Mtindo Wa Kusujudu Baada Ya Kupata Ushindi Katika Michezo Akiwa Hakuvaa Nguo Za Sheria Unakubalika?

 

Mtindo Wa Kusujudu Baada Ya Kupata Ushindi Katika 

Michezo Akiwa Hakuvaa Nguo Za Sheria Unakubalika?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Asaalam alaikum kwa mara nyengine tena ndugu zangu wa alhidaaya napenda kurejea suala langu tena kwenu. Kwamba je? Kusujudu wakati wa michezo hasa unapokuwa unashiriki katika michezo ikiwa wewe mwenyewe binafsi au mfano wako ukichukulia wakati huo tuseme unakua umevalia vifaa vya michezo ambavyo haviendani na sheria za kiislam labda umevaa kaptula fupi nk sana vitendo hivi hutokea mwanzoni mwa mchezo wenyewe au baada ya kupatikana ushindi. Tunaomba jibu tupate kuelimishana asante.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Mwanzo tufahamu kuwa michezo mingi yenye kumpatia nguvu Muislamu imehimizwa sana na Uislamu. Hata hivyo, michezo yenyewe ni lazima ifanywe katika mtindo ambao Uislamu unataka sio kwa misingi ya taasisi za michezo ambazo hazina Dini. Kukubali Waislamu na nchi za Waislamu kupeleka washindani katika mashindano hayo wakiwa wamevaa nguo za utovu wa adabu, kinyume na sheria ni kosa kubwa. Hii yote inaonyesha jinsi gani tulivyokengeuka katika kufuata sheria yetu au tukaona mashindano ni bora zaidi kuliko hata kutii amri ya Allaah Aliyetukuka au Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Kukubali huko ni kuifanyia istihzai Dini, na hakuna Muislamu mwenye Imani yake atakayekubali kufanya hivyo. Ikiwa ni hivyo mwana michezo huyo anaweza kufanya lolote atakalo baada ya kushinda. Lakini je, kufanya kwake huko kunakubaliwa kisheria? Jibu ni kuwa mtu huyo atakuwa anafanya makosa ya ziada baada ya kosa lake la kwanza. Na kufanya hivyo ni kuifanyia istihzai Dini yetu. Papo mahali pengi pa kufanyia sijdah kwa ajili ya Allaah Aliyetukuka hata kiwanjani lakini kwa jinsi hiyo haifai.

 

Tufahamu sijdah ya kushukuru ipo katika Dini yetu Tukufu lakini ni katika kheri inayokufikia wala sio katika michezo kama mpira au nyenginezo katika michezo tena katika hali ambayo Muislamu haifai kuwa kwayo, mathalan utakuta hayo ni mashindano ya kombe la pombe, au yanadhaminiwa na kampuni ya pombe, kamari, n.k. kama tuonavyo leo hii katika nchi nyingi. Kisha mtu huyo huyo anayeshiriki mashindano kama hayo, huku akiwa hajastiri ‘awrah yake, unamkuta baada ya kufunga goli anasujudu. Je, anasujudu kufurahia kushinda mashindano ya kombe la pombe au kamari au upuuzi mwengine wa kidunia? La, hayo hayafai na yanakebehi Uislam badala ya kuutangaza.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share