SWALI:
Assalaam 'Alaykum Warahmatullah,
Tunaamini kweye vikao vyema malaika huwa wanatuzunguka, tunauliza jee wakati huu tulionao malaika wanaweza kuwa na sisi kwa kujitokeza kwa njia ya kiumbe kama binaadamu au vyenginevyo hata bila kuwajua kama ilivyokuwa nyakati za mitume (kuja kwa Jubril kufundisha dini), kwenda kwa watu wa Lut nakadhalika??
JIBU
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Bila ya shaka Malaika wanatuzunguka tunapokuwa katika vikao vya madarasa ya kujifunza Dini yetu. Ama kujitokeza kwao katika hali ya ubinaadamu, hatukupata mafunzo yenye dalili kuwa huenda hali ikawa hivyo kwetu. Tuliyojifunza ni
“Kwenye Hadiyth iliyopokewa na Al-Bayhaqiy, mama wa waumini Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha) alimwambia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amjulishe wakati Jibriyl (‘Alayhis Salaam) atakapomjia yeye (Mtume). Kila Jibriyl (‘Alayhis Salaam) alipowasili, mama wa waumini Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha) hakuweza kumuona na akawa kila mara anamuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama keshakuja na kama Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anamuona , Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawa anamuitikia kwa kukubali kuwa anamuona, kisha akamwambia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akae karibu yake na akawa bado Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anamuona Jibriyl (‘Alayhis Salaam), na kisha akamtaka Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akae kwenye mapaja yake ili kuhakikisha kuwa kama bado Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) atakuwa anamuona (maana yeye hakuwa anaweza kumuona Jibriyl), na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuhakikishia kuwa bado anamuona, hata mama wa waumini Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha) alipofunua kichwa chake wakati bado Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kakaa kwenye mapaja yake, na huku akiendelea kumuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ikiwa bado anamuona Jibriyl (‘Alayhis Salaam), hapo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamjibu hapana, na kusema kuwa yeye (Jibriyl) si shetani; bali ni Malaika…”
Kwenye Hadiyth hii tunaona kuwa mama wa waumini Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha) hakuweza kumuona Malaika huyo, bali Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa Sallam) tu peke yake. Na pia tunapata kujua kuwa Malaika ni wenye staha kubwa na hayaa na ndio sababu ya Jibriyl (‘Alayhis Salaam) kuondoka kwa kuwa mama wa waumini alifunua kichwa chake na hivyo yeye kuona hayaa na kuondoka. Hadiyth hiyo hata hivyo, haijatujulisha alikuwa katika umbo lipi japokuwa hakuwa katika umbo la kibinaadam, kwani kama angekuwa kwenye umbo la kibinaadam, bila shaka mama wa waumini Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha) angelimuona.
Pia kuna Hadiyth mbalimbali ambazo tumejua kuwa Jibriyl (‘Alayhis Salaam) alimwendea Mtume
Allaah (Subhaananu wa Ta’ala) Amewapa Malaika uwezo wa kujibadili kwa njia mbalimbali. Kama Alivyomtuma Jibriyl (‘Alayhis Salaam) kwa Maryam (‘Alayhas Salaam) akiwa katika umbile la kibinaadam
((وَاذْكُرْ فِي الْكِتَابِ مَرْيَمَ إِذِ انتَبَذَتْ مِنْ أَهْلِهَا مَكَانًا شَرْقِيًّا))
((Na mtaje Maryam katika Kitabu, pale alipojitenga na jamaa zake mahali upande wa mashariki))
((فَاتَّخَذَتْ مِن دُونِهِمْ حِجَابًا فَأَرْسَلْنَا إِلَيْهَا رُوحَنَا فَتَمَثَّلَ لَهَا بَشَرًا سَوِيًّا))
((Na akaweka pazia kujikinga nao. Tukampelekea Roho wetu (Jibriyl), akajifananisha kwake sawa na mtu))
((قَالَتْ إِنِّي أَعُوذُ بِالرَّحْمَن مِنكَ إِن كُنتَ تَقِيًّا))
(((Maryam) akasema: Hakika mimi najikinga kwa Mwingi wa Rehma Aniepushe nawe, ukiwa ni mcha Mungu))
((قَالَ إِنَّمَا أَنَا رَسُولُ رَبِّكِ لِأَهَبَ لَكِ غُلَامًا زَكِيًّا))
(((Malaika) akasema: Hakika mimi ni mwenye kutumwa na Mola wako ili nikubashirie tunu ya mwana aliyetakasika)) [Maryam: 16-19]
Na pia tunaona Malaika walivyokwenda kwa Nabii Ibraahiym (‘Alayhas Salaam) kwa maumbile ya wanaadam,
((وَلَقَدْ جَاءتْ رُسُلُنَا إِبْرَاهِيمَ بِالْبُشْرَى قَالُواْ سَلاَمًا قَالَ سَلاَمٌ فَمَا لَبِثَ أَن جَاء بِعِجْلٍ حَنِيذٍ ))
((Na wajumbe wetu walimjia Ibraahiym kwa bishara njema, wakasema: Salama! Naye akasema: Salama! Hakukaa ila mara akaleta ndama wa kuchoma))
((فَلَمَّا رَأَى أَيْدِيَهُمْ لاَ تَصِلُ إِلَيْهِ نَكِرَهُمْ وَأَوْجَسَ مِنْهُمْ خِيفَةً قَالُواْ لاَ تَخَفْ إِنَّا أُرْسِلْنَا إِلَى قَوْمِ لُوطٍ))
((Basi alipoona mikono yao haimfikilii aliwatilia shaka, na akawaogopa. Wakasema: Usiogope! Hakika sisi tumetumwa kwa kaumu ya Luutw)) [Huud: 69-70]
Pia tunaona kwenye Aayah nyingine kuwa Malaika walitumwa kwa Nabi Luutw (‘Alayhis Salaam) wakiwa katika sura za binaadam wenye kuvutia
((وَلَمَّا جَاءتْ رُسُلُنَا لُوطًا سِيءَ بِهِمْ وَضَاقَ بِهِمْ ذَرْعًا وَقَالَ هَذَا يَوْمٌ عَصِيبٌ))
((Na wajumbe wetu walipokuja kwa Luutw aliwahuzunukia na akawaonea dhiki. Akasema: Hii leo ni siku ngumu!)) [Huud: 77]
Na ingawa katika Qur-aan wametajwa kuwa Malaika huteremka kwetu katika hali mbali mbali, lakini hatuwezi kujua wanatajuia katika umbile gani. Hapa katika
((تَنَزَّلُ الْمَلَائِكَةُ وَالرُّوحُ فِيهَا بِإِذْنِ رَبِّهِم مِّن كُلِّ أَمْر))ٍ
((Huteremka Malaika na Roho (Jibriyl) katika usiku huo kwa idhini ya Mola waokwa kila jambo)) [al-Qadr: 4
Mfano mwingine katika hali ya sakaraatul-mawt ya waja wema ambapo kutokana na Aayah hizi hapa chini kwamba Malaika huzungumza nao wanapowatoa roho zao, hatuwezi kujua vipi wanazungumza nao; katika maumbile ya ki Malaika au ya kibinaadamu au ya kutoonekana kabisa:
((إِنَّ الَّذِينَ قَالُوا رَبُّنَا اللَّهُ ثُمَّ اسْتَقَامُوا تَتَنَزَّلُ عَلَيْهِمُ الْمَلَائِكَةُ أَلَّا تَخَافُوا وَلَا تَحْزَنُوا وَأَبْشِرُوا بِالْجَنَّةِ الَّتِي كُنتُمْ تُوعَدُونَ))
(( نَحْنُ أَوْلِيَاؤُكُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ وَلَكُمْ فِيهَا مَا تَشْتَهِي أَنفُسُكُمْ وَلَكُمْ فِيهَا مَا تَدَّعُونَ))
(( نُزُلًا مِّنْ غَفُورٍ رَّحِيمٍ))
((Hakika waliosema: Mola wetu ni Allaah! Kisha wakanyooka sawa, hao huwateremkia Malaika wakawaambia: Msiogope, wala msihuzunike; nanyi furahini kwa Pepo mliyokuwa mkiahidiwa))
((Sisi ni vipenzi vyenu katika maisha ya dunia na katika Akhera, na humo mtapata kinachotamaniwa na nafsi zenu, na humo mtapata mtakavyovitaka))
((Ni takrima itokayo kwa Mwenye kughufuria, Mwenye kurehemu)) [Fusw-Swilat: 30-32]
Au katika hali ya sakaraatul-mawt ya watu waovu wanapowapiga nyuso na migongo
((وَلَوْ تَرَى إِذْ يَتَوَفَّى الَّذِينَ كَفَرُواْ الْمَلآئِكَةُ يَضْرِبُونَ وُجُوهَهُمْ وَأَدْبَارَهُمْ وَذُوقُواْ عَذَابَ الْحَرِيقِ))
((Na laiti ungeliona Malaika wanapowafisha wale waliokufuru wakiwapiga nyuso zao na migongo yao, na kuwaambia: Ionjeni adhabu ya Moto)) [Al-Anfaal: 50].
Hayo ndiyo yaliyotajwa na yaliyothibiti, vinginevyo ni lazima kuwe na maelekezo
Na Allaah Anajua zaidi