Kwa Nini Waislamu Tukiswali Tunaelekea Qiblah?

SWALI:

Mimi swali langu; (1) Kwa nini waislamu tunaelekea kibla wakati wa ibada zote?

 

 


 

JIBU:

AlhamduliLLaah - Himdi Na Sifa Zote Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani ndugu yetu kwa swali hili linalohusiana na kuelekea Waislamu wanaposwali.

Mwanzo tunapenda kuieleza ibara inayosema, “Waislamu tunaelekea Qiblah wakati wa Ibaadah zote”. Ibara hii si kweli kwani Ibaadah ambayo Waislamu wanaelekea Qiblah ni Swalah peke yake. Hakika ni kuwa zipo Ibaadah nyengine ambazo hufai kuzifanya ukielekea Qiblah mfano ni kukidhi haja ndogo au kubwa. Katika maagizo ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni kutokipa Qiblah mgongo wala kukielekea. Ibaadah ya Funga, Zakah, Hijjah, Jihaad, kufanya kazi, kusoma si lazima uelekee Qiblah. Lakini ufahamu na ibara hii imekuja kwa ule muono wetu finyu kuwa Ibaadah ni Swalah peke yake.

Ifahamike kuwa Ibaadah katika Uislamu ni kila jambo la halali unalolifanya ili kupata ridhaa ya Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala). Ukifanya jambo hilo unapata thawabu. Hivyo, zimekuja Hadiyth kutufahamisha kuwa hata kustarehe na mkeo ni aina ya Ibaadah na unapata thawabu kwayo (Muslim).

Sasa labla tukija katika mas-ala ya Swalah na kuelekea Qiblah ni kuwa hili ni agizo kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) na mtihani kwetu. Je, katika amri hii tutakuwa ni wenye kusitasita au vipi? Muislamu ni yule ambaye amejisalimisha kabisa kwa Allaah na pindi anapopatiwa amri anakuwa ni mwenye kuitii bila ya wasiwasi wa aina yoyote. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasema: “

Haiwi kwa mwanamume aliyeamini wala mwanamke aliyeamini, Allaah na Mtume Wake wanapokata shauri, wawe na hiari katika jambo hilo. Na mwenye kumuasi Allaah na Mtume Wake, hakika amepotea upotevu ulio wazi kabisa” (33: 36).

Muislamu mzuri ni yule anayesema:

 “Tumesikia na tumetii” (2: 285).

Na kutii huko kunakufanya wewe uwe miongoni mwa wenye ilimu kwani wao ndio wenye kusema hivyo:

Na wale waliozama katika ilimu husema: ‘Tumeziamini zote zimetoka kwa Mola wetu’. Na hawakumbuki hayo isipokuwa wenye akili” (3: 7).

Hakika ni kuwa kuelekea sehemu fulani katika maombi au Ibaadah fulani au zote ni jambo ambalo linaeleweka sana na Waislamu na wale waliokuwa Waislamu lakini wakapotosha vitabu vyao kama Mayahudi na Manasara. Hili lipo wazi katika maandiko na halina utata. Hebu tutazame baadhi ya Aayah za Qur-aan zinazozungumzia jambo hilo.

Waislamu walikuwa wanaelekea al-Quds kabla ya kuhamia Madiynah na baada ya hapo waliendelea kuelekea huko kwa muda wa miezi 16 au 18 kabla ya kubadilishwa Qiblah na Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) kuelekea al-Ka‘bah au Msikiti Mtukufu wa Makkah. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasema:

  “Bila shaka! Tumekuona ukielekeza uso wako mbinguni. Kwa hakika, Tutakubadilishia Qiblah ambacho kitakuridhisha, kwa hivyo geuza uso wako kuelekea Masjidul-Haraam (Msikiti Mtukufu wa Makkah). Na popote watu wako watakapokuwa, geuzeni nyuso zenu huko. Bila shaka, watu waliopewa Vitabu (Mayahudi na Manasara) wanajua vizuri kuwa huu ndio ukweli kutoka kwa Mola wao. Na Allaah hajaghafilika na wanayoyafanya” (2: 144).

Anasema tena Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala):

 “Na popote unapoanza (kwa Swalah), geuza uso wako kuelekea Masjidul-Haraam, na popote mutakapo kuwa elekezeni nyuso zenu huko (Makkah mutakapo kuwa mnaswali)… ” (2: 150).

Mayahudi waliokuwa Madiynah walipiga makelele sana kuhusu kubadilishwa Qiblah. Qur-aan iliwarudi kuwa sehemu zote ni za Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala), Naye ndiye pekee Mwenye kuweka Qiblah kwa mtu mwenye kuswali. Tafadhali tazama Surah 2, Aayah 142 – 143.

Hao wajinga walisema: “Bila shaka, Swalah za Waislamu kwa miaka yote iliyopita zimepotea na hawatapata thawabu zozote, kwani hazikufanywa kwa kuelekea katika Qiblah kilicho sahihi”. Akajibu Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala): “Na Allaah hatazifanya imani zenu kupotea bure”. (2: 143)  

Kumaanisha Swalah zenu zilifanywa katika Qiblah kilicho kuwa sahihi kilichoridhiwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala).

Ibara hii hapa ni muhimu sana, Anaposema Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala): “Bila shaka, watu waliopewa Vitabu (Mayahudi na Manasara) wanajua vizuri kuwa huu ndio ukweli kutoka kwa Mola wao. Na Allaah hajaghafilika na wanayo yafanya” (2: 144). Hakika ni kuwa nao pia walikuwa wakielekea sehemu fulani walipokuwa katika maombi yao lakini baada ya kubadilishwa Qiblah walikataa hilo japokuwa wanaelewa vyema kuwa hiyo ni haki.

Jambo hili la kuelekea sehemu fulani katika maombi linatekelezwa hata na baadhi ya makabila yanayofuata dini za kitamaduni. Mfano hai ni Wakikuyu wanaoishi Kenya ambao wanaelekea mlima Kenya. Huzuni ni kuwa waliopewa Vitabu walibadilisha maandiko ili kukidhi maslahi na matashi ya binafsi, lakini hakika hii wanaijua zaidi ya watoto wao.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share