009-Asbaabun-Nuzuwl: Al-Anfaal Aayah 009: إِذْ تَسْتَغِيثُونَ رَبَّكُمْ فَاسْتَجَابَ لَكُمْ أَنِّي مُمِدُّكُم بِأَلْفٍ مِّنَ الْمَلَائِكَةِ مُرْدِفِينَ

 

 أسْبابُ النُّزُول

Asbaabun-Nuzuwl

Sababu Za Kuteremshwa (Baadhi Ya  Suwrah Na Aayaat Za Qur-aan)

 

Imekusanywa na: Alhidaaya.com

 

Al-Anfaal: 9

 

 

09-Na pale mlipomuomba uokovu Rabb wenu Naye Akakuitikieni kuwa: Hakika Mimi Nitakusaidieni kwa Malaika elfu wafuatanao mfululizo

 

 

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

إِذْ تَسْتَغِيثُونَ رَبَّكُمْ فَاسْتَجَابَ لَكُمْ أَنِّي مُمِدُّكُم بِأَلْفٍ مِّنَ الْمَلَائِكَةِ مُرْدِفِينَ﴿٩﴾

 

Na pale mlipomuomba uokovu Rabb wenu Naye Akakuitikieni kuwa: Hakika Mimi Nitakusaidieni kwa Malaika elfu wafuatanao mfululizo. [Al-Anfaal: 9]

 

 

Sababun-Nuzuwl: 

 

 

Amesimulia ‘Umar bin Al-Khatwwaab  (رضي الله عنه)  Ilipokuwa siku ya vita vya Badr, Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) aliwatazama washirikina wakiwa ni elfu moja na Swahaba zake ni mia tatu na kumi na tisa. Basi Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alielekea Qiblah akanyoosha mikono yake akiomba kwa Rabb wake: “Ee Allaah, Nitimizie Yale Uliyoniahidi. Ee Allaah, Nipe yale Uliyoniahidi. Ee Allaah, kikundi hiki kidogo cha Waislamu kikiangamia, hutoabudiwa tena katika ardhi.” Akaendelea kuomba kwa Rabb wake akinyoosha mikono yake huku ameelekea Qiblah mpaka ridaa (vazi la juu ya nguo kama kanzu au joho) lake likamuanguka kutoka mabegani mwake. Abuu Bakr akamjia akaliokota ridaa lake na akamwekea mabegani. Kisha akamgeukia nyuma akasema: Ee Nabiy wa Allaah, Du’aa yako hii kwa Rabb wako itakutosheleza kwani Atakutimizia yale Aliyokuahidi. Hapo Allaah (عز وجل) Akateremsha:

 

إِذْ تَسْتَغِيثُونَ رَبَّكُمْ فَاسْتَجَابَ لَكُمْ أَنِّي مُمِدُّكُم بِأَلْفٍ مِّنَ الْمَلَائِكَةِ مُرْدِفِينَ﴿٩﴾

Na pale mlipomuomba uokovu Rabb wenu Naye Akakuitikieni kuwa: Hakika Mimi Nitakusaidieni kwa Malaika elfu wafuatanao mfululizo. [Al-Anfaal: 9]

 

Basi Allaah Akamsaidia kwa kumteremshia Malaika. 

 

 

Abuu Zumayl amesema kwamba Hadiyth imesimuliwa kwake na Ibn ‘Abbaas ambaye amesema: “Siku hiyo, pindi Muislamu alipokuwa anamfukuza kafiri aliyekuwa anamwendea mbele yake, alisikia mpigo wa mjeledi na sauti ya mpandaji farasi akisema: “Tangulia ee Zumayl! Basi alimtazama kafiri ambaye hapo alianguka chini akiwa amelala chali. Alipomtazama aliona pua yake ina kovu na uso umechanwa kama kwamba umepigwa na mjeledi na uso umegeuka rangi ya kijani kutokana na sumu. Answaariy mmoja alikuja akamhadithia hayo Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Umesema kweli, huo ni msaada kutoka mbingu ya tatu.” Basi siku hiyo Waislamu waliwaua watu sabini na wakawateka sabini.  Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akamwambia Abuu Bakr na ‘Umar (رضي الله عنهما): “Nini ushauri wenu kuhusu mateka hawa?” Abuu Bakr akasema: “Hao ni watoto wa ‘ammi zetu na jamaa zetu. Naona kuwa uwaache baada ya kuwatoza fidia ili tupate nguvu dhidi ya makafiri, na ‘asaa Allaah Awahidi katika Uislamu.”  Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Je, ee ‘Umar unaonaje wewe?” Akasema: “Hapana! Wa-Allaahi ee Rasuli wa Allaah, mimi sioni anavyoona Abuu Bakr, lakini ninaloona ni kuwa utukabidhi tuwakate vichwa vyao! Basi mkabidhi ‘Aqiyl kwa ‘Aliy ili amkate kichwa chake. Na nikabidhi mimi ‘fulani’ (jamaa wa ‘Umar) ili nimkate mimi kichwa chake, kwani hao ni viongozi wa makafiri na ndio mashujaa wao. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akaunga mkono aliyoyasema Abuu Bakr lakini hakuunga mkono niliyoyasema mimi. Siku ya pili, nilipomwendea Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) nimekuta yeye na Abuu Bakr wamekaa kitako huku wanalia. Nikasema: Ee Rasuli wa Allaah, nijulishe kinachokuliza wewe na Swahibu yako ili nami nilie pamoja nanyi au angalau nijilize kwa kuwaonea huruma. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Nalia kutokana na yaliyomtokea Swahibu wako kuchukua fidia (kwa mateka). Nimeonyeshwa adhabu yao iliyokaribia chini ya mti huu (akaashiria mti ulio karibu naye). Kisha Allaah (عز وجل) Akateremsha:

 

مَا كَانَ لِنَبِيٍّ أَن يَكُونَ لَهُ أَسْرَىٰ حَتَّىٰ يُثْخِنَ فِي الْأَرْضِ ۚ تُرِيدُونَ عَرَضَ الدُّنْيَا وَاللَّـهُ يُرِيدُ الْآخِرَةَ ۗ وَاللَّـهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ﴿٦٧

Haikumpasa Nabiy yeyote awe ana mateka mpaka apigane vikali mno kuwaua na kuwajeruhi (maadui wa Allaah) nchini. Mnataka vitu vya dunia, na hali Allaah Anataka (mpate vya) Aakhirah. Na Allaah Ndiye Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote.

 

لَّوْلَا كِتَابٌ مِّنَ اللَّـهِ سَبَقَ لَمَسَّكُمْ فِيمَا أَخَذْتُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ﴿٦٨﴾

Lau kama si hukumu iliyotangulia kutoka kwa Allaah bila shaka ingekupateni kwa yale mliyoyachukua adhabu kuu.

 

فَكُلُوا مِمَّا غَنِمْتُمْ حَلَالًا طَيِّبًا ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ﴿٦٩﴾

Basi kuleni katika ghanima mlizozipata, ni halali na ni vizuri, na mcheni Allaah. Hakika Allaah Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu. [Al-Anfaal: 67-69]

 

 

 

 

Share