Kuzinyoa Nyusi Za Katikati Zilizozidi Sana Na Kuungana

 

Kuzinyoa Nyusi Za Katikati Zilizozidi Sana Na Kuungana

 

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

Mimi ni kijana ambaye nyusi zangu zimetanda. Yaani zimeshikana. swali ni kuwa mimi huzinyoa hizi za katikati. Je hii pia haifai?

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Miongoni mwa ya  kupindukia mipaka katika kujipamba, ni ambayo yameharamishwa na Uislamu, nayo ni kuchonga nyusi, nako ni kutoa nywele za nyusi kwa ajili ya kuzifanya ziinuke au ziwe sawa. Hawa wenye kufanya hivyo wamelaaniwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).

 

 

Jambo hili huzidi kuwa haramu kwani ni alama ya wanawake waovu au wasiokuwa Waislamu.

 

 

Hadiyth ifutayo inatuonyesha uharamu wake:

 

‘Abdullaah bin Mas’uwd (Radhwiya Allaahu 'anhu)  alisema: “Allaah Anawalaani wanaopiga chale na wanaotaka kupigwa chale, na wanaochonga nyusi na wanaochonga meno wakaacha mwanya kwa sababu ya uzuri, wanaobadilisha maumbile Aliyoyaumba Allaah.” Mwanamke mmoja akamlaumu juu ya jambo hilo (la kulaani). Akasema (‘Abdullaah): “Kwa nini nisimlaani aliyelaaniwa na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na ilhali iko ndani ya Kitabu cha Allaah? Allaah Aliyetukuka Anasema: ((Na lolote analokupeni Rasuli (صلى الله عليه وآله وسلم) basi lichukueni, na analokukatazeni, basi acheni. [Al-Hashr (59: 7)])). [Al-Bukhaariy na Muslim, Abuu Daawuwd, At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Ibn Maajah] 

 

 

Imaam Al-Haafidhw Zakiyyud-Diyn 'Abdil-'Adhwiym bin 'Abdil-Qawiyy Al-Mundhiriy katika kitabu chake Tahdhiyb at-Targhiyb wat Tarhiyb minal Ahaadiyth asw-Swihaah, uk. 353 – 354 anatueleza faida ya Hadiyth tuliyoinukuu hapo juu kwa kusema: "Kuharamishwa kuungwa nywele, kuchonga meno, wenye kuchanja, kuchonga nyusi na matendo ya kujipamba ambayo yanakaza ngozi na kukataza kutokeza kwa mikunjo na miaka kusonga. Hekima ya kuharamishwa haya yote ni kule kubadilisha maumbile ya Allaah na kutoa picha ya ughushi, udanganyifu na uongo. Yanapodhihiri mambo haya haramu katika jamii, ni dalili kubwa ya uharibifu, ubadhirifu dhahiri na kuipatia dunia umuhimu. Kila mara anapozidi mwanamke kukimbia nyuma ya umbo la uongo, ndipo anauendea haraka uzee, hivyo kupoteza uzuri wake na kuwa ajuza mapema."

 

 

Ikiwa nyusi za mwanamke au za mwanamume zimezidi kuwa nyingi hadi zinaning'inia na kufunika macho na kuleta taathira ya uonaji, inafaa kuzitoa sehemu hiyo inayosababisha tatizo.

 

 

Ama kuhusu nyusi kuungana, ikhtilaaf za ‘Ulaamaa zimepatikana, kuna wanaosema inafaa kuzinyoa kwa kuona kwamba hiyo si sehemu ya nyusi. Na kuna wanaokataza kwa kuwa wameona kwamba madamu hazileti madhara ya uonaji hakuna sababu ya kuzitoa kwani kuzitoa ni kwa ajili ya kuleta uzuri.

 

 

Kutokana na ikhtilaaf hizo tunaona kwamba, ikiwa nyusi hizo za katikati zilizoungana zikiwa hazina madhara yoyote ni bora kuziacha, na hunda utakapoanza kuzinyoa ukafikia kuzinyoa na hizo ambazo si za katikati na ukaingia kwenye laana zilizotajwa katika Hadiyth na pia ukashawishika kwa kuzinyoa hizo, ukawa unafikia kuzitengeneza na nyusi zako za kawaida kwa kuhisi kunakupendeza na hivyo ukawa umeshatumbukia kwenye makatazo na madhambi.

 

 

Bonyeza kiungo kifuatacho kwa maelezo zaid:

 

Kunyofoa Au Kunyoa Au Kuchonga Nyusi Ni Kulaaniwa na Allaah

 

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

Share