Kashika Mimba Ya Zinaa, Mumewe hana uzazi, Amjulishe Mumewe Au Atoe Mimba?

SWALI

 

Assalam alaikum, Namshukuru Mungu Mola wa viumbe vyote. Ama baada ya haya nina tatizo naomba nisaidiwe mimi ni mwanamke ambaye nimeolewa na huu ni mwaka wa 3 lakini sikujaaliwa kupata mtoto na kwa upande wangu sikuwa na tatizo ila mume wangu ndio mwenye tatizo la kizazi lakini anatumia dawa za sunna. Kwa bahati mbaya na kwa hamu niliyokuwa nayo ya mtoto nikafanya kosa nikatembea nje siku 1 na wala sikukusudia kuwa nitakuwa na mimba Ibilisi tuu kanihadaa, baada ya 2 weeks nikajihisi nina mimba na hivi ni miezi 2.

Jamani sasa mtoto wa mume au wa nje nifanyeje, nilipomueleza mume alifurahi sana lakini naogopa nitasema nini mimi kwake na kwa Mungu sasa mnanishauri vipi nifanye. Au niitowe pia naogopa dhambi mbili kwa pamoja kuuwa na kuzini nje nisaidieni. Natarajia majibu ya kuniongoza mazuri NA MUNGU ATANISAIDIA.


 

JIBU

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mimba ya zinaa. Mara nyingi sisi hufanya makosa yaliyo makubwa mbele ya Allaah Aliyetukuka nasi tukawa ni wenye kusema bahati mbaya au Iblisi ndiye aliyekushawishi. Kudhania hivyo halitusaidii sisi na lolote wala chochote bali linatupatia sisi muhula na nafasi ya kufanya mengine na kisha kutoa hoja hizo hizo.

 

Haiwezekani kuwa ukawa umefanya tendo kama la zinaa kisha useme sikukusudia kwani kitendo hicho kinajumlisha mambo mengi sana. Mwanzo unaanza kumtongoza mwanamme au yeye akutongoze, mzungumze, mpeane miadi na mfanye kitendo chenyewe ambacho ni kibaya sana. Allaah Aliyetukuka na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wametuhimiza sana kuwa na subira katika mambo yetu yote. Kutokuwa na subira ndiko kumekutia katika njia panda. Na lau kama ungekuwa ni mwenye kuifikiria ile Aayah ya Suratush Shuuraa (42): 49-50 hungekuwa na tatizo kwani ungefahamu ya kuwa watoto wote wanatoka kwa Allaah. Hivyo, tatizo la ni kuhusu hilo na kuhangaika kutafuta madawa n.k.?

 

Kitendo ulichokifanya kimekufikisha katika njia panda na hilo limekufanya wewe uanze kufikiria maovu: Je, nitoe mimba au niseme uongo kwa mume wangu? Kuua kiumbe ni katika dhambi kubwa na kuhusu uongo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema kuwa Muumini hawezi kabisa kusema uongo. Njia iliyobaki ni kumwambia kweli mume wako, upate radhi za Allaah Aliyetukuka kuliko kumwambia uongo ukapata radhi ya mume lakini ukakasirikiwa na Allaah Aliyetukuka. Kisha ukisema uongo utakuwa umefanya dhuluma kwani huenda mkazaa na mumeo watoto kwani hakuna ugonjwa usiokuwa na dawa na hapo anapoaga dunia mtoto wako huyu wa kwanza wa nje ya ndoa akamrithi babake wakati ambapo katika sheria hafai kumrithi.

 

Ushauri wetu ni kuwa sema ukweli kwa mumeo na huenda ikawa na natija nzuri zaidi. Baada ya hapo unafaa ufanye toba ya kweli kweli kwa Mola wako kwa kutekeleza masharti yafuatayo:

 

 

1.     Kuacha maasiya hayo.

2.     Kujuta kwa kufanya uovu huo.

3.     Kuazimia kuwa hutarudia tena kosa hilo.

 

 

Twakutakia kila mafanikio hapa duniani na Akhera.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share