Kutoa Mimba Kabla Ya Roho Kutiwa Miezi Minne Nini Hukmu Yake?

SWALI:

 

Asalamu alaaikum

 

Naomba kujua dhambi za kutoa mimba pamoja hukumu yake na vipi mtu anaweza kutubu toba kwa Mwenyezi Mungu akasamehewa. Kwa mfano mtu amepata mimba ya mwezi mmoja baadae akaitoa kabla ya miezi minne ya kutiwa roho hicho kiumbe?

 

Ahsante


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu kwa swali lako kuhusu kutoa mimba.

Mimba ikishaingia hata ikiwa iko katika kiwango kidogo hata siku moja kinakuwa ni kiumbe mbali na kuwa hakijatiwa roho. Uislamu umekataza kiumbe kuuliwa isipokuwa kukiwa na dharura hiyo. Allaah Aliyetukuka Anasema:

Wala msiwaue wana wenu kwa kuogopa umasikini. Sisi Tunawaruzuku wao na nyinyi. Hakika kuwaua hao ni khatia kubwa” (al-Israa’ (17): 31).

 

Kwa mwenye kumuua mtoto wake kwa makusudui hatokuwa ni mwenye kuuliwa kishari’ah lakini atakuwa na dhambi kubwa mbele ya Allaah Aliyetukuka. Itabidi atubie na arudi kwa Allaah Aliyetukuka ili aweze kusamehewa. Masharti ya kutubia ni kama yafuatayo:

1.     Ujute kwa kosa ulilolifanya la kuua mtoto.

2.     Kujivua na kujiondoa katika maasiya.

3.     Kuazimia kutorudia tena kosa hilo la kuua.

 

Ukiweza kutimiza masharti haya basi Allaah Aliyetukuka Atakusamehe madhambi yako hayo ya kuua.

 

Mimba inaweza kutolewa ikiwa mwanamke ataambiwa na daktari mzoefu na aliyebobea katika taaluma ya kizazi na awe Muislamu mcha Mngu kuwa kuendelea kubeba mimba hiyo itakuwa ni hatari kwa mama. La si hivyo basi itakuwa haifai kuitoa kabisa na mwenye kutoa atakuwa na dhambi kubwa mbele ya Allaah Aliyetukuka.

Tafadhali bonyeza viungo vifuatavyo upate manufaa zaidi:

Kutoa Mimba - Hukmu Na Kafara Yake

Mume Amemuambia Asizae Tena, Huku Ameoa Mke Wa Pili Ambaye Anazaa, Naye Ameshika Mimba, Je Aitoe?

Kutoa Mimba Ikiwa Ikiachwa, Mtoto Atakuwa Mgonjwa Au Kufariki Baadaye

Anaweza Kutoa Mimba Msichana Aliyebakwa?

Kutoa Mimba Isiyotimia Mwezi, Yaani Kabla Haijapuliziwa Roho, Atakabiliwa Na Hukumu Ya Kuua? Na Ataweza Kusamehewa?

Amekula Vidonge Kutoa Mimba Nini Hukmu Yake?

 

 

Na Allaah Aliyetukuka Anajua zaidi

 

Share