090 - Al-Balad

 

الْبَلَد

 

090-Al-Balad

 

090-Al-Balad: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

لَا أُقْسِمُ بِهَـٰذَا الْبَلَدِ ﴿١﴾

1. Naapa kwa mji huu (wa Makkah).[1]

 

 

 

وَأَنتَ حِلٌّ بِهَـٰذَا الْبَلَدِ ﴿٢﴾

2. Nawe (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) umehalalishiwa ufanye utakavyo katika mji huu (kuua au kusamehe).

 

 

 

وَوَالِدٍ وَمَا وَلَدَ ﴿٣﴾

3. Na Naapa kwa mwenye kuzaa (Aadam) na aliowazaa (wanaadam).

 

 

 

لَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ فِي كَبَدٍ ﴿٤﴾

4. Kwa yakini Tumemuumba binaadam katika tabu na mashaka ya kuendelea.

 

 

 

أَيَحْسَبُ أَن لَّن يَقْدِرَ عَلَيْهِ أَحَدٌ ﴿٥﴾

5. Je, anadhani kwamba hakuna yeyote atakayemweza?

 

 

 

يَقُولُ أَهْلَكْتُ مَالًا لُّبَدًا ﴿٦﴾

6. Anasema: Nimeangamiza mali tele.

 

 

 

أَيَحْسَبُ أَن لَّمْ يَرَهُ أَحَدٌ ﴿٧﴾

7. Anadhani kwamba hakuna yeyote anayemuona?

 

 

 

أَلَمْ نَجْعَل لَّهُ عَيْنَيْنِ ﴿٨﴾

8. Je, kwani Hatukumpa macho mawili?

 

 

 

وَلِسَانًا وَشَفَتَيْنِ ﴿٩﴾

9. Na ulimi na midomo miwili?

 

 

 

وَهَدَيْنَاهُ النَّجْدَيْنِ ﴿١٠﴾

10. Na Tukambainishia njia mbili (ya haki na upotofu)?[2]

 

 

 

فَلَا اقْتَحَمَ الْعَقَبَةَ ﴿١١﴾

11. Basi hakujiingiza kwa juhudi njia ya tabu na mashaka. 

 

 

 

وَمَا أَدْرَاكَ مَا الْعَقَبَةُ ﴿١٢﴾

12. Na nini kitakachokujulisha nini hiyo njia ya tabu na mashaka?

 

 

 

 

فَكُّ رَقَبَةٍ ﴿١٣﴾

13. Ni kuacha huru mtumwa.[3]

 

 

 

أَوْ إِطْعَامٌ فِي يَوْمٍ ذِي مَسْغَبَةٍ ﴿١٤﴾

14. Au kulisha katika siku ya ukame.[4]

 

 

 

يَتِيمًا ذَا مَقْرَبَةٍ ﴿١٥﴾

15. Yatima aliye jamaa wa karibu.[5]

 

 

 

أَوْ مِسْكِينًا ذَا مَتْرَبَةٍ ﴿١٦﴾

16. Au maskini aliye hohehahe.

 

 

 

ثُمَّ كَانَ مِنَ الَّذِينَ آمَنُوا وَتَوَاصَوْا بِالصَّبْرِ وَتَوَاصَوْا بِالْمَرْحَمَةِ ﴿١٧﴾

17. Kisha akawa miongoni mwa wale walioamini, na wakausiana kusubiri na wakausiana huruma.

 

 

 

أُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ الْمَيْمَنَةِ ﴿١٨﴾

18. Hao ndio watu wa kuliani.

 

 

 

وَالَّذِينَ كَفَرُوا بِآيَاتِنَا هُمْ أَصْحَابُ الْمَشْأَمَةِ ﴿١٩﴾

19. Na wale waliokufuru Aayaat (na Ishara, Dalili) Zetu wao ndio watu wa kushotoni.

 

 

 

عَلَيْهِمْ نَارٌ مُّؤْصَدَةٌ ﴿٢٠﴾

20. Juu yao ni moto uliofungiwa kila upande.

 

 

 

 

[1] Utukufu Wa Makkah Na Fadhila Zake:

 

Utukufu wa Makkah na fadhila zake zmetajwa katika Aayah kadhaa. Miongoni mwa Kauli Zake Allaah (سبحانه وتعالى) ni:

 

إِنَّ أَوَّلَ بَيْتٍ وُضِعَ لِلنَّاسِ لَلَّذِي بِبَكَّةَ مُبَارَكًا وَهُدًى لِّلْعَالَمِينَ ﴿٩٦﴾ 

Hakika nyumba ya awali iliyowekwa kwa ajili ya watu (kufanya ‘ibaadah) ni ile ambayo iko Bakkah (Makkah), yenye barakah na mwongozo kwa walimwengu. [Aal-'Imraan (3:96)]

 

Na pia:

 

وَضَرَبَ اللَّـهُ مَثَلًا قَرْيَةً كَانَتْ آمِنَةً مُّطْمَئِنَّةً يَأْتِيهَا رِزْقُهَا رَغَدًا مِّن كُلِّ مَكَانٍ فَكَفَرَتْ بِأَنْعُمِ اللَّـهِ فَأَذَاقَهَا اللَّـهُ لِبَاسَ الْجُوعِ وَالْخَوْفِ بِمَا كَانُوا يَصْنَعُونَ﴿١١٢﴾

Na Allaah Amepiga mfano wa mji (wa Makkah) uliokuwa katika amani na utulivu, inaufikia riziki yake maridhawa kutoka kila mahali, kisha ukakufuru Neema za Allaah. Basi Allaah Akauonjesha funiko la njaa na khofu kwa sababu ya yale waliyokuwa wakitenda. [An-Nahl (16:112)]

 

Rejea Al-An’aam (6:92) kwenye Fadhila za mji wa Makkah (Ummul-Quraa).

 

Bonyeza viungo vifuatavyo kupata faida nyenginezo:

 

02- Historia Fupi Ya Makkah Na Kuhusu Hajj Na 'Umrah

 

05-Buluwgh Al-Maraam: Kitabu Cha Hajj: Mlango Wa Sifa Za Hijjah Na Kuingia Makkah

 

096-Aayah Na Mafunzo: Masjid Al-Haraam Ni Ya Kwanza Kuanzishwa Duniani

 

[2] Njia Ya Hidaaya Na Ya Upotofu:

 

Rejea Al-Insaan (76:3) kwenye faida.

 

[3] Fadhila Za Kuacha Huru Mtumwa:

 

Hadiyth ifuatayo imetaja fadhila mojawapo ambayo ni kuepushwa mtu na moto kwa kila kiungo kimoja cha mtumwa:

 

عَنْ أَبِي، هُرَيْرَةَ عَنِ النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم قَالَ ‏ "‏ مَنْ أَعْتَقَ رَقَبَةً مُؤْمِنَةً أَعْتَقَ اللَّهُ بِكُلِّ إِرْبٍ مِنْهَا إِرْبًا مِنْهُ مِنَ النَّارِ ‏"

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Yeyote atakayemwacha huru mtumwa Muislamu, Allaah Atakiokoa na moto kila kiungo chake sambamba na kila kiungo cha mtumwa.” [Muslim]

 

Bonyeza pia viungo vifuatavyo kupata faida tele nyenginezo:

 

03-Riyaadhw Asw-Swaalihiyn: Mlango Wa Fadhila za Kuacha Huru Watumwa

 

15-Buluwgh Al-Maraam: Kitabu Cha Ukombozi - كِتَابُ اَلْعِتْقِ

52-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Kuacha huru mtumwa, kutoa sadaka na kuhiji humnufaisha Muislamu

 

[4] Himizo La Kulisha Mafaqiri, Masikini Na Wahitaji:

 

Rejea Al-Insaan (76:8) kwenye faida tele. Na pia rejea Al-Qalam (68:17) kwenye kisa cha watu wa shamba waliozuia mafuqara na masikini wasipate swadaqa ya mazao ya shamba la baba yao baada ya kufariki kwake. Na pia kisa katika Hadiyth, cha mtu aliyekuwa akitoa swadaqa mazao yake, na faida nyenginezo.

 

[5] Himizo La Kulea Yatima Na Fadhila Zake Na Maonyo Ya Kula Mali Zao:

 

Kumlea, kumkirimu na kumfanyia ihsaan yatima kuna fadhila tele. Na yatima aliye na uhusiano wa damu kuna fadhila mara mbili kama alivyotafsiri Imaam Ibn Kathiyr kwa kutaja Hadiyth ifuatayo:

 

 عن سلمان بن عامر رضي الله عَنْهُ ، عن النَّبيّ صلى الله عليه وسلم: (( الصَّدَقَةُ عَلَى المِسكينِ صَدَقةٌ ، وعَلَى ذِي الرَّحِمِ ثِنْتَانِ : صَدَقَةٌ وَصِلَةٌ )) رواه الترمذي ، وَقالَ : (( حديث حسن )) .

Amesimulia Salmaan bin 'Aamir (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: "Swadaqa kwa maskini ni swadaqa, na kumpa jamaa ina ujira mara mbili: Ni swadaqa na kuunga ujamaa." [At-Tirmidhiy, na akasema Hadiyth Hasan]

 

Rejea Al-Fajr (89:17) kwenye maelezo na faida kuhusu Amri Na Himizo La Kuwakirimu  Yatima Na Fadhila Zake.

 

 

 

Share