Vipi Kumshukuru Allaah Kwa Neema Zake Nyingi Zisizohesabika

SWALI:

 

Asalaam Aleiqum,

 

Kwanza sina budi na kumshukuru Allah Subhabana wa Taala aloniwezesha kunifikisha siku nyengine ili niweze kuwasiliana na nyinyi.

Pili sina budi na kukushukurini kwa majibu na maelekezo yenu mema na nasema ahsnteni. Wazee wa zamani wanasema uliza ujinga upate uerevu, na mimi nimeuliza na nimepata maelekezo mema nasema ahsanteni.

Ama ibada zangu zote ninazozifanya nafanya kwa "Allah", na shida zangu zote nazielekeza kwake kwa kuamini kuwa yeye ndie mfumbuzi pekee, na hakuna mwengine. Na ndio maana nikasema rakaa zangu za mwanzo 2 baada ya salamu husoma yale majina yake 99 kwa kumshukuru na neema na ukarimu wake. Labda nikueleze kwanini nafanya hivyo?  Usingizi ni kufa, maana ukilala roho huondoka kwa uwezo Allah, hukurejeshea tena roho yako na ukajiona imeshaondoka tu kitandani, sasa hapa ndipo ninapomshukuru Allah kwa yafutayo:-

 

 1 kunijaalia uzingizi mnono na kunirejeshea roho yangu tena, navuta pumzi bila taabu, nimenyanyua mikono yangu inakwenda juu a miguu yangu inatembea vizuri, macho yanaona almurdi viungo vyangu vyote vinafanya kazi sawa, basi hapo ndipo niposhukuru kwa ufalme.

 

2. kunijaalia kunilete katika umati huu wa Muhammed ukiwa ndio umati bora na umati wa mwisho, pasina  ulemavu wowote wa kiwili wili.

 

3. Kunifikisha huu umri niliofikia siku ya leo, nikikumbuka wenzangu wangapi wameshaondoka na kutangulia mbele ya haki na kuwacha kila kitu nyuma, wakiwemo watoto/wajukuu/wazee/waume wao wapenzi,

 

4. Akanijaalia anakipa mume mwenye imani, mapenzi na mashikiano mazur, na akatufungulia kizazi kiliokuwa kitulivu, tukatia harusi zao na kushuhudia vizazi vyao (alhamdullillah).

 

5. Mimi mwenyewe akanijaalia kibarua chenye mafanikio mema, kibarua ambacho kinaniwezesha kuyatatua matatizo yangu.

Basi kwa kufikiria hayo, mimi ndio huleta hizo rakaa mbili na majina yake Allah kwa kumshukuru kwa hayo na mengi mengi.

 

Kumbe nilikuwa nakosea? Namuomba Allah anisamehe kwani nimetenda hayo bila kujua na kwa kipindi kirefu sana.

Sasa hebu nifahamishe njia gani ya kuweza kumshukuru Allah kwa hizi neema zake?

Kusali na sali, quaraani nasoma kila nikimaliza msahafu naanza tena, ambazo hukusanya na kufanya ni hitma kwa wazee wangu na kuzihitimisha kila tarehe 27 Ramadhan ambazo wakati mwingi nina kua nin hitma 4.

Naomba kuelelimishwa, na inshallah M/Mungu atujaalia kila tunamkosea atusamehe, kwani yeye ni mwingi wa msamaha. (amin)

 kwa majina yake matukufu 99 kwa kumshukuru kwa neema na ukaramu wake.


 

 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Tunamshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwa ne'ema hii ya kuona ndugu zetu mmo katika jitihada kubwa ya kujifunza mengi katika dini yenu, khaswa Dada zetu ambao ni muhimu sana kwao kujifunza mafunzo sahihi ili waweze kuwapa watoto wetu wa Kiislamu msingi bora kabisa wa elimu sahihi ya dini yao iwafae katika maisha yao ya duniani na Akhera.

 

Hakika Ne'ema za Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) ni nyingi sana hazihesabiki kama Alivyotaja Mwenyewe mara mbili katika Qur'aan:

 

 ((وَآتَاكُم مِّن كُلِّ مَا سَأَلْتُمُوهُ وَإِن تَعُدُّواْ نِعْمَتَ اللّهِ لاَ تُحْصُوهَا إِنَّ الإِنسَانَ لَظَلُومٌ كَفَّارٌ))

 

((Na Akakupeni kila mlichomuomba. Na mkihisabu neema za Allaah hamtaweza kuzihesabu. Hakika mwanaadamu ni dhaalimu mkubwa, mwenye kuzikufuru neema))[Ibraahiym:34]  

Vile vile :

((وَإِن تَعُدُّواْ نِعْمَةَ اللّهِ لاَ تُحْصُوهَا إِنَّ اللّهَ لَغَفُورٌ رَّحِيمٌ))

 

((Na mkihisabu neema za Allaah, hamtaweza kuzihesabu. Hakika Allaah ni Mwenye maghfira, Mwenye kurehemu)) [An-Nahl:18]

 

Kutokana na maneno Yake hayo Mola Mtukufu, tutaona kwamba kwa vyovyote tutakavyomshukuru hatutaweza kutimiza shukurani Kwake kutokana na wingi wa ne'eema Zake, Naye pia amesema:

((وَقَلِيلٌ مِّنْ عِبَادِيَ الشَّكُورُ))

((Ni wachache katika waja wangu wanaoshukuru)) [Sabaa:13]

 

Wasiomshukuru sana Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) hakika wanakosa faida kubwa kwani Mola Mtukufu Ametangaza kuwa kila mja anapomshukuru Humzidishia ne'ema hizo:

((وَإِذْ تَأَذَّنَ رَبُّكُمْ لَئِن شَكَرْتُمْ لأَزِيدَنَّكُمْ))

((Na alipotangaza Mola wenu: Mkishukuru Nitakuzidishieni)) [Ibraahiym: 7]

 

 Na hakika hivyo unavyofanya ni dalili ya iyman kubwa kwamba unatambua ne'ema za Mola wako na uko katika jitihada ya kumshukuru kwa kuzikumbuka neema Zake hizo,  kwani kumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) ni kutumia kila chema Alichotujaaliya kuwa nacho, ikiwa ni mwili, basi ni kutumia viungo vyake kwa yale yatakayomridhisha, hivyo; masikio ayatumie mtu kwa kusikilizia yale tu Yanayomridhisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala), macho yatazame yale tu yanayomridhisha na kadhalika. Na ikiwa ni ne'ema ya mali basi pia ni kuitumia kwa yale yatakayomridhisha kama kutoa sadaka na kadhalika. Ikiwa ni ne'ema ya kupata watoto basi kuitumia ne'ema hiyo kwa kuwapa malezi bora watoto wako waongoke katika dini yao. Ikiwa ni ne'ema ya kujaaliwa mume mwema, basi ni kumtii mume wako amri zake na kutimiza wajibu wako kwake. Ikiwa ni ne'ema ya elimu basi uitumie kwa kuifundisha elimu hiyo kwa wenzako, ikiwa ne'ema ya kupata rizki basi itunze hiyo rizki bila ya kuifanyia israaf na kadhalika.

Amesema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth iliyotoka kwa ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhumaa):

 

  ((نعمتان مغبون فيهما كثير من الناس  الصحة والفراغ)) البخاري

 

((Ne'ema mbili zimeghafilikiwa na watu wengi; siha na faragha [wakati])) [Al-Buhaariy]

 

Tunapotambua kuwa hatuwezi kuzihesabu ne'ema za Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) haina maana kwamba ndio tuache kumshukuru au tumshukuru kidogo tu, bali tunaweza kujitahidi kumshukuru kwa njia nyingi tukimuomba Atupokelee shukurani zetu. Na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakuacha kutufundisha namna ya kumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)  kama tutakavyoelezea.

 

Kwanza tutambue kuwa kumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)  kunaweza kuwa ama kwa moyo, kwa kukiri na kwa vitendo. Na mafundisho mengi tumeyapata katika Sunnah ya kumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) machache ni kama yafuatayo:

 

 

1-Kila unapopata ne'ema au kuona, au kukumbuka fanya sajda moja inayoitwa 'Sajdatu-shukr', na sio kuswali Raka'a mbili kama wengi wanavyofikiria kuwa kuna Swalah inayoitwa Swalaatu-shukr.

 

 

2-Katika nyiradi za kila siku asubuhi ukisema du'aa hii ifuatayo utakuwa umetekeleza  shukurani ya siku nzima, na ukiisoma jioni utakuwa umetekeleza shukurani ya usiku mzima

اللّهُـمَّ ما  أَصْبَـَحَ بي مِـنْ نِعْـمَةٍ أَو بِأَحَـدٍ مِـنْ خَلْـقِك، فَمِـنْكَ وَحْـدَكَ لا شريكَ لَـك، فَلَـكَ الْحَمْـدُ وَلَـكَ الشُّكْـر

 

“Ee Allaah sikuamka na neema yoyote au kati ya kiumbe Chako chochote, na neema ila inatoka Kwako hali ya kuwa Peke Yako Huna mshirika, ni Zako  Himdi Zote na ni Zako shukurani” 

 

3-Amesema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

  ((أفضل الذكر لا اله إلا الله، وافضل الدعاء: الحمد لله))   رواه الترمذي حديث حسن

 

((Dhikri bora kabisa ni Laa ilaaha illa Allaah  na du'aa bora kabisa ni Alhamdulillah)) [At-Tirmidhiy hadiyth hasan]

 

 

4- Kutoka kwa ibn 'Umar kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

 

 ((إن عبدًا من عباد الله قال: يا رب، لك الحمد كما ينبغي  لجلال وجهك وعظيم سلطانك، فعضلت بالملكين فلم يدريا كيف يكتبانها، فصعدا إلى السماء فقالا يا رب،  إن عبدا قد قال مقالة لا ندري كيف نكتبها،  قال الله -وهو أعلم بما قال عبده-:  ماذا قال عبدي؟ قالا يا رب إنه قد قال: يا رب لك الحمد كما ينبغي   لجلال وجهك  وعظيم سلطانك. فقال الله لهما: اكتباها كما قال عبدي حتى يلقاني فأجزيه بها))  إبن ماجه

 

((Mja katika waja wa Allaah alisema: “Ee Mola wangu! Zako wewe tu Himdi njema Unayestahiki kushukuriwa kama inavyopasa Utukufu Wako na nguvu Zako kubwa kabisa”. Malaika wawili walibabaika hawakujua vipi waandike maneno hayo (jinsi alivyomtukuza utukufu wa Mola wake) Wakaenda kwa Allaah wakasema: Ee Mola wetu! Hakika mja wako kasema aliyoyasema na wala hatujui vipi tuyaandike. Akasema Allaah: “Kwani kasema nini mja wangu?” (Na Allaah Anajua aliyoyasema mja Wake bila ya malaika kumwelezea) Wakasema amesema: Ee Mola wangu! Zako Wewe tu Himdi njema Unayestahiki kushukuriwa kama inavyopasa Utukufu Wako na nguvu Zako kubwa kabisa. Allaah Akasema: “Yaandikeni kama alivyosema mja Wangu mpaka atakaponikuta (siku ya malipo) basi nitampa jazaa yake kwa hayo (aliyoyasema) )) [Ibn Maajah 2:1249]

 

 

Kusoma kwako Qur-aan na kukhitimisha kisha kuanza tena na kuendelea hivyo hivyo pia ni mojawapo ya njia ya kumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala. Lakini makosa unayofanya ni kukusanya hizo khitma siku ya tarehe 27 ya Ramadhaan kwa niya ya kuwombea wazazi wako. Hakuna dalili ya uthibitisho katika Qur-aan au Sunnah kwamba thawabu za kusoma Qur-aan zinamfikia maiti, bali unaweze kuwafanyia wema wazazi waliofariki ni kuwatolea sadaka, kuwafanyia hajj na mema yoyote mengine kwa niya yao na Insha Allaah thawabu zitawafikia.

 

Kusoma majina ya Allaah 99 hakuna ubaya lakini sio kuyasoma kwa nia ya kumshukuru, kwani kila jina la Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) lina Sifa fulani, kwa hiyo unaweza kuyatumia kwa kumuomba jambo fulani kutokana na ile sifa inayolingana na jina lenyewe, mfano ukitaka Akughufurie madhambi utasema 'Yaa Ghafuwru', ukitaka Akusamehe utasema 'Yaa 'Afuwwu' ukitaka Akuruzuku utasema 'Yaa Razzaaqu', ukitaka kumshukuru utasema 'Ya Shakuru", 'Yaa Hamiydu' na kadhalika. Inakupasa ujue maana ya majina Yake Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)  na Sifa Zake ndipo utaweza kuyatumia inavyopasa.

 

 

Na Allah Anajua zaidi

 

 

 

Share