Mtu Mwenye Majivuno Atasamehewa?

SWALI:

 Assalam alaykum

Kwanza napenda kumshukuru Allah kwa kuniweza kupata nafasi hii ya kuweza kuuliza maswali na kutujaalia kuwa na maustadh ambao wanajitolea kuelimisha jamii ya kiislamu. Swali langu lilikuwa je mtu akiwa ana swali, anatoa zaka, na anafanya ibada nyingine lakini mtu huyo huyo anatokea mtu wenye majivuno je Allah anaweza kumsamehe. Au hato msamehe kama hajaomba msamaha. Kama kumbukumbu zangu ziko sawa basi nakumbuka kusoma aya ambayo inasema kuwa Allah atawasamehe na atawafutia waumini walio tenda wema makosa yao  kwa kuwa wamefuata haki. Lakini pia kuna aya ambayo inasema.

 GHAAFIR 60. Na Mola wenu anasema: Niombeni nitakuitikieni. Kwa hakika wale ambao wanajivuna na kuniabudu Mimi wataingia Jahannamu wadhalilike.

Katika aya inaonyesha ubaya wa kujivuna. Swali langu la pili ni je majivuno yanaweza kuharibu amali zote za mtu na hatimaye ikamwingiza motoni? Na je kama umejevuna bila kujua au kukusudia je utakuwa na dhambi? Hayo ndio maswali yaliokuwa yanatatiza. Asante kwa muda wako wala mimi sina uwezo wa kulipa kwa juhudi zako juu ya kuwasaidia watu kuelekea kwa Allah ila mwenyewe Allah.

 


 

JIBU:

Sifa zote njema anastahiki Allah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Salah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), ahli zake, Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani kwa swali lako kuhusu toba. Ni kitu kilicho wazi kuwa kosa lolote ambalo mwanadamu na hasa Muislamu analofanya ni lazima aombe msamaha. Na anapoomba msamaha ni lazima atimize masharti ya toba. Wamesema wanavyuoni:

“Toba ni wajibu kwa kila dhambi. Ikiwa dhambi aliyoifanya mja ni baina mja na Allah aliyetukuka haiingiliani na haki ya binadamu,  itakuwa na sharti tatu:

Ya kwanza: Kuacha maasiya.

Ya pili: Kujuta kwa kufanya hayo maasiya.

Ya tatu: Kuazimia kutorudia tena kosa lile milele.

Likikosekana sharti moja katika hizi tatu basi toba haitosihi”.

Na ikiwa dhambi iliyofanywa  ina mafungamano na mwanaadamu sharti za kupata toba zinakuwa ni nne: “Sharti hizo tatu zilizotajwa hapo juu na ya nne ni kuirudisha haki ya yule mtu, ikiwa ni mali au kitu chengine chochote umrudishie. Ni wajibu kwa Muislamu kutubu (kuomba msamaha) kwa madhambi yote. Ikiwa atatubia baadhi ya dhambi husihi toba yake kwa dhambi ile na zinabaki zile zilizobakia. Hii aya ambayo umeitoa inafanana na aya mbili katika Suratun Nisaa’ ambazo zina maana zifuatazo:

((Hakika Mwenyezi Mungu Hasamehe kushirikishwa, na Husamehe yaliyo duni ya hilo kwa Amtakaye. Na anaye mshirikisha Mwenyezi Mungu basi hakika amezua dhambi kubwa)) (4: 48). Na: ((Hakika Mwenyezi Mungu Hasamehi kushirikishwa na kitu. Lakini Yeye Husamehe yasiyokuwa hayo kwa Amtakaye. Na anayemshirikisha Mwenyezi Mungu basi huyo amepotea upotovu wa mbali)) (4: 116).

Lakini katika mas-ala haya, Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anatuweka wazi kuwa Yeye Anasamehe madhambi yote na wala tusikate tamaa katika hilo kwani Yeye Ametuahidi pale Aliposema:

((Sema: Enyi waja wangu waliojidhulumu nafsi zao! Msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu Husamehe dhambi zote. Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. Na rejeeni kwa Mola wenu Mlezi, na silimuni kwake, kabla ya kukujieni adhabu. Kisha hapo hamtanusuriwa)) (39: 53 – 54).

Hivyo, maadamu mtu atatubia kikweli kweli basi atasamehewa. Ikiwa dhambi kubwa zaidi ambayo ni shirki husamehewa mtu seuze majivuno.  

Hakika kwa mwenye kutaka msamaha wa kweli basi hata madhambi yake hubadilishwa na Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) kuwa mema pindi anapojibadilisha na kutenda yaliyo mema. Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:  

((Isipo kuwa atakayetubu, na akaamini, na akatenda vitendo vyema. Basi hao Mwenyezi Mungu Atayabadilisha maovu yao yawe mema. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. Na aliyetubu na akafanya mema, basi hakika huyo ametubu kweli kweli kwa Mwenyezi Mungu)) (25: 70 – 71).

Hakika kujivuna ni jambo ambalo limekatazwa kabisa katika Uislamu. Hili ni kosa ambalo linaharibu mema ya Muislamu na wanaadamu, hivyo tufanye juhudi katika kujitoa katika kosa hilo. Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema, "Allah Aliyetukuka amesema: ((Kibri ni vazi Langu na utukufu ni vazi Langu la chini na Nitamtia motoni yeyote anayeshindana Nami katika moja ya hivyo viwili)) [Abu Daawuud kutoka kwa Abu Hurayrah  (Radhiya Allaahu 'anhu)

Na amesema tena: ((Mtu mmoja alipokuwa anatembea, huku anaburuza nguo yake kwa kibri, alifanywa amezwe na ardhi na ataendelea kudidimia ndani yake mpaka Siku ya Kiyama)) [Al-Bukhari kutoka kwa Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu 'anhu)].

Na amesema tena (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Allah Hatomwangalia mja Siku ya Kiyama kwa sababu ya kuburuza nguo yake kwa kibri))  [Al-Bukhaariy kutoka kwa Abu Hurayrah na Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu 'anhu)]  

Na amesema tena: ((Yeyote atakaye kufa bila ya kuwa na kibri, utovu wa uaminifu katika ngawira na deni ataingia peponi)) [At-Tirmidhiy, Ibn Maajah na ad-Daarimiy kutoka kwa Thawbaan (Radhiya Allaahu 'anhu)].

 Na amesema tena: ((Yeyote mwenye chembe ndogo ya kibri katika moyo wake hataingia peponi)) [Muslim kutoka kwa Ibn Mas‘uud (Radhiya Allaahu 'anhu)].   

 Na zipo aya nyingi zinazoelezea kuhusu kibri na sifa hiyo inaharibu 'amali kabisa na hivyo kumuingiza mtu motoni.

Ikiwa umekuwa na sifa hiyo bila ya kujua Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atakusamehe lakini pindi unapofahamu na kujua hilo inabidi ufanye juhudi kubwa kuiacha tabia hiyo. Allah Anasema:

 ((Hakika toba inayokubaliwa na Mwenyezi Mungu ni ya wale wafanyao uovu kwa ujinga, kisha wakatubia kwa haraka. Hao ndio Mwenyezi Mungu Huwakubalia toba yao, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na ni Mwenye hekima)) (4: 17).

Twatumai tutakuwa tumejibu maswali yako yote.

Na Allah Anajua zaidi.

 

Share