Kwa Nini Wanaume Wamepewa Cheo/Fadhila/Mamlaka Zaidi Kuliko Wanawake?

SWALI:

 

Assalamu alayum warahmatu llahi taala wabarakatu. Naomba kuuliza maSWALI: ambayo yananiumiza kichwa changu na kila ninaemuuliza naona sijafaidika bado na majibu ninayoyapata. Kwa nini mwanamme ana cheo kikubwa kuliko mwanamke katika uislam wakati mwanamke ana kazi kubwa kuliko mwanamme? Mwanamke anazaa, anashughulikia nyumba na watoto, anamshughulikia mume kama mtoto mchanga, mwanamke ni mtu mwenye kazi masaa ishirini na nne hapumziki, mwanamme kazi anayoifanya ni kutafuta kijio. Lakini tunaambiwa kwamba kama kuna kusujudu baada ya M Mungu tungeambiwa tusujudie waume zetu, na mirathi wao wamepewa mingi kuliko wanawake, lazima ukitoka uage wao si lazima, wao wamepewa uwezo wa kuoa mke mwengine, wamepewa uwezo wa kutoa talaka, na mambo mengi ambayo mwanamke hakupewa, swali langu liko hapo.

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mwanamme kupewa cheo zaidi kuliko mwanamke.

 

Hakika hili ni suala ambalo linaonekana hivyo na watu hasa kwa ajili ya kasumba ambazo zinatiwa na wasiokuwa Waislamu wasiouelewa Uislamu na haki inayompatia kila mmoja.

 

Awali ya yote inatakiwa tufahamu kuwa aliyempatia haki kila mmoja wetu ni Allaah Mtukufu ambaye Anamjua kila mmoja wetu na kila analostahiki. Hakika ukichambua haki zilizoko kwa kila mmoja wetu utakuta kuwa mwanamke amepatiwa haki zaidi na Uislamu kuliko mwanamme. Tutajaribu katika jibu letu kuangazia yote yaliyoulizwa na ndugu yetu.

 

Kabla ya kuendelea na kuangazia haki na wajibu wa mwanamke na fadhila zake, tuangalie mwanamke alivyokuwa akifanywa kabla ya kukamilishwa Uislamu kwa kuja kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kwa mfano:

 

1.    Katika Bara Arabu mwanamke alikuwa hana hadhi, akiuliwa pindi anapozaliwa (an-Nahl [16]: 58 – 59), kurithiwa na hata watoto wake wa kambo pindi alipokuwa mumewe, kunyimwa urithi kabisa na mengineo mengi.

 

2.   Mwanamke katika ustaarabu wa Kigiriki alikuwa ni chombo cha kuondolea matamanio ya kiwiliwili cha mwanamme; hivyo alikuwa akiuzwa kama machungwa sokoni. Socrates alisema: “Mwanamke ni chanzo cha machafuko yote duniani, yeye ni kama mti wa dafali ambao sura ya nje ni ya kuvutia mno lakini iwapo ndege ataula basi ni wazi atakufa”

 

.

3.   Ama mwanamke katika Ukristo hana thamani kabisa.  Kulingana na Biblia, mwanamke hana utukufu kwa sababu ameumbwa kwa ajili ya mwanamme (1 Wakorintho 11: 7 – 10). Vile vile yeye ni najisi (Ayubu 14: 1 – 4), ndiye asili ya dhambi (Mwanzo 3: 12) na kadhalika.

 

 

4.    Mwanamke katika Ubaniyani alikuwa akichomwa hadi kufa na mumewe iwapo mume atakufa kabla yake na kutokuwa na uhuru kabisa wa aina yoyote.

 

 

5.   Mwanamke wa Kirumi alikuwa ni pambo kwa mwanamme na kwa kuwafurahisha wafalme alikuwa anaimbishwa akiwa uchi. Na tabia hii ya kishenzi imebakia hadi leo.

 

 

6.    Mwanamke wa Kichina alikuwa hana haki yoyote katika jamii, na mumewe alikuwa ana haki ya kuuza mwili wa mkewe kwa wanaume wengine. Naye alirithiwa kama mali na jamaa za mumewe pindi anapoaga dunia.

 

 

7.   Ama mwanamke wa kisasa katika tamaduni mbali mbali amekuwa ni chombo cha kuridhisha wanaume kwa njia moja au nyingine. Hakuna bidhaa yoyote inayouzwa bila kuonyesha mwanamke kwenye matangazo.

 

Tukija katika Uislamu Allaah Aliyetukuka Amempatia kila mmoja kati ya mwanamme na mwanamke majukumu, haki na wajibu wake kulingana na maumbile yake. Hata hivyo, mwanamme amepatiwa daraja ya juu kuliko mwanamke. Anasema Aliyetukuka:

Wanaume ni walinzi wa wanawake; kwa sababu Allaah Amewafadhilisha baadhi yao kuliko wengine, na kwa sababu ya mali zao wanazozitoa” (an-Nisaa’ [4]: 34).

 

 

Ama majukumu yao yanakuwa ni wenye kusaidiana ili kuleta mabadilko mazuri katika jamii. Utapata kwa suala lingine mwanamke yuko juu ya mwanamme na kwa jambo jingine ni mwanamme mwenye jukumu kubwa zaidi.

 

Uislamu umetangaza kabisa kuwa asili ya mwanamke na mwanamme ni moja:

Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi ambaye Amekuumbeni kutokana na nafsi (asili) moja. Na Akamuumba mkewe kutoka katika nafsi ile ile. Na Akaeneza kutokana na wawili hao wanaume na wanawake wengi” (an-Nisaa’ [4]: 1).

Na Mtume (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

Hakika wanawake ni ndugu wa wanaume” (Abu Daawuud na at-Tirmidhiy).

 

Ama katika Uislamu hakuna kosa la asili ambalo analaumiwa mwanamke bali wote wanalaumiwa kwa kushawishiwa na Shaytwaan:

Lakini Shaytwaan aliwatelezesha wote wawili na akawatoa katika hali waliyokuwa nayo” (al-Baqarah [2]: 36).

Na pia:

Wakasema: Mola wetu! Tumedhulumu nafsi zetu, na kama Hutatusamehe, bila shaka tutakuwa miongoni mwa wenye hasara” (al-A‘raaf [7]: 23).

Hivyo, wote walikosa na wakasamehewa, kwa hiyo kutokuwa na makosa baada ya hapo.

 

Mwanamme na mwanamke wapo sawa katika malipo lau mmoja wao atatenda mema. Anasema Aliyetukuka:

Na mwenye kutenda mema akiwa mwanamme au mwanamke naye ni Muumini, basi hao wataingia Peponi wakiruzukiwa bila hesabu” (al-Ghaafir [40]: 40).

Na pia,

Hakika Mimi sipotezi juhudi ya mfanya juhudi miongoni mwenu akiwa mwanamme au mwanamke” (aal-‘Imraan [3]: 195).

Pia waweza kutazama kuhusu haya katika Suratun Nahl: 97 na pia Suratul Ahzaab: 35.

 

Na mwenye kufanya uhalifu ima wa kuiba au kuzini, akiwa mwanamke au mwanamme atapata adhabu hiyo hiyo. Tazama adhabu ya wizi katika Suratul al-Maa’idah: 38 na uzinzi katika Suratun Nuur: 2.

 

Pia Uislamu umempatia kila mmoja wao usawa wa kiuchumi na kumiliki mali, kufanya biashara baina ya jinsia hizo mbili. Allaah Aliyetukuka Anasema:

Na wala msitamani vile ambavyo Allaah Amewafadhilisha baadhi yenu kuliko wengine. Wanaume wanayo sehemu (haki kamili) ya walivyo vichuma na wanawake pia wanayo sehemu (haki kamili) ya vile walivyo vichuma” (an-Nasaa’ [4]: 32).

Na kwa ajili hii tunaona vipi wanawake katika enzi tofauti waliweza kuusaidia Uislamu na Waislamu kwa pesa zao, mfano mmoja ni Mama wa Waumini Khadijah (Radhiya Allaahu ‘anha).

 

Mwanamke naye ana haki sawa katika kurithi kile ambacho kimeachwa na jamaa wa karibu. Kwa hilo, Allaah Aliyetukuka Anasema: “Wanaume wana sehemu katika mali wanayoacha wazazi na jamaa wakaribu. Na wanawake pia wana sehemu katika yale waliyoacha wazazi na jamaa wa karibu” (an-Nisaa’ [4]: 7).

Hata hivyo, Uislamu umempatia mwanamme sehemu mbili kwa moja anayopata mwanamke. Huenda hilo likaonekana ni dhuluma kwa mwanamke, lakini tukiona hekima kwa mgao huo tunaweza kugundua kuwa pengine mwanamme amepata sehemu ndogo zaidi kwa mgao huo. Kwa muhtasari mwanamme amepatiwa sehemu kubwa zaidi katika urithi kuliko mwanamke katika shari’ah ya Kiislamu. Na hiyo ni kwa sababu zifuatazo:

 

1. Mwanamme amelazimishwa kutoa mahitaji kwa mkewe, wanawe, jamaa zake wa karibu, tofauti na mwanamke ambaye hakukalifishwa kishari’ah kutoa mahitaji yoyote. Kwa hiyo, mali anayopata mwanamme inatumika kwa watu wengi ilhali ya mkewe itakuwa ni yake anaweza kuweka akiba, wala hatolazimika kutoa senti moja katika mali aliyorithi kwa ajili ya watu wengine.

 

 

2.  Mwanamme anawajibika kutoa mahari kumpa mwanamke wakati akioa ilhali mwanamke yeye hatoi mahari bali ndiye anayepatiwa mahari tena anayotaka yeye.

 

3.  Wajibu wa kuwaelimisha watoto, kuwatibu wenye kumtegemea na kuwatunza ni wa mume. Kwa hivyo, urithi wake wote utatumika kwa mambo kama hayo, ilhali urithi wa mwanamke ni wake naye hana wajibu kama huo.

 

Labda tuchukue mfano wa mzazi aliyekufa akaacha mvulana na msichana na akiwa amebakisha 30,000. Kwa mgao wa Kiislamu ikiwa hakuna mrithi mwengine, mvulana atapata 20,000 na msichana 10,000. Na endapo wote wawili wamefikisha umri wa kuoa na kuolewa, na kila mmoja atalipa au kulipwa elfu kumi (10,000). Kwa minajili hiyo, mvulana atatoa 10,000 na kubakisha 10,000, ilhali msichana akipata 10,000 atakuwa na pesa taslimu 20,000. Hizi pesa za msichana ni zake na anaweza kuzitumia kwa njia yoyote atakayo ilhali mvulana pesa alizobaki nazo itabidi azitumie kumtazama mkewe na watoto atakaporuzukiwa. Msichana hata akizaa jukumu la kumtazama yeye pamoja na mtoto/ watoto ni la mumewe. Na lau ikitokea sinto fahamu (su-u tafaahum) baina ya mume na mkewe, na kutokea talaka msichana huyo atarudi kwa kaka yake na ni jukumu la kaka kumtazama katika hali zote zile.

 

Pia Uislamu umeweka nidhamu kuwa wazazi wanatakiwa wawalee watoto wote bila ya kuwabagua kati yao kulingana na jinsia zao. Allaah Aliyetukuka Anatuambia:

Enyi Mlioamini! Jiokoeni nafsi na jamaa zenu na moto ambao kuni zake ni watu na mawe” (at-Tahriym [66]: 6).

Na Mtume wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mwenye watoto wa kike watatu au dada watatu au watoto wa kike wawili au dada wawili akawalea vyema na akamcha Allaah kwa ajili yao basi atapata Pepo” (at-Tirmidhiy).

Na hivyo, hapa tunapata msisitizo wa umuhimu wa kuwalea watoto wa kike kwa wema na njia nzuri.

 

Uislamu umempatia haki mwanamke kwa kumuelimisha sawa na mwanamme na umesisitiza sana kupewa elimu wanawake tangu awali ya risala yake kupitia kwa Mtume wa mwisho (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Allaah Aliyetukuka Ametujulisha kwamba wenye kumuogopa yeye kikweli ni watu wenye elimu bila kubagua jinsia,

Na kwa hakika wanaomuogopa Allaah katika viumbe Vyake ni wenye elimu” (al-Faatwir [35]: 28).

 

Pia jinsia zote mbili zina jukumu la kuamrisha mema na kukataza maovu. Hiyo ni kama Alivyosema Aliyetukuka:

Na Waumini wanaume na Waumini wanawake ni marafiki wao kwa wao. Huamrisha yaliyo mema na kuyakataza maovu” (at-Tawbah [9]: 71).

 

Inatakiwa tufahamu kuwa kila mmoja – kati ya mwanamme na mwanamke ni mchungaji na ana jukumu kila mmoja katika Nyanja yake katika maisha. Mume na mke wanatakiwa wasaidiane katika kutengeneza jamii kwa njia iliyo nzuri zaidi.

 

Yapo majukumu mengine ambayo yanampasa mwanamme peke yake, miongoni mwayo ni kuitazama nyumba yake na pia kuipigania Dini ya Allaah Aliyetukuka. Mwanamke hapaswi kuitazama nyumba ila tu anapotaka kumsaidia mumewe na hiyo itakuwa ni ihsani kwa upande wake. Ama Jihadi wanawake, hawana uwajibu wa kutekeleza hilo. Na kwa ajili ya kutazama nyumba zao, wakati mmoja wanawake walimtuma msemaji wao, Asmaa’ bint Yaziyd as-Sakan (Radhiya Allaahu ‘anha) alikuwa kwa Mtume (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa yupo pamoja na Maswahaba zake, ambaye alisema: “Ewe Mtume wa Allaah! Umetumwa kwa wanawake na wanaume, nasi tumekuamini. Hata hivyo, wanaume wanapata fadhila zote kwani wao wanahudhuria Swalah pamoja nawe, wanapata kujifunza kwako na wanapigana katika njia ya Allaah ilhali sisi twawatazama watoto wao wakiwa hapo. Je, nasi tutapata nini?” Akasema: “Kukaa kwenu nyumbani mnashirikiana nao katika thawabu”.

 

Uislamu umetambua kazi kubwa ya mwanamke, hasa katika kubeba mimba, kuzaa na kumlea mtoto na kwa ajili hiyo, Allaah Aliyetukuka Anasema:

Na Tumemuusia mwanaadamu wazazi wake – mama yake ameichukua mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu, na kumnyonyesha na kumuachisha kunyonyesha katika miaka miwili – ya kwamba Unishukuru Mimi na wazazi wako” (Luqmaan [31]: 14).

 

Na Mtume wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa: “Ni nani aliye na haki wa usuhuba wangu?” Akasema: “Mama”. Kisha nani? Akasema: Mama. Kisha nani? Akasema: Mama. Kisha nani? Akasema: Baba” (al-Bukhaariy na Muslim).

 

Na Mtume wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametoa dhamana kwa mwanamke ambaye ataswali Swalah zake tano, kufunga mwezi wa Ramadhaan na kumtii mumewe kuwa ataingia Peponi kwa mlango wowote atakao.

 

Ama kuhusu talaka ameachiwa mume kwa sababu yeye ni mvumilivu zaidi na anaweza kuzuia hasira zake kwa wakati ambao alikuwa afanye jambo ambalo litaleta hasara katika jamii. Mara nyingi mwanamke hisia zake zinakwenda na yale mabadiliko ambayo anakabiliana nayo katika maisha yake na mwilini mwake mabadiliko ambayo mwanamme hana kwa kiasi cha mwanamke. Mwanamke ni mwepesi wa kuchukua hatua za haraka kisha kujuta baadaye mbali kabisa na mwanamme. Bila shaka, mwanamke pia amepatiwa aina mbili za talaka – Khul’ (kujitoa na kujivua katika ndoa) na pia kupitia kwa Qaadhi ikiwa mume ana makosa.

 

Ukitazama katika haya tuliyoyaeleza utakuta kuwa mwanamke amepatiwa fadhila kubwa na Uislamu kwa yale majukumu wafanyao na kazi zao nzuri.

 

Tunatumai majibu haya yataondosha shaka shaka ulizokuwa nazo na ambazo zinachangiwa sana na makafiri na wale Waislamu haswa wanawake wanaodai kupigania haki za wanawake wanaotumiwa na makafiri.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share