Mwanamke Kupaka Dawa Ya Nywele

 

Mwanamke  Kupaka Dawa Ya Nywele  

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Asalam Aleykum.

 

Mie nilikuwa nauliza jee? Mwanamke wa Kiislam aliyeolewa au hata kama hayaolewa kupaka dawa kwa ajili ya kumpambia mumewe inafaa?

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Ni wajibu kwa mwanamke wa Kiislamu ambaye ameolewa kumpambia mumewe na pia mume kumpambia mkewe ili kila mmoja ajitayarishe kwa mwenziwe. Ikiwa mwanamke ameolewa au hajaolewa anaweza kujipamba akiwa ndani ya nyumba na pambo hilo litaonekana na maharimu zake pekee. Allah Anasema:

 

وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا ۖ وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَىٰ جُيُوبِهِنَّ ۖ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا لِبُعُولَتِهِنَّ أَوْ آبَائِهِنَّ أَوْ آبَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ أَبْنَائِهِنَّ ...

Wala wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa yale yanayodhihirika. Na waangushe khimaar (shungi) zao mpaka vifuani mwao, na wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa kwa waume zao, au baba zao, au baba za waume wao, au wana wao.... [An-Nuwr: 31].

 

 

Pambo la mwanamke linajumlisha sehemu zake za kimaumbile kama uso, nywele na sehemu nyingine za kuvutia za mwili wake na nyongeza za uzuri wa bandia kama nguo, vito vya thamani, vipodozi na mfano wake. Haifai kwa mwanamke yeyote Muislamu kutoka nyumbani kwake akiwa amejipaka vipodozi au manukato.

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametutaka sisi tuzikirimu nywele zetu kwa kuzitazama vyema, kuzipaka mafuta na hata kuzitia hinna na katm (mmea kutoka Yemen). 

 

 

Dawa za nywele kwa maana kuwa ni mafuta ya kulainisha nywele, zinaweza kutumiwa ikiwa zitabaki katika misingi ya Uislamu, miongoni mwayo ni:

 

1.   Isiwe ni yenye kumdhuru mwenye kutumia: Chochote chenye madhara mengi kuliko manufaa kwa mwanadamu kinakuwa ni haramu. Allah Anasema:

 

يَسْأَلُونَكَ عَنِ الْخَمْرِ وَالْمَيْسِرِ ۖ قُلْ فِيهِمَا إِثْمٌ كَبِيرٌ وَمَنَافِعُ لِلنَّاسِ وَإِثْمُهُمَا أَكْبَرُ مِن نَّفْعِهِمَا ۗ 

Wanakuuliza kuhusu pombe na kamari. Sema: Katika viwili hivyo mna dhambi kubwa na (baadhi ya) manufaa kwa watu. Na dhambi yake viwili hivyo ni kubwa kuliko manufaa yake.[Al-Baqarah: 219].

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Haifai kudhuru wala kulipana madhara" [Ibn Maajah na ad-Daaraqutniy].

 

2.    Ikiwa zitamlazimu kutotia maji kichwani, hivyo hutaweza kutawadha wala kuoga na Swalah zitakuwa ni zenye kukupita au kupoteza muda mwingi kuwa katika saloon ili kutiwa hizo dawa badala ya kutekeleza mambo muhimu. Pia jambo hili litakufanya kutoweza kutekeleza haki zako kama mke kwa mume ambayo ni ‘Ibadah na thawabu kubwa.

 

3.    Wanawake wengine wenye kutia madawa ya nywele huwakatalia wanaume zao unyumba kwa kuogopa kwenda kuoga janaba na hivyo nywele zake kupata maji na kuua nguvu za yale madawa na hivyo hali ya nywele kurudia ugumu wake au uasili wake wa mwanzo. Hili ni jambo ovu kabisa na linapelekea katika madhambi kwa mwanamke wa namna hiyo.

 

 

Na ifahamike kuwa mambo ya mapambo ya nywele ambayo yamekatazwa kabisa na sheria ya Kiislamu. Mfano wake ni kukata au kukatwa nyusi kwani katika hili Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amemlaani mwenye kukata na mwenye kukatwa.

 

"Allah Amemlaani mwanamke anayefanya tatoo (chanjo za kujichora) Na mwenye kuomba kufanyiwa, na anayetoa nyusi na mwenye kuomba kutolewa na anayechonga meno kuweka nafasi (mwanya), kubadilisha maumbile ya Allaah kwa ajili ya kupata uzuri". [Al-Bukhaariy Imetoka kwa 'Abdullah Ibn Mas'uud (Radhwiya Allaahu 'anhu)]

 

 

Na pia Uislamu umekataza mtu kuvaa wigi au kuongeza vipande vya nywele ikiwa ni za kwake au za mtu mwingine au ni za bandia. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amewalaani wanawake wenye kazi ya kuunganisha (kutia) watu wigi (au vipande vya nywele) na wanawake wenye kuungiwa hizo nywele.

 

"Mwanamke wa Ki-Answaar aliyemuozesha binti yake ambaye nywele zake zilianza kung'ooka.  Mwanamke huyo wa Ki-Answaar alikuja kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)  na kumtajia kwamba: "Mumewe (mume wa mwanangu) ameona kwamba nimwachie avae nywele za bandia" Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema, "Usifanye hivyo kwani Allah Huteremsha laana Yake kwa  wanawake kama hao wanaoongeza nywele za bandia"   [Al-Bukhariy 7:133  kutoka kwa Bibi 'Aisha (Radhwiya Allaahu 'anha)]

 

 

Kwa hiyo  ieleweke kuwa mambo haya yakifanywa na wanaume uovu unakuwa mkubwa zaidi na ni madhambi makubwa.

 

 

Tanbihi:

Hapa hatuzungumzii kuchoma nywele na kupaka mkorogo. Hayo hayana mashaka kuwa ni haraam na hayafai kabisa.

Wala haifai kujipaka mafuta ya mwili ya kujichubua. Yote hayo ni madhara na kubadilisha maumbile.

 

 

Kwa dada zetu wenye kutumia madawa haya wahakikishe hawaonyeshi nywele zao kwa wasio Maharimu zao, kwani wengi wenye kubadilisha nywele zao huwa wanataka waonekane na wanaume wasiowahusu ambao wanaweza kuwaoa na matokeo yake ni kufungua milango ya zinaa. Pia tuwe na tahadhari kwani madawa mengi yana madhara kwa nywele, kichwa na ngozi kwa sababu ya kemikali kali zilizomo ndani yake. Ikiwa kunapatikana dawa za kiasili haswa zile ambazo zinatoka nchi za Kiarabu kama Yemen au nchi nyingine kama Pakistan ambazo hazikuongezwa kemikali, basi ni bora zaidi kutumia hizo kuliko hizi za viwandani. Na kwa sasa dawa hizo zinapatika kwa wingi katika nchi tofauti.

 

Tukumbuke kuwa wanazuoni wengine wamekataa katu kata wanawake kubadilisha nywele zao kwani huko ni kubadilisha maumbile ambayo ameumbiwa na Muumba. Na kwa upande mwengine hii ndio rai yenye usalama zaidi kutokana na matatizo ambayo tumeyataja hapo juu yanayotokana na madhara ya madawa hayo, na pia vishawishi vinavyotokana na mabadiliko hayo kuwafanya wanawake wengine kuonyesha wanaume wasio Maharimu zao, na pia matatizo ya wanawake wengine kuwanyima waume zao unyumba kwa kuchelea kuoga na kuharibu nywele zao.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share