Nampenda Lakini Nashindwa Kumwambia

SWALI:

nimewahi kutuma swali langu illa kwa uwezo wa Allaah sijajibiwa: nikwamba mimi ni mwana mama ambae nimempenda mwanaume ila nimeshindwa kumwambia nae amemtaliki mkewe na mi piya mume amenitaliki sasa ninamfaham kwa tabia njema bwana huyo na nimempenda sasa nifanyeje kwa ajili ya Allaah maa salam.

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani dada yetu kwa swali lako hilo zuri. Suala hili tayari tumelijibu kwa kitambo sasa au ikiwa si hilo basi limefanana. Tofauti ya hili na lile la awali ni kubadilishwa ibara tu. Hakika ni tatizo kubwa kuwa wavulana hawataki kuoa na wasichana nao siku hizi hawataki kuolewa. Hivyo, inakuwa ili kutekeleza uchu wa kimaumbile huwa wavulana na wasichana wanafanya urafiki na kutekeleza hilo kupitia kwa zinaa ambao ni haramu.

Tufahamu kuwa ndoa ni jambo muhimu sana na ni njia ya kutekeleza tendo la kimapenzi kwa njia ya halali pamoja na kufuata kanuni za kimaumbile na zile za sharia. Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatuambia: “Mimi naswali na ninalala, ninafunga na kula na nimeoa wanawake. Yeyote atakayekengeuka (kuipa mgongo) Sunnah yangu si katika mimi” (al-Bukhaariy na Muslim).

Wazazi wa wasichana wengi au wasichana wenyewe wanaona haya sana kuweza kumposa mvulana ambaye anaona kuwa atamfaa. Hili si jambo geni kwani tunapata binti ya yule mzee mcha Mungu alipomshauri babake kuhusiana na Nabii Muusa (‘Alayhis Salaam). Qur-aan inasema: “Akasema mmoja wa wale wawili: ‘Ewe baba yangu! Mkodi huyu, bila shaka mbora uwezaye kumwajiri ni mwenye nguvu, mwaminifu’. Akasema: ‘Mimi nataka nikuoze mmojawapo kati ya binti zangu hawa wawili kwa kunitumikia miaka minane” (28: 26 – 27).

Si mfano huo tu bali Siyrah ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) inatupatia mwongozo mzuri katika hilo. Hapa tunampata mama wa waumini Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha) ambaye alimtuma rafiki yake wa kike amuulize Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anaonaje ikiwa atamuoa yeye kwani yeye yuko tayari. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) naye hakusita bali alikubali kufunga naye Nikaah.

Pia tunapata kisa cha ‘Umar bin al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye baada ya binti yake, Hafswa (Radhiya Allaahu ‘anha) kumaliza eda alianza kumtafutia mume kwa kwenda kwa Abu Bakr na ‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘anhuma) ili wamuoe binti yake.

Kwa hiyo, hilo ni jambo ambalo lipo.

Ama kuhusu kadhiya yako pia unaweza kufanya hivyo hivyo kwa kumtuma mtu mwaminifu aende amuelezee ile raghba yako ya kuwa unataka akuoe. Lakini chukua tahadhari kwa kutazama zile sifa za mume wa Kiislamu anazo ili usije ukajiingiza katika shimo. Chukua wakati kwa kuulizia kuhusu tabia zake, Dini yake, maadili yake na matendo yake. Tumia watu mbali mbali wakuletee maalumati hayo kuhusu huyo kijana. Ikiwa utaridhika na Dini na maadili yake basi swali Swalatul Istikhaarah kumtaka Allaah Aliyetukuka ushauri kuhusu hilo. Ikiwa mambo yote yapo sawa wakati huo utamtuma mtu ili amuulize kama atakuwa tayari kumuoa. Ikiwa atajibu ndio aje nyumbani kwenu kukuposa rasmi na hapo ndoa ifungwe.

Soma kuhusu Swalah ya Istikhaarah katika viungo vifuatavyo:

Muda Wa Swalah ya Istikhaarah

Kwa Nini Tuswali Istikhaarah Na Iswaliwe Kwa Ajili Ya Nini?

Tunakutakia tawfiki katika hilo.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share