Sifanani Na Baba Yangu Je ni Mtoto Wa Haraam?

 

Sifanani Na Baba Yangu Je ni Mtoto Wa Haraam?

 

www.alhidaaya.com

 

 

SWALI: 

 

 

Salam aleykum  mimi na baba yangu hatufanani kwa sura wala rangi yani  wengi wamekuwa wakisema kuwa si baba yangu tokea kwa siri hadi dhahiri je nifanyeje ili kujua ukweli katu siwezi kumuliza mama juu ya hilo kwani kwa mila zetu ni utovu wa adabu tafadhali nisaidie. 

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho 

 

Kwanza kabisa inapasa kufahamika kuwa hakuna mtoto haraam kwa kuwa ki Shariy’ah mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa si mwana haraam,  bali kitendo ndicho kilicho cha haraam. Na mtoto hana makosa kabisa mbele ya Shariy’ah na anapokuwa mkubwa na akawa mwema basi wema wake utamuingiza yeye Jannah (Peponi).

 

 

Kutofanana na mzazi si suala geni kwani liliwahi kutokea pia wakati wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba     alikuja Bedui kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumwambia: "Ee Rasuli wa Allaah! Mke wangu amezaa mtoto mweusi sana …" [Al-Bukhaariy, Muslim]

Mume na mke hawakuwa rangi hiyo, hivyo alikuwa na shaka akilini mwake. Hii ilikuwa ni kumjulisha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa yule mtoto si wake. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimchukulia kwa akili yake na mifano ambayo anaweza kuifahamu vyema kabisa. Akamuuliza: "Je, una ngamia?" Yule bwana Akajibu: “Naam.” Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: "Je, rangi zao ni zipi?" Akasema: "Nyekundu". Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: "Je, wapo walio rangi ya hudhurungi?" Bedui Akajibu: “Naam.” ndio. Hapo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)   akamuuliza: "Hii rangi imetoka wapi?" Yule mtu akasema: "Huenda ameirithi." Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: "Huyu pia huenda akawa ameirithi." [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

Hivi sasa tunaelewa kuwa kufanana huku kunatokana na jeni “genes” (sehemu ya DNA inayorithisha tabia au umbile fulani). Hizi jeni zinakuwa ni zenye kurithiwa na mtoto kutoka kwa mzazi hata kama ni babu au babu wa babu. Allaahs (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema yafuatayo kuhusu kuwa na rangi mbali mbali:

 

وَمِنَ النَّاسِ وَالدَّوَابِّ وَالْأَنْعَامِ مُخْتَلِفٌ أَلْوَانُهُ كَذَٰلِكَ ۗ  

Na miongoni mwa watu na viumbe wanaotembea na wanyama wa mifugo, wenye kutofautiana rangi zake kadhalika. [Faatwir: 28]

 

 

Hili ni jambo kila mtu akichunguza anaweza kuliona hata katika familia yake, yeye na ndugu zake.

 

Katika hali yako pia inawezekana kuwa labda umefanana kwa njia moja au nyingine na mababu zako waliopita kwa upande wa mama au baba. Hivyo, usitilie maanani jambo hilo kwani huenda ikawa ni wasiwasi wa kutoka kwa shaytwaan unahitaji kinga kutoka kwa Allaah (‘Azza wa Jalla).    Maadamu mama yako ni mwema, mtiifu na mtu wa ibaadah, basi usiwe na shaka hizo kumhusu.

 

Hapa tunapenda kutanabahisha kuwa ni makosa kwa watu ambao hawakushuhudia kitendo hicho cha zinaa kueneza uvumi kuwa mtoto fulani wa haram,  khasa ikiwa mwanamke anayetuhumiwa ni mwema aliyeshika Dini yake barabara. Bila shaka, wale wenye kueneza uvumi huo watakuwa wameingia katika madhambi makubwa.

 

Ikiwa bado una shaka kwa kuwa maneno ya waja bado yanasambaa itabidi ukae na mamako kitako na umuulize kwa adabu na heshima zote kwani hutaweza kuliweka kwa muda mwingi zaidi bila wewe kupata madhara. Ikiwa unaona hilo ni gumu itabidi utumie khalati zako walio karibu na mama yako ili wamuulize, lakini itabidi utafute mbinu mwenyewe ya kuweza kupata uhakika wa suala hilo. Lakini pindi itakapokuwa uhakika ni kuwa sio baba yako (tunaomba isiwe hivyo), basi utambue kuwa wewe huna makosa yoyote mbele ya Allaah, bali unaweza kuwa ni mja kipenzi kabisa cha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  ikiwa utabakia katika taqwa (kumcha Allaah).   Makosa yatakuwa ni ya mama yako naye atakuwa amefanya dhulma kwa kutokumjulisha mumewe kuwa wewe sio mtoto wake, kwani hapa kuna haki za Mirathi ambazo zinapasa zitimizwe kwa haki pindi itakapofikia hali kuhitajika.

Tunamuomba Allaah (‘Azza wa Jalla) Akuwafikishe katika hilo na huo uwe ni uvumi usio na uhakika wowote.  

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share