Masharifu Wasioswali Wana Maovu Na Maasi Watukuzwe? Je, Wao Bora Kuliko Mja Anayefuata Shari'ah?

 

SWALI:

Salamun alykum jamia, rehma na amani zitufikie wote kwa ujumla, na mwenyezi mungu atuzidishie imani kwa sote.

Swali langu lilikuwa kutaka kujuwa kama masharifu tuna haki ya kuwahishimu na kuwapa heshima hata kama wao hawasali na wanafanya mambo kinyume na shariya ya kiislamu, kwa mfano wanalewa, hawafungi ramadhani wanasema uwongo wanatenda vitendo vingine hata kuvitaja siwezi.... swali ni hivi je wao bora zaidi kuliko sisi hata kama sisi tunafata sharia ya kiislamu, na woa hawafati basi wao ni bora kwa sababu ni masharifu tukiwaona wajibu wetu kuwa busu mikono yao na kuwapa heshima kubwa  hatuna haki ya kuwahukumu kwa lolote kutokana  darja lao  kubwa kwa mwenyezi mungu kuliko sisi tunayefanya ibada, ibada yao 1 sawa na sisi 10  

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu utukufu wa binadamu. Tufahamu kuwa Uislamu umekuja kuwaweka sawa wanaAadamu wote, ubora unakuja tu kwa uchaji Mwenyezi Mungu sio kwa ukoo au kabila. Kama ingekuwa Masharifu ni bora, hivyo basi wale ambao tungetakiwa tuwaheshimu zaidi miongoni mwao ni Abu Twaalib na Abu Lahab kwani wote walikuwa ami zake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) lakini Qur-aan imetufahamisha wazi kabisa kuwa Abu Lahab ataingia Motoni.

Qur-aan na Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zimetuwekea msingi ya uadilifu na usawa. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Enyi watu! Hakika Sisi Tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na Tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Allaah ni huyo aliye mcha Mungu zaidi katika nyinyi. Hakika Allaah ni Mwenye kujua, Mwenye habari” (49: 13).

Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) naye ametuambia katika Hijjah yake ya mwisho:

"Hakuna ubora kwa mweupe juu ya mweusi, wala Mwarabu juu ya asiyekuwa Mwarabu, ila kwa ucha Mungu".

Amesema tena (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

"Enyi Maquraysh! Jinunueni nafsi zenu kutoka kwa Allaah, kwani mimi sitowafaa kitu kwa Allaah. Enyi Bani 'Abdi Manaaf, sitowafaa kitu kwa Allaah. Ewe Swafiyyah (shangazi yake), sitokufaa kitu kwa Allaah. Ewe Faatwimah (binti Muhammad) niombe utakalo, lakini sitokufaa kitu kwa Allaah" (Ahmad).

Na katika Hadiyth yake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatuambia kuwa yeyote atakayecheleweshwa kwenda Peponi kwa sababu ya amali zake kuwa ni nzuri hatatangulizwa mbele katika kuingia katika Pepo na nasaba yake. Hii ni kwa Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

"… Na mwenye kucheleweshwa kwa amali yake haitamtanguliza nasaba yake" (Ahmad na Muslim).

Kwa hiyo, awe mtu ni Mquraysh au Sharifu kama anavyodai lakini hafuati kanuni zilizowekwa na Allaah Aliyetukuka na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na haswa kwa kufanya madhambi makubwa basi hafai mtu kama huyo kuheshimiwa bali anatakiwa asusiwe kwa anayofanya. Huenda kufanywa hivyo akahisi makosa aliyonayo na kurudi katika Dini kwa kufuata maagizo ya Aliyetukuka.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share