Swalaatul-Ghaaib Kumswalia Swalaah Maiti Aliyefia Mbali

 

Swalaatul-Ghaaib: Kumswalia Swalaah Maiti Aliyefia Mbali

 

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

Je inafaa kwa waisilam kumsalia maiti ikiwa hayupo mbele yao?  Ama kuwa nchi nyengine au sehemu nyengine mji ulele.

 

   

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

 

Wametofautiana 'Ulamaa kuhusu Swalaatul-Ghaaib (Swalaah ya Jeneza ya Asiyekuwepo). 

 

Imaam Ash-Shaafi’iy na Imaam Ahmad wamekwenda kwa mtazamo wa kuwa jambo hili lafaa kishari’ah kwa kutolea dalili hoja zao kwa Hadiyhh ifuatayo:

 

 

Kutoka kwa Abuu Hurayrah  (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)    alitangaza kifo cha Mfalme An-Najjaashiy siku aliyokufa akatoka nao katika Mswalla akapanga safu nao akapiga Takbira nne.   [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

 

Alimuombolezea An-Najaashiy katika siku ailiyofariki, na akatoka na Swahaba zake kwenda kumswalia katika kiwanja, kisha akawatangulia kwenye safu na akapiga takbira nne. 

 

 

Inajulikana kuwa huyu An-Najaashiy alikuwa ni Mfalme kule Uhabashi (Ethiopia) alikuwa Mkiristo mwanzo na kisha alisilimu kwa siri na alipofariki Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)   alijulishwa kifo chake na akamswalia.

 

Ama Imaam Abuu Haniyfah na Imaam Maalik wamekwenda katika msimamo kuwa Swalaatul-Ghaaib haifai ki-Shariy’ah. Na hoja yao ni jawabu lao kuhusiana na kisa cha An Najaashiy kuswaliwa na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni jambo lenye kumhusu (Khususiyaat) Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) pekee. Na inawezekana kuwa kitanda cha An-Najaashiy kilinyanyuliwa hadi kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)   na akamswalia mbele ya hadhara.

 

 

Na wakasema (upande wa Mahanafi na Maalik) kuwa, Haikupokelewa kuwa wakati wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alikuwa akiwaswalia wale wanaokufa ambao wako mbali naye. Na wakasema kuiacha (huko kumswalia aliyefariki mbali) ni Sunnah. Na hata kuifanya kwake ni Sunnah, na hakuna njia yoyote inayowezekana ya wale baada ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kubebewa na kuletewa kitanda cha Maiti aliyefia mbali ili waiswalie! Kwa hiyo kufanya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  hivyo kulikuwa ni Makhsusi tu kwake yeye.

 

 

Na Imaam Ahmad katika moja ya riwaya zake mbili, ameonelea ikiwa ni mtu muhimu katika Uislaam, au mwenye mchango mkubwa katika Dini anaweza kuswaliwa. Kasema, “Atakapokufa mtu mwema, aswaliwe.” Na muono huu pia baadhi ya ‘Ulamaa wa karibuni wameufuata.

 

 

Ama kilicho bora zaidi kwa muono wa ‘Ulamaa  wakubwa, ni kuwa, Swalaatul-Ghaaib inamstahikia ki-Shariy’ah yule ambaye amefariki katika nchi au eneo ambalo hakuna wa kumswalia (Hakuswaliwa huko alipofia). Ama yule aliyefariki na akaswaliwa huko alipofariki, basi hakuna haja ya kumswalia Swalaatul-Ghaaib. Na hili ndilo walilolikubali na kulipitisha ‘Ulamaa  na Imaam wakubwa wa zamani na wa sasa. Ndio msimamo wa   Al-Khatwaabiy, Ar-Rawayaaniy na amelieleza hilo Imaam Abuu Daawuwd katika Sunnan, mlango wa ‘Swalaah kwa Muislam aliye katika ardhi nyingine palipo na Washirikina.’

 

 

 

Na huu ndio msimamo wa Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyyah na mwanafunzi wake hodari Ibnul Qayyim, Kasema Imaam Ibnul Qayyim katika kitabu chake maarufu cha Zaadul Ma’ad: “…Na amesema Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyyah: Kilicho sahihi ni kuwa, ikiwa Aliyeghibu (maiti) aliyefia katika nchi au sehemu ambayo hakuswaliwa, basi ataswaliwa Swalaatul-ghaaib. Kama alivyoswali Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kumswalia An-Najaashiy kwani yeye alikufa akiwa miongoni Makafiri na hakuswaliwa. Na kama angekuwa ameswaliwa huko alipokuwa, basi asingeswaliwa tena kwani ile faradhi ya kumswalia maiti ingekuwa ishatekelezwa.”

 

 

Na kauli hiyo ya Shaykhul-Islaam kutoka kwa mwanafunzi wake, ndio pia katika riwaayah nyingine ya Imaam Ahmad.

 

 

Na muono huu unatiliwa nguvu sana na matukio wakati wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Makhalifa wake waongofu kwani walikufa wengi miongoni mwa Swahaba katika sehemu na maeneo mbalimbali nje ya pale alipokuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  na hata Makhalifa wake baadaye, na hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa hao waliokufa maeneo ya mbali, waliswaliwa Swalaatul-ghaaib. Na asili katika masuala ya ‘Ibaadah ni ‘Tawqiyfiyah’ kukifu hadi papatikane dalili ya kishariy’ah kuhusu kufanyika au kutofanyika kwa jambo.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

 

Share