Kuweka Madawa Ya Nywele Na Kuvaa Nywele Za Bandia

SWALI:

Assalam aleikum. wabbad dada yangu anataka kua na ujuzi wa kuwatengeneza wenzake nywele na kama walivyo watengezaji huwa wanatumia baadhi ya madawa ambayo si ya sawa au nama yoyote ile ya kuweka nywele bandia au lengine lolote. je ni yapi muhimu ayazingatie wakati anapofanya kazi hii ili mie ni mnasihi afanye au asifanye. Shukran

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwako kwa kumtakia mwenzio mazuri ya hapa duniani na Kesho Akhera. Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Akujazi na akupatie kila jema na mafanikio katika Nyumba mbili. Hakika ni kuwa, “Dini ni kupeana nasaha.” [Muslim, Abu Daawuud na an-Nasaaiy].

Na Jariyr bin Abdillaah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema: “Nilimbai Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya kusimamisha Swalah, kutoa Zakaah na kumnasihi kila Muislamu.” [Al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud na an-Nasaaiy].

Kazi yoyote ambayo Muislamu anaifanya au anataka kuifanya ni lazima atazame kuwa inakwenda sambamba na kanuni za Sharia. Bila hivyo, inakuwa ni haramu kwake kuifanya. Katika mas-ala ya kusema kuwa utumiaji wa madawa ya nywele unaleta madhara kwa mwenye kuwekewa na mwenye kuweka. Ikiwa sifa ya madawa hayo ni hivyo basi itakuwa haifai kisheria kwani msingi wake muhimu: “Haifai kudhuru wala kulipana madhara.” [Ibn Maajah na ad-Daaraqutniy].

Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema: “Wala msijitie kwa mikono yenu katika maangamizo” [Al-Baqarah 2: 195].

Na pia, “Wala msijiue” [An-Nisaa 4: 29].

Hakika ni kuwa madawa haya ya kemikali ya nywele yanaleta madhara makubwa sana na hivyo Uislamu unachunga maslahi ya mwanadamu na hautaki awe ni mwenye kudhurika.

Ama kuunganisha au kuunganishwa nywele za bandia ni jambo ambalo limekatazwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Imam Abu Zakariyya Yahyaa an-Nawawiy ana mlango haswa kuhusu kuongeza au kuongezwa nywele katika kitabu chake Riyaadh asw-Swaalihiyn. Dalili za hilo ni kama zifuatazo:

Allaah Aliyetukuka Anasema:

Wao hawawaombi badala yake Yeye ila wanawake, wala hawamuombi ila Shetani aliyeasi. Allaah Amemlaani. Naye Shetani alisema: Kwa yakini nitawachukua sehemu maalumu katika waja wako. Na hakika nitawapoteza na nitawatia matamanio, na nitawaamrisha, basi watakata masikio ya wanyama, na nitawaamrisha, basi watabadili maumbile ya Allaah. Na mwenye kumfanya Shetani kuwa ni mlinzi wake badala ya Allaah, basi huyo amekhasiri khasara ya dhahiri” [An-Nisaa 4: 117 – 119].

 

Imepokewa kwa Asmaa’ (Radhiya Allaahuanha) kwamba mwanamke fulani alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Ee Mtume wa Allaah! Binti yangu amepatwa na surua zikapuputika nywele zake, nami nimemuozesha; Je, niziunganishe?” Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamjibu: “Allaah Amemlaani mwenye kuunganisha nywele zake (au nywele za mwengine kwa nywele nyengine) na mwenye kuungwa (au kuvaa nywele hizo)” [Al-Bukhaariy, Muslim na an-Nasaaiy].

Na katika riwaya nyengine: “Mwenye kuunganisha nywele na mwenye kumtaka mwengine amfanyie kazi hiyo (mwenye kutamani kuzivaa nywele hizo za bandia)”. Na mama wa waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahuanha) ameeleza Hadiyth kama hiyo. [Al-Bukhaariy, Muslim na an-Nasaaiy].

 

Pia imepokewa kwa Humayd bin ‘Abdir-Rahmaan kuwa alimsikia Mu‘awiyah (Radhiya Allaahuanhuma), mwaka wa Hijjah, akiwa juu ya mimbari, akiwa ameshika nywele zilizokatwa katika mikono ya Harasiy (Mtoto wa Amiri), akasema: “Enyi watu wa Madinah! Wako wapi wanazuoni wenu? Nimemsikia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akikataza tabia hii (nywele za bandia) na alikuwa akisema: ‘Hakika walihiliki Bani Israili pale wake zao walipoichukua tabia hii (ya kuunganisha nywele)’” [Al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na an-Nasaaiy].

Na imepokewa kwa Ibn ‘Umar (Radhiya Allahuanhuma) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amemlaani mwenye kuunganisha nywele zake na mwenye kutaka mwengine amuunganishe nywele hizo na mchanjaji kwenye mwili na mwenye kuchanjwa. [Al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud na at-Tirmidhiy].

 

Hizi ni dalili za wazi kuhusu hilo uliloliuliza na tunatumai utaweza kumnasihi kwa kumkinaisha dada yetu ili asifanye kazi hiyo ya kuunganisha nywele bandia. Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Amfanikishe kuacha kazi hiyo na kupatiwa badali iliyo nzuri zaidi.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share