Ameoa Mwanamke Mshirikina Na Hataki Hadi Sasa Kubadili Dini Yake Nini Hukmu Ya Ndoa Yake?

 

SWALI:

 

Asaalam alukum

Swali langu nimeowa mke budist kwa dini ya Kiislam na mke mpaka sasa hajabadili dini je nimuache?au nifanye nini?

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema zamstahikia Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Rehma na amani zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukran kwa swali lako.

Ukweli ni kuwa hamkuoana bali mlikuwa mkiishi na wewe pekee ulikuwa ukizini, kwani yeye katika dini yake hakuna kitu chenye kuitwa zinaa.

Kadhalika ni vyema uelewe kuwa hakuna ndoa baina ya Muislamu na mshirikina hata kama atakuvutia namna gani; Allaah Anasema:

Wala msiwaoe wanawake washirikina mpaka waamini. Na mjakazi Muumini ni bora kuliko mshirikina hata akikupendezeni. Wala msiwaoze (binti zenu) wanaume washirikina mpaka waamini. Na mtumwa mwanamume Muumini ni bora kuliko mshirikina hata akikupendezeni. Hao wanaitia kwenye Moto, na Allaah Anaitia kwenye Pepo na maghfira kwa idhini Yake. Naye Huzibainisha Aayah Zake kwa watu ili wapate kukumbuka. Al-Baqarah: 221

Na hata kama itafungishwa na ‘sheikh’ wa namna gani ndoa hiyo haikubaliki katika Uislamu na wala haitakiwi kuwa ni ndoa ya Kiislamu kama ulivyoiita.

Cha kufanya ni kuwa huyo toka mwanzo hakuwa mkeo bali alikuwa hawara wako na wewe ulikuwa ukizini na kama umezaa nae watoto sio wako kishari’ah hawakurithi wala huwarithi na huyo hawara wako hakurithi wala humrithi, na huyo aliyekuozesheni ana jukumu mbele ya Mola, na wewe unachotakiwa ni kuachana naye mara moja na kurudi kwa Mola wako. Kwani ulikuwa ukizini bali ulihalalisha zinaa au ulihalalishiwa zinaa na huyo aliyekuozesha kama alikuwa alielewa kuwa unaoa mshirikina na akakuozesha; na kwa kutumia hila ya kusema umeoa na hilo ni baya sana kuhalalilisha Alichokiharamisha Allaah.

Huyu si mkewe na achana naye haraka, fanya tawbah kwa yaliyopita na baada ya hapo tafuta mwanamke wa Kiislam mwenye Dini. Wapo wanawake wengi wa Kiislamu pande zote za ulimwengu hivyo hana mtu udhuru wa kutumbukia kwa washirikina ila tu yule aliye mjinga na Dini yake, au yule mwenye matamanio ya kutupatupa mbegu zake kila anapoona pamevutia na kasha hukihalalisha kwa kutumia lugha mbalimbali kama wanavyohalalisha Mashia uzinifu wao kwa kuiita Mut’ah (starehe yao ya muda) kuwa ni ndoa.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

 

 

Share