Ikiwa Swalaah Ya Alasiri Imeadhiniwa Na Kuna Maiti Mtaswali Kwanza Au Mtamswalia Maiti?

SWALI:

ASALAM ALEHKUM

NATUMAI WOTE WAZIMA

SWALI LANGU NAOMBA KUJUA KAMA KABLA YA ALASIRI UNAMAITI AMBAYO INAITAJI KUSWALIWA, NA ADHANA YA ALASIRI IMESHA ITA JE MTAANZA KUSWALI ALASIRI AU MTASWALIA MAITI KWANZA MWENYEZI MUNGU AWAZIDISHIE IMANI NA AWAKINGE NA HUSUDA. KAZI NJEMA.


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Molawa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu kwa swali lako kuhusu kuswali Swalaah ya maiti kabla ya Swalaatul ‘Aswr.

Swalaah ya maiti inatofautiana na Swalaah za faradhi kwa kuwa haina muda maalumu. Inaweza kuswaliwa wakati wowote hata katika nyakati ambazo Swalaah za kawaida za Sunnah hazifai kutekelezwa. Hii ni rai ya wanachuoni wa Ki-Hanafi na Ki-Shaafi'iy. Ahmad, Ibn al-Mubaarak na Is-haaq wana rai kuwa inachukiza kuswali Swalaah ya maiti jua linapochomoza, zawali na wakati wa kukuchwa jua, isipokuwa katika kesi inapohofiwa kuchelewesha kwake mwili unaweza kuharibika.

 

Hivyo, hatujapata Hadiyth inayoonyesha kuwa ni bora kuswaliwa maiti kabla ya Swalaatul ‘Aswr au baada yake.

Hata hivyo, inafahamika kuwa Swalaah ya maiti ni bora kuswaliwa watu wakiwa wengi kama alivyopokea 'Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) kuwa:

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ‘Muislamu anapokufa na Swalaah yake ya janaza ikahudhuriwa na mamia ya Waislamu, na wote wakamuombea asamehewe kwa Ikhlaasw, anasamehewa” (Ahmad, Muslim na at-Tirmidhiy).

Na katika Hadiyth nyengine ya Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) aliyesema:

Nimemsikia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ‘Anapokufa Muislamu na kikundi cha watu arobaini wasiomshirikisha yeyote na Allaah, wakamswalia, maombi yanakubaliwa, naye anasamehewa” (Ahmad, Muslim na Abu Daawuud).

 

Kwa minajili ya kupata watu wengi, itakuwa bora maiti aswaliwe baada ya Swalaah ya Al-‘Aswr.

 

Hivyo, Swalaah ya faradhi hutangulizwa kwanza inapofika wakati wake kisha huswaliwa Swalaah ya maiti.

 Na Allaah Anajua zaidi

 

Share