Amali Za Kutenda Ayyaamut-Tashriyq: Tarehe 11, 12, 13 Dhul-Hijjah Na Katazo La Swiyaam

Amali Za Kutenda Ayyaamut-Tashriyq: Tarehe 11, 12, 13 Dhul-Hijjah

 Na Katazo La Kufunga (Swiyaam)

 

 www.alhidaaya.com

 

 

 

Ayyaamut-Tashriyq ni masiku yanayoanzia siku ya pili baada ya ‘Iyd ambayo ni tarehe 11, 12 na 13 Dhul-Hijjah. Masiku haya yameitwa At-Tashriyq kwa sababu Hujaji walikuwa wakikatakata nyama na kuzianika juani. Na pi siku hizi hujulikana kwa: ‘Siku za Minaa'

 

‘Amali za kutenda na yaliyokatazwa:

 

a) Kumdhukuru Allaah ('Azza wa Jalla) kwa Wingi:

 

Katika siku hizi inampasa Muislamu azidishe kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kama Anavyosema:

((وَاذْكُرُواْ اللّهَ فِي أَيَّامٍ مَّعْدُودَاتٍ)

((Na mdhukuruni Allaah katika siku za kuhesabika.)) [Al-Baqarah: 203]

 

Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) amesema: Siku za kuhesabika ni siku za tashriyq (11, 12, 13 Dhul-Hijjah) na siku maalumu ni siku za kumi za mwanzo za Dhul-Hijjah. [Al-Qurtwubiy: 3.3]

 

Pia kutamka Tabkiyr Al-Muqayyad (Takbiyr za nyakati maalumu za kukadirika) imekusudiwa kila baada ya Swalaah ya fardhi. Rejea kiungo kifutacho kupata maelezo na faida:

 

Ukumbusho Wa Takbiyr Katika Masiku Kumi Na Tatu Ya Dhul-Hijjah: Tarehe 1–13 Dhul-Hijjah

 

b) Haifai kufunga (Swawm) katika Ayyamut-Tashriyq: 

 

Haifai kufunga masiku haya ya Tashriyq hata kama mtu alikuwa na mazowea ya Swawm za Sunnah kama vile Jumatatu, Alkhamiys au Ayyaamul-Biydhw. Dalili ya makatazo ni katika Hadiyth ifuatayo:   

 

عن أبي هريرة  أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ بَعَثَ عَبْدَ اللَّهِ بْنَ حُذَافَةَ يَطُوفُ فِي مِنًى أَنْ: ((لَا تَصُومُوا هَذِهِ الْأَيَّامَ فَإِنَّهَا أَيَّامُ أَكْلٍ وَشُرْبٍ وَذِكْرِ اللَّهِ عَزَّ وَجَلَّ))

Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimtuma 'Abdullaah bin Hudhaafah azunguke Minaa na atangaze: "Msifunge siku hizi, kwani hizi ni siku za kula na kunywa na kumdhukuru Allaah ‘Azza wa Jalla.” [At-Twabariy 4: 211]

 

Lakini anaweza mtu kufunga tarehe 14, 15 na 16 kukamilisha siku tatu ili apate fadhila za kufunga siku tatu kila mwezi. [Fataawaa ibn Baaz]

 

 

Wa biLlaahi At-Tawfiyq

 

 

Share