Kutia Rangi Nywele Inafaa?

 

 Kutia Rangi Nywele Inafaa?

 

Alhidaaya.com

 

Swali La Kwanza

 

Asalam Alaykum,

 

Kwanza kabisa nawatakia kila la kheri na barka ktk maisha yenu ya hapa duniani na kesho akhera amin. Pili suali langu ni hili:-

Ninaruhusiwa kuweka rangi ktk nywele zangu sio hina nakusudia hizi rangi za nywele zinazouzwa madukani. jee inafaa?

 

Swali La Pili

 

Assalam Alaykum Shekh, swala langu nihili: nilivojua mimi kutia rangi nyuwele haifai lakin, kunamtu mwenzangu mmoja kaolewa na mume shekh, na alivomuliza mumuwe jee kutia rangi inafaa, mumewe kamjibu, inafaa lakin, tu usiende kichawazi yaan kuonesha watu  yaan kujistiri, lakin mimi sijamini inafaa na wakati nilivyo juu mie haifai? Naomba nijibiwe shukran......

 

Swali La Tatu

Kuweka dawa ya nywele kufanya nywele zako zipendeza, ni dhambi??

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Nasi pia tunakutakia kila la kheri na fanaka hapa duniani na Kesho Aakhirah.Tulivyoyasoma maswali hayo mawili ya mwanzo, ni dhahiri kwetu kuwa ni kama swali moja kwa kufanana kwake. Kutia rangi ni kwa yule mwenye mvi katika kichwa chake au kidevu. Hili ni katika mapambo kuwa watu wa Kitabu (Mayahudi na Manasara) wanajizuilia na kutia rangi mvi na kuzibadilisha wakidhani kuwa kujitengeneza na kujipamba ni kinyume na ucha wa Allaah  kama wanavyofanya watawa wao.

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwakataza Waislamu kuigiza watu wengine na kufuata nyendo zao, ili wawe daima kinyume na kutambulikaa na mambo yao. Abu Hurayrah [Radhwiya Allaahu ‘anhu] anasimulia kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Hakika Mayahudi na Manasara hawatii rangi mvi zao basi nendeni kinyume nao" [Al-Bukhaariy]

 

 Amri hii si lazima ni kwa wenye kutaka kama inavyodhihirisha matendo ya Swahaba. Abu Bakr na ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) walikuwa wakitia rangi nywele zao na ‘Aliy, Ubay bin Ka‘b na Anas (Radhwiya Allaahu ‘anhum) walikuwa hawatii. 

 

Je, ni rangi gani ambayo yafaa kwa mtu kupaka? Ama mzee mkongwe, ambaye kichwa na kidevu chake kimejaa mvi, basi haifai kwake kutumia rangi nyeusi. Ndio maana siku alipokuwa Abu Bakar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) wakati ilipotekwa Makkah huku amembeba baba yake, Abu Quhaafah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) mpaka akamweka mbele ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na akaona kichwa chake kilivyojaa mvi alisema: "Badilisheni hizi mvi lakini msimtumilie nyeusi" [Muslim].

 

Baadhi ya Swahaba walikuwa wakitumia katumu ambao ni aina ya mmea kutoka Yemen unaotoa rangi nyekundu iliyowiva na kukoza sana au hina ambayo ni rangi nyekundu.

 

Rangi na hina au katumu zinafanana kwa kuwa zote zinabadilisha rangi ya nywele na hata umbile lake la kawaida. Lakini hakika ni kuwa rangi hii ya kemikali ina tofauti kubwa sana na hina kwani hii ya awali huwa inatiwa kemikali ambayo inaweza kuleta madhara. Kwa hiyo, ni juu yetu kutazama ile kanuni muhimu kuwa: “Chenye kumletea madhara mwanadamu huwa kwake ni haramu”. Ni bora kwetu kuachana na rangi hizo ila tu tunapoyakinisha kuwa hazina madhara kwetu. Ni chache zenye sifa hiyo.

 

Inajulikana kuwa mwanamke wa Kiislamu hafai kwenda kichwa wazi ikiwa ametia dawa au hakutia. Kichwa chake ni lazima kifunikwe ila tu akiwa nyumbani na mumewe pamoja na walio maharimu zake. Msingi ni kama tulivyotaja juu, ikiwa rangi hizo hazitamletea madhara kutakuwa hapana shida. Afya na siha ya Muislamu ni muhimu zaidi kuliko kitu chengine chochote. Kwa hiyo, ni salama zaidi kwetu sisi kama Waislamu kutumia hina, katumu au mimea mingine ambayo itatia rangi nywele zetu. Kwa maumbile yake miti katika asili yake haina madhara kwa matumizi ya mwanadamu. 

 

Ama kuhusu Swali la tatu, jibu lake ni kama tulivyoeleze hapo majibu ya maswali mawili ya mwanzo.

 

Kwa muhtasari ni kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Hakika Allaah Aliyetukuka ni Mzuri na Hakubali ila zuri" [Muslim]. Kutia rangi nywele ni miongoni mwa mapambo ambayo imeruhusiwa kwa Muislamu kwa kubadilisha mvi na pia kuziweka nywele katika hali nzuri.

 

Kile ambacho hakiruhisiwi ni kwa mkongwe kutia rangi nyeusi au ikiwa kama zilivyo rangi za siku hizi kwa sababu ya kutengenezwa na kemikali zinakuwa na madhara. Pindi inapojulikana kuwa rangi hizo zina madhara basi inakuwa haifai kwa Muislamu kutumia. Na ni kidogo zisizokuwa na madhara kwa miili yetu. 

 

 

Na Allaah Anajua zaidi 

 

 

Share