Kuweka Matanga Ni Sunnah?

 

Kuweka Matanga Ni Sunnah?

 

Alhidaaya.com

 

SWALI:

 

Naomba kujua haya matanga wanao fanya baada ya kufariki mtu wanalala siku tatu katika nyumba ya mtu aliyefiwa ni sunna iliyfanywa Nabiy (s.a.w)?

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Muda wa msiba katika Uislamu unatakiwa usizidi siku tatu, kama mtu anaweza kujizuia na kustahamili, hata siku moja inatosha kuomboleza na si lazima siku tatu. Na katika siku hiyo/hizo za msiba haifai watu kumkalifisha aliyefiwa kwa kushinda na kulala kwake hadi apaswe kuwakirimu kwa chakula. Mara nyingi huwa ni kujikalifisha kwa mtu hadi akope pesa kutayarisha chakula cha watu wengi.

 

 

Na hii imekuwa ni ada katika jamii yetu kuweka matanga ya siku tatu hadi siku saba wengine. Na mtu asipofanya hivyo huonekana kama hakumthamini mfiwa wake na pia ataonekana kama ni mtu wa ajabu katika jamii!

 

 

Ubaya mwingine wa kuweka matanga ni kusababisha mkusanyiko wa watu na hakuna la maana litakalofanywa ila yatatendeka mambo ya bid'ah kama kusoma Qur-aan au nyiradi kwa pamoja na wakati mwingine utakuwa ni wa mazungumzo ya siasa, mipira, upuuzi wa kidunia, kusengenyana na kucheza karata, dhumna, na wengine kula mirungi, kuvuta sigara na mengineo ya haraam. 

 

 

Sunnah ni watu kumfanyia chakula aliyefiwa  kama tulivyopata mafunzo kwa Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipofariki  Ja'afar bin Abi Twaalib (Radhwiya Allaahu 'anhu) aliwaambia Swahaba: 

 

(أطعموا آل جعفر طعاماً فقد أتاهم ما يشغلهم)) رواه أبو داود وصححه الألباني في أحكام الجنائز

((Watengenezeeni familia ya Ja'afar chakula kwani wamefikwa na jambo lenye kuwashughulisha)) [Abu Daawuwd na ameipa daraja ya Swahiyh Shaykh Al-Albaaniy katika Ahkaam Al-Janaaiz]

 

 

Tafadhali ingia katika viungo vifuatavyo upate mafunzo kuhusu yanayopasa na yasiyopasa kutendwa anapofariki mtu.

 

 

Khitma – Kutokufaa  Na Madhara Yake

 

Kumsomea Khitmah Maiti, Kumchinjia Na Kumuombea Du'aa Kwa Pamoja

 

Kufukiza Ubani Wakati Wa Kuomba Du'aa Inafaa?

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share