Skip navigation.
Home kabah

Wasia Muhimu Kwa Mahujaji

Ukht Muznah Faraj

Alhamdulillahi Rabbil alamiyn waswalaatu wassalaamu 'ala ashrafil anbiyaa walmursalin nabiyyina Muhammadin wa 'alaa alihii waswahbihii ajmaiin waman tabiahum bi-ihsaani ilayaumi d’diyn.  Ammaa ba’ad:

 

1-     Unatakiwa kuwa karibu na watu wema na wenye elimu ili uweze kufaidika nao katika mambo yanayo husu hijjah.

2-     Kujizowesha subira, na kuvumilia pale utakapo udhiwa, na kuto kuwaudhi ndugu zako na kutolipiza mabaya bali ufanye wema.

3-     Kujiweka mbali na uwongo, udanganyifu, kuiba, kusengenya, kufitinisha na istihzai (kuwacheza shere watu na kuwadharau).

4-     Kujihadhari na kuwagusa wanawake kwa makusudi, kuwaangalia, na uwastiri wanawake wako ulio fatana nao (wavae hijabu zao vizuri itakiwavo na sheriya) pindi kunapokuwa na wanaume.

5-     Kuwa mpole wakati wa kuuza na kununuwa, kutowa kauli nzuri bila kuzozana na matendo yako yawe ni mazuri mpaka Mwenyeezi Mungu Akurehemu.

6-      Kutumia msuwaki kwani kunamridhisha Allah.

Kasema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ((assiwaak matw’haratun lilfam, mardhaatun lilrabbi))

((Kupiga msuwaki kunatwaharisha mdomo na kunamridhisha Mola mtukufu)) “imepokewa na Bukhari”

 

7-      Na uchukuwe zawadi pamoja na tende, maji ya zamzam;

Amesema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ((mau zamzam limaa shuriba lahu))

((Maji ya zamzam ni kwa ile nia uliyokunywea))

 “sahihi imepokewa na Ahmad”

8-     Jihadhari na uvutaji sigara,  kwa sababu inadhuru afya na kuwaudhi walio karibu yako pia kupoteza mali, kwa kufanya hivyo ni haramu kwa kauli ya Allah (Subhaanahu wa Ta'ala)

((Wayuhillu lahumut twayyibaati wa yuharrimu 'alayhimul khabaith))

(Na Mwenyeezi Mungu) kawahalalishia vilivyo vizuri na kawaharamishia vilivyo vibaya))“Qur’aan: 7:157”

 

9-     Ndevu ni pambo la wanaume, basi jihadhari na kuzinyoa usije ukavunja amri ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  Amesema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)

((Juzzuu ashshawaarib waarkhuul lihya wa khaaliful majuus))

((Kateni masharubu na fugeni ndevu kutofautiana na wamajuus)) {imepokewa na Muslim}

(Majuus (waabudu moto) ni watu wakisifika kwa tabia mbovu wakati wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

10-   Kukithirisha sana kusoma Qur’aan tukufu na kuzingatiya pamoja na kuyafanyia kazi yaliyokuwemo ndani ya Qur’aan, na kumtaja Mwenyeezi Mungu kwa wingi, kuomba duaa, swala na kusikliza durusu zenye faida.

11-   Usiache kuamrisha mema na kukataza maovu lakini bas kwa hikma na mawaidha mazuri pamoja na upole na maneno laini.

12-  Pindi utakapo ona mijadala isiyokuwa na faida basi achana nayo hata wewe ukiwa katika haki, kwani kuna watu waovu hutafuta sababu au wapate nafasi ya kuitukana dini si kwaujinga kwamba wanauliza ili wajuwe bali ni ubishi wa dhaahir hata akipewa dalili ya sawa bado kang'ang'ana, kwa namna kama hiyo Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza.  Kwa kauli yake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

((Ana zaiymun bibaytin fiy rabadhil jannah liman tarakal mara’a wain kaana muhiqqan))

((Mimi nitamdhamini nyumba katikati ya pepo kwayule mtu atakae acha mijadala hata ikiwa yuko katika haki))

“Sahihi imepokewa na Abu Daawuud”

13-   Harakisha kufanya hajji pindi tu pale utapokuwa na mali ya kutosha kwenda na kurudi huko, wala usifikirie matumizi baada ya hajji kama vile zawadi n.k. ukaacha kwenda hajji hali uwezo wakwenda na kurudi unao lakini ukafikiria nikirudi nitatumia nini au sina pesa ya kununuwa zawadi wakati Mwenyeezi Mungu hakubali udhuru huo.

Basi fanya haraka kabla hujakuwa mgonjwa au kuishiwa na mali au kufa hali yakuwa uko katika maaswi, kwa sababu hajji ni nguzo miongoni mwa nguzo za kiislamu, na ndani yake kuna faida kubwa katika dunia na akhera.

14-  Muhimu kabisa ni kujikurubisha na kujilazimisha katika kila matatizo kwa Mwenyeezi Mungu peke Yake, kumuomba Yeye pasipo Mungu mwingine, kama Alivyo sema Allah:

((Qul innamaa ad’uu rabbiy walaa ushriku bihi ahada))

((Sema: “Ninamuabudu Mola wangu tu wala simshirikishi na yoyote”))

“Qur’aan:72:20”

15-    Ukumbuke nawe ukiwa makkah kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikaa makkah muda wa miaka kumi na tatu (13) akiwaita watu katika kumpwekesha Allah (Subhaanahu wa Ta'ala)

(Tawhidi: LAA ILAHA ILLALLAH) Na maana yake: Hakuna apasae kuabudiwa kwa hakki isipokuwa Mwenyeezi Mungu peke yake. Na kwa hakika hiyo Tawhid ni itikadi sahihi anayo itakidi mtu kwamba Mwenyeezi Mungu yuko juu ya arshi,

Kama alivyo sema Allah: ((Arrahmanu alal arshish stawaa))

((Ndie Mungu Mwenye rehma Aliyetawala juu ya kiti (chake) cha enzi))

“Qur’aan: 20:5”

16-  Imeharamishwa kwa Mwanamke kusafiri kwenda hajji bila yakuwa na mahrim (mahrim, ni ndugu anae muhusu mwanamke kwa karibu zaidi katika wanaume, mfano: Mwanamume ambae ni haramu kumuowa.) au awe na mumewe.

Kwa kauli ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

Amesema ((walaa tusaafirul mar’at illa dhiy mahrim))

((Wala asisafiri mwanamke isipokuwa awe na mahrim)).

 

WALLAHU A’ALAM