Kuchangia Katika Harusi Yenye Maasi

 

Kuchangia Katika Harusi Yenye Maasi

 

Alhidaaya.com 

 

 

Swali:

 

Assalamu Alaykum

 

Mimi nina ndugu waliyo kutana katika kikao cha harusi kuhusu wa fanye nini, kuhusu harusi ya mtoto wa ammi yao.

Mama yake bwana harusi akasema yeye anataka maulidi tu. Na hiyo sisi tunayaona ni bida. Lakini kuna wingine katika kikao hicho waliyo hudhuriya wakiwa ni ndugu zake huyo mume na shangazi zake na baba yake wao wakasema wa nataka reception ya ni (party) na hiyo nim kusanyiko ya wanaume na wanawake. Ndugu zangu mimi wakayakata hayo wanayoyotaka na wakawambiya Allaah hayaridhi kabisa haya nao wamishkiliya kufanya hivyo hivyo ndivyo watakavyo fanya baada ya nikaha wata fanya reception na hao ndugu zangu wametakiwa kutoa mchango wa harusi sasa wao wanogopa kutoa hizo pesa ikiwa zita fanyiwa mambo ya munkar. Tunaomba kama kuna nansaha zaidi tuwapatie huwenda wa kazingatia.

 

Vipi hao watoe mchango wa harusi?

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Hapana shaka kwamba Waislamu kusaidiana katika shida na mahitaji mbali mbali ni amali njema tulizoamrishwa kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ ۚ

Na Waumini wanaume na Waumini wanawake ni marafiki wandani wao kwa wao, [At-Tawbah: 71]

 

Vile Vile tunapata mafunzo mengi kuhusu kuamiliana kwa wema na kusaidiana kutoka Hadiyth mbali mbali mojawapo ifuatayo:

((إِنَّ الْمُؤْمِنَ لِلْمُؤْمِنِ كَالْبُنْيَانِ يَشُدُّ بَعْضُهُ بَعْضًا))  وَشَبَّكَ أَصَابِعَهُ   رواه البخاري ومسلم    

"Hakika Muumini Kwa Muumini ni kama jengo, wanashikamana pamoja" Akafungamisha Vidole vyake pamoja [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Ama kusaidia katika shughuli ambazo zina maovu, maasi na uzushi kama ulivyotaja, bila shaka ni jambo ambalo halimpasi Muislamu kuchangia, kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

وَتَعَاوَنُوا عَلَى الْبِرِّ وَالتَّقْوَىٰ ۖ وَلَا تَعَاوَنُوا عَلَى الْإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ ۚ 

Na shirikianeni katika wema na taqwa, na wala msishirikiane katika dhambi na uadui. [Al-Maaidah :2]

 

Jambo la mwanzo linalokupasa ufanye wewe na ndugu zako ambao AlhamduliLLaah mmeyaona kuwa ni mambo maovu, ni kuzidi kuwalingania katika kuacha hayo maovu bila ya kuchoka kwani hii ni amri kutoka kwa Rabb wetu na Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika kuamrishana mema na kukatazana maovu. Unaweza kuchukua mada mbali mbali zilizomo Alhidaaya ambazo zimekataza maovu hayo, kuwachapishia na kuwapa kila mmoja asome. Baadhi yake tunakuwekea tayari hapa:

 

Ikhtilaatw (Kuchanganyika Wanaume Na Wanawake)

 

Zijue Sababu Za Kumfanya Muislam Asisherehekee Maulidi

 

Mawlid – Mtazamo Wa Kishari'ah

 

Vile vile chapisha Maswali na Majibu yafuatayo:

 

Kuchangia Na Kushiriki Shughuli Za Bid-ah Ni Dhambi?

 

Kusoma Maulidi Kwenye Harusi Badala Kupiga Ngoma Inafaa?

 

Watakapoitikia wito na kukubali kuacha maovu hayo, hakuna budi kuwasaidia katika mchango wa kutekeleza shughuli hiyo muhimu, lakini wakishikilia watakavyo basi haikupasini kuchangia kwani mtakuwa mnachangia katika maasi na mtachuma dhambi. Kuchangia huko ni kama mfano wa kuchangia katika maasi mengine kutokana na kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth zifuatazo: 

عن أنس قال  : لعن رسول الله صلى الله عليه وسلم في الخمر عشرة : عاصرها , ومعتصرها , وشاربها , وحاملها , والمحمولة إليه , وساقيها , وبائعها , وآكل ثمنها , والمشتري لها , والمشتراة له   رواه الترمذي وابن ماجه

Kutoka kwa Anas kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amelaani mambo kumi yanayohusiana na ulevi; mwenye kuukamua (kuutengeneza), Mwenye kutengenezewa, mnywaji, mbebaji, anayebebewa, anayeendesha (kuupeleka ulevi), muuzaji, anayekula thamani yake, anayenunua na anayeuza. [At-Tirmidhiy na Ibn Maajah)

 

Vile vile katika kuchangia riba: 

عن جابر رضي الله عنه عن النبي صلى الله عليه وسلم : ((لعن الله آكل الربا، وموكله، وكاتبه وشاهدي))  مسلم

Kutoka kwa Jaabir (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Allaah Amelaani anayekula riba, anayewakilisha, anayeandika na anayeshuhudia)) [Muslim]

 

Kwa hiyo kutokuchangia kwenu katika shughuli zenye maasi kutawaweka katika Ridhaa Ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwani Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((مَنْ أَعْطَى لِلَّهِ تَعَالَى وَمَنَعَ لِلَّهِ تَعَالَى وَأَحَبَّ لِلَّهِ تَعَالَى وَأَبْغَضَ لِلَّهِ تَعَالَى وَأَنْكَحَ لِلَّهِ تَعَالَى فَقَدْ اسْتَكْمَلَ إِيمَانَهُ))   أحمد   والترمذي   وأبو داود    وحسنه الألباني .

((Yeyote atoaye kwa ajili ya Allaah, akazuia kwa ajili ya Allaah, Akapenda kwa ajili ya Allaah, Akachukia kwa ajili ya Allaah, akaoa kwa ajili ya Allaah, atakuwa ameikamilisha Iymaan yake)) [Ahmad, At-Tirmidhiy Abu Daawuud na Shaykh Al-Albaaniy ameipa daraja ya Hasan]

 

Hata kuhudhuria katika shughuli hizo pia hazifai na haitomaanisha kwamba mmekata mawasiliano na undugu, bali itakuwa ni kujihifadhi kwenu kutokana na kuona na kusikiliza maovu. Muwafahamishe jamaa zenu kwamba pindi watakapoacha hayo maovu basi mtakuwa tayari kuchangia kwa hali na mali.  

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share