Ametoa Kiapo Bila Kukusudia, Atoe Kafara Au Afanye Nini?

SWALI:

 

Assalam alaykum wa Rahmatullah;

Shukrani kwa mashekhe na wandeshaji wa Alhidaaya. Ningependa kuuliza swali kuhusu malipo ya kiapo ambacho hakikusudiwa. Je nini hukmu ya mtu kuapa kutofanya kitu bila ya kukusudia? Je, mtu huyu anawajibika kulipia kiapo? Niliapa kiapo lakini sikukusudiya kuapa, kiapo kilinitoka tu kwa sababu ya hasira. Na mtu niliyomuapia ni mtoto, kumnyan'ganya toy na kumwambia kuwa sitompa tena, kisha kwa huruma nikarudi kumpa, na makusudio yangu yalikuwa ni kumfanya atulie asinisumbue lakini siku. Je ninatakiwa kufunga siku tatu kwa vile siwezi kutumiza masharti ya mwanzo ya kiapo? Ahsante.


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuapa kiapo bila ya kukusudia.

 

Mwanzo tungependa kuwausia wazazi au walezi wawe makini na wasiwe na hasira hasa kwa watoto, kwani watoto hao huwa wanawatazama wazazi na walezi wao kama kielelezo chema kwao. Watoto wanatakiwa walelewe vyema kwa maadili mema. Miongoni mwa maadili mema ya walezi kwa watoto wao na watu wengine ni kuweza kuzima hasira zao pindi wanapoudhiwa.

 

Hakika ni kuwa kiapo au yamini kutambuliwa kisheria ni lazima itimize masharti fulani. Yamini ambayo inahitajia kafara ni ile inayofanywa kwa jina la Allaah Aliyetukuka, ama ile inayofanywa kwa asiyekuwa Allaah haifai na ni haramu. Na masharti yaliyopo kuwajibisha kafara anapoapa mtu kwa jina la Allaah Aliyetukuka ni kama yafuatayo:

 

1.     Iwe yamini (kiapo) imefanywa kwa mwenye kuapa kukusudia kutenda kwa jambo la mustakbali linalowezekana. Na haiwi kutekeleza ila kwa mustakabali wa wakati, sio uliopita. Na atakapokula yamini bila ya kusudio kwayo, kama vile kusema: Hapana, naapa kwa Allaah; Na ndio, naapa kwa Allaah. Naye katika hilo hajakusudia yamini, na hakika limetokea hilo ulimini bila kukusudiwa, huo utakuwa ni upuuzi. Kwa hilo, hakutakuwa na kafara yoyote, nayo ni kwa kauli ya Aliyetukuka: “Allaah Hatakushikeni kwa viapo vyenu vya upuuzi, lakini Atakushikeni kwa mnavyoapa kweli kweli kwa makusudio” (al-Maa’idah [5]: 89). Na Hadiyth ya ‘Aa’ishah (Radhiya Allaahu ‘anha) marfuu’ kuhusu laghwu (upuuzi) katika yamini kuwa, “Hayo ni maneno ya mtu nyumbani kwake: Sivyo hivyo, WaLlaahi (Naapa kwa Allaah); Na ndio, WaLlaahi” (Abu Daawuud)

2.     Awe amekula kiapo kwa khiari sio kulazimishwa na yeyote. Ikiwa amelazimishwa yamini yake haitachukuliwa kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Ummah wangu umenyanyuliwa makosa, kusahau na kwa wanayotendeshwa nguvu kwayo” (Ibn Maajah na ad-Daraqutwniy).

3.     Kuacha kutekeleza yamini, kwa kufanya alichokulia kiapo kwa kuacha au kuacha alichokula kiapo katika kuifanya kwa kuchagua kwa kukumbushwa yamini hiyo. Akiacha kutekeleza kwa kusahau yamini yake au kutenzwa nguvu, hatokuwa na kafara juu yake, kwani hana dhambi kwayo. Hii ni kwa kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) tuliyoitaja hapo juu. Na akivua katika yamini yake, kama kwa kusema: Naapa kwa Allaah nitafanya kadhaa Akipenda Allaah, hatokuwa ameacha yamini yake akivunja hilo; kwa sharti akusudie kuvua kuunganisha yamini kwa lafdhi au hukumu. Hii ni kwa kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Aliyeapa kwa kusema: Apendapo Allaah, hatokuwa ameacha” (Ahmad, at-Tirmidhiy, Abu Daawuud na an-Nasaa’iy). Ikiwa hatokusudia kuvua (isipokuwa), bali alikusudia kwa kauli yake: “Akipenda Allaah”, kupata Baraka kwa lafdhi hii, sio kuunganisha. Au asiseme: “Akipenda Allaah”, ila baada ya kupita wakati wa kumaliza lafdhi ya yamini bila udhuru, hakutomfalia chochote kuvua huku. Na pia panasemwa: Kutamfaa kule kuvua, hata ikiwa hakutaka hilo ila baada ya kumaliza yamini, hata kama ataambiwa na baadhi ya waliokuwepo hapo: “Sema: Akipenda Allaah”, itamnufaisha. Na akasema Ibn Taymiyah: “Hii ndio rai iliyo sawa”.

 

Baada ya hayo tuliyo yatanguliza hapo juu ni wazi kuwa kiapo chako hicho ni katika laghwu, hivyo hakuna kafara juu yako. Hata hivyo, ni muhimu sana kwa Muislamu asiwe ni mwenye kuapa kila wakati kwa mambo madogo kama mfano wa hayo ya kwako na mtoto kama ulivyofanya. Muislamu anatakiwa aseme yaliyo mazuri na akiwa hana cha kusema basi anyamaze na hilo litakuwa bora zaidi kwake.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share