ya Allaah. Na wakikoma, basi hakika Allaah kwa wanayoyatenda Ni Mwenye Kuona.

 

 

 

 

 

 

وَإِن تَوَلَّوْا فَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ مَوْلَاكُمْ ۚ نِعْمَ الْمَوْلَىٰ وَنِعْمَ النَّصِيرُ﴿٤٠﴾

40. Na wakikengeuka, basi jueni kwamba Allaah ni Mawlaa[10] wenu; Mawlaa Mzuri Alioje, na Mnusuruji Mzuri Alioje!

 

 

 

 

 

 

وَاعْلَمُوا أَنَّمَا غَنِمْتُم مِّن شَيْءٍ فَأَنَّ لِلَّـهِ خُمُسَهُ وَلِلرَّسُولِ وَلِذِي الْقُرْبَىٰ وَالْيَتَامَىٰ وَالْمَسَاكِينِ وَابْنِ السَّبِيلِ إِن كُنتُمْ آمَنتُم بِاللَّـهِ وَمَا أَنزَلْنَا عَلَىٰ عَبْدِنَا يَوْمَ الْفُرْقَانِ يَوْمَ الْتَقَى الْجَمْعَانِ ۗ وَاللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ﴿٤١﴾

41. Na jueni ya kwamba ghanima[11] yoyote mnayoipata (vitani), basi humusi yake ni ya Allaah na Rasuli, na jamaa wa karibu, na mayatima, na maskini, na wasafiri (walioharibikiwa), ikiwa nyinyi mumemwamini Allaah na yale Tuliyoyateremsha kwa mja Wetu siku ya upambanuzi; siku yalipokutana makundi mawili (vita vya Badr) na Allaah juu ya kila kitu Ni Mweza.

 

 

 

 

إِذْ أَنتُم بِالْعُدْوَةِ الدُّنْيَا وَهُم بِالْعُدْوَةِ الْقُصْوَىٰ وَالرَّكْبُ أَسْفَلَ مِنكُمْ ۚ وَلَوْ تَوَاعَدتُّمْ لَاخْتَلَفْتُمْ فِي الْمِيعَادِ ۙ وَلَـٰكِن لِّيَقْضِيَ اللَّـهُ أَمْرًا كَانَ مَفْعُولًا لِّيَهْلِكَ مَنْ هَلَكَ عَن بَيِّنَةٍ وَيَحْيَىٰ مَنْ حَيَّ عَن بَيِّنَةٍ ۗ وَإِنَّ اللَّـهَ لَسَمِيعٌ عَلِيمٌ﴿٤٢﴾

42. Pale nyinyi mlipokuwa kando ya bonde la karibu, na wao (Makafiri) walipokuwa kando ya bonde la mbali, na msafara (wa mali zao) ulikuwa uko chini yenu. Na lau mngeliahidiana basi mngelikhitalifiana katika miadi hiyo, lakini ili Allaah Akidhie jambo lililokuwa lazima litendwe ili ahiliki (kwa ukafiri) yule wa kuhiliki kwa hoja bayana na ahuike (kwa imaan) mwenye kuhuika kwa hoja bayana. Na kwamba Allaah bila shaka Ni Mwenye Kusikia yote, Mjuzi wa yote.

 

 

 

 

 

إِذْ يُرِيكَهُمُ اللَّـهُ فِي مَنَامِكَ قَلِيلًا ۖ وَلَوْ أَرَاكَهُمْ كَثِيرًا لَّفَشِلْتُمْ وَلَتَنَازَعْتُمْ فِي الْأَمْرِ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ سَلَّمَ ۗ إِنَّهُ عَلِيمٌ بِذَاتِ الصُّدُورِ﴿٤٣﴾

43. Pale Allaah Alipokuonyesha usingizini mwako kwamba wao ni wachache. Na lau Angelikuonyesha kuwa wao ni wengi, basi mngelivunjikwa moyo, na mngelizozana katika jambo hilo (la kupigana), lakini Allaah Amesalimisha (hayo). Hakika Yeye Ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani.

 

 

 

 

 

وَإِذْ يُرِيكُمُوهُمْ إِذِ الْتَقَيْتُمْ فِي أَعْيُنِكُمْ قَلِيلًا وَيُقَلِّلُكُمْ فِي أَعْيُنِهِمْ لِيَقْضِيَ اللَّـهُ أَمْرًا كَانَ مَفْعُولًا ۗ وَإِلَى اللَّـهِ تُرْجَعُ الْأُمُورُ﴿٤٤﴾

44. Na pindi (Allaah) Alipokuonyesheni machoni mwenu, pale mlipokutana, kuwa wao ni wachache na Akakufanyeni nyinyi kuwa wachache machoni mwao ili Allaah Akidhie jambo lililokuwa lazima litendwe. Na kwa Allaah Pekee hurejeshwa mambo yote.

 

 

 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا لَقِيتُمْ فِئَةً فَاثْبُتُوا وَاذْكُرُوا اللَّـهَ كَثِيرًا لَّعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ﴿٤٥﴾

45. Enyi walioamini! Mtapokutana na kikosi (cha makafiri), basi simameni imara, na mdhukuruni Allaah kwa wingi ili mpate kufaulu.

 

 

 

 

 

وَأَطِيعُوا اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَلَا تَنَازَعُوا فَتَفْشَلُوا وَتَذْهَبَ رِيحُكُمْ ۖ وَاصْبِرُوا ۚ إِنَّ اللَّـهَ مَعَ الصَّابِرِينَ﴿٤٦﴾

46. Na mtiini Allaah na Rasuli Wake, na wala msizozane, mtavunjikwa moyo, na nguvu zenu zitatoweka, na subirini. Hakika Allaah Yu Pamoja na wanaosubiri.

 

 

 

 

 

 

وَلَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ خَرَجُوا مِن دِيَارِهِم بَطَرًا وَرِئَاءَ النَّاسِ وَيَصُدُّونَ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ ۚ وَاللَّـهُ بِمَا يَعْمَلُونَ مُحِيطٌ﴿٤٧﴾

47. Na wala msiwe kama wale waliotoka majumbani mwao kwa majivuno na riyaa-a[12] (kujionyesha) kwa watu, na wanazuia Njia ya Allaah. Na Allaah Ni Mwenye Kuyazunguka yote wanayoyatenda.

 

 

 

 

 

وَإِذْ زَيَّنَ لَهُمُ الشَّيْطَانُ أَعْمَالَهُمْ وَقَالَ لَا غَالِبَ لَكُمُ الْيَوْمَ مِنَ النَّاسِ وَإِنِّي جَارٌ لَّكُمْ ۖ فَلَمَّا تَرَاءَتِ الْفِئَتَانِ نَكَصَ عَلَىٰ عَقِبَيْهِ وَقَالَ إِنِّي بَرِيءٌ مِّنكُمْ إِنِّي أَرَىٰ مَا لَا تَرَوْنَ إِنِّي أَخَافُ اللَّـهَ ۚ وَاللَّـهُ شَدِيدُ الْعِقَابِ﴿٤٨﴾

48. Na pindi shaytwaan alipowapambia amali zao na akasema: Hakuna watu wa kukushindeni leo, na mimi ni mlinzi wenu. Vilipoonana vikosi viwili, (shaytwaan) alirejea nyuma akigeuka[13] na kusema: Hakika mimi nimejitoa dhima nanyi (sihusiki), hakika mimi naona msiyoyaona, hakika mimi namkhofu Allaah. Na Allaah Ni Mkali wa Kuakibu.

 

 

 

 

 

إِذْ يَقُولُ الْمُنَافِقُونَ وَالَّذِينَ فِي قُلُوبِهِم مَّرَضٌ غَرَّ هَـٰؤُلَاءِ دِينُهُمْ ۗ وَمَن يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ فَإِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ﴿٤٩﴾

49. Na waliposema wanafiki na wale walio na maradhi katika nyoyo zao[14]: Dini yao (hawa Waislamu) imewaghuri. Na anayetawakali kwa Allaah (atashinda tu kwani), hakika Allaah Ni Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote.

 

 

 

 

وَلَوْ تَرَىٰ إِذْ يَتَوَفَّى الَّذِينَ كَفَرُوا ۙ الْمَلَائِكَةُ يَضْرِبُونَ وُجُوهَهُمْ وَأَدْبَارَهُمْ وَذُوقُوا عَذَابَ الْحَرِيقِ﴿٥٠﴾

50. Na lau ungeliona pale Malaika wanapowafisha wale waliokufuru, wanawapiga nyuso zao na migongo yao na (wanawaambia): Onjeni adhabu iunguzayo!

 

 

 

 

 

ذَٰلِكَ بِمَا قَدَّمَتْ أَيْدِيكُمْ وَأَنَّ اللَّـهَ لَيْسَ بِظَلَّامٍ لِّلْعَبِيدِ ﴿٥١﴾

51. Hayo ni kwa yale (maovu) yaliyotangulizwa na mikono yenu, na hakika Allaah Si Mwenye Kudhulumu waja.

 

 

 

 

 

 

كَدَأْبِ آلِ فِرْعَوْنَ ۙ وَالَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ ۚ كَفَرُوا بِآيَاتِ اللَّـهِ فَأَخَذَهُمُ اللَّـهُ بِذُنُوبِهِمْ ۗ إِنَّ اللَّـهَ قَوِيٌّ شَدِيدُ الْعِقَابِ﴿٥٢﴾

52. Ni kama mwenendo wa watu wa Firawni na wale wa kabla yao. Walizikufuru Aayaat (Ishara, Dalili, Hoja) za Allaah. Basi Allaah Akawachukua kwa sababu ya madhambi yao. Hakika Allaah Ni Mwenye nguvu zote, Mkali wa Kuakibu.

 

 

 

 

 

ذَٰلِكَ بِأَنَّ اللَّـهَ لَمْ يَكُ مُغَيِّرًا نِّعْمَةً أَنْعَمَهَا عَلَىٰ قَوْمٍ حَتَّىٰ يُغَيِّرُوا مَا بِأَنفُسِهِمْ ۙ وَأَنَّ اللَّـهَ سَمِيعٌ عَلِيمٌ﴿٥٣﴾

53. Hayo ni kwa kuwa Allaah Hakuwa Mwenye Kubadilisha neema yoyote Aliyoineemesha kwa watu mpaka wao wabadilishe yaliyomo ndani ya nafsi zao. Na hakika Allaah Ni Mwenye Kusikia yote, Mjuzi wa yote.

 

 

 

 

 

كَدَأْبِ آلِ فِرْعَوْنَ ۙ وَالَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ ۚ كَذَّبُوا بِآيَاتِ رَبِّهِمْ فَأَهْلَكْنَاهُم بِذُنُوبِهِمْ وَأَغْرَقْنَا آلَ فِرْعَوْنَ ۚ وَكُلٌّ كَانُوا ظَالِمِينَ﴿٥٤﴾

54. Ni kama mwenendo wa watu wa Firawni na wale wa kabla yao. Walikadhibisha Aayaat (Ishara, Dalili, Hoja) za Rabb wao, Tukawaangamiza kwa sababu ya madhambi yao, na Tukawagharikisha watu wa Firawni, na wote walikuwa madhalimu.

 

 

 

 

 

إِنَّ شَرَّ الدَّوَابِّ عِندَ اللَّـهِ الَّذِينَ كَفَرُوا فَهُمْ لَا يُؤْمِنُونَ﴿٥٥﴾

55. Hakika viumbe viovu kabisa mbele ya Allaah ni wale waliokufuru nao hawaamini.

 

 

 

 

 

الَّذِينَ عَاهَدتَّ مِنْهُمْ ثُمَّ يَنقُضُونَ عَهْدَهُمْ فِي كُلِّ مَرَّةٍ وَهُمْ لَا يَتَّقُونَ﴿٥٦﴾

56. Ambao umepeana nao ahadi, kisha wanavunja ahadi yao kila mara, na wala hawamwogopi na kumstahi Allaah.

 

 

 

 

 

فَإِمَّا تَثْقَفَنَّهُمْ فِي الْحَرْبِ فَشَرِّدْ بِهِم مَّنْ خَلْفَهُمْ لَعَلَّهُمْ يَذَّكَّرُونَ﴿٥٧﴾

 

57. Basi mkiwashinda vitani (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم), waadhibu vikali ili wakimbie mbali walio nyuma yao wapate kuwaidhika.

 

 

 

 

 

 

وَإِمَّا تَخَافَنَّ مِن قَوْمٍ خِيَانَةً فَانبِذْ إِلَيْهِمْ عَلَىٰ سَوَاءٍ ۚ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُحِبُّ الْخَائِنِينَ﴿٥٨﴾

58. Na kama ukikhofu khiyana kwa watu basi watupilie (ahadi yao) ili iwe sawasawa (kusiweko tena kuahidiana). Hakika Allaah Hapendi makhaini.

 

 

 

 

 

وَلَا يَحْسَبَنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا سَبَقُوا ۚ إِنَّهُمْ لَا يُعْجِزُونَ﴿٥٩﴾

59. Na wala wasidhanie kabisa wale waliokufuru kwamba wao wamesabiki mbele (kuokoka). Hakika wao hawataweza kushinda (kukwepa Adhabu ya Allaah).

 

 

 

 

 

وَأَعِدُّوا لَهُم مَّا اسْتَطَعْتُم مِّن قُوَّةٍ وَمِن رِّبَاطِ الْخَيْلِ تُرْهِبُونَ بِهِ عَدُوَّ اللَّـهِ وَعَدُوَّكُمْ وَآخَرِينَ مِن دُونِهِمْ لَا تَعْلَمُونَهُمُ اللَّـهُ يَعْلَمُهُمْ ۚ وَمَا تُنفِقُوا مِن شَيْءٍ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ يُوَفَّ إِلَيْكُمْ وَأَنتُمْ لَا تُظْلَمُونَ﴿٦٠﴾

60. Na waandalieni nguvu[15] (za kiakili na kila aina za silaha) na farasi waliofungwa tayari kwa vita muwaogopeshe kwao maadui wa Allaah na maadui zenu, na wengineo wasiokuwa wao, hamuwajui, (lakini) Allaah Anawajua. Na chochote mkitoacho katika Njia ya Allaah mtalipwa kikamilifu, nanyi hamtodhulumiwa.

 

 

 

 

 

وَإِن جَنَحُوا لِلسَّلْمِ فَاجْنَحْ لَهَا وَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ ۚ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ﴿٦١﴾

61. Na kama (maadui) wakielemea kwenye amani basi nawe ielemee na tawakali kwa Allaah. Hakika Yeye Ni Mwenye Kusikia yote, Mjuzi wa yote.

 

 

 

 

 

وَإِن يُرِيدُوا أَن يَخْدَعُوكَ فَإِنَّ حَسْبَكَ اللَّـهُ ۚ هُوَ الَّذِي أَيَّدَكَ بِنَصْرِهِ وَبِالْمُؤْمِنِينَ﴿٦٢﴾

62. Na wakitaka kukuhadaa, basi hakika Allaah Anakutosheleza. Yeye Ndiye Ambaye Amekusaidia kwa Nusra Yake, na kwa Waumini.

 

 

 

 

 

وَأَلَّفَ بَيْنَ قُلُوبِهِمْ ۚ لَوْ أَنفَقْتَ مَا فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا مَّا أَلَّفْتَ بَيْنَ قُلُوبِهِمْ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ أَلَّفَ بَيْنَهُمْ ۚ إِنَّهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ﴿٦٣﴾

63. Na Akaunganisha nyoyo zao. Lau ungelitoa vyote vilivyomo ardhini, basi usingeliweza kuunganisha nyoyo zao, lakini Allaah Amewaunganisha. Hakika Yeye Ni Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote.

 

 

 

 

 

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ حَسْبُكَ اللَّـهُ وَمَنِ اتَّبَعَكَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ﴿٦٤﴾

64. Ee Nabiy! Allaah Anakutosheleza wewe pamoja na Waumini waliokufuata.  

 

 

 

 

 

 

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ حَرِّضِ الْمُؤْمِنِينَ عَلَى الْقِتَالِ ۚ إِن يَكُن مِّنكُمْ عِشْرُونَ صَابِرُونَ يَغْلِبُوا مِائَتَيْنِ ۚ وَإِن يَكُن مِّنكُم مِّائَةٌ يَغْلِبُوا أَلْفًا مِّنَ الَّذِينَ كَفَرُوا بِأَنَّهُمْ قَوْمٌ لَّا يَفْقَهُونَ﴿٦٥﴾

65. Ee Nabiy! Shajiisha Waumini kupigana vita. Wakiweko miongoni mwenu (Waumini) wahimilivu ishirini basi watawashinda (makafiri) mia mbili. Na wakiweko miongoni mwenu mia, watawashinda elfu katika wale waliokufuru, kwa kuwa wao ni watu wasiofahamu. 

 

 

 

 

الْآنَ خَفَّفَ اللَّـهُ عَنكُمْ وَعَلِمَ أَنَّ فِيكُمْ ضَعْفًا ۚ فَإِن يَكُن مِّنكُم مِّائَةٌ صَابِرَةٌ يَغْلِبُوا مِائَتَيْنِ ۚ وَإِن يَكُن مِّنكُمْ أَلْفٌ يَغْلِبُوا أَلْفَيْنِ بِإِذْنِ اللَّـهِ ۗ وَاللَّـهُ مَعَ الصَّابِرِينَ﴿٦٦﴾

66. Sasa Allaah Amekukhafifishieni na Amejua kwamba kuna udhaifu kwenu. Hivyo basi wakiweko miongoni mwenu (Waumini) wahimilivu mia, watawashinda (makafiri) mia mbili. Na wakiweko miongoni mwenu (Waumini) elfu, wawatashinda (makafiri) elfu mbili kwa Idhini ya Allaah. Na Allaah Yu pamoja na wenye subira.

 

 

 

 

 

مَا كَانَ لِنَبِيٍّ أَن يَكُونَ لَهُ أَسْرَىٰ حَتَّىٰ يُثْخِنَ فِي الْأَرْضِ ۚ تُرِيدُونَ عَرَضَ الدُّنْيَا وَاللَّـهُ يُرِيدُ الْآخِرَةَ ۗ وَاللَّـهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ﴿٦٧﴾

 

 

67. Haikumpasa Nabiy yeyote awe ana mateka mpaka apigane vikali mno kuwaua na kuwajeruhi (maadui wa Allaah) nchini. Mnataka vitu vya dunia, na hali Allaah Anataka (mpate vya) Aakhirah. Na Allaah Ni Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote.

 

 

 

 

 

لَّوْلَا كِتَابٌ مِّنَ اللَّـهِ سَبَقَ لَمَسَّكُمْ فِيمَا أَخَذْتُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ﴿٦٨﴾

68. Lau kama si hukumu iliyotangulia kutoka kwa Allaah, bila shaka ingekupateni adhabu kuu mno kwa vile mlivyochukua.

 

 

 

 

 

فَكُلُوا مِمَّا غَنِمْتُمْ حَلَالًا طَيِّبًا ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ﴿٦٩﴾

69. Basi kuleni katika ghanima mlizozipata, ni halali na ni vizuri, na mcheni Allaah. Hakika Allaah Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu.

 

 

 

 

 

 

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّمَن فِي أَيْدِيكُم مِّنَ الْأَسْرَىٰ إِن يَعْلَمِ اللَّـهُ فِي قُلُوبِكُمْ خَيْرًا يُؤْتِكُمْ خَيْرًا مِّمَّا أُخِذَ مِنكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ۗ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ﴿٧٠﴾

70. Ee Nabiy! Waambie wale waliomo mikononi mwenu katika mateka: Kama Allaah Akijua kheri yoyote katika nyoyo zenu, Atakupeni ya bora kuliko vilivyochukuliwa kwenu, na Atakughufurieni. Na Allaah Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu.

 

 

 

 

 

وَإِن يُرِيدُوا خِيَانَتَكَ فَقَدْ خَانُوا اللَّـهَ مِن قَبْلُ فَأَمْكَنَ مِنْهُمْ ۗ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ﴿٧١﴾

71. Na wakitaka kukufanyia khiyana, basi wao wamekwishamfanyia khiyana Allaah kabla yake, Naye Akakuwezesha kuwashinda. Na Allaah Ni Mjuzi wa yote, Mwenye Hikmah wa yote.

 

 

 

 

 

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَهَاجَرُوا وَجَاهَدُوا بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنفُسِهِمْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَالَّذِينَ آوَوا وَّنَصَرُوا أُولَـٰئِكَ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ ۚ وَالَّذِينَ آمَنُوا وَلَمْ يُهَاجِرُوا مَا لَكُم مِّن وَلَايَتِهِم مِّن شَيْءٍ حَتَّىٰ يُهَاجِرُوا ۚ وَإِنِ اسْتَنصَرُوكُمْ فِي الدِّينِ فَعَلَيْكُمُ النَّصْرُ إِلَّا عَلَىٰ قَوْمٍ بَيْنَكُمْ وَبَيْنَهُم مِّيثَاقٌ ۗ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ﴿٧٢﴾

72. Hakika wale walioamini na wakahajiri (Muhaajirina) na wakafanya Jihaad kwa mali zao na nafsi zao katika Njia ya Allaah, na wale waliowapa makazi (Answaar) na wakanusuru (Dini ya Allaah), hao ni marafiki wandani na walinzi, wao kwa wao. Na wale walioamini lakini hawakuhajiri, hamna nyinyi wajibu wowote wa kuwalinda mpaka wahajiri. Na wakikuombeni msaada katika Dini, basi ni juu yenu kuwasaidia isipokuwa juu ya watu mliofungamana nao mapatano baina yenu na wao. Na Allaah Ni Mwenye Kuona myatendayo.

 

 

 

 

 

وَالَّذِينَ كَفَرُوا بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ ۚ إِلَّا تَفْعَلُوهُ تَكُن فِتْنَةٌ فِي الْأَرْضِ وَفَسَادٌ كَبِيرٌ﴿٧٣﴾

73. Na wale waliokufuru ni marafiki wandani na walinzi, wao kwa wao. (Nanyi Waislamu) Msipofanya hivi itakuweko fitnah katika ardhi na ufisadi mkubwa.

 

 

 

 

 

وَالَّذِينَ آمَنُوا وَهَاجَرُوا وَجَاهَدُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَالَّذِينَ آوَوا وَّنَصَرُوا أُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُؤْمِنُونَ حَقًّا ۚ لَّهُم مَّغْفِرَةٌ وَرِزْقٌ كَرِيمٌ﴿٧٤﴾

74. Na wale walioamini na wakahajiri na wakafanya Jihaad katika Njia ya Allaah, na wale waliotoa makazi na wakanusuru, hao ndio Waumini wa kweli. Watapata maghfirah na riziki karimu.

 

 

 

 

 

وَالَّذِينَ آمَنُوا مِن بَعْدُ وَهَاجَرُوا وَجَاهَدُوا مَعَكُمْ فَأُولَـٰئِكَ مِنكُمْ ۚ وَأُولُو الْأَرْحَامِ بَعْضُهُمْ أَوْلَىٰ بِبَعْضٍ فِي كِتَابِ اللَّـهِ ۗ إِنَّ اللَّـهَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ﴿٧٥﴾

75. Na wale walioamini baada (ya hijra) na wakahajiri na wakafanya Jihaad pamoja nanyi, basi hao ni miongoni mwenu. Na ndugu wa uhusiano wa damu wanastahikiana wenyewe kwa wenyewe (kwa kurithiana), katika Sharia ya Allaah. Hakika Allaah Ni Mjuzi wa kila kitu.

 

 

 

 

 

[1] Ghazwat-Badr (Vita Vitukufu Vya Badr):

 

Vita vitukufu vya Badr vimetajwa katika Aayah zifuatazo za Suwrah hii Al-Anfaal:

 

 (5-10), (12), (15-19), (37-40), (42-47), (64-70). Na Allaah Mjuzi zaidi.

 

Hali kadhaalika vita vya Badr vimetajwa katika Suwrah Aal-‘Imraan.

 

Badr ni jina la mji ulioko kilomita mia na khamsini mbali na Madiynah. Mahali hapo kulikuwa na bonde tu na kisima kilichokuwa milki ya mtu aitwaye “Badr.” Na hii ni kauli mojawapo ya ‘Ulamaa; Rejea Aal-‘Imraan (3:123).  

 

Vita vikubwa vya Badr vilitokea Ramadhwaan ya kumi na saba, asubuhi ya siku ya Ijumaa, mwaka wa pili baada ya Hijrah.

 

Kulikuwa na msafara wa biashara wa makafiri ukiongozwa na Abu Sufyaan ambaye alikuwa bin ammi wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم). Bint yake Abu Sufyaan aliyeitwa Habiybah, alikuwa mke wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم). Hapo Abu Sufyaan alikuwa bado ni kafiri kisha akaja kusilimu katika mwaka wa Fat-h Makkah (Ushindi wa Makkah). 

 

Msafara huo uliotoka Sham ulikuwa unarudi Makkah ukiwa na watu wasiozidi arubaini, na msafara ulibeba mali nyingi mno ya watu wa Makkah. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) aliona ni fursa ya kulipiza kisasi kwa makafiri waliowalazimisha Wasilamu kuziacha mali zao Makkah walipohajiri kwenda Madiynah.  Waislamu hawakujua kama msafara huo utakuja kugeuka kuwa vita vya kupambanua haki na batili. Makafiri wa Quraysh waliandaa jeshi kubwa la watu wakiongozwa na Abu Jahal bin Hishaam na vigogo vya Quraysh wa Makkah. Waliandaa pia nguvu za farasi na ngamia wengi.  Waislamu walipopata khabari ya jeshi kubwa lilowakabili waliingiwa khofu kubwa kwa sababu walikuwa wachache na hawana silaha za kutosha, na baadhi yao wakatoa nyudhuru. Basi Waislamu ikawa ima wakabiliane na jeshi kubwa la Quraysh au waukabili msafara wapate kuteka mali. Lakini Allaah (سبحانه وتعالى) Alitaka na Aliqadiria wakabiliane na jeshi la Quraysh ili kudhihirike pambanuo la haki na batili kwa Qudra Yake Allaah (سبحانه وتعالى). 

 

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akasimama kuomba; Rejea Suwrah hii Al-Anfaal (8:9). Na Allaah (سبحانه وتعالى) Akatoa Ahadi Yake na Akateremsha Miujiza Yake kama kuteremsha maelfu ya Malaika wawatie nguvu Waislamu kupigana vita na makafiri wa Quraysh.

 

Pia Allaah (سبحانه وتعالى) Alifanya Kuwaua makafiri pale Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alipowarushia mchanga: Rejea Suwrah hii Al-Anfaal (8:17).

 

Pia Allaah (سبحانه وتعالى) Akawateremshia Waislamu utulivu wakapata usingizi mzito hadi wakaota na Akawateremshia mvua ya kujitwaharisha, na Akathibitisha miguu yao ardhini; Rejea Suwrah hii Al-Anfaal (8:11). Na miujiza mengineyo ambayo Aayah tukufu zinaendelea kutaja. Basi katika vita hivi Makafiri wakubwa wa Quraysh waliuliwa wakiwemo vigogo vyao wakubwa Abu Jahal, na ‘Utbah bin Rabiy’ah. Na kwa Rehma ya Allaah (سبحانه وتعالى) na Uwezo Wake Akajaalia ushindi kwa Waislamu juu ya kuwa wao walikuwa ni wachache.

 

Hakika ilikuwa Vita vya Miujiza vinavyosisimua pindi mtu akipata ilimu ya Tafsiyr yake pamoja na Hadiyth husika.

 

 

[2] Maana Ya Istighaathah Na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Aliomba Duaa Siku Ya Vita Vya Badr Anusuriwe:

 

Istighaathah maana yake ni kuomba uokozi kwa ambaye ataweza kuokoa kutokana na hali ya shida, dhiki na kukaribia kudhurika au kuangamia. Na istighaathah kwa Allaah (سبحانه وتعالى) inajumuisha kujidhalilisha Kwake na kuitakidi kwamba hakuna mwengine atakayeweza kuokoa isipokuwa Yeye.

 

[3] Tofauti Ya Ikabu Na Adhabu: Rejea Al-Hashr (59:4).

 

[4] Kukimbia Vita Vya Jihaad Ni Miongoni Mwa Dhambi Saba Zinazoangamiza:

 

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) : Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)  amesema: “Jiepusheni na mambo saba yanayoangamiza!” Wakauliza: Ni yepi hayo ee Rasuli wa Allaah? Akasema: “Ni kumshirikisha Allaah, sihri (uchawi), kuua nafsi Aliyoiharamisha Allaah isipokuwa kwa haki, kula riba, kula mali ya yatima, kukimbia wakati wa kupambana na adui, na kuwatuhumu uzinifu wanawake Waumini waliohifadhika walioghafilika”. [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

[5] Aayah hii imeteremshwa siku ya Vita vya Badr. [Sunan Abiy Daawuwd, Kitaab Al-Jihaad, Hadiyth ya Abuu Sa’iyd, na ameisahihisha Al-Albaaniy] 

 

[6] Allaah Hana Sifa Mbaya Ila Analipiza Uovu. Rejea Aal-‘Imraan (3:54).

 

[7] Ada Ya Makafiri Kuhimiza AdhabuRejea Al-Hajj (22:47), Swaad (38:16), Ash-Shuwraa (42:18).

 

[8] Uwepo Wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Ulikuwa Ni Neema Kwa Makafiri Kutokuadhibiwa. Na Fadhila Za Istighfaar (Kuomba Maghfirah)

 

Imaam As-Sa’diy  (رحمه الله)  amesema:  “Kutokana na kauli yao hiyo ya Aayah (32) ya kuomba adhabu) ni dhahiri kuwa wao ni wajinga wapumbavu, madhalimu. Lau kama Allaah Angewaharakishia adhabu basi wasingebakia kuishi. Lakini Allaah Amewakinga na adhabu kwa sababu ya uwepo wa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) miongoni mwao. Basi uwepo wa Rasuli (صلى الله عليه وآله وسلم) ni amani kwao kutokana na adhabu.” [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

Fadhila Za Istighfaar (Kuomba Maghfirah):

 

Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema kuwa Hakuwaadhibu makafiri kwa sababu ya kuomba kwao maghfirah. Hivyo inadhihirisha kwamba kuomba maghfirah inasababisha kutokuadhibiwa na Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Huwd (11:3) kwenye faida kadhaa na fadhila za kuomba Istighfaar.

 

[9] Desturi Ya Allaah (سبحانه وتعالى): 

 

Ni kuadhibu na kuangamiza makafiri na wanafiki wa nyumati za nyuma zilizokadhibisha Rusuli Wake na Ishara Zake. Na kwamba ushindi unakuwa daima kwa Rusuli Wake.  Na desturi hii hutoiona kamwe kubadilika. Na Allaah (سبحانه وتعالى) Anataja hayo mara kadhaa katika visa vya nyumati za nyuma. Rejea Aal-‘Imraan (3:137).

 

[10] Mawlaa "مَوْلَى":  Rejea Faharasa Ya Majina Ya Allaah (سبحانه وتعالى).

 

[11] Ghanima: Ngawira Inayopatikana Baada Ya Kupigana Vita:   

 

Ghanima (ambalo ni neno la Kiarabu  ("غنيمة" ni mali inayopatikana kwa kutekwa baada ya ushindi katika vita kama mifugo, watu, mazao, zana na kadhalika kama ilivyotajwa katika Suwrah hii na Al-Fat-h (48:19-20). Ama mali inayopatikana bila ya kupigana vita, hii inaitwa katika Qur-aan Al-Fay-u "الفَيْءُ" ambayo imetajwa katika Al-Hashr (59:6-7).

 

[12] Riyaa-a (Kujionyesha Kwa Watu): Ni Shirki Inayobatilisha Amali:

 

Hii ni riyaa-a ya kwenda katika Jihaad. Na juu ya hivyo kusudio la wanafiki lilikuwa ni kuzuia watu njia ya Allaah.  Rejea Az-Zumar (39:65) kwenye maelezo kuhusu aina za shirki

 

[13] Shaytwaan Huwapotosha Watu Kisha Huwakanusha Na Kuwagueka:

 

Rejea pia Suwrah Ibraahiym (14:22), Al-Israa (17:64) kwenye maelezo bayana.

 

[14] Nyoyo Zenye Maradhi:

 

Rejea Suwrah Muhammad (47:20) kwenye maelezo na rejea mbalimbali kuhusu nyoyo zenye maradhi.

 

Rejea pia Al-Hajj (22:46) kwenye maelezo kuhusu maana ya moyo uliopofuka.

Rejea pia Ash-Shu’araa (26:88-89) kwenye ufafanuzi na maelezo kuhusu moyo uliosalimika.

 

[15] Maana Ya قُوَّةٍ:

 

Imekusudiwa pia kujifunza kutupa mishale kama ilivyotajwa katika Hadiyth: Amesimulia ‘Uqbah bin ‘Aamir (رضي الله عنه) : Nimemsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)    alipokuwa juu ya minbar akisema:

وَأَعِدُّوا لَهُمْ مَا اسْتَطَعْتُمْ مِنْ قُوَّةٍ

Na waandalieni nguvu zozote mziwezazo …” Tanabahi! Hakika Al-Quwwah ni Ar-Ramyu (kutupa mshale, kulenga kwa kutumia silaha), hakika Al-Quwwah ni Ar-Ramyu, hakika Al-Quwwah ni Ar-Ramyu.” [Muslim]

 

Pia kujifunza ushujaa, mipango ya kuandaa jeshi mbali na hayo yaliyotajwa ya kujiandaa kwa silaha za kila aina zikiwemo ndege za vita, mizinga, bunduki, gari za ardhini na boti za baharini, ngome, mahandaki, mashine za ulinzi na mengineyo yote ya vita ili Waislamu waweze kuwashinda maadui zao.

 

Share