Hajj Na ‘Umrah

 

Hajj Na ‘Umrah

 

Imekusanywa Na Kufasiriwa Na

Muhammad Faraj Saalim As-Sa’iy (Rahima Allaahu)

 

Alhidaaya.com

 

 

Utangulizi

 

Shukrani zote ni zake Allaah, tunashuhudia kuwa hapana anayepaswa kuabudiwa isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ni Rasuli wake.

 

Ameufikisha ujumbe na kuifikisha amana, kwa hivyo tunakuomba Rabb wetu umsalie na kumsalimu Nabiy wako huyu mtukufu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na Aali yake na Swahaba wake watukufu - Aamin.

 

Amma baad,

 

Allaah Anasema: 

 وَلِلَّـهِ عَلَى النَّاسِ حِجُّ الْبَيْتِ مَنِ اسْتَطَاعَ إِلَيْهِ سَبِيلًا ۚ وَمَن كَفَرَ فَإِنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ عَنِ الْعَالَمِينَ ﴿٩٧﴾ 

Na kwa ajili ya Allaah imewajibika watu watekeleze Hajj katika Nyumba hiyo kwa mwenye uwezo. Na atakayekufuru, basi hakika Allaah ni Mkwasi kwa walimwengu. [Aal-‘Imraan–97]

 

‘Ulamaa wote wamekubaliana kuwa Hajj ni moja katika nguzo tano za Kiislamu, na ni fardhi ijulikanayo kuwa ni ya lazima. Atakayekanusha kuwajibika kwake huwa ni kafiri aliyertadi na kutoka katika dini ya Kiislamu.

 

Wanavyuoni wengi wanasema kuwa: Hajj imefaradhishwa katika mwaka wa sita baada ya Hijra, (baada Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa saalihi wa sallam) kuhamia Madiynah).

 

Mwanachuoni maarufu Ibnil Qayyim, katika kitabu chake kiitwacho Zaadul Ma-ad, yeye amesema kuwa Hajj imefaridhishwa mwaka wa tisa, pale ilipoteremshwa aayah isemayo:

 

 وَأَتِمُّوا الْحَجَّ وَالْعُمْرَةَ لِلَّـهِ ۚ 

Na timizeni Hajj na ‘Umrah kwa ajili ya Allaah.  [Al-Baqarah: 196]

 

Ni Katika Amali Bora

 

Amesimulia Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa:

 

"Amali ipi iliyo bora?"

Akajibu:

"Imani juu ya Allaah na Rasuli wake"

Akaulizwa: “Kisha ipi?”

Akasema:

"Kisha Jihadi katika njia ya Allaah".

"Kisha ipi?"

Akasema:

"Kisha Hajj iliyokubaliwa".

 

Anasema As-Sayid Saabiq, mwandishi wa kitabu ‘Fiq-hus Sunnah’:

 

"Hajj iliyokubaliwa ni ile isiyochanganyika na maovu.”

 

Al-Hassan Al-Basry yeye amesema:

 

"Hajj iliyokubaliwa ni ile iliyomfanya aliyehiji anaporudi akawa anaipenda akhera yake kuliko dunia.”

 

Wajumbe Wa Allaah

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Mahujaji na wenye kufanya ‘Umrah ni wageni wa Allaah. Wanachomuomba anawapa, na wakiomba maghfira anawaghufiria.”

 

[Imepokewa na An-Nasai, Ibni Majah, Ibni Khuzaymah na Ibni Hibban]

 

Kwa hivyo kila aliyebahatika atambue kuwa tokea siku ile alipoamua kwenda kuhiji, keshakuwa mgeni wa Rabb wake Subhanahu wa Ta’aalaa, na kwa ajili hiyo anatakiwa awe mtu anayekistahiki cheo hicho. Na anapokuwa katika Ibada hiyo tukufu asigombane wala kuzozana na Mahujaji wenzake.

 

Zimepokelewa Hadiyth nyingi zinazotufahamisha kuwa atakayehiji bila kufanya maovu wala kugombana wala kuzozana, hapana zawadi nyingine anayoistahiki isipokuwa Jannah.

 

Inawajibika Hapo Hapo

 

Imamu wakubwa kama vile Abu Hanifa na Maalik na Ahmad bin Hanbal na baadhi ya wanafunzi wa Imam Ash-Shaafi’iy wanasema:

 

"Hajj inamwajibikia kila mtu toka pale anapokuwa na uwezo.

 

Kwa sababu Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Anayetaka kuhiji basi aharakishe, kwa sababu huenda akaumwa, mnyama wake akazeeka au akapatwa na shida (akazitumia pesa zake).”

 

Na katika hadithi nyengine amesema:

 

“Fanyeni haraka mkahiji, maana hajui mmoja wenu atapatwa na nini.” [Imepokewa na Ahmad, Al-Bayhaqiy, At-Twahaawiy na Ibn Maajah]

 

Kuhiji Kwa mali Ya Kukopa

 

Kutoka kwa Abdullah bin Abu Auf (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema:

“Nilimuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya mtu asiyewahi kuhiji iwapo anaruhusiwa kukopa kwa ajili ya kuhiji?” Akaniambia; “La, (asifanye hivyo)”. [Imepokewa na Al-Bayhaqiy]

 

Hajj Ya Mwenye Deni

 

Kamati ya kudumu ya Utafiti wa Kielimu na Utoaji Fatwa imetoa fatwa kuhusiana na suala la Hajj ya mwenye deni kwa kueleza yafuatayo:

 

Moja ya masharti ya Hajj ni uwezo, na mtu kuwa na uwezo wa mali wa kuifanya Hajj. Ikiwa mtu ana deni ambalo anadaiwa na mkopeshaji na mkopeshaji akawa hakubali yule mtu aende Hajj bila kumlipa pesa zake, basi hatoruhusika kwenda Hajj hadi alipe deni analodaiwa, kwani mtu huyo atahesabika si mwenye uwezo wa kwenda Hajj. Lakini endapo mkopeshaji hatomshikilia alipe pesa zake na ima kamruhusu aende Hajj hali ya kuwa ana deni lake, basi anaweza kwenda na Hajj yake kwa hali hiyo itakubalika.

[Fataawa al-Lajnah ad-Daaimah 11/46]

 

Na katika Fatwa nyingine, Kamati ya Kudumu ya Fatwa walipoulizwa swali kuhusu Hajj ya mwenye deni la nyumba ambalo muulizaji alisema anapaswa kulilipa kwa awamu, ilieleza ifuatavyo:

 

Uwezo wa kutekeleza Hajj ni moja ya masharti ya kuwa kwake ni waajib. Ikiwa una uwezo wa kulilipa deni hilo kwa awamu ambayo imekutana na wakati wa Hajj, basi unaweza kwenda baada ya kulilipa deni katika awamu hiyo. Lakini ikiwa huwezi kulipa deni hilo kwa awamu hiyo, basi ahirisha Hajj hadi utakapopata uwezo kwani Allaah Anasema:

 

 ۗ وَلِلَّـهِ عَلَى النَّاسِ حِجُّ الْبَيْتِ مَنِ اسْتَطَاعَ إِلَيْهِ سَبِيلًا ۚ 

Na kwa ajili ya Allaah imewajibika watu watekeleze Hajj katika Nyumba hiyo kwa mwenye uwezo.  [Aal ‘Imraan: 97]

 

Na at-Tawfiyq ni kutoka kwa Allaah

 

[Al-Lajnah ad-Daaimah lil Buhuuth al-‘Ilmiyyah wal Iftaa 11/45]

 

Naye Mwanachuoni Shaykh Muhammad bin Swaalih al-‘Uthaymiyn anasema:

 

Deni linalodaiwa linapaswa kutangulizwa kulipa kuliko Hajj, kwani wajibu wa kulilipa unawekwa mbele kuliko mtu kwenda kutekeleza Hajj. Hivyo, anapaswa mtu kulipa kwanza deni kisha ndio kwenda Hajj. Na ikiwa hatobakiwa na chochote au kitakachobaki hakimtoshelezi gharama za kwenda Hajj, basi atasubiri hadi Allaah Amjaalie uwezo wa kwend akuitekeleza nguzo hiyo. Lakini likiwa ni deni lenye kuwa na muda mrefu aliopewa mkopeshwa la kulilipa siku za mbele, hivyo, kwa hali hii hata kama mkopeshaji akimruhusu au asimruhusu kwenda Hajj, hatoruhusika kwenda Hajj ikiwa hana uhakika au dhamana ya kulilipa kwa ule muda aliopewa/waliokubaliana na mkopeshaji.

 

Kwa hali hiyo tunasema: Ikiwa mtu anadaiwa deni, na anafahamu kuwa ana uwezo wa kulilipa kwa muda aliopewa (hata ikiwa ni mbeleni baada ya Hajj), basi Hajj kwa hali hiyo inakuwa ni wajibu kwake japokuwa ana deni. [Fataawa Ibn ‘Uthaymiyn, 21/96]

 

Kuhiji Kwa Mali Ya Haramu

 

Imepokewa kutoka kwa At-Tabarani kuwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Anapotoka mwenye kuhiji kwa pesa njema akauweka mguu wake juu ya kipandio cha mnyama wake, akasema: "Labbayka Allahumma labbayk", (Nakuitikia ee Rabb wangu nakuitikia) hujibiwa na msemaji kutoka mbinguni, "Labbayka wa Sa’adayka (Mwitikio wako umekubaliwa na utafurahi kwa amali yako njema hii), kwa sababu zawadi yako (chakula na vifaa vyako) ni vya halali, na mnyama wako ni wa halali, na Hajj yako inakubaliwa na haina madhambi".

 

Lakini anapotoka anayeihiji kwa pesa za haramu akauweka mguu wake juu ya kipandio cha mnyama wake akasema, "Labbayka Allahumma labbayk" (Nakuitikia ee Rabb wangu nakuitikia), hujibiwa kutoka mbinguni, "Laa labbayaka walaa sa’adayka. (Hakukubaliwi kuitikia kwako wala hutolipwa mema), kwa sababu vifaa vyako ni vya haramu na pesa zako ni za haramu na Hajj yako ni ya dhambi na wala haikubaliwi".

 

Kwanza – ‘Umrah

 

Miyqaat (Mipaka)

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameweka Miyqaat ‘mipaka’ maalum ambayo yeyote anayekwenda Makkah kwa nia ya kuhiji au kufanya ‘Umrah haruhusiwi kuivuka kabla ya kutia nia ya Ihraam mwahala hapo. Amewawekea watu wa Madiynah mji wa Dhul Hulayfah kuwa ni Mpaka wao. Mji huu unajulikana pia kwa jina la Abaar ‘Ali, nao upo Madiynah, kiasi cha Kilomita 450 mbali na Makkah.

 

Akawawekea watu wa Sham mji wa Al-Juhfa kuwa ni Miyqaat yao. Na Miyqaat ya watu wa Najd ni Qarn al Manazil. Amma watu wa Yemen Miyqaat yao ni mji wa Yalamlam. Na watu wa Iraaq Miyqaat yao ni Dhaata ‘Irq.

 

Hii ni mipaka aliyoiweka Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kisha akasema:

 

“Hiyo ni mipaka yao na ya kila apitae njia hizo, kwa wasio wakazi wa miji hiyo, kwa kila atakaye kuhiji au kufanya ‘Umrah.”

 

Mtu anapowasili katika mipaka hiyo anatakiwa aoge, ajisafishe, akate makucha na kujitia manukato akitaka. (Si vizuri kujitia manukato katika vazi la Ihraam, ingawaje si haram kufanya hivyo, isipokuwa sharti iwe kabla ya kutia nia ya kuhiji).

 

Unaweza kukoga na kuvaa Ihraam (vazi la kuhijia) pamoja na kufanya yote hayo ukiwa nyumbani kwako, hotelini au popote ulipofikia kabla ya kuifikia mipaka hiyo, isipokuwa nia lazima uitie ufikapo penye mipaka hiyo.

 

Vizuri Kuswali Kabla Ya Kutia Niyyah

 

Utakapofika katika mojawapo ya mipaka iliyotajwa ukiwa bado hujaswali Swalah ya fardhi ya wakati huo, basi ni bora kuswali kwanza kisha utie niyyah. Amma ukiwa umekwishaswali, basi ni vizuri (si lazima) kusali raka’ah mbili Sunnah ikiwa wakati huo si katika nyakati zinazokatazwa kuswali, kisha unatia niyyah kwa kusema: “Labbayka ‘Umrah

 

Kisha unaanza kufanya Talbiyah kwa kusema:

 

“Labbayka Allaahumma Labbayk. Labbayka Laa Shariyka Laka Labbayk, Inna Lhamda Wanni-‘mata Laka Wal Mulk Laa Shariyka Lak.”

 

Unaendelea hivyo njia yote, wanaume wanasema kwa sauti kubwa na wanawake kwa sauti ndogo huku ukimuomba Allaah maghfira na kumdhukuru kwa wingi.

 

Unatakiwa pia uwe ukimswalia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa wingi pamoja na kuamrisha mema na kukataza maovu unapokuwa safarini mpaka utakapowasili Makkah.

 

Hukmu Ya Talbiyah

 

Talbiyah ni kutamka "Labbayka Allaahumma Labbayk. Labbayka Laa Shariyka Laka Labbayk, Inna Lhamda Wanni-‘mata Laka Wal Mulk Laa Shariyka Lak.”

 

‘Ulamaa wote wamekubaliana kuwa Talbiyah ni kitendo kilichotolewa amri juu yake.

 

Kutoka kwa Ummus-Salama (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) amesema:

 

“Nilimsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ‘Enyi watu wa nyumba ya Muhammad, anayehiji kati yenu anyanyuwe sauti yake anapofanya Talbiyah.” [Imepokewa na Imam Ahmad na Ibni Hibban]

 

‘Ulamaa wamekhitilafiana katika hukmu yake, katika wakati wake, na katika kuichelewesha.

 

Imam Ash-Shaafi’iy na Imam Ahmad wanasema kuwa kitendo hicho ni Sunnah na kwamba mtu anatakiwa aanze kufanya Talbiyah mara baada ya kutia nia ya Ihraam. Na iwapo ametia nia ya Hajj kisha asifanye Talbiyah, basi Hajj yake inasihi na wala haina tatizo lolote.

 

Imam Maalik, yeye anaona kuwa kitendo hicho ni Wajib na mtu asipofanya Talbiyah baada ya kutia nia ya Ihraam, akaendelea hivyo muda mrefu bila kufanya Talbiyah, basi inampasa kuchinja mnyama.

 

Fadhila Zake

 

Imesimuliwa na Jaabir (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Muislam yeyote atakayefanya Talbiyah tokea asubuhi mpaka jua linapozama, dhambi zake zitafutwa na atarudi (akiwa hana dhambi) kama alivyokuwa siku aliozaliwa na mama yake.” [Imepokewa na Ibni Majah]

 

Imesimuliwa pia na Abu Hurayrah kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

 

“Kila mwenye kuinyanyua sauti yake kwa kufanya Talbiyah, anapewa bishara (njema), na kila mwenye kufanya Takbir (kutamka 'Allaahu Akbar') anapewa bishara (njema)” Akaulizwa: “Ee Rasuli wa Allaah, bishara ya Jannah?” Akasema: “Ndiyo”) [Imepokewa na At-Tabaraniy na Sa’iyd bin Mansuur]

 

Kunyanyua Sauti Katika Talbiyah

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Alinijia Jibriyl akaniambia: “Waamrishe sahibu zako wanyanyuwe sauti zao katika Talbiyah, kwani hiyo ni katika alama za Hajj.” [Imepokewa na Ibni Majah. Imam Ahmad, Ibni Khuzaymah na Al Hakim]

 

Na kutoka kwa Abubakar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema:

 

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa: “Amali gani iliyo bora katika Hajj?” Akajibu: Al ajji wa thajji” (Kunyanyua sauti katika kufanya Talbiyah na kuchinja.” [Imepokewa na At-Tirmidhiy na Ibni Majah]

 

 Twawaafu ya ‘Umrah

 

Unapowasili Makkah unaanza kufanya ‘Umrah kwa taratibu ifuatayo:

 

Unatufu’, kwa kuizunguka Al-Ka’abah mizunguko saba ukianzia penye jiwe jeusi (Al Hajar al aswad)ukiwa mbali na jiwe hilo anzia sawa na jiwe jeusi.

 

Kabla ya kuanza kutufu lielekee Jiwe jeusi kisha linyoshee mkono (ukiweza kulifikia na kulibusu au kuligusa bila ya kuumiza watu ni vizuri), la kama utasababisha madhara kwa watu au kwa nafsi yako, inatosha kuliashiria tu kwa mkono wa kulia kwa mbali huku ukisema: Bismillahi Allaahu Akbar Kisha unaizunguka Al-Ka’abah ikiwa kushotoni kwako mizunguko saba.

 

Kwa wanaume ni vizuri katika mizunguko mitatu ya mwanzo kukimbia kidogo kidogo mfano wa mtu anayekimbia juu ya mchanga, na mizunguko minne iliyobaki unakwenda mwendo wa kawaida. Wanawake wanakwenda mwendo wa kawaida katika mizunguko yote saba.

 

Wakati wote huo unatakiwa uwe ukisoma du’aa zozote ulizohifadhi. Hapana kisomo maalum au du’aa maalum, bali unaweza kuomba du’aa yoyote na kwa lugha yoyote, na unaweza pia kusoma sura ulizohifadhi katika Qur-aan.

 

Al-Ka’abah ina nguzo nne, na maarufu katika hizo ni nguzo ya jiwe jeusi na nguzo iliyo kabla yake ambayo ni nguzo ya Yaman (Ar-Rukn al-Yamani). Unapoifikia nguzo ya Yaman (Ar-Rukn al-Yamani) ni vizuri kuigusa. Hutakiwi kuibusu wala kuiashiria kama unavyolifanyia jiwe jeusi. Na unapokwenda baina ya nguzo hiyo ya Yamani na Jiwe Jeusi ni vizuri kuomba na kuikariri du’aa ifuatayo.

 

“Rabbana Aatina Fidduniya Hasanatan Wa Fil Aakhirati Hasanatan Wa Qinaa ‘Adhaaba Nnaar”.

 

Na maana yake ni:

 

Rabb wetu tupe katika dunia yaliyo mema, na katika akhera (tupe) yaliyo mema, na utuepushe na adhabu ya Moto).

 

Unaendelea hivyo mpaka utakapolifikia Jiwe jeusi. Hapo utakuwa umekwishamaliza mzunguko wa mwanzo, na utaanza mzunguko wa pili kwa kunyanyua mkono wa kulia huku ukiliashiria tena jiwe jeusi na kusema: “Allaahu Akbar”, kisha utatenda yale yale uliyotenda katika mzunguko wa mwanzo, mpaka umalize mizunguko saba.

 

Kila unapolifikia jiwe jeusi au unapokuwa sawa nalo, unanyanyua mkono wa kulia na kulielekea jiwe huku ukisema: “Allaahu Akbar”

 

Maqaam Ibraahiym

 

Ukishamaliza kutufu mara saba, unakwenda kuswali raka’a mbili nyuma ya Maqaam Ibraahiym. Katika raka’a ya mwanzo unasoma Alhamdu na Qul ya ayyuha l kaafiruun na katika raka’a ya pili unasoma Alhamdu na QulhuwAllaahu ahad.

 

Usipoweza kuswali penye Maqaam Ibraahiym kwa sababu ya msongamano mkubwa wa watu, unaweza kuswali popote karibu na hapo au popote mbali na hapo sharti iwe ndani ya msikiti.

 

Kunywa Maji Ya Zamzam

 

Baada ya kumaliza kutufu na kuswali raka’a mbili penye Maqam Ibrahim, ni vizuri kunywa maji ya Zamzam. Unaweza kunywa kutoka katika majagi ya maji yaliyoenezwa msikitini hapo, na unaweza pia kwenda penye mifereji (mabomba) ya maji ya Zamzam yaliyokuwepo penye uwanja wa Swafaaa na Marwah.

 

“Imepokewa kutoka kwa Al-Bukhaariy na Muslim kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikunywa maji ya Zamzam kisha akasema: Maji haya yamebarikiwa, yanamshibisha mwenye njaa na yanamponesha mgonjwa.”

 

Sa’ay Baina Ya Swafaaa Na Marwahh

 

Swafaaa na Marwah ni vilima viwili vilivyoelekezana, vilivyomo ndani ya msikiti upande wa kisima cha Zamzam.

 

Ukimaliza kutufu na kunywa maji ya Zamzam, unakwenda penye jabali Swafaaa kwa ajili ya kuanza kufanya ibada ya Sa'ayi, baina ya majabali Swafaaa na Marwah.

 

Unaanza kwa kupanda Swafaaa huku ukisema:

Inna Swafaa wal Marwahta min shaairi llah". kisha unasema "Abdau maa badaa llahu bihi”, na maana yake ni:

 

(“Hakika Swafaaa na Marwah ni katika alama za kuadhimisha dini ya Allaah. Ninaanza pale alipoanzia Allaah. (Ambaye ndani ya Qur-aan tukufu ameanza kulitaja jabali Swafaaa kisha Marwah).

Si lazima kutamka maneno hayo, lakini hi ni kwa sababu Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alisema na kufanya hivyo.

 

Unapowasili juu ya Swafaaa unaelekea Qiblah kisha unasema:

 

الحمد لله - الله اكبر - لا إِلهَ إلاَّ اللهُ وَحْدَهُ لا شَرِيكَ لَهُ، لَهُ المُلْكُ وَلَهُ الحَمْدُ وهُوَ عَلى كُلِّ شَيءٍ قَديرٌ، لا إِلَهَ إلا اللهُ وَحْدَهُ أَنْجَزَ وَعْدَهُ، وَنَصَرَ عَبْدَهُ وَهَزَمَ الأَحْزَابَ وَحْدَهُ.

“Alhamdu Lillahi Allaahu Akbar La Ilaha Illa Llahu Wahdahu Laashariyka Lahu Wahuwa Alaa Kulli Shay-In Qadiir. La Ilaha Illa Llahu Wahdau, Anjaza Waadahu Wanawsara ‘Abdahu Wahazamal Ahzaaba Wahdahu” Unasema hivyo mara tatu.

 

Hivi ndivyo alivyofanya Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam). Kama hukuweza (kutokana na zahma au kama hujaweza kuhifadhi vizuri) basi unasoma hata mara moja tu, au unaomba du’aa yoyote na kusoma chochote unachoweza kusoma. Kisha teremka na ufanye "Sa’ay ya Umra”.

 

Na Sa’ay ni kwenda baina ya Swafaaa na Marwah mara saba (Kwenda, inahisabiwa mara moja, na kurudi mara moja). Ni vizuri kukimbia kidogo kidogo kila unapozifikia alama za kijani zilizo ukutani baina ya Swafaa na Marwah, lakini wanawake, wao wanakwenda mwendo wa kawaida. Ukifika Marwah, unapanda juu na kusema pamoja na kufanya yale uliyoyafanya ulipokuwa juu ya Swafaaa. Hakuna katika Twawaafu wala katika Sa’ay, du’aa au kisomo maalum. Soma chochote na omba du’aa yoyote.

 

Kujihalalisha

 

Ukishamaliza kufanya Sa’ay, unapunguza nywele zako au unazinyoa zote. Kwa wanaume ni vizuri kunyoa, kama alivyofanya na kupendekeza Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam). Lakini wanawake, wao wanapunguza kidogo tu.

 

Hapo utakuwa umekwisha maliza ibada ya ‘Umrah na unaweza kuvua nguo za Ihraam na kuvaa nguo zako za kawaida. Na kinakuhalalikia kila kitu ulichoharamishiwa ulipokuwa katika Umrah, hata mkeo. (Kama ni ‘Umrah ya Hajj unaisubiri tarehe 8 Dhul-Hajj ili uanze ibada ya Hajj.)

 

Fadhila Za Kunyoa Nywele Zote

 

Kutoka kwa Abdillahi bin ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Allaah Awarehemu walionyoa (nywele zote)” Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) wakasema: “Na waliopunguza je ewe Rasuli wa Allaah?” Akasema: “Allaah awarehemu walionyoa (nywele zote).” Wakasema: “Na waliopunguza je ewe Rasuli wa Allaah?” Akasema: “Allaah awarehemu walionyoa (nywele zote).” Wakasema: “Na waliopunguza je ewe Rasuli wa Allaah?” Akasema: “Na waliopunguza.”

 

Katika Hadiyth hii Nabiy, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amewaombea rehema mara tatu walionyoa nywele zote na akawaombea mara moja tu waliopunguza.

 

Tunamuomba Allaah atuingize katika Rahmah Yake – Aamin

 

Hajj

 

Tarehe nane Dhul Hajj inaitwa “Siku ya Attarwiyah, nayo ni siku inayoanza Ibada za Hajj. Likishatoka jua la siku hiyo, oga na uvae nguo zako za Ihraam ukiwa nyumbani, hotelini au popote ulipofikia mjini Makkah au nje yake kisha sema: Labbayka Hajj”. Masharti ya Ihraam ni yale yale tuliyoyataja hapo mwanzo katika ibada ya ‘Umr ah.

 

Asubuhi ya siku hiyo Mahujaji wanaondoka Makkah kuelekea Minaa na wanaswali mahali hapo Swalah ya Adhuhuri, Alasiri, Magharibi, Isha ya siku hiyo, pamoja na Swalah ya Alfajiri ya siku ifuatayo. Kila Swalah inaswaliwa katika wakati wake Qasran (kwa kufupisha). Unazifupisha Swalah za raka’a nne unaziswali raka’a mbili, ama Swalah ya Magharibi unaiswali kwa ukamilifu – raka’a tatu.

 

‘Arafah

 

Hukmu yake

 

Kusimama y ni nguzo kubwa kupita zote katika nguzo za Hajj, na hii inatokana na Hadiyth ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema:

 

Al Haju ‘Arafah – (Kusimama) Arafa ndiyo Hajj yenyewe - atakayewahi usiku wa kujikusanya kabla ya kuingia alfajiri (ya siku ya ‘Arafah) basi amewahi”.)) [Imepokewa na Imam Ahmad pamoja na ma Imam wengine wa Hadyith]

 

Kusimama ‘Arafah

 

Likishatoka jua la tarehe tisa Dhul Hajj, Mahujaji wanaondoka Minaa na kuelekea ‘Arafah kwa utulivu na tahadhari, huku wakisema: “Allaahu Akbar – au “Laa ilaaha illa Allaah” au huku wakilabiy kwa kusema:

 

“Labbayka Allahumma Labbayk Labbayka Laa Shariyka Laka Labbayk - Inna Lhamda Wanni’mata Laka Wal Mulk Laa Shariyka Laka.”

 

Wanakwenda kwa utulivu bila kuwaudhi wenzao, na wanaziswali Swalah za Adhuhuri na Alasiri wakati mmoja hapo ‘Arafah, Qasran, zote wakati wa Adhuhuri, kwa adhana moja na iqama mbili.

 

Ni vizuri kubaki katika sehemu ya Namirah, mahali ulipo msikiti mkubwa wa Namirah na wasiingie ‘Arafah mpaka baada ya wakati wa zawaal (Kiasi cha saa sita za mchana).

 

Hii siyo lazima, hasa kutokana na zahma za hapo ‘Arafah siku hiyo, isipokuwa ni bora kama ikiwezekana. Hakikisha kuwa umo ndani ya mipaka ya ‘Arafah, na unapokuwa mahali hapo patakatifu, zidisha kuomba du’aa na kumtaja Rabb wako huku ukiwa umeelekea Qiblah, kwa sababu siku hiyo na mahali hapo ndipo watu wanapoghufiriwa madhambi yao yote na kurudi makwao kama siku waliyozaliwa.

 

Nyakati za jioni tafuta sehemu za juu juu. Panda, kisha elekea Qiblah na unyanyue mikono yako juu huku ukiomba, kama alivyofanya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Imesimuliwa na Jaabir (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Hakuna siku bora kwa Allaah kuliko siku kumi za (mwanzo) za Dhul Hajj”. Mtu mmoja akamuuliza: “Siku hizo ni bora, au mtu anapokuwa katika Jihadi kwa muda huo?” Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuambia: “Siku hizo ni bora kuliko idadi ya siku hizo katika Jihadi fiy sabiili Llah. Na hapana siku iliyo bora kwa Allaah kuliko siku ya ‘Arafah. Allaah Subhanahu wa Ta’aalaa huwaambia Malaika wake kwa fahari: “Tazameni waja wangu, wamekuja nywele zao zikiwa zimetimka, wamejaa mavumbi, wametoka kila sehemu za mbali wakitaraji rehema Zangu na wala hawakuwahi kuiona adhabu Yangu”. Hakuna siku ambayo Allaah anawaepusha watu wengi na moto kuliko siku hiyo”. [Imepokewa na Abu Ya’ala – Al-Bazzaar – Ibn Khuzaymah na Ibn Hibbaan]

 

Imepokewa pia kuwa Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema:

 

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisimama ‘Arafah wakati jua linakaribia kuzama, akasema: “Ee Bilaal! Ninyamazishie watu.” Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu), akainuka na kuwataka watu wanyamaze. Kisha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

 

“Enyi watu! Alinijia Jibril hivi punde na kunipa salam zitokazo kwa Rabb wangu. (Kisha) Akasema: ‘Allaah Subhanahu wa Ta’aalaa amewaghufiria watu wa ‘Arafah na watu wa Masha'ari l haraam (Muzdalifah).” Akainuka ‘Umar bin Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akauliza: “Hizi (salam na haya maghfira) ni kwa ajili yetu peke yetu?” Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema: “Hizi ni zenu na za wote watakaokuja (hapa) baada yenu mpaka siku ya Qiiyaamah.” ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akasema: “Kheri za Allaah ni nyingi na nzuri.”

 

Imesimuliwa na Ibnul Mubarak kutoka kwa Sufyaan Ath-Thawriy kuwa:

 

'Mtu anapokuwa hapo anatakiwa ajishughulishe na kuomba du’aa pamoja na kumtaja Allaah sana ili arudi akiwa amefaidika na ameghufiriwa, na asiwe katika waliokula hasara siku hiyo kwa kuyakosa maghfira ya Allaah.'

 

Jua likishazama Mahujaji wanaondoka ‘Arafah na kuelekea Muzdalifah. (Usiswali Magharibi hapo ‘Arafah).

 

Muzdalifah

 

Unapokuwa Muzdalifah utaswali Swalah ya Magharibi na ‘Ishaa wakati wa ‘Ishaa, raka’a tatu za Magharibi kisha mbili za ‘Ishaa kwa adhana moja na Iqama mbili. Kisha utabaki hapo mpaka baada ya Swalah ya Alfajiri.

 

Ukiwa hapo utaomba du’aaa kwa wingi huku ukinyanyua mikono yako juu na kuelekea Qiblah kama alivyofanya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).

 

Ukiwa Muzdalifah utaokota mawe ya kupigia Jamaraat. (Jamaraat ni milingoti mikubwa mitatu ya mawe yanayopigwa hapo Minaa ambayo watu wengine huyaita Mashetani). Unaokota mawe saba tu, (si lazima kuokota mawe yote hapo Muzdalifah), na mawe mengine utaweza kuokota ukiwa Minaa. Unaweza pia kuokota mawe yote ukiwa hapo kama ukitaka.

 

Minaaa

 

Utaondoka Muzdalifa kwa utulivu na kuelekea Minaa baada ya Swalah ya Alfajiri na kabla ya kutoka jua.

 

Utakapowasili Minaaa unafanya yafuatayo:

 

1.  Unalipiga Jamaratul ‘Aqabah ambalo watu wanaliita Shetani Mkubwa, lililo karibu na Makkah kwa mawe saba, moja baada ya jingine. Kila unaporusha jiwe unasema:

 

“Allaahu Akbar".

 

(Haijuzu kuvurumisha mawe yote saba kwa pamoja).

 

Jamaraat’ si mashetani kama wanavyoitakidi baadhi ya watu wenye kuvurumisha mawe kwa ghadhabu na kutukana na wengine huvurumisha mawe makubwa wakidhani kuwa wanampiga na kumkomesha shetani. Hayo yote hayajuzu, kwa sababu Jamaraat’ yamewekwa kwa ajili ya kujikumbusha tu namna gani Nabiy Ibraahiym mahali hapo alivyompiga mawe shetani aliyejaribu kumshawishi asimchinje mwanawe kama alivyoamrishwa na Rabb wake.

 

Kwa hivyo mtu anatakiwa arushe mawe madogo sana na kuyapiga Jamaraat kwa nia ya kutii amri ya Allaah tu, bila ya kuingiza fikra nyingine.

 

Kwa wale wasiojiweza wanaweza kumwakilisha mtu awapigie, na mtu mmoja anaweza kuwakilishwa na wengi.

(Kumbuka siku ya mwanzo unalipiga mawe Jamarat moja tu, tofauti na siku zilizobaki unapoyapiga mawe Jamaraat zote tatu).

 

2.    Chinja mnyama wako, na ni vizuri kama utakula katika nyama hiyo na nyengine utawapa masikini.

 

3.    Punguza au nyoa nywele zako. (kunyoa nywele zote ni bora zaidi), na mwanamke anakata nywele zake kidogo tu.

 

Utaratibu huu ni bora zaidi ingawaje unaweza kutanguliza hiki kabla ya kile. Ukimaliza kupiga mawe, kuchinja na kunyoa, unakuwa umekwisha jihalalisha uhalalisho mdogo na unaweza kuvaa nguo zako za kawaida na kufanya yote uliyokatazwa ulipokuwa na Ihraam, isipokuwa tu huwezi kumwingilia mkeo mpaka umalize Twawaaful Ifaadhwah (Twawaafu ya Hajj).

 

Twawaaful Ifaadhwah

 

Hukmu yake

 

Maulamaa wote wamekubaliana kuwa Twawaaful Ifaadhwah (Twawaafu ya Hajj) ni katika nguzo za Hajj, na kwamba asiyetufu Twawaafu hiyo Hajj yake inabatilika.

 

Na hii inatokana na kauli Yake Subhanahu wa Ta’aalaa Aliposema:

 

 ثُمَّ لْيَقْضُوا تَفَثَهُمْ وَلْيُوفُوا نُذُورَهُمْ وَلْيَطَّوَّفُوا بِالْبَيْتِ الْعَتِيقِ ﴿٢٩﴾

Kisha wamalize ‘ibaadah zao; wajisafishe taka zao na watimize nadhiri zao, na watufu kwenye Nyumba ya Kale. (Al-Ka’bah).   [Al-Hajj: 29]

 

Ukishamaliza shughuli za hapo Minaa, unakwenda Makkah na unafanya Twawaaful Ifaadhwah, nako ni kuizunguka Al-Ka’abah mara saba na kufanya kama ulivyofanya katika Twawaafu ya ‘Umrah. Kisha unafanya Sa’ay, kutembea baina ya Swafaaa na Marwah na kufanya kama ulivyofanya mara ya mwanzo ulipofanya ‘Umrah.

 

Ukishamaliza, unakuwa umekwisha jihalalishia halalisho kubwa na kwa hivyo, hata mkeo anakuhalalikia. Unaweza kuiahirisha Twawaafu ya Ifaadhwah mpaka baada ya kumaliza shughuli zote za Minaa.

 

Ukishamaliza Twawaafu ya Ifaadhwah unarudi Minaa na unabaki hapo usiku wa tarehe 11, 12 na 13 kwa wasiokuwa na haraka. Hizo zinaitwa siku za Tashriyq. Inatosha kama utabaki hapo usiku wa tarehe 11 na wa 12 tu.  Katika siku 2 au 3 hizo unapiga mawe Jamaraat zote tatu kila siku kwa mpangilio ufuatao:

 

Anza kupiga Jamaraat la mbali na Makkah, (Jamaraat dogo) kisha la kati, kisha Kubwa (Jamarat al Aqaba). Kila moja piga kwa mawe saba huku ukisema: "Allaahu Akbar", kila unaporusha jiwe. Hii ni kwa siku tatu zilizobaki.

 

Nyakati Za Kupiga Mawe

 

Siku ya An-Nahr – Sikukuu mosi, usipige mawe mpaka jua lichomoze:

 

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa Muzdalifah aliwatanguliza Minaa watu dhaifu na wazee na wanawake, akawaambia: “Musirushe mawe mpaka jua litoke”. [Imepokewa na At-Tirmidhiy]

 

Mwenye udhuru anaweza kuchelewesha mpaka kabla ya Magharibi, lakini ni vizuri kupiga mawe baada ya kutoka jua na kabla haijaingia Magharibi kwa asiyekuwa na udhuru. (Baadhi ya ‘Ulamaa wanajuzisha kupiga mawe baada ya Magharibi kwa udhuru, lakini bora ujaribu kupiga kabla jua kuzama).

 

Wakati wa kurusha mawe kwa siku mbili zilizobaki au siku tatu kwa wale wasiotaka kuharakisha, ni baada ya Zawal (wakati wa adhuhuri pale jua linaposogea kidogo baada ya kuwa katikati).

 

Kuomba Du’aa

 

Ni vizuri kuelekea Qiblah na kuomba du’aa baada ya kumaliza kupiga kila Jamaraat isipokuwa Jamaraat la mwisho. Hadiyth iliyosimuliwa na Al-Bukhaariy na Imam Ahmad inasema:

 

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akeshapiga kila Jamaraat kwa mawe saba akisimama na kuelekea Qiblah na kuomba du’aa, isipokuwa baada ya kulipiga Jamaraat la mwisho hakusimama.” [Imepokewa na Al-Bukhaariy na Imam Ahmad]

 

Siku Ya Kuharakisha

 

Ikiwa unataka kubaki hapo kwa mda wa siku mbili tu, basi siku ya tarehe Kumi na mbili Dhul Hajj ambayo hujulikana kama ni "Yawmul isti’ijaal" - Siku ya Kuharakisha – unapiga mawe na kuondoka Minaa kabla ya jua kuzama, na ikiwa utakawia kuondoka ukawepo hapo baada ya juwa kuzama itakubidi ubaki hapo siku moja zaidi. Ni vizuri kubaki usiku wa tatu ikiwa huna cha kukushughulisha.

 

Twawaaful Wida’a

 

Unapotaka kurudi nchini kwako baada ya kumaliza shughuli za Hajj, unatufu Twawaaful wida’a, (Twawaafu ya kuaga) nayo ni kama ifuatavyo:

 

Unatufu Al-Ka’abah mara saba na kufanya kama ulivyofanya katika Twawaafu za mwanzo, lakini mara hii bila ya kufanya Sa’ay baina ya Swafaa na Marwah.

 

Share