051 - Adh-Dhaariyaat

 

   الذَّارِيَات

 

051-Adh-Dhaariyaat

 

 

051-Adh-Dhaariyaat: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com 

 

 

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

 

وَالذَّارِيَاتِ ذَرْوًا﴿١﴾

1. Naapa kwa (pepo) zinazopeperusha vumbi kuzitawanya.

 

 

 

فَالْحَامِلَاتِ وِقْرًا﴿٢﴾

2. Kisha Naapa kwa (mawingu) yanayobeba mzigo wa maji.  

 

 

 

فَالْجَارِيَاتِ يُسْرًا﴿٣﴾

3. Kisha Naapa kwa (merikebu) zinazotembea kwa wepesi.

 

 

 

فَالْمُقَسِّمَاتِ أَمْرًا﴿٤﴾

4. Kisha Naapa kwa (Malaika) wenye kugawanya amri.

 

 

 

إِنَّمَا تُوعَدُونَ لَصَادِقٌ﴿٥﴾

5. Hakika mnayoahidiwa bila shaka ni kweli.

 

 

وَإِنَّ الدِّينَ لَوَاقِعٌ﴿٦﴾

6. Na hakika malipo bila shaka yatatokea.

 

 

وَالسَّمَاءِ ذَاتِ الْحُبُكِ﴿٧﴾

7. Naapa kwa mbingu zilizojaa njia madhubuti.

 

 

إِنَّكُمْ لَفِي قَوْلٍ مُّخْتَلِفٍ﴿٨﴾

8. Hakika nyinyi bila shaka mko katika kauli inayokhitilafiana.

 

 

 

يُؤْفَكُ عَنْهُ مَنْ أُفِكَ﴿٩﴾

9. Ameghilibiwa kwayo anayeghilibiwa (kuhusu haki).

 

 

قُتِلَ الْخَرَّاصُونَ﴿١٠﴾

10. Wameangamia wanaobuni uongo.

 

 

الَّذِينَ هُمْ فِي غَمْرَةٍ سَاهُونَ﴿١١﴾

11. Ambao wamo katika mfuniko wa mghafala, wenye kupurukusha (kuhusu Aakhirah).

 

 

يَسْأَلُونَ أَيَّانَ يَوْمُ الدِّينِ﴿١٢﴾

12. Wanauliza: Lini hiyo Siku ya malipo?

 

 

يَوْمَ هُمْ عَلَى النَّارِ يُفْتَنُونَ﴿١٣﴾

13. Siku wao watakapoteswa motoni.

 

 

 

ذُوقُوا فِتْنَتَكُمْ هَـٰذَا الَّذِي كُنتُم بِهِ تَسْتَعْجِلُونَ﴿١٤﴾

14. Onjeni adhabu yenu. Haya ndiyo ambayo mlikuwa mkiyahimiza.

 

 

 

إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي جَنَّاتٍ وَعُيُونٍ﴿١٥﴾

15. Hakika wenye taqwa watakuwa katika Jannaat na chemchemu.[1] 

 

 

 

آخِذِينَ مَا آتَاهُمْ رَبُّهُمْ ۚ إِنَّهُمْ كَانُوا قَبْلَ ذَٰلِكَ مُحْسِنِينَ﴿١٦﴾

16. Wakichukua yale Atakayowapa Rabb wao. Hakika wao walikuwa kabla ya hapo ni wahisani.

 

 

 

كَانُوا قَلِيلًا مِّنَ اللَّيْلِ مَا يَهْجَعُونَ﴿١٧﴾

17. Walikuwa kidogo tu katika usiku wakilala kwa raha.

 

 

وَبِالْأَسْحَارِ هُمْ يَسْتَغْفِرُونَ﴿١٨﴾

18. Na kabla ya Alfajiri wakiomba Maghfirah.[2]

 

 

 

وَفِي أَمْوَالِهِمْ حَقٌّ لِّلسَّائِلِ وَالْمَحْرُومِ﴿١٩﴾

19. Na katika mali zao kuna haki maalumu kwa mwenye kuomba na asiyeomba.

 

 

 

 

وَفِي الْأَرْضِ آيَاتٌ لِّلْمُوقِنِينَ﴿٢٠﴾

20. Na katika ardhi kuna Aayaat (Ishara, Dalili, Mazingatio) kwa wenye yakini.[3]

 

 

 

 

وَفِي أَنفُسِكُمْ ۚ أَفَلَا تُبْصِرُونَ﴿٢١﴾

21. Na katika nafsi zenu, je hamuoni?

 

 

 

 

وَفِي السَّمَاءِ رِزْقُكُمْ وَمَا تُوعَدُونَ﴿٢٢﴾

22. Na katika mbingu kuna riziki yenu na yale mnayoahidiwa.

 

 

 

 

فَوَرَبِّ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ إِنَّهُ لَحَقٌّ مِّثْلَ مَا أَنَّكُمْ تَنطِقُونَ﴿٢٣﴾

23, Basi Naapa kwa Rabb wa mbingu na ardhi, hakika hiyo ni haki kama nyinyi mnavyotamka.

 

 

 

 

هَلْ أَتَاكَ حَدِيثُ ضَيْفِ إِبْرَاهِيمَ الْمُكْرَمِينَ﴿٢٤﴾

24. Je, imekufikia hadithi ya wageni wahishimiwao wa Ibraahiym?

 

 

 

 

إِذْ دَخَلُوا عَلَيْهِ فَقَالُوا سَلَامًا ۖ قَالَ سَلَامٌ قَوْمٌ مُّنكَرُونَ﴿٢٥﴾

25. Walipoingia kwake wakasema: Salaam! Akasema: Salaam watu wasiotambulikana.

 

 

 

فَرَاغَ إِلَىٰ أَهْلِهِ فَجَاءَ بِعِجْلٍ سَمِينٍ﴿٢٦﴾

26. Akaondoka bila kuhisiwa kuelekea kwa ahli yake, akaleta ndama aliyenona.

 

 

 

 

فَقَرَّبَهُ إِلَيْهِمْ قَالَ أَلَا تَأْكُلُونَ﴿٢٧﴾

27. Akawakurubishia pale walipo, akasema: Mbona hamli?

 

 

 

 

فَأَوْجَسَ مِنْهُمْ خِيفَةً ۖ قَالُوا لَا تَخَفْ ۖ وَبَشَّرُوهُ بِغُلَامٍ عَلِيمٍ﴿٢٨﴾

28. Akawaogopa ndani ya nafsi yake. Wakasema: Usikhofu! Na wakambashiria ghulamu mjuzi.

 

 

 

 

فَأَقْبَلَتِ امْرَأَتُهُ فِي صَرَّةٍ فَصَكَّتْ وَجْهَهَا وَقَالَتْ عَجُوزٌ عَقِيمٌ﴿٢٩﴾

29. Mkewe akawakabili kwa ukelele wa furaha, akajipiga usoni na kusema: Kikongwe, tasa!

 

 

 

 

قَالُوا كَذَٰلِكِ قَالَ رَبُّكِ ۖ إِنَّهُ هُوَ الْحَكِيمُ الْعَلِيمُ﴿٣٠﴾

30. Wakasema: Hivyo ndivyo Alivyosema Rabb wako. Hakika Yeye Ndiye Mwenye Hikmah wa yote, Mjuzi wa yote. 

 

 

 

 

قَالَ فَمَا خَطْبُكُمْ أَيُّهَا الْمُرْسَلُونَ ﴿٣١﴾

31. (Ibraahiym) akasema: Basi nini shughuli yenu mloikusudia enyi Wajumbe?

 

 

 

 

قَالُوا إِنَّا أُرْسِلْنَا إِلَىٰ قَوْمٍ مُّجْرِمِينَ ﴿٣٢﴾

32. Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwa watu wahalifu.

 

 

 

 

لِنُرْسِلَ عَلَيْهِمْ حِجَارَةً مِّن طِينٍ ﴿٣٣﴾

33. Ili Tuwavurumishie mawe ya udongo.[4]

 

 

 

مُّسَوَّمَةً عِندَ رَبِّكَ لِلْمُسْرِفِينَ ﴿٣٤﴾

34. Yaliyotiwa alama kutoka kwa Rabb wako kwa wapindukao mipaka.

 

 

 

 

فَأَخْرَجْنَا مَن كَانَ فِيهَا مِنَ الْمُؤْمِنِينَ ﴿٣٥﴾

35. Basi Tukawatoa humo wale waliokuwa Waumini.

 

 

 

 

فَمَا وَجَدْنَا فِيهَا غَيْرَ بَيْتٍ مِّنَ الْمُسْلِمِينَ ﴿٣٦﴾

36. Lakini Hatukukuta humo isipokuwa nyumba moja tu ya Waislamu.

 

 

 

 

وَتَرَكْنَا فِيهَا آيَةً لِّلَّذِينَ يَخَافُونَ الْعَذَابَ الْأَلِيمَ ﴿٣٧﴾

37. Na Tukaacha humo Aayah (Athari) kwa wale wanaoogopa adhabu iumizayo.

 

 

 

 

وَفِي مُوسَىٰ إِذْ أَرْسَلْنَاهُ إِلَىٰ فِرْعَوْنَ بِسُلْطَانٍ مُّبِينٍ ﴿٣٨﴾

38. Na kwa Muwsaa (pia ipo athari), Tulipomtuma kwa Firawni na miujiza bayana.

 

 

 

فَتَوَلَّىٰ بِرُكْنِهِ وَقَالَ سَاحِرٌ أَوْ مَجْنُونٌ ﴿٣٩﴾

39. Akakengeuka (akitegemea nguvu) na askari na wasaidizi wake akasema: Mchawi au majnuni.[5]

 

 

 

فَأَخَذْنَاهُ وَجُنُودَهُ فَنَبَذْنَاهُمْ فِي الْيَمِّ وَهُوَ مُلِيمٌ ﴿٤٠﴾

40. Tukamchukuwa na jeshi lake, kisha Tukawavurumisha katika bahari nailhali yeye ni mwenye kujiletea mwenyewe lawama.

 

 

 

 

وَفِي عَادٍ إِذْ أَرْسَلْنَا عَلَيْهِمُ الرِّيحَ الْعَقِيمَ ﴿٤١﴾

41. Na kwa kina ‘Aad, Tulipowapelekea upepo wa adhabu, mkame.

 

 

 

 

مَا تَذَرُ مِن شَيْءٍ أَتَتْ عَلَيْهِ إِلَّا جَعَلَتْهُ كَالرَّمِيمِ ﴿٤٢﴾

42. Haukuacha chochote ulichokifikia ila ulikifanya kama kilichobungulika na kuoza.

 

 

 

وَفِي ثَمُودَ إِذْ قِيلَ لَهُمْ تَمَتَّعُوا حَتَّىٰ حِينٍ ﴿٤٣﴾

43. Na kwa kina Thamuwd walipoambiwa: Stareheni kwa muda.

 

 

 

 

فَعَتَوْا عَنْ أَمْرِ رَبِّهِمْ فَأَخَذَتْهُمُ الصَّاعِقَةُ وَهُمْ يَنظُرُونَ ﴿٤٤﴾

44. Wakafanya ufidhuli kuhusu Amri ya Rabb wao, basi ikawachukuwa radi na umeme angamizi na huku wao wanatazama.

 

 

 

فَمَا اسْتَطَاعُوا مِن قِيَامٍ وَمَا كَانُوا مُنتَصِرِينَ ﴿٤٥﴾

45. Basi hawakuweza kusimama na wala hawakuwa wenye kujinusuru. 

 

 

 

 

وَقَوْمَ نُوحٍ مِّن قَبْلُ ۖ إِنَّهُمْ كَانُوا قَوْمًا فَاسِقِينَ ﴿٤٦﴾

46. Na watu wa Nuwh hapo kabla. Hakika wao walikuwa kaumu mafasiki.

 

 

 

 

وَالسَّمَاءَ بَنَيْنَاهَا بِأَيْدٍ وَإِنَّا لَمُوسِعُونَ ﴿٤٧﴾

47. Na mbingu Tumezijenga kwa nguvu na qudra, na hakika Sisi Ndio Wenye Kupanua.

 

 

 

وَالْأَرْضَ فَرَشْنَاهَا فَنِعْمَ الْمَاهِدُونَ ﴿٤٨﴾

48. Na ardhi Tumeitandaza, basi Wazuri Tulioje Sisi wa Kutayarisha!

 

 

 

 

وَمِن كُلِّ شَيْءٍ خَلَقْنَا زَوْجَيْنِ لَعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ ﴿٤٩﴾

49. Na kila kitu Tumeumba jozi mbili; dume na jike ili mpate kukumbuka.

 

 

 

 

فَفِرُّوا إِلَى اللَّـهِ ۖ إِنِّي لَكُم مِّنْهُ نَذِيرٌ مُّبِينٌ ﴿٥٠﴾

50. Basi kimbilieni kwa Allaah. Hakika mimi kwenu ni mwonyaji bayana kutoka Kwake.

 

 

وَلَا تَجْعَلُوا مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ ۖ إِنِّي لَكُم مِّنْهُ نَذِيرٌ مُّبِينٌ ﴿٥١﴾

51. Na wala msifanye pamoja na Allaah mwabudiwa mwingine, hakika mimi kwenu ni mwonyaji bayana kutoka Kwake.

 

 

 

 

كَذَٰلِكَ مَا أَتَى الَّذِينَ مِن قَبْلِهِم مِّن رَّسُولٍ إِلَّا قَالُوا سَاحِرٌ أَوْ مَجْنُونٌ ﴿٥٢﴾

52. Ndio kama hivyo, hawakuwafikia wale wa kabla yao Rasuli yeyote isipokuwa walisema: Mchawi au majnuni.[6]

 

 

أَتَوَاصَوْا بِهِ ۚ بَلْ هُمْ قَوْمٌ طَاغُونَ ﴿٥٣﴾

53. Je, wameusiana kwa hayo?  Bali wao ni watu wenye kupindukia mipaka ya kuasi.

 

 

فَتَوَلَّ عَنْهُمْ فَمَا أَنتَ بِمَلُومٍ ﴿٥٤﴾

54. Basi jitenge nao (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم), kwani wewe si mwenye kulaumiwa kabisa.

 

 

 

وَذَكِّرْ فَإِنَّ الذِّكْرَىٰ تَنفَعُ الْمُؤْمِنِينَ ﴿٥٥﴾

55. Na kumbusha, kwani hakika ukumbusho unawafaa Waumini.[7]

 

 

 

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ ﴿٥٦﴾

56. Na Sikuumba majini na wana Aadam isipokuwa waniabudu.

 

 

 

 

مَا أُرِيدُ مِنْهُم مِّن رِّزْقٍ وَمَا أُرِيدُ أَن يُطْعِمُونِ ﴿٥٧﴾

57. Sitaki kutoka kwao riziki yoyote, na wala Sitaki wanilishe.

 

 

 

 

إِنَّ اللَّـهَ هُوَ الرَّزَّاقُ ذُو الْقُوَّةِ الْمَتِينُ ﴿٥٨﴾

58. Hakika Allaah Ndiye Mwingi wa Kuruzuku, Mwenye Nguvu Madhubuti.[8]

 

 

 

فَإِنَّ لِلَّذِينَ ظَلَمُوا ذَنُوبًا مِّثْلَ ذَنُوبِ أَصْحَابِهِمْ فَلَا يَسْتَعْجِلُونِ ﴿٥٩﴾

59. Basi hakika wale waliodhulumu watakuwa na sehemu ya adhabu kama sehemu ya adhabu ya wenzao, basi wasihimize.

 

 

 

 

فَوَيْلٌ لِّلَّذِينَ كَفَرُوا مِن يَوْمِهِمُ الَّذِي يُوعَدُونَ ﴿٦٠﴾

60. Basi ole kwa wale waliokufuru kutokana na Siku yao ambayo wanaahidiwa.

 

 

 

[1] Fadhila Za Kuamka Usiku Kwa Ajili Ya Ibaada:

 

Aayah hii inaanza kutaja fadhila za Qiyaamul-Layl. Kisha Aayah namba (17-18) inataja sifa za Waumini wanaoacha usingizi wao wakaamka kwa ajili ya kumdhukuru Allaah (سبحانه وتعالى).

 

Na Allaah (سبحانه وتعالى) Anahimiza Qiyaamul-Layl katika Suwrah kadhaa za Qur-aan na kutaja baadhi ya fadhila zake. Na katika Sunnah, fadhila tele zimetajwa. Miongoni mwazo ni: 

 

(i)  Qiyaamul-Layl Ni Swalaah Bora Baada Ya Swalaah Za Fardhi:

 

Hadiyth ya Abu Hurayrah (رضي الله عنه) na kwa riwaayah mbalimbali:

(أَفْضَلُ الصَّلاةِ بَعْدَ الْفَرِيضَةِ صَلاةُ اللَّيْلِ) رواه مسلم

“Swalaah iliyo bora kabisa baada ya fardhi ni Swalaah ya usiku.”  [Muslim]

 

(ii) Kuswali Na Kusoma Japo Aayah Chache:

 

عبدالله بن عمرو عن النبي صلى الله عليه وسلم ((من قام بعشرِ آياتٍ لم يُكتبْ من الغافلينَ ، ومن قام بمئةِ آيةٍ كُتبَ من القانتينَ ومن قام بألفِ آيةٍ كُتبَ من المُقَنْطِرينَ)) صحيح أبي داود  

 

Amesimulia ‘Abdullaah bin ‘Amr (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Atakayesimama usiku kuswali na akasoma Aayah kumi, hatoandikiwa kuwa miongoni mwa walioghafilika, na atakayesimama kuswali akasoma Aayah mia, ataandikiwa ni miongoni mwa watiifu, na atakayesimama kuswali akasoma Aayah elfu, ataandikwa miongoni mwa wenye mirundi (ya thawabu).’ [Abuu Daawuwd, Al-Albaaniy ameisahihisha: Swahiyh Abiy Daawuwd (1398), Swahiyh Al-Jaami’ (6439)]

 

(iii) Kufutiwa Madhambi, Kuondoshewa Maradhi):

 

عن بلال، أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: عليكُم بقيامِ اللَّيلِ ، فإنَّهُ دَأْبُ الصَّالِحينَ قبلَكُم ، و قُربةٌ إلى اللهِ تعالى ومَنهاةٌ عن الإثمِ و تَكفيرٌ للسِّيِّئاتِ ، ومَطردةٌ للدَّاءِ عن الجسَدِ

 

Amesimulia Bilaal (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Shikamaneni na Qiyaamul-Layl (kuswali usiku), kwani ni desturi za Swalihina (waja wema) kabla yenu, na kujikurubisha kwa Allaah, na inazuia madhambi, inafuta maovu na inaondosha maradhi mwilini.” [Ahmad na At-Tirmidhiy, na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh Al-Jaami (4079)]

 

(iv) Allaah (سبحانه وتعالى) Huteremka Mbingu Ya Dunia. Rejea Al-Mulk (67:16) kwenye Hadiyth inayothibitisha kuwa Anateremka thuluthi ya mwisho ya usiku kusikiliza na kukidhia haja za Waja Wake wanaoamka usiku kwa ajili ya ibaada.

 

Rejea pia Al-Israa (17:79), As-Sajdah (32:16), Al-Muzzammil (73:1-6).

 

Pia bonyeza viungo vifuatavyo kupata faida nyenginezo:

 

Fadhila Na Faida Za Qiyaamul-Layl

 

19-Swahiyh Al-Bukhaariy: Kitabu Cha Tahajjud (Swalaah Ya Qiyaam Usiku) - كتاب التهجد

 

 

[2] Kuomba Maghfirah Kabla Ya Alfajiri:

 

Bonyeza viungo vifuatavyo kupata faida kadhaa za maudhui hii:

 

017-Aayah Na Mafunzo: Fadhila Za Kuomba Maghfirah Kabla Ya Alfajiri

 

04-Tawbah Hukmu Na Fadhila Zake: Nyakati Bora Za Kuomba Tawbah

 

Tawbah: Hukmu Na Fadhila Zake

 

Rejea An-Nisaa (4:110), Huwd (11:3) kwenye maelezo bayan na rejea mbalimbali. Pia At-Tahriym (66:8), Nuwh (71:10).  

 

[3] Ishara, Dalili Za Ardhini Zinazothibitisha Tawhiyd Ya Allaah (عزّ وجلّ) :

 

Ishara na Dalili nyingi ardhini na mbinguni zimetajwa katika Qur-aan. Rejea Rejea Yuwsuf (12:105), Fusw-Swilat (41:53). Bali Qur-aan nzima inathibitisha Tawhiyd ya Allaah (سبحانه وتعالى), yakiwemo na mafundisho kutoka kwa Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم).

 

Imaam As-Sa’diy (رحمه الله)  amesema: Hapa Allaah (عزّ وجلّ) Anawaita Waja Wake watafakari na wazingatie:

 

وَفِي الْأَرْضِ آيَاتٌ لِّلْمُوقِنِينَ﴿٢٠﴾

“Na katika ardhi kuna Aayaat (Ishara, Dalili, Mazingatio) kwa wenye yakini.”

 

 Inajumuisha ardhi yenyewe na yote yaliyomo humo kama milima, bahari, mito, miti na mimea ambavyo vyote vinaashiria kwa mwenye kutafakari na kuzingatia maana zake, juu ya Utukufu wa Muumbaji wake na Upana wa Mamlaka Yake, na ueneaji usio na ukomo wa Ihsaan Yake, na jinsi Ujuzi Wake unavyovizunguka vitu vyote vinavyoonekana na vilivyofichika.  [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

[4] Adhabu Na Maangamizi Ya Kaumu Za Awali:

 

Kuanzia Aayah hii na zinazoendelea, panatajwa baadhi ya kaumu za awali, na maangamizi na adhabu zao baada ya kuwakanusha Rusuli wa Allaah. 

 

Rejea Al-‘Ankabuwt (29:40)  kwenye maelezo na uchambuzi kuhusu: Makafiri wa nyumati za nyuma na aina za adhabu zao.

 

[5] Firawni Kumpachika Nabiy Muwsaa (عليه السّلام) Sifa Ovu: 

 

Rejea Suwrah hii namba (52).

 

[6] Makafiri Kuwapachika Rusuli Wao Sifa Ovu:

 

Sifa ovu kadhaa alipachikwa nazo Nabiy Muwsaa (عليه السّلام) na adui wake Firawni.  Mara amwite mchawi mjuzi, mara majnuni, mara muongo. Rejea Suwrah hii Adh-Dhaariyaat (51:39), Al-A’raaf (7:109), Al-Israa (17:101), Twaahaa (20:63), Ash-Shu’araa (26:34), Ghaafir (40:24), Az-Zukhruf (43:49).  

 

Na ada hiyo ilikuwa pia ni ada ya makafiri wengineo wa awali kuwapachika sifa ovu Rusuli wao kama Anavyosema haya Allaah (سبحانه وتعالى)  katika Aayah hii:

 

كَذَٰلِكَ مَا أَتَى الَّذِينَ مِن قَبْلِهِم مِّن رَّسُولٍ إِلَّا قَالُوا سَاحِرٌ أَوْ مَجْنُونٌ ﴿٥٢﴾

“Ndio kama hivyo, hawakuwafikia wale wa kabla yao Rasuli yeyote isipokuwa walisema: Mchawi au majnuni.” [Adh-Dhaariyaat (51:52)]

 

Hali kadhaalika, Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) pia alipachikwa sifa ovu na washirikina wa Makkah. Rejea Al-Furqaan (25:4) kwenye uchambuzi wa sifa hizo na rejea zake mbalimbali.

 

[7]  Umuhimu Wa Kukumbushana Mambo Ya Dini:

 

Aayah hii ni kama Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):

 

فَذَكِّرْ إِن نَّفَعَتِ الذِّكْرَىٰ ﴿٩﴾ سَيَذَّكَّرُ مَن يَخْشَىٰ ﴿١٠﴾

 

“Basi kumbusha ikiwa unafaa ukumbusho. Atakumbuka yule anayeogopa.” [Al-A’laa (87:9-10]

 

Na Allaah (سبحانه وتعالى) Akasisitiza katika Aayah nyingi kukumbushana mambo ya Dini ikiwa ni pamoja na kuamrishana mema na kukatazana maovu. Rejea Aal-‘Imraan (3:104), (3:110) (3:114), At-Tawbah (9:71), (9:112).

 

Bonyeza pia viungo vifuatavyo:

 

023-Riyaadhw As-Swaalihiyn: Mlango Wa Kuamrisha Mema Na Kukataza Maovu

 

104-Aayah Na Mafunzo: Umuhimu Wa Kuamrisha Mema Na Kukataza Maovu

 

Na katika kiungo kifuatacho, kuna tahadharisho la daaiyah (mlinganiaji wa mambo ya Dini):

 

024-Riyaadhw Asw-Swaalihiyn: Mlango Wa Adhabu Kali Kwa Mwenye Kuamrisha Mema Au Kukataza Maovu Kisha Kauli Yake Ikawa Kinyume Na Matendo Yake

 

Na katika kiungo kifuatacho, kuna makala tele zenye maudhui mbalimbali za kukumbushana ambazo zitamsaidia Muislamu kuamrisha mema na kukataza maovu:

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun - لُؤْلُؤ مَّنثُور

 

Na kuna Hadiyth tele zinazotilia mkazo maudhui hii ya kukumbusha watu mambo ya Dini, kuamrisha mema na kukataza maovu. Na kazi hii, ni kazi ya Rusuli wote wa Allaah (سبحانه وتعالى) na imeisitizwa mno kwa Waumini, na fadhila zake ni nyingi na adhimu. Bonyeza kiungo kifuatacho:

 

Hadiyth: Fadhila Za 'Ilmu Na 'Ulamaa - أَحاديثُ عَنْ فَضْلِ الْعِلْم وَالْعُلَمَاء

 

[8] Kuwa Na Nguvu Ni Katika Sifa Za Allaah:

 

‘Aqiydah ya Ahlus-Sunnah wal-Jama’aah ni kuthibitisha Sifa za Allaah (سبحانه وتعالى)    kama zilivothibitishwa katika Qur-aan na Sunnah. Hivyo basi, Allaah (سبحانه وتعالى) Anaposema kuwa  Yeye ni Qawiyy (Mwenye Nguvu), sisi ni lazima tuamini kuwa Ana nguvu. Na Anaposema Kuwa Yeye Ana Qudra (Uwezo),  sisi ni lazima tuamini kuwa Anao Uwezo. Lakini Sifa hizo za Nguvu Zake, au Uwezo Wake, hazifanani kabisa na kiumbe chochote kile!

 

Rejea Huwd (11:37), Twaahaa (20:46).

 

Rejea pia Al-Baqarah (2:165), Al-Anfaal (8:52), Huwd (11:66), Al-Ahzaab (33:25), Ghaafir (40:22), Al-Hajj (22:40), (22:74).

 

 

 

Share