Ufafanuzi Kuhusu Aayah Inayosema “Mali Zenu Na Watoto Wenu, Wake Zenu Fitna”

SWALI:

 

Assalamu aleykum warahmatullah wabarakat

 

Imetajwa katika Qur-ani tukufu kuwa mali zenu, wake zenu, na watoto ni fitna kwenu. Kama mume anaichukulia aya hii moja kwa moja tu bila hata kuona hiyo fitna ya mke na watoto, madam imetajwa tu basi kwake yeye mke na watoto ni jamii au ni kitu cha mwisho katika maisha yake wala hakipi umuhimu wake inavyotakiwa na ilivyosunniwa, na pia kwake yeye ni watu wa kuwa sacrificed for anything at anytime. Je hii ni sawasawa? Naomba ufafanuzi wa jambo hili na aya yenyewe katika Qur-an na makusudio yake kiwazi kwani ina affect not only the motherhood, but hata the social behaviour and the self esteem (confidence) of the innocent growing children

 

Kwanza kabisa natoa shukurani kwa waanzilishi na wahusika wote wa Alhidaya, Mwenyezi mungu atawajaalia kila lenye kheri fildunia wal akhira.

Niliwahi kutuma suala langu kuhusu mada ya hapo juu "vipi mke na watoto huwa ni fitna?"Lakini sikuona jibu bado. Naomba radhi kwa kuchanganya lugha. Shukran


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu ufafanuzi wa Aayah inayosema kuwa wake na mali zenu, na watoto wenu ni fitna. Hakika Aayah hii imeeleweka vibaya kama vile zilivyoeleweka nyingine ambazo kwa kuzielewa vibaya kunaleta athari mbaya katika jamii yetu ya Kiislamu.

Mwanzo kabisa Aayah yenye maana hiyo japokuwa hazikujumlishwa aina zote hizo tatu. Na maana ya Fitnah iliyotumika ni mitihani. Allaah Aliyetukuka Anasema:

Enyi mlioamini! Hakika miongoni mwa wake zenu na watoto wenu wamo maadui zenu. Basi tahadharini nao. Na mkisamehe, na mkapuuza, na mkaghufiria basi hakika Allaah ni Mwingi wa maghfira, Mwenye kurehemu” (64: 14).

 

Katika Aayah hii inatueleza makundi mawili uliyotaja hapo juu; wake na watoto ni maadui zenu kwa kuwa lau hamtokaa nao vyema basi watakwenda kuwashitaki Kesho Akhera mbele ya Allaah Aliyetukuka. Waume wamepatiwa majukumu ya kukaa na wake zao kwa wema kwa kuwapatia yote ambayo wanafaa wapewe. Ikiwa hayo hayatofanyika atakwenda kushitakiwa Siku ya Qiyaamah, siku ambayo kila mmoja atamkimbia mwenziwe. Ndio kwa ajili ya hiyo Allaah Aliyetukuka Akasema:

Enyi mlioamini! Jilindeni nafsi zenu na ahli zenu na Moto ambao kuni zake ni watu na mawe” (66: 6).

 

 

Ama kuwa watoto ni fitnah (jaribio) ni kuwa baba ana wajibu kumlea mtoto wake kwa njia nzuri, kwa kumlisha vyema, kumsomesha na kumpatia maadili. Kutofanya hivyo ni kufeli (kuanguka) mtihani. Na vile vile mali, mali inatakiwa itumiwe katika kumridhisha Allaah Aliyetukuka na kutoitumia katika maasi. Kwa ajili hiyo Akasema Aliyetukuka:

Hakika mali yenu na watoto wenu ni jaribio. Na kwa Allaah upo ujira mkubwa” (64: 15).

 

Na kama Muislamu ataweza kuupita mtihani huu basi atapata ujira mkubwa kama Alivyosema Aliyetukuka:

Na jueni ya kwamba mali zenu na wana wenu ni Fitna (mtihani), na kwamba kwa Allaah upo ujira mkubwa” (8: 28).

 

Linalotakiwa ni kuwa haifai wake, watoto na mali kumsahaulisha mmoja wenu na kukosa kufanya mema kama kumtaja Allaah kwa wingi kutekeleza ‘Ibaadah Zake na mambo mengine mema. Kwa ajili hiyo, Allaah Aliyetukuka Akawahutubu Waumini kwa kuwaambia:

Enyi mlioamini! Yasikusahaulisheni mali yenu, wala watoto wenu, kumkumbuka Allaah. Na wenye kufanya hayo ndio waliokhasiri” (63: 9).

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share