Maiti Asiyefaa Kuswaliwa

 

SWALI:

 Naomba kuuliza maswali mawili kuhusiana na maiti kwa vile nimependezewa sana na uchambuaji wa namna mnavyojibu mas-al na InshaAllaah ALLAAH (SW) awazidishie ilmu mtufumbue macho na sisi.

1. Je, ni maiti wa aina gani wakiiislam ambae hafai kuswaliwa kabla ya kuzikwa tukiachilia mbali yule ambae keshaharibika kwa kuoza

 
Majibu naomba yawe na ushahidi wa mambo mawili:-

1. QUR’AN AU

2. HADITH SAHIHI

 


JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Asli katika sheria yetu tukufu ni kuwa Muislamu yeyote anapofariki ni wajibu kwa jamii ya Kiislamu kumuosha, kumkafini, kumswalia na kumzika. Hizi ni amali ambazo ni Fardhi Kifaya kwa itifaki ya wanachuoni. Amali hizo zikitekelezwa na baadhi ya Waislam wao watapata thawabu na ambao hawakutekeleza hawana dhambi lakini iwapo jamii itakosa kufanya hayo basi jamii nzima ipo katika dhambi.

 

Ama kuhusu maswali yako ni kuwa Qur-aan haijatutajia kuhusu mas-ala ya kuswaliwa maiti na hukumu zake. Majibu katika masuala haya tunayapata katika Sunnah za Bwana Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kauli za Maswahaba na wanachuoni wema wenye ilimu na ikhlaas. Miongoni mwa maiti wa Kiislam ambaye huzikwa bila ya kuswaliwa ni:

 

  1. Mtoto tumboni akitoka au kuzaliwa kabla hajafika miezi minne: Hii inatokana na Hadiyth ya kuwa mtoto tumboni hutiwa roho akiwa na miezi minne. Imepokewa na Ibn Mas‘uwd (Radhiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema, ametuhadithia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), naye ni mkweli wa kusadikika:
  2. Hakika mmoja wenu hukusanywa umbile lake katika tumbo la mamake siku arobaini akiwa tone, kisha anakuwa pande la damu kwa muda huo huo, kisha anakuwa pande la nyama kwa muda huo. Baada ya hapo hutumwa Malaika akampuliza roho…” [Al-Bukhaariy na Muslim] Hivyo, Imaam An-Nawawiy katika Al-Majmuw‘ (Mj. 5, uk. 256) na Ibn Qudaamah katika al-Mughniy (Mj. 2, uk. 522) wameona kuwa mtoto kama huyo huwa haoshwi kwa kuwa ni kama pande la damu au nyama iliyomtoka mama.

 

  1. Mashahidi katika Vita vya Jihaad: Hii ni kwa mujibu wa Hadiyth ya Jaabir bin 'Abdillaah (Radhwiya Allaahu 'anhuma) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliamuru baada ya Vita vya Uhud wazikwe mashahidi na damu zao. Hawakuoshwa wala kuswaliwa. [Al-Bukhaariy, Ahmad na Abuu Daawuud]

 

 Na Allaah Anajua zaidi

 

 


Share