Anajaribu Kufanya Mema Lakini Ana Tabia Chafu Ya Kuondosha Matamanio Kwa Mkono Na Vifaa, Afanyeje Kujiepusha Shaytwaan ?

SWALI:

 

Assalam alaikum

 

Naomba munisaidie kuhusu suala hili. Mr X anapata taabu sana kuhusu matamanio ya nafsi yake yeye mwenyewe yaani anajitamani yeye mwenyewe, kwa njia ya mikono yake na baadhi ya vitu vingine vya kumpa yeye hamu ya kutimiza haja yake. Na huyo Mr. X kashaoa na mkewe anamtimizia haja zake kama inavyostahiliwa kutimiziwa lakini yeye bado anapokua peke yake humkufuru Mwenyezi mungu subhanahu wataala, kwa kujitamani yeye mwenyewe au kuangalia baadhi ya mambo ya matamanisho ili atimize azma yake. Na vilevile Mr X anajitahidi kujikurubisha katika kumtii Allah subhana wa taala, kama kusali sala zote tano baadhi huzisali Msikitini na baadhi huzisali Nyumbani na wakati mwingine hujitahidi kuhudhuria darsa mbalimbali na kuwakataza watu kutokufanya mabaya asioyataka Allah subhanahu wataala. Na yote hayo machafu anayoyafanya anajua hasa kua hivi ninavyofanya sio mwenendo unaokubalika katika imani ya kiislam, lakini anajikuta ni mwingi wa kufanya hayo mambo machafu mpaka anajiona kua yeye kama katekwa kijinsia kimaumbile, maana anajua kama vibaya na ndani ya moyo wake halipendi, na mema anajitahidi kufanya lakini haya mabaya ndio yameshamiri zaidi. SASA AFANYE NINI MPAKA AMSHINDE HUYU IBLISI ALIYEMKABIL>

NAOMBA TUMSAIDIE MR X>

SHUKRAN>


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu ndugu anayejaribu kufanya mema lakini kuzidiwa na uchu wa nafsi yake dhaifu.

 

Hakika ni kuwa mwanaadamu ana maumbile ya kutamani na kufanya maovu. Maovu yanavutia na yanazidi kujikita katika maisha ya mwanaadamu kwa njia moja au nyingine. Baadhi yake ni kutokana na mtu kuwa mbali na Allaah Aliyetukuka kwa matendo na maneno, kutojiweka katika kufuata Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kufuata matamanio, upungufu wa Imani, kuwa na marafiki wabaya, kutoishi na Qur-aan, kuwa na wakati mwingi wa faragha, kutokumbuka mauti na mengineyo.

 

Kwa kuwa nafsi inaamrisha mabaya inabidi Muislamu ajitahidi kujitoa katika nafsi mbaya, kuifikia nafsi yenye kujilaumu na hatimaye kupanda na kufika katika nafsi iliyotulia. Allaah Aliyetukuka Anasema:

Nami sijitoi lawamani. Kwa hakika nafsi ni mno kuamrisha maovu, isipokuwa ile ambayo Mola wangu Aliyoirehemu. Hakika Mola wangu ni Msamehevu na Mwenye kurehemu” (Yuusuf [12]: 53).

Hata hivyo kulingana na maelezo juu ya kumhusu huyo ndugu, inaonekana kuwa yupo baina ya nafsi inaoamrisha maovu na ile yenye kujilaumu. Na kwa ajili hiyo ni lazima ajinasue kutoka katika hali hiyo ambayo si nzuri na itamfikisha mahali ambapo ni pabaya.

 

Kulingana na maelezo inaonyesha kuwa ameshindwa kujizatiti na kujiondoa katika mabaya mbali ya kuwa yeye anaamrisha mema. Na lau atakuwa ni mwenye kuzingatia Aayah zifuatazo basi huenda zikamtoa kwa aliyonayo.

Allaah Aliyetukuka Anasema:

Enyi mlioamini! Kwa nini mnasema msiyoyatenda? Ni chukizo kubwa mno kwa Allaah kuwa mnasema msiyoyatenda” (Asw-Swaff [61]: 2 – 3).

 

Na pia kutazama Hadiyth zinazozungumzia adhabu anayopata mwenye kuamrisha mema naye akawa anafanya mabaya. Tukumbuke Hadiyth ya Usaamah bin Zayd bin al-Haarith (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kuwa amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

Ataletwa mtu Siku ya Qiyaamah, naye ataingizwa Motoni. Matumbo yake yatatoka nje, naye atayashikilia akiwa anazunguka kama anazunguka punda kwa mtambo. Watu wa Motoni watakusanyika na kusema: ‘Ewe fulani una nini? Si ulikuwa ukiamrisha mema na kukataza mabaya?’ Atasema: ‘Ndio, nilikuwa nikiamrisha mema lakini siyafanyi na nikikataza mabaya, nami nikiyaendea” (Ahmad, al-Bukhaariy na Muslim). Ikiwa atakumbushwa kuhusu hayo huenda yakamfanya ajirekebishe.

 

 

Huyo ndugu anahitaji ushauri nasaha kwa yale anayokumbana nayo. Inatakikana akalishwe chini na kuzungumziwa kwa anayoyafanya na jinsi ya kujitoa, kwani akitopigana na nafsi yake itampeleka mahali pabaya. Kwa kutazama yanayomfika, twaona lau atafanya yafuatayo, basi ataweza kujiondoa katika madhambi hayo:

 

1.     Inaonyesha ana wakati wa faragha mwingi sana ndio anapatia fursa ya kufanya hayo ya madhambi. Na dawa tayari tumepatiwa, nayo ni kujaribu kuwa na mtu na hasa mke wake anapokuwa nyumbani. Hii itamsaidia endapo anajihisi kutekeleza zinaa ya mkono amwite mkewe aweze kustarehe naye. Na ikiwa mkewe hayupo nyumbani basi ajipatie jambo la kumshughulisha hapo nyumbani au nje ili asiipate hiyo faragha. Hapo nyumbani itakuwa ni kumsaidia mkewe kazi za usafi au kufanya shughuli nyengine yoyote ambayo itampatia yeye thawabu na kupata mapenzi ya mkewe. Ikiwa hilo lamshinda, basi atoke nje ya nyumba na kwenda kufanya mazoezi. Hilo linaweza kupatikana kwa kwenda uwanjani au gym na kadhalika. Kwa kuwa akiwa faragha anafanya vitu ambavyo vinamlipua, atumie wakati wake kwa kutazama video za mawaidha na vipindi vyenye kufaidisha.

2.     Kwa mtu mwenye matamanio kama hayo, mbali na kuwa mmesema kuwa mkewe anamtimizia haja za kumstarehemesha inaonekana kuwa yeye mwenyewe hafikii kilele. Mke anaweza kweli akaona hivyo lakini shahawa ya mume imepita hilo. Hivyo, inatakiwa ashauriwe mume aoe mke mwengine wa kuweza kujaliza kwa yale asiyoyapata kwa mke wa kwanza.

3.     Inabidi ajizoezeshe kufunga kwani kufunga kunaondoa hayo matamanio ya ziada ya mwanamme. Awe na ada ya kufunga Jumatatu na Alkhamiys.

4.     Kuwa na marafiki wema na wazuri ambao watakuwa kioo kwake na kumnasihi katika hayo mambo na mengineyo.

5.     Kuisoma Qur-aan kwa kuielewa na kujaribu kuitia kimatendo maishani mwake.

6.     Kukumbuka mauti na kuwa siku moja atasimamishwa mbele ya Allaah Aliyetukuka na hakutakuwa na mkalimani baina yake na Mola Wake.

7.     Kutaamali zile adhabu ambazo anatarajiwa kuzipata kwa kufanya kinyume na anayoamrisha. Hasa aitaamali hiyo Hadiyth tuliyoitaja hapo juu.

8.     Awe kila wakati anaomba kinga kutoka kwa Allaah Aliyetukuka hasa anapopata zile pepesi za Shaytwaan na wasiwasi wake.

9.     Awe anasoma zile Adhkaar za asubuhi na jioni na kumuomba kwa dhati Allaah Aliyetukuka kumuondoshea hayo.

10.             Afanye juhudi kubwa kujirekebisha, kwani Allaah Aliyetukuka Humsaidia anayejisaidia. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Hakika Allaah Habadili yaliyoko kwa watu mpaka wabadili wao yaliyomo nafsini mwao” (Ar-Ra‘d [13]: 11).

 

Bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi:

 

 

Nini Hukumu Ya Kujichua Sehemu Za Siri Au Kujisaga?.

 

Kutumia Kitu Kujitoa Matamanio Nini Hukmu Yake

 

 

 

Na tunatarajia kwa tawfiki ya Allaah Aliyetukuka atakuwa ni mwenye kutengea katika yaliyo bora na ya kheri zaidi.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share