Swalaatul-Ghaaib: Kumswalia Maiti Asiyekuweko Kabla Hajaswaliwa Huko Alipofariki Inajuzu?

 

SWALI:

 

Asalaam alaykum. Mimi nina swali kuhusu utata unaojitokeza kuhusu maiti wa mbali.

 

Swali la kwanza, iwapo mtu amefiwa na maiti wa mbali, mfano mimi ninaishi uk na maiti yupo Africa kipi muhimu au bora kukifanya; kumswalia aliyefariki au kumsomea hitma. Kwa sababu kuna mtafaruku unajitokeza huku tulipo huwenda ukatugawa mafungu baadae (Allaah Atunusuru).

 

Swali la pili, je !naweza kumswalia maiti aliyekuwa Africa kabla ya wao kumswalia?mfano nimepata habari saa nne  usiku za uk  ambapo Africa ni saa saba usiku nikaamua kumswalia muda ule ule nilo pata habari ,hii nitakuwa nimefanya makosa? Akhsante

 

 


 

JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

 

 

 Shukran kwa swali lako zuri ambalo limewagawa Waislamu kwa kutokuwa makini katika kutumia dalili. Swalah ya jeneza ya ghaibu (kwa maiti) aliyekufa mbali iliswaliwa mara moja tu na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumswalia mfalme wa

Ethiopia, Najjaash. Hadithi kuhusu suala hili inapatinakana katika Swahiyh ya Muslim. Kwa dalili hiyo wapo wanaosema kuwa inajuzu kumswalia maiti wa mbali kwa hoja hiyo. Lakini hoja hiyo haiko mahali pake munaasib kwa sababu ya kwamba kulikuwa hakuna wakumswalia Najjaash huko Ethiopia ndio Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamswalia Madiynah. Pili, hata kama alikuwa amezikwa kwa kuwa walikuwa wapo Waislamu Ethiopia hawakuwa ni wenye kujua jinsi yake hasa ya kuswaliwa.

 

Hivyo, Swalah ya jeneza kwa maiti wa mbali inafaa tu ikiwa hakuswaliwa huko alikokufa. Ikiwa ameswaliwa itakuwa haifai kwako au kwa mwengine yeyote kumswalia tena. Na kwa nini tujipatie taklifu hiyo ilhali Swalah ya jeneza ni Fardh Kifaayah (faradhi ya kutosheleza) wakifanya baadhi inakuwa wale ambao hawakuweza kutekeleza hilo hawana madhambi yoyote. Hakika ni kuwa yale ya faradhi huwa hatuyafanyi tunataka kujitweka yale ambayo hayatupasi kwa wakati mmoja au mwingine. Ni muhali kabisa kwa maiti kufa katika nchi yoyote ya Afrika Mashariki kisha asiwe ni mwenye kuswaliwa. Swalah hiyo inafanywa hata kwa Muislamu ambaye hana mtu yeyote katika mji au kijiji.

 

Ama kuhusu kumsomea maiti wako khitma haifai kwani kisomo cha Qur-aan hakimfikii maiti. Yapo mambo ya muhimu kwetu sisi kumfanyia maiti ikiwa kweli tunamtakia mema na kheri. Wanachuoni wanasema kuwa halifanywi jambo la uzushi isipokuwa Sunnah moja ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hufa na kuondoka katika utendaji kazi wa watu (Waislamu).

 

Vitu vya muhimu kwetu sisi kufanya ikiwa kweli tunawatakia maiti zetu kheri ni kama vifuatavyo:

 

1.       Kumwombea duaa Allaah Amsamehe maiti wako.

2.       Kumtolea sadaka.

3.       Kumlipia madeni ikiwa anayo.

4.       Kumhijia ikiwa yeye hakupata kwenda nawe una uwezo na ushawahi kwenda Hijjah.

5.       Ikiwa alikuwa ameweka nadhiri na hakuwahi kuitekeleza basi umtekelezee.

 

Soma zaidi kuhusu khitma:

 

 

Khitmah Kutokufaa Na Madhara Yake

 

Kumsomea Khitmah Maiti, Kumchinjia Na Kumuombea Duaa Kwa Pamoja

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Kumswalia maiti kabla hajaswaliwa haifai

kama tulivyoeleza. Ikiwa nawe utataka kumswalia kabla ya wengine itabidi uwaarifu jamaa zake kuwa wewe peke yako unamswalia hivyo wao walio nyumbani ambao ni wengi wasimswalie tena. Kufanya hivyo kutakuwa ni kinyume cha mafunzo ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na hapo hapo itakuwa humpendi maiti wako. Kwa nini itakuwa hivyo? Sababu ni kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametoa fadhila za mtu kumswaliwa na watu wengi ni dalili tosha ya wema wake. Sasa ikiwa utamswalia wewe peke yako inayakinisha kutomtakia mema maiti huyo wako. Ikiwa hauko nyumbani tosheka na kufanya hayo mengine, na Allaah Aliyetukuka Atakulipa kwa nia yako njema.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

 

 

Share