Kwa Nini Uislamu Unataka Ushahidi Wa Wanawake Wawili Badala Ya Mmoja Kama Wanaume?

SWALI:

 

Assalam alaykum.

Mimi ni mwislamu na nimekabiliwa na swali ambalo linanitatiza mimi kwa sababu nimeulizwa na wengi wasiokuwa waislamu.Ijapokuwa nimejaribu kulijibu kwa elimu nilionayo naona bado hawajaridhika. Maswali ni mawili na ni yafuatayo:

1. Katika Qur'an tukufu wanaume waumini wamebashiriwa pepo na wameahidiwa wanawake wazuri ambayo hawajaingiliwa na binadamu yeyote wala jini. Je wananwake wamebashiriwa hayo? NA kuna maulama wanaosema waumini wa kiislamu waaume watafufuliwa na wake zao.

2. Utamwelezaje asiye muislamu kwa nini mwanamke kauli yake ni nusu ya mwanamume. Yaani ikiwa ni shahidi basi wanawake wanne wanatakikana au wanaume wawili.

Ninavyoamini mimi kila jambo la kiislamu tulioamrishwa kuna maana yake na alhamdulillah mengi nimetafuta maana na nikayapata.Ningependa kusikia mwislamu mwenzangu angejibu nini akiulizwa na asiyekuwa mwislamu maswali haya.

Shukran wa jazakAllaahu kheir.

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani kwa suala lako nyeti kuhusu mwanamke. Hakika ni kuwa Uislamu ulikuja kumtoa mwanmke katika minyororo aliyokuwa amefungwa nayo. Suala la mwanamke limezua mjadala mkubwa sana katika ulimwengu kwa sababu ya ujahili. Hata Waislamu wamekuwa katika njia panda kwa sababu hiyo hiyo. Mbali na ujahili, athari ya tamaduni za kimagharibi zimewafanya watu wasijue uhakika kuwahusu.

 

Mengi yamesemwa kuhusu hadhi na majukumu ya mwanamke wa Kiislamu. Yote haya yametokea kwa sababu ya nadharia zisizokuwa na msingi wowote wa dini. Wapotofu wa Kimagharibi mpaka sasa wana fikra chafu dhidi ya Uislamu. Hii ni dhahiri kulingana na makala ya mwandishi wa Woman in Islam (Mwanamke katika Uislamu): "Katika kipindi cha miaka 15 kuanzia nilipoingia katika Uislamu, nimeulizwa maswali mengi kuhusu maisha ya Muislamu na wasiokuwa Waislamu na marafiki zangu… wanauliza: Je, katika Uislamu, mnaamini kuwa mwanamke ana roho? Waislamu wanawake hawaswali au kwenda Makkah, je wanafanya hayo? Pepo ni kwa wanaume peke yao au sivyo?" Mengi ni kuwa mwanamke hana haki ya ilimu, kutoa rai, kuwa na akiba yake ya rasilmali au pesa, na kadhalika. Haya ni maswali ambayo yanaulizwa na yataendelea kuulizwa.

 

Ukitaja kujua neema ambayo Uislamu imempatia mwanamke soma kuhusu wanawake wanavyofanywa katika staarabu nyingine. Utakuta kuwa Uislamu umemuenzi mwanamke kwa kumpatia uhuru wa kumiliki atakacho, kuchuma, anashirikiana na mwanaume katika kunyanyua viwango vya maadili, kufanya Da'wah, kupata ilimu na kufundisha, kutoa rai na maoni, kushiriki katika Jihadi na mengineo mengi. Amepatiwa hadhi ya kijamii kama mama, mke, dada, binti, na kadhalika.

 

Hakika ni kuwa Pepo katika Uislamu na utukufu unategemea utendaji kazi na amali zake njema anazofanya. Wapo wanawake ambao wataingia motoni kama vile wanaume, na wapo wanawake ambao wataingia Peponi kama vile wanaume. Amali njema ni muhimu sana katika kufanikisha wepesi wa kuingia Peponi. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anatueleza kuwa ubora mbele yake ni uchaji Mungu. Hivyo ikiwa mwanamke ana Imani na taqwa zaidi atakuwa karibu zaidi na Allaah kama Alivyosema Aliyetukuka: "Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Allaah ni huyo aliye mchamngu zaidi katika nyinyi. Hakika Allaah ni Mwenye kujua, Mwenye khabari." (49: 13).

 

Ama kuhusu kuingia Peponi Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) katika Ayah nyingi Anatufahamisha dhahiri shahiri: "Mwenye kutenda uovu hatalipwa ila sawa na huo uovu wake, na anayetenda wema, akiwa mwanamume au mwanamke, naye ni Muumini, basi hao wataingia Peponi, waruzukiwe humo bila ya hisabu" (40: 40).

 

Pia, "Mola  wao, akayakubali maombi yao akajibu: Hakika sipotezi kazi ya mfanya kazi miongoni mwenu, akiwa mwanamume au mwanamke, kwani ni nyinyi kwa nyinyi. Basi waliohama, na waliotolewa makwao, na wakateswa katika Njia yangu, na wakapigana, na wakauliwa, kwa yakini Mimi nitawafutia makosa yao, na kwa yakini nitawaingiza katika Mabustani yanayopita mito kati yake. Hayo ndiyo malipo yanayotoka kwa Allaah. Na Allaah Kwake yapo malipo mema kabisa" (3: 195).

 

Na Amesema: "Mwenye kutenda mema, mwanamume au mwanamke, naye akawa ni Muumini, Tutamhuisha maisha mema; na tutawapa ujira wao kwa bora ya waliyokuwa wakiyatenda" (16: 97).

 

Uislamu umetufanya sote, wanawake na wanaume kuwa ndugu moja kama Alivyosema: "Hakika Waumini ni ndugu, basi patanisheni baina ya ndugu zenu, na mcheni Allaah ili mrehemewe " (49: 10).

 

Pia ifahamike kuwa maamrisho yote ya 'Ibadah yameamriwa kwa wanaume na wanawake bila kubagua. Vile vile mwanamke au mwanaume akifanya kosa wanapata adhabu sawa kabisa. Kwa mfano mwanamke au mwanaume akiiba, Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amebaini adhabu zao: "Na mwizi mwanamume na mwizi mwanamke, ikateni mikono yao , hayo ni malipo ya waliyo yachuma, ndiyo adhabu ya mfano itokayo kwa Allaah. Na Allaah ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima" (5: 38 ).

 

Vile vile anapozini mwanamke anapatiwa adhabu sawa na mwanamme, kama Alivyosema Aliyetukuka: "Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume, mtandikeni kila mmoja katika wao bakora mia. Wala isikushikeni huruma kwa ajili yao katika hukumu ya Allaah, ikiwa nyinyi mnamuamini Allaah  na Siku ya Mwisho. Na lishuhudie adhabu yao kundi la Waumini" (24: 2).

 

Katika Aayah moja, Allaah Aliyetukuka Amebaini matendo chungu nzima ambayo yanafaa yafanywe na jinsiya zote mbili. Hapo hapo akaahidi Aliyetukuka kuwa mwenye kufanya hayo basi atapata maghfira na ujira mkubwa. Allaah Anasema: "Hakika Waislamu wanaume na Waislamu wanawake, na Waumini wanaume na Waumini wanawake, na watiifu wanaume na watiifu wanawake, na wasemao kweli wanaume na wanawake, na wanaosubiri wanaume na wanawake, na wanyenyekevu wanaume na wanawake, na watoao sadaka wanaume na wanawake, na wanaofunga wanaume na wanawake, na wanaojihifadhi tupu zao wanaume na wanawake, na wanaomdhukuru Allaah kwa wingi wanaume na wanawake, Allaah Amewaandalia msamaha na ujira mkubwa" (33: 35).

 

Hivyo, wanawake wamebashiriwa Pepo na neema nyingi sana. Wakati wa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwabashiria wanawake miongoni mwa Swahabiyah ishirini kuwa wataingia Peponi kulingana na Hadiyth kadhaa. Miongoni mwao ni Khadiyjah bint Khuwaylid, 'Aaishah bint Abubakar, Zaynab bint Jahsh, Hafswah bint 'Umar, Faatwimah bint Rasuul, Asmaa bint Abubakar, Umm Sulaym Rumayswaa' bint Milhaan, Asmaa bint Yaziyd, Nusaybah bint Ka'b, Sumayyah bint Khabbaat, Barakah bint Tha'labah na wengineo.

 

Hilo la kuwa wanaume watakaoingia Peponi wamebashiriwa wanawake ambao ni hurul 'ayn (wanawake wenye macho mazuri na makubwa) ni kweli kwani Aayah za Qur-aan zipo wazi kuhusu hilo. Zipo Aayah kadha kuhusu hili lakini inatosha kunukuu moja. Allaah Aliyetukuka Anatueleza: "Watakuwemo humo wanawake watulizao macho yao; bin Aadam yoyote hajawagusa kabla yao (hao waume zao) wala jini" (55: 56). Sehemu hii ya pili ambayo tumeipigia msitari imekaririwa tena katika surah hii hii ayah ya 74.

 

Wanawake Peponi watakuwa ni aina mbili. Aina ya kwanza ni wale wanawake wa duniani waliotenda matendo mema, Allaah Aliyetukuka Atawajazi na kuwaingiza Peponi pamoja na waume zao ikiwa walikuwa wema pia. Anasema Allaah Mtukufu: "Na wanawake watukufu (hawa waliokuwa nao duniani). Tutawaumba kwa umbo bora zaidi). Na Tutawafanyia vijana kama kwamba ndio mwanzo wanaolewa. Wanapendana na waume zao walio hirimu moja na wao" (56: 34 – 37).

 

Pia, "Na wale walioamini na wakafuatwa na vizazi vyao na watoto wao katika imani, Tutawakutanisha nao hao jamaa zao, wala Hatutawapunja kitu katika thawabu za vitendo vyao; kila mtu atalipwa kwa kile alichokichuma" (52: 21).

 

Hizi Aayah zinaonyesha ikiwa mumeishi hapa duniani kama mume na mke kwa wema Allaah kwa rehema Yake Atawaungisha tena muishi pamoja lakini wakati huu nyote mtakuwa vijana hata kama mlikufa mkiwa wazee.

 

Wanawake aina ya pili ni wale walioumbwa na Allaah Aliyetukuka kwa ajili ya Pepo tu. Hawa watakuwa ni wenye kupewa wanaume waliowema kama jazaa yao. Kwa vile wanaume kimaumbile kuanzia hapa duniani ni wenye kuoa wake wengi Allaah pia Akhera Atawatunukia hadhi hiyo hiyo. Hekima ya hilo linajulikana na Allaah. Lakini kwa kuzingatia hekima ya mwanamume kuruhusiwa kuoa zaidi ya mke mmoja tutapata busara ya hilo ndilo hilo litakavyokuwa Peponi. Huku si kuwadunisha wanawake bali ni Muumba kuangalia maslahi na maumbile ya kila mmoja. Hapa leo ikiwa utamfanya mke mmoja awe na waume wanne basi utampatia shida na mtihani mkubwa mwanamke huyo, lakini kwa mwanaume ni jambo la kawaida tu.

 

Ama kuhusu swali lako la pili ni jambo ambalo liko wazi kabisa kwa udhaifu wa wanawake katika kukumbuka mas-ala ya nambari na hesabu.

 

Hakika ni kuwa kauli ya mwanamke si nusu. Inaonyesha hapa mmechanganya baina ya mambo mawili tofauti.

 

Suala la kwanza ni je, ushahidi wa mwanamke ni nusu wa ule wa mwanamme? Hakika jambo hili lipo wazi kabisa kwa kila mwenye kutaka ukweli bila ya kuwa na ubaguzi wala nadharia zake mwenyewe za awali. Kwa hukumu hii mwanamke hajadunishwa wala kudharauliwa. Hakika ni kuwa hukumu hii inakwenda sambamba na maumbile yake na saikolojia ya mwanamke inakuwa wazi kulingana na dondoo za wana-saikolojia, wataalamu wa magonjwa ya akili na tafiti za kitabibu.

 

Ayah hii ya Qur-aan: “Enyi walioamini! Mnapokopeshana deni kwa muda ulio wekwa, basi andikeni. Na mwandishi aandike baina yenu kwa uadilifu, wala mwandishi asikatae kuandika. Aandike kama alivyo mfunza Allaah. Na mwenye deni juu yake aandikishe; naye amche Allaah, Mola wake  Wala asipunguze chochote ndani yake. Na akiwa mwenye kudaiwa ni mtu aliye pumbaa au mnyonge au hawezi kuandikisha mwenyewe, basi aandikishe mlinzi wake kwa uadilifu. Na mshuhudishe mashahidi wawili katika wanaume wenu. Ikiwa hapana wanaume wawili, basi mwanamume mmoja na wanawake wawili katika mnao waridhia kuwa mashahidi. Ili ikiwa mmoja wao akipotea, mmoja wao amkumbushe mwengine. Na mashahidi wasikatae waitwapo. Wala msipuuze kuliandika deni likiwa dogo au kubwa mpaka muda wake. Hayo ndiyo haki zaidi mbele ya Allaah, na ndiyo sawa zaidi kwa ushahidi, na vyema zaidi ili msiwe na shaka. Ila ikiwa ni biashara ya mkono-kwa-mkono baina yenu, basi hapo si vibaya kwenu msipoiandika. Lakini mnapo uziana wekeni mashahidi. Wala asitiwe matatani mwandishi wala shahidi. Na mkifanya hivyo basi hakika hilo ni kosa kwenu. Na mcheni Allaah. Na Allaah ni Mjuzi wa kila kitu.” (2: 282) inazungumzia hitaji hilo la ushahidi kuhusu kukopeshana.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anatoa muongozo kwa mambo yanayohusiana na majukumu ya pesa. Katika kipengele hiki, hitaji la kuandika mahusiano ya pesa limenukuliwa kwa mkazo, "Basi iandikeni". Baada ya hapo ayah inazungumzia kuhusu wajibu wa mwandishi au mhusika wa kutayarisha mkataba kwa ibara za kisasa. Ayah pia, inagusia ikiwa mhusika (mkopaji) ni mpumbavu au mnyonge au hawezi kuandikisha, basi walii wake awe ni mwenye kuchukua jukumu hilo kwa niaba yake na achague mashahidi wawili walio waadilifu. Ifahamike kuwa hili linatokea tu ikiwa mhusika hana uwezo wa kuandika mkataba. Kwa hiyo, mashahidi wanakuwa ndio wenye kuchunga kuwa haki lazima ifanyike.

 

Baada ya hapo ndio Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anaweka sharti la kuita mashahidi wawili wanaume na ikiwa hawapo basi mwanaume na wanawake wawili. Kisha Aayah inaelezea umuhimu wa kuandikiana ikiwa mkataba wenyewe ni mkubwa au mdogo. Qur-aan inazidi kutuelimisha kuwa kuwa si mara zote inawezekana kuandikiana mikataba hivyo, ikiwa haiwezekani basi kuwe na mashahidi wenye kushuhudia hilo.

 

Lengo hasa la kutoa utangulizi huo ni kuwavutia watu kwa ile hakika kuwa ushahidi wa wanawake hapa hauhusiani na hadhi yao bali ni juu ya mikataba ya kibiashara. Hapa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anatubainishia wazi kuwa wanaotakiwa ni mashahidi wanne bila kubagua kama ni wanawake au wanaume. Pale ambapo Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anatulezea kuhusu ushahidi wa wanaume wawili au mwanaume na wanawake wawili ni katika mas-ala ya deni. Anasema Aliyetukuka: "Na mshuhudishe mashahidi wawili katika watu wenu wanaume (Waislamu). Lakini ikiwa hakuna wanaume wawili, basi mwanamume mmoja na wanawake wawili; katika wale mnaowakubali kuwa mashahidi. Ili kama mmoja wao (katika wale wanawake) akipotea, mmoja wao amkumbushe mwingine" (2: 282).

 

Ifahamike kuwa Allaah, Muumbaji, kwa hekima Yake isiyo kifani Anatoa maagizo ambayo yana manufaa tele kwa wanadamu. Yeye ndiye Muumbaji, hivyo, Anajua jambo ambalo litamsaidia mwanadamu mwenyewe. Katika mas-ala haya Allaah   (Subhaanahu wa Ta'ala) kwa hekima Yake iliyo ya juu Ameweka hivyo kwa sababu ya kuwa wanawake si wazoefu katika mas-ala ya hesabu, hivyo wakiwa wawili wanaweza kukumbushana ikiwa mmoja wao ataghafilika. Wanawake hawakuwa ni wenye kujishughulisha katika biashara, hivyo kuwa jambo zito kwao na kwa kuwa halipo akili mwao anaweza kusahau mara moja.

 

Katika enzi hii ya sayansi tunaweza kupata umuhimu wa hukumu na sharia hii. Mengi yamevumbuliwa kuanzia wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kila kukicha uvumbuzi mwingi zaidi unakuwa ni wenye kufanyika. Wanawake huwa wana duara la matatizo ya kisaikolojia kila mwezi. Alama za mfadhaiko zinakuwa ni zenye kuonekana mwanzo wa mimba, wakati wa mimba na baada yake, hali ya kukakita damu, shida ya kifiziolojia na saikolojia kwa ajili ya utasa na matatizo ya kisaikolojia baada ya kutisha (kuharibika mimba). Ni katika hali hizi ndio wanawake wanapata uchovu wa kisaikolojia ambao unaleta mfadhaiko, kukosa umakinifu, akili kuwa pole na ukosefu wa hifdhi kwa muda mfupi.

 

Utafiti unaonyesha kuwa wasichana kabla ya kupata ada yao ya mwezi wanapata mabadiliko ya kisaikolojia. Maelezo ni kama yafuatayo: "Tafiti nyingi zimeripoti kuwa kuna ongezo la athari hasi katika kipindi kabla ada ya mwezi. Katika hayo ni hisia nyingi ikijumlisha kusumbua, mfadhaiko, wasiwasi, huzuni, kujihisi kuwa hako salama, machofu, upweke, kudondokwa na machozi, kukosa utulivu na mabadiliko ya hali. Katika tafiti nyingi, watafiti wameona shida kutofautisha baina ya athari hasi…" (Psychological Medicine, Monograph Suppliment 4, 1983, Cambridge University Press, uk. 6).

 

Naye C. Shreeves ameandika: "Nguvu za umakinifu na hifadhi zinapungua ni jambo la kawaida katika kipindi kabla ya mwanamke kuingia katika ada yake. tatizo hili linaweza kutatuliwa tu ugonjwa wenyewe utatibiwa" (The Pre-Menstrual Syndrome).

 

Wakati wanawake wakiwa na mimba wanapata mfadhaiko na matatizo ya kiakili na hofu (Psychiatry in Practice, Oktoba-Novemba 1986, uk. 6). Matatizo kama haya yanaendelea mimba inapokua kubwa. Nako kukatika kwa damu ambako kunaanza katikati ya miaka thelathini hadi hamsini kunakuja na shida zake nyengine. Kuhusu hili Dkt. Jennifer al-Knopf anasema: "…Wanawake hawajui miili yao inawafanya nini.. Baadhi yao wanaripoti ishara ya udhoofu kwa kutokwa jasho usiku, kutopata usingizi, mwasho, mbadiliko wa hali, kupoteza hifdhi kwa muda, kuumwa na kichwa, kupatwa na kukojoa ambao si kawaida na kuongeza mwili. Mabadiliko haya yanapatikana kwa kupungua kwa hormoni za kike kama oestrogen na progesterone, ambazo zinatawala mduara wa uzazi" (Newsweek International, 25 Mei 1992) 

 

Kuharibu mimba kwa mwanamke kunamletea mabadiliko mengine ya kisaikolojia na athari nyingine hasi. Wanawake wanakuwa na wasiwasi kwa asilimia kubwa zaidi kuliko wanaume pamoja na kuwa na hamu.

 

Kwa yaliyopatikana na wana-saikolojia, wataalamu wa akili na watafiti kama tulivyonukuu hapo juu tunaweza kuelewa kauli ya Aliyetukuka: "Na mshuhudishe mashahidi wawili katika watu wenu wanaume (Waislamu). Lakini ikiwa hakuna wanaume wawili, basi mwanamume mmoja na wanawake wawili; katika wale mnaowakubali kuwa mashahidi. Ili kama mmoja wao (katika wale wanawake) akipotea, mmoja wao amkumbushe mwingine" (2: 282).

 

Ndio Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatuusia: " Wafanyieni wema wanawake. Mwanamke ameumbwa na ubavu, na sehemu iliyopinda zaidi ni ya juu. Ukijaribu kuinyoosha itavunjika, na ukiiacha itabaki kama ilivyo. Kwa hiyo, watendeeni wema wanawake". Katika riwaya nyingine: " Ukijaribu kuunyoosha utamvunja na kumvunja ni kumtaliki" (Al-Bukhaariy na Muslim).

 

Maneno ya Aayah hii yaonyesha kwa uwazi kabisa kuwa msingi wa kanuni hii si kubagua baina ya jinsia lakini ni uwezo wa kuhifadhi wa wanawake. Aayah inatoa hakika ya kibayolojia – kuwa wanawake si wazuri katika kukumbuka vitu kama wanaume. Hii ndio sababu, ikiwa tutakubali ushahidi wa wanawake katika kesi za deni, ni lazima wawe wawili, ili kwa wakati wowote wa mustakbali, ikiwa wanahitajika kutoa ushahidi, mmoja wao ataweza kufidia udhaifu wa hifdhi wa mwenziwe.

 

Utafiti wa sasa kuhusu suala hili umeyakinisha ukweli huu wa Qur-aan, kuwa hifdhi na kumbukumbu za wanawake ni dhaifu kuliko za wanaume. Wanasayansi wa Urusi wametafiti hili kwa kina, na hitimisho lao lilichapishwa katika kitabu. Ufupisho wake ulitokea katika gazeti moja India ukiwa na anwani, "Uwezo wa Kuhifadhi S". "Wanaume wana uwezo mkubwa zaidi wa kuhifadhi na kufanyia kazi maalumati ya hesabu kuliko wanawake, lakini wanawake ni wazuri zaidi kwa maneno na kauli". Alisema mwanasayansi wa Urusi , "Wanaume wanatawala masomo ya hesabu kwa kuwa na sifa ya kuhifadhi ya kipekee" (Dr. Vladimir Konovalov, Memorising Ability, New Delhi edition of the Times of India, Januari 18, 1985).

 

Mbali na serikali ya Kenya kutaka kuona kuwa wasichana nao wanafanikiwa katika somo la hesabu pamoja na masomo ya sayansi utakuta kila matokeo yanapotoka yanakuwa ni kama yale ya miaka iliyopita. Ni wasichana wachache wanaofaulu katika mitihani hiyo kuliko wavulana.

 

Mas-ala ya pili ni kuwa, je ushahidi wa mwanamke ni sawa na wa mwanaume au wake ni duni zaidi? Hili lipo wazi kabisa katika Aayah kadhaa ila hii ya deni. Tunaposoma katika Suratun Nuur pale ambapo Allaah Aliyetukuka Anatufahamisha: "Na wale wanaowasingizia wanawake watahirifu (kuwa wamezini), kisha hawaleti mashahidi wanne" (24: 4).

 

Pia tunasoma kuhusu mashahidi wa wasiya: "Enyi walioamini! Wekeni mawasii wawili wenye uadilifu miongoni mwenu wakati wa kuusia yanapomfikia mauti mmoja wenu" (5: 106).

 

Pia: "Wale wanaowasingizia wake zao kuwa wamezini na hawana mashahidi ila nafsi zao, basi ushahidi wa mmoja wao utakuwa kushuhudia…" (24: 6).

 

Pia kuhusu talaka, anasema Aliyetukuka: "Basi wanapofika muda wao, ima warejeeni muwaweke kwa wema au farikianeni nao kwa wema; na mshuhudishe mashahidi wawili waadilifu miongoni mwenu" (65: 2).

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share