Makundi 73 Yaliyotajwa Na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Yote Yapo? Lipi Litakalookoka?

 

Makundi 73 Yaliyotajwa Na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)

Yote Yapo?  Lipi Litakalookoka?

 

Alhidaaya.com

 

SWALI:

 

Aslam alykum swali langu nilitakakujua nini maana ya wahabi, answali sunna, shia, manihaji sarafu, na ni yapi makundi aliyoyatabili Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni yapi au ayajafika au makundi yetu nisahii.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Jina hili la al-Wahhaab ni jina moja miongoni mwa majina ya Allaah Aliyetukuka yaliyo mazuri na matukufu. Maana yake halisi ni Mpaji, kwani ni Yeye pekee Aliyetukuka ndiye Mwenye uwezo wa kumpatia kila mmoja katika walimwengu bila kuishiwa. Hata hivyo, karne mbili zilizopita katika nchi ya Saudia kulitokea Shaykh aliyekuwa akipinga sana uzushi na kuwataka watu warudi katika Sunnah za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Shaykh huyo alikuwa akiitwa Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab.

 

Kwa ajili ya jina la baba yake, Wakaamua wale waliokuwa wamejikita katika uzushi na shirki na upotofu (Masufi na Mashia na Makhawaarij) kwa chuki zao kumpachika Imaam huyo na Shaykh huyo jina la Wahabi na wale waliokubaliana naye wakapachikwa jina la Mawahabi! Hata hivyo hakuna kabisa kikundi chochote kinachojulikana kwa jina hilo. Na wenye kuitwa hivyo hawalitambui jina hilo na hawakubali wenyewe kujiita au kuitwa hivyo. Bila shaka, watu wenye msimamo huo wa Sunnah, wanajulikana zaidi kwa jina la Ahlus Sunnah wal Jama’ah au Salafi wenye kufuata Salafus Swaalih (watu wema waliotangulia waliojikita katika kufuata Sunnah ya Nabiy [Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam]).

 

Kundi ambalo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitwambia tushikane nalo ni lile lenye kufuata Sunnah zake kikamilifu na pia Sunnah za Makhalifa waongofu. Kwa hivyo, kundi lolote ambalo litakuwa linawapinga Makhalifa na kuwatusi kama vile Shia watakuwa wako mbali na Uislamu.

 

Maana ya Answaar as-Sunnah ni Waislamu ambao wanaitetea na kuilinda Sunnah ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa jinsi inavyotakiwa na kuidhibiti isipotee au kusahaulika na Waislamu.

 

Ama Ushia ni mfumo wa watu waliopotea njia kwa kuwaona kuwa Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) si lolote si chochote bali walikufuru na kuritadi baada ya kuaga dunia kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), pamoja na itikadi zao nyingi chafu. Vilevile makundi kama Khawaarij nao hawako mbali na Mashia kwa itikadi zao potofu. Na Masufi pamoja na kujidai wao ni Ahlus Sunnah, lakini wametoka katika njia ya Nabiy, Swahaba na wema waliopita kwa kuingiza ushirikina na uzushi na kuzusha mengi ambayo hayapo kwenye Dini yetu.

 

Ama Manhaj Ya Salafi ni mfumo wa Dini sahihi uliochukuliwa kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na ndio njia aliyokuwa nayo yeye na Swahaba zake na watu wema waliotangulia katika Dini.

 

Imaam Ibn Hajar Al-‘Asqalaaniy amesema katika kulifasiri tamko la as-Salaf: "Makusudio yake ni Swahaba na wale walokuja baada yao wakafuata mwendo wa Swahaba." [Fat-hul Baariy, Mj. 6, Uk. 66]

 

Amepokea Imaam Muslim kutoka kwa Muhammad bin ‘Abdillaah kuwa amesema: "Nilimsikia ‘Ali bin Shaqiyq akisema, ‘Nilimsikia ’Abdullaah bin al- Mubaarak akisema mbele za watu, ‘Wacheni musichukue hadiyth ya ‘Amru bin Thaabit, kwani yeye alikuwa akitukana ma-Salaf’, na muradi wake hapa ni Swahaba."

 

Akasema Imaam al–Awzaa’iy: "Isubirishe nafsi yako katika kufuata Sunnah na usimame pale waliposimama watu na useme yale waliyoyasema watu na ujizuie na yale waliyojizuia nayo watu na ufuate njia ya watu wako wema walotangulia kwani itakutosheleza".

 

Na muradi wa watu wema hapa, ni Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum). Kwahiyo yatosheleza kulingana na aqwaal zilizopita yakuwa tamko la Salafi kusudio lake ni zama za Swahaba na walokuja baada yao wakafuata mwendo wao.

 

Ama tamko hili katika kutumika kwake katika upande wa zama au muda ni tamko ambalo hukusudiwa kwa zile qarne tatu bora ambazo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alosema:

 

"Bora ya watu ni wa qarne au zama zangu, kasha ni wale watakaokuja baada yao, kisha watakao kuja baada yao".

 

Na wala haimaanishi yakuwa madh-hab ya Salafi yameshapita kwa sababu ya kupita karne zile tatu, Laa! bali kila mwenye kufuata mwendo wao kwa wema pia yumo katika njia ya ki-Salafi kama tunavyoona katika Taariykh ya kwamba mwisho wa zama hizo hizo za Maswahaba kulitokea vipote viovu pamoja na kuwa walikuwa katika karne bora.

 

Kwa hivyo linadhihiri tamko hili hapa kuwa kila anayefuata mwenendo waliokuwa nao Maswahaba kwa wema mpaka siku ya Qiyaamah, na wale waloshikamana na ‘Aqiydah Swahiyh na mwenendo alokuwa nao Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake pasi na kukhitalifiana.

 

Kwa hivyo Manhaj ya Salafi ni sifa Nzuri ya Muislamu kujipamba nayo wala si jambo geni lililozuliwa kama wanavyodai baadhi ya watu.

 

Amesema Imaam Ibn Taymiyyah:

"Wala si aibu kwa yule mwenye kudhihirisha madh-hab ya Salafi na kujinasibisha nayo na kujifakhiri nayo, kwani hayakuwa madh-hab ya Salafi isipokuwa ni madh-hab ya haki". [Majmu’ al-Fataawa Mj.4 Uk.149]

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitabiri kuwa yeyote atakayeishi kwa muda mrefu miongoni mwetu ataona tofauti kubwa sana. Wakati huo ukifika anatakiwa Muislamu ayashike kwa magego yake maelekezo na Sunnah za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na Sunnah za Makhalifa waongofu.

 

Mwanachuoni Shaykh Swaalih Al-Fawzaan amesema: “Iwapo Manhaj ya mtu ni sahihi, basi huyo atakuwa peponi. Kwa hivyo ikiwa alikuwa juu ya Manhaj ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na manhaj ya Salafus Swaalih basi huyo atakuwa ni mmoja wa wakaazi wa Peponi kwa ruhusa ya Allaah (Subhaanhu wa Ta’aalaa). Na kinyume chake, iwapo atakuwa juu ya Manhaj ya wapotofu basi atahofishwa na moto." [Al-Ajwibah al-Mufiydah uk.77].

 

Tafadhali bonyeza viungo vifutavyo upate manufaa zaidi:

 

Ahlus Sunnah wal Jama’ah Ni Nini? Ipi Historia Yake Na Malengo Yake? Na Zipi Kasoro Zake?

 

Nini Maana Ya Manhaj Ya Salafiyyah?

 

Makundi 72 Yatakayoingia Motoni

 

Imaam Muhammad Ibn Abdul Wahhaab - Maisha Yake Na Harakati Zake

 

Uwahabi: Ufafanuzi Na Majibu Juu Ya Majungu Dhidi Ya Shaykh Muhammad 'Abdul-Wahhaab

 

Kwa Nini Waislamu Wamegawanyika Katika Makundi Tofauti Ya kuelewa Dini Yao?

 

Nabii ‘Iysa Atakua Katika Kundi Gani Miongoni Mwa Makundi 73?

 

 

Na Allaah Aliyetukuka Anajua zaidi

 

Share