Ratiba Ya ‘Ibaadah Za Kutekeleza Siku Tukufu Ya ‘Arafah

 

Ratiba Ya ‘'Ibaadah Za Kutekeleza Siku Tukufu Ya ‘Arafah

 

Ibaadah Za Siku Moja Kwa Malipo Matukufu Mno!

 

Imeandaliwa na Umm Sumayyah

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Kabla ya yote, weka niyyah safi kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kutekeleza ‘ibaadah hizi na pia omba du’aa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akujaalie tawfiyq ya kuweza kutekeleza ‘ibaadah Siku hii tukufu ya ‘Arafah bila ya kushindwa au kulegea kwa sababu fadhila zake ni tukufu mno.

 

 

Hakika hii sio siku ya kutoka nje kuzurura au kutembelea watu, wala sio siku ya kwenda madukani wala sio siku ya kustarehe, bali sio siku ya kujishughulisha na lolote lile isipokuwa kubakia nyumbani au Msikitini kwa wanaume na kubakia katika kumdhukuru Allaah ('Azza wa Jalla) na kutekeleza 'Ibaadah makhsusi za siku hii tukufu.

 

 

1-Lala mapema usiku wake; Yaani tarehe 8 Dhul-Hijjah. Weka niyyah moyoni kufunga (Swawm) Siku ya ‘Arafah ufutiwe madhambi ya miaka miwili kutokana na Hadiyth:

 

عَنْ أَبِي قَتَادَةَ رضي الله عنه أن النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ :  ((صِيَامُ يَوْمِ عَرَفَةَ أَحْتَسِبُ عَلَى اللَّهِ أَنْ يُكَفِّرَ السَّنَةَ الَّتِي قَبْلَهُ وَالسَّنَةَ الَّتِي بَعْدَهُ )) أخرجه مسلم

Abuu Qataadah (Radhwiya Allaahu 'anhu) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Swawm ya 'Arafah nataraji (kwa Allaah) kufuta madhambi ya mwaka uliopita na wa baada yake)) [Muslim]

 

 

2-Amka mapema kabla ya alfajiri kwani kuna fadhila tele za kuamka usiku kufanya ‘ibaadah, miongoni mwazo ni zifuatazo:

 

Allaah (‘Azza wa Jalla) Huteremka hadi mbingu ya dunia kututakabalia du’aa, kutukidhia haja na kutughufuria dhambi kama ilivyotajwa katika Hadiyth ifuatayo:

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْه)ُ أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) قَالَ:  ((يَنْزِلُ رَبُّنَا تَبَارَكَ وَتَعَالَى كُلَّ لَيْلَةٍ إِلَى السَّمَاءِ الدُّنْيَا حِينَ يَبْقَى ثُلُثُ اللَّيْلِ الآَخِرُ يَقُولُ: مَنْ يَدْعُونِي فَأَسْتَجِيبَ لَهُ ، مَنْ يَسْأَلُنِي فَأُعْطِيَهُ ، مَنْ يَسْتَغْفِرُنِي فَأَغْفِرَ لَهُ))

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Rabb wetu Tabaaraka wa Ta’aalaa) Huteremka [kwa namna inavyolingana na utukufu Wake] kila siku katika mbingu ya dunia [ya kwanza] inapobakia thuluthi ya mwisho ya usiku na Husema: Nani ananiomba Nimtakabalie? Nani ananitaka jambo Nimpe? Nani ananiomba maghfirah Nimghufurie?)) [Al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuwd, At-Tirmidhiy, Ibn Maajah, Ahmad]

 

Du’aa Kutakabaliwa Katika Saa Ya Usiku:

 

عَنْ جَابِرٍ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ)  قَالَ: سَمِعْتُ النَّبِيَّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم)َ يَقُولُ: ((إِنَّ فِي اللَّيْلِ لَسَاعَةً لاَ يُوَافِقُهَا رَجُلٌ مُسْلِمٌ يَسْأَلُ اللَّهَ خَيْرًا مِنْ أَمْرِ الدُّنْيَا وَالآَخِرَةِ إِلاَّ أَعْطَاهُ إِيَّاهُ وَذَلِكَ كُلَّ لَيْلَةٍ))

Imepokelewa kutoka kwa Jaabir (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: Nimemsikia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Hakika katika usiku bila shaka kuna saa haimuwafikii mtu Muislamu anayemwomba Allaah khayr katika mambo ya dunia au Aakhirah ila Atampa, na hiyo ni kila usiku)) [Muslim (757), Swahiyh Al-Jaami’ (2130)]

 

 

 

3-Swali Tahajjud japo rakaa 2 na witr na uombe du'aa wakati wa kusujudu au baada ya Tashahhud kabla ya kutoa Salaam, kwani humo du’aa hutaqabaliwa:

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رَضِيَ اللَّه عَنْهُ) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) قَالَ: ((أَقْرَبُ مَا يَكُونُ الْعَبْدُ مِنْ رَبِّهِ وَهُوَ سَاجِدٌ فَأَكْثِرُوا الدُّعَاءَ))

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mja huwa karibu kabisa na Rabb   wake anapokuwa anasujudu, kwa hiyo zidisheni du'aa)) [Muslim (482), Abu Daawuwd, An-Nasaaiy, Ahmad]

 

Na pia

 

عَنْ أَبِي أُمَامَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قِيلَ يَا رَسُولَ اللَّهِ، أَيُّ الدُّعَاءِ أَسْمَعُ؟ قَالَ: ((جَوْفَ اللَّيْلِ الآخِرِ وَدُبُرَ الصَّلَوَاتِ الْمَكْتُوبَاتِ))

Imepokelewa kutoka kwa Abu Umaamah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema:  Ilisemwa: Ee Rasuli wa Allaah, du’aa ipi inayosikilizwa zaidi (inayotakabaliwa zaidi)? Akasema: ((Sehemu ya mwisho ya usiku na baada ya kila Swalaah ya faradhi))  [At-Tirmidhiy Hadiyth Hasan, Swahiyh At-Tirmidhiy (3499) Swahiyh At-Targhiyb (1648)]

 

 

 

4-Baadae kula daku na fanya Istighfaar mpaka karibu na Swalaah ya Alfajiri kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amewasifu Waja Wake wanaoomba maghfirah wakati huu na Amewaahidi Jannah:

 

 الصَّابِرِينَ وَالصَّادِقِينَ وَالْقَانِتِينَ وَالْمُنفِقِينَ وَالْمُسْتَغْفِرِينَ بِالْأَسْحَارِ﴿١٧﴾

Wenye kusubiri na wasemao kweli, na watiifu, na watoaji mali katika njia ya Allaah na waombao maghfirah kabla ya Alfajiri. [Aal-‘Imraan: 17]

 

Na pia,

 

 إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي جَنَّاتٍ وَعُيُونٍ﴿١٥﴾

 Hakika wenye taqwa watakuwa katika Jannaat na chemchemu.

 

آخِذِينَ مَا آتَاهُمْ رَبُّهُمْ ۚ إِنَّهُمْ كَانُوا قَبْلَ ذَٰلِكَ مُحْسِنِينَ﴿١٦﴾

Wakichukua yale Atakayowapa Rabb wao. Hakika wao walikuwa kabla ya hapo ni wahisani.

 

كَانُوا قَلِيلًا مِّنَ اللَّيْلِ مَا يَهْجَعُونَ﴿١٧﴾

Walikuwa kidogo tu katika usiku wakilala kwa raha. 

 

وَبِالْأَسْحَارِ هُمْ يَسْتَغْفِرُونَ﴿١٨﴾

Na kabla ya Alfajiri wakiomba maghfirah.

[Adh-Dhaariyaat: 15-18]

 

 

 

 

5-Jiandae na Swalaah ya Alfajiri, tawadha tena na uombe du'aa baada ya wudhuu ya kuomba Jannah kwani ina fadhila zifuatazo:

 

عَنْ عُمَرَ بْنِ الْخَطَّابِ (رَضِيَ اللَّه عَنْهُ) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ): ((مَا مِنْ مُسْلِمٍ يَتَوَضَّأُ فَيُحْسِنُ الْوُضُوءَ ثُمَّ يَقُولُ: أَشْهَدُ أَنْ لاَ إِلَهَ إلاَّ اللَّهُ وَأَشْهَدُ أَنَّ مُحَمَّدًا عَبْدُهُ وَرَسُولُهُ، إلاَّ فُتِحَتْ لَهُ ثَمَانِيَةُ أَبْوَابِ الْجَنَّةِ يَدْخُلُ مِنْ أَيِّهَا شَاءَ))

Kutoka kwa ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakuna Muislamu yeyote anayetawadha akatia vizuri wudhuu wake, kisha akasema: “Ash-hadu anlaa ilaaha illa-Allaah wa ash-hadu anna Muhammadan ‘Abduhu wa Rasuwluhu [Nashuhudia kwamba hapana muabudiwa wa haki isipokuwa Allaah, na nashuhudia kwamba Muhammad ni mja Wake na Rasuli Wake] ila atafunguliwa milango minane ya Jannah ataingia wowote apendao)) [Ibn Maajah – Swahiyh Ibn Maajah (385)]

 

 

 

 

6-Kisha swali rakaa 2 kabla ya Swalaah ya Alfajiri kwani Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

(( ركْعتا الفجْرِ خيْرٌ مِنَ الدُّنيا ومَا فِيها ))   رواه مسلم

((Rakaa mbili (za Sunnah) kabla ya Alfajiri ni kheri kuliko duniya na yaliyomo ndani yake) [Muslim]

 

Swali Swalaah ya Alfajiri kisha leta *takbiyr baada ya salaam kisha soma Adhkaar baada ya Swalaah na ubaki kwenye mswala usome Adhkaar za asubuhi kisha Msabihi Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa kila aina za Tasbiyh na soma Qur-aan mpaka jua lichomoze.

 

*Takbiyratul-Muqayyad inaanza hapa baada ya kila Swalaah za fardhi mpaka inapoingia Magharibi ya siku ya mwisho ya Tashriyq (tarehe 13 Dhul-Hijjah).

 

 

 

7-Baada ya dakika 15-20 kuchomoza kwa jua swali rakaa 2 za Ishraaq (au Dhuwhaa) ili upate thawabu za Hajj na Umrah.

 

عن أنس عن النبي صلى الله عليه وسلم ، أنه قال: ((مَنْ صَلَّى الْغَدَاةَ فِي جَمَاعَةٍ ثُمَّ قَعَدَ يَذْكُرُ اللَّهَ حَتَّى تَطْلُعَ الشَّمْسُ ، ثُمَّ صَلَّى رَكْعَتَيْنِ ، كَانَتْ لَهُ كَأَجْرِ حَجَّةٍ ، وَعُمْرَةٍ ، تَامَّةٍ ، تَامَّةٍ ، تَامَّةٍ)) رواه الترمذي (586) أخرج الترمذي  صححه الألباني .

Imetoka kwa Anas kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayeswali Alfajiri katika Jamaa'ah kisha akakaa anamdhukuru  Allaah mpaka likachomoza jua kisha akaswali Raka'ah mbili, atapata ujira kama ujira wa kwenda Hajj na 'Umrah ulio kamili kamili kamili)) [Imetolewa na At-Tirmidhiy na kaisahihisha Al-Albaaniy]

 

 

 

8-Ukiweza endelea na adhkaar na du’aa au lala kidogo ili upate afya ya kufanya ibaadah nyengine za siku hii tukufu ya ‘Arafah.

 

 

9-Ukiamka tawadha kisha swali rakaa 2 au 4, au 6, au 8 za Dhuwhaa ambayo ina fadhila zifuatazo:

 

عـَن أبي ذَرٍّ رضي الله ُ عنه ، عن النـَبي ِّ صلـَّى الله عليه وسلم قال: ((يـُصـْبـِحُ عـَلى كـُلِّ سـُلامى مـِنْ أحـَدِكـُمْ صـَدَقةُ: فـَكُل تـَسْبـِيحـَةِ صـَدَقةٌ ،وَ كُل تـَحمِيدة صـَدَقةٌ ، وكُلُ تـَهْـليْلةٌ صـَدَقـَةٌ، وكُلُّ تـَكْبِيْرةِ صـَدقةٌ ، وأمرٌ بالمـَعرُوف صـَدقةٌ ، ونـَهىٌ عـَنِ المـُنْكرِ صـَدقةٌ ويـُجْزئ مـِنْ ذلكَ رَكـْعتـَانِ يـَركَعُهُما مـنَ الضـُّحى))  رواه مسلم

Kutoka kwa Abu Dharr (Radhiya Allahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa alihi wa sallam) amesema: ((Kila kiungo katika mwili wenu hupambaukiwa kikihitaji kutolewa sadaka, kwa hiyo kila tasbiyh (kusema ‘SubhaanaAllah’) ni sadaka na kila tahmiyd (kusema ‘AlhamduliLlaah’) ni sadaka na kila tahliyl (kusema ‘La Ilaaha Illa Allah’) ni sadaka  na kila takbiyr (kusema ‘Allahu Akbar’) ni sadaka na kuamrisha mema ni sadaka na kukataza maovu ni sadaka na itamtosheleza (Mtu) kwa Rakaa mbili za Dhuhaa)) [Muslim]

 

 

10-Endelea kufanya adhkaar, istighfaar na kusoma Qur-aan na soma sana Adhkaar hii makhsusi ya Siku ya ‘Arafah:

 

  لَا إِلَهَ إِلاَّ اللهُ وَحْدَهُ لا شَرِيْكَ لَهُ، لَهُ الـمُلْكُ، ولَهُ الـحَمْدُ، وَهُوَ عَلَى كُلِّ شَيءٍ قَدِير

 

'Laa Ilaaha illa Allaah Wah-dahu laa shariyka Lahu, Lahul-Mulku wa-Lahul-hamdu wa Huwa 'alaa kulli shay-in Qadiyr

 

Hapana mwabudiwa wa haki ila Allaah, Hana mshirika, ufalme wote ni Wake, na Himdi zote ni Zake, Naye ni Mweza wa kila kitu daima)) [Swahiyh At-Tirmidhiy (3/184), Silsilatu Al-Ahaadiyth Asw-Swahiyhah (4/6)]

 

 

11-Swali Dhuhuri pamoja na sunnah 4 kabla yake na 2 baada kisha na ukiweza 2 nyengine za kuepushwa na moto. Kisha leta takbiyr baada ya Salaam.   Endelea kutamka Adhkaar makhsusi ya siku ya ‘Arafah iliyotajwa katika nukta nambari 9 na Takbiyratul-Mutwlaq (ya nyakati na mahali popote) huku ukisubiri kusikiliza khutba ya ‘Arafah.

 

 

12-Swali ‘Asr kisha leta takbiyr na soma adhkaar za jioni.

 

 

13-Baina ya nyakati soma Qur-aan au tamka Adhkaar makhsusi ya Siku ya ‘Arafah. Kabla ya Adhaan ya maghrib na endelea kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na  fanya Istighfaar, omba du'aa khasa du’aa ya kuachwa huru kutokana na moto na usiwasahao Waislaamu wenzio kwa du'aa.

 

 

14-Ikiadhiniwa Maghrib futuru na usisahao du'aa kwa wingi kwani du'aa ya mwenye Swawm hairudishwi kama ilivyothibiti katika Hadiyth:

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ): ((ثَلاَثَةٌ لاَ تُرَدُّ دَعْوَتُهُمْ، الإِمَامُ الْعَادِلُ، وَالصَّائِمُ حَتَّى يُفْطِرَ، وَدَعْوَةُ الْمَظْلُومِ يَرْفَعُهَا اللَّهُ دُونَ الْغَمَامِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَتُفْتَحُ لَهَا أَبْوَابُ السَّمَاء،وَيَقُولُ بِعِزَّتِي لأَنْصُرَنَّكِ وَلَوْ بَعْدَ حِينٍ))

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: (([Watu] Watatu hazirudishwi du'aa zao; Imaam muadilifu, mwenye Swawm mpaka afuturu, na du'aa ya aliyedhulumiwa, Anainyanyua Allaah bila ya mawingu Siku ya Qiyaamah na inafunguliwa milango ya mbingu na Anasema: Kwa Utukufu Wangu, Nitakunusuru japo baada ya muda.))[Swahiyh At-Tirmidhiy (2526) Ibn Maajah, Ahmad]

 

 

15-Swali ‘Ishaa na ulale mapema tena uweze kuamka Tahajjud na uombe du’aa kwani huu ni usiku mtukufu mno pia.

 

 

Hizo ni Nasaha kwa mpangilio, ila Nasaha ni kwamba isikupitie saa bila ya kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) khasa kwa Adhkaar makhsusi ya Siku ya ‘Arafah iliyotajwa katika nambari 9, na vile vile kutamka Takbiyratul-Mutwlaq (ya nyakati zozote na mahali popote). Na ukiweza kutekeleza  haya kwa masiku yote tisa ni bora zaidi maana thawabu zake ni nyingi mno!

 

 

Allaah Atujaalie katika ambao wataokolewa na moto na kughufuriwa madhambi yao Aamiyn.

 

 

Wa biLLaahit-tawfiyq

 

 

 

Share