Wazazi Hawataki Nifunge Ndoa Hadi Nimalize Kusoma Nami Niko Katika Zinaa, Nifanyeje?

 

SWALI

:

Asalam Aleikum warahmatullahi wabarakatu

kuna kijana nimependana nae na wote tunataka kufungan ndoa lakini wazazi wangu hawataki mpaka nimalize kusoma.kusubiri sio tatizo,lakini nipo katika zinaa ambayo nashindwa kujizuia.je  nifanyeje? hali yakua nataka kuachana na machafu ni mrudie mola wangu ili nisitirike? Maana huwa najuta kila nnaporudia dhambi hiyo hiyo. Je, nini hukumu ya ndoa bila ya idhini ya wazazi kwa niya ya kupata stara na uongofu?

Allah Akuoongoeni nyote. Ameen.

 


JIBU:

AlhamduliLlaah - Himdi Na Sifa Zote Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Tunakushukuru kwa swali lako muhimu sana na tunafurahiwa kuona kwamba ndugu zetu wa Kiislamu wako katika khofu ya kumuasi Mola wao na wako tayari kujikinga na madhambi wayafanyayo. 

Wazee wako wanapasa wafahamu kuwa wanafanya makosa  kukukatalia kufunga ndoa na hali unataka mwenyewe sana jambo hilo. Na kama sababu yao ni kuwa hadi umalize kusoma, hilo sio tatizo kwani wanawake wangapi wanaoelewa na huku wanaendelea kusoma?

Vile vile wazee hao wanakwenda kinyume na amri ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم inayosema:

    ((إِذَا خَطَبَ إِلَيْكُمْ مَنْ تَرْضَوْنَ دِينَهُ وَخُلُقَهُ فَزَوِّجُوهُ إِلَّا تَفْعَلُوا تَكُنْ فِتْنَةٌ فِي الْأَرْضِ وَفَسَادٌ عَرِيضٌ))   رواه الترمذي   وقال الألباني : حسن

((Atakapoposa kwenu yule mtakaeridhika na dini yake, na tabia yake, basi muozesheni, kwani kutokufanya hivyo itakuwa fitna katika ardhi (duniani) na ufisadi mpana (mkubwa) )) [At-Tirmidhiy kasimulia na Shaykh Albaaniy amesema ni Hadiyth Hasan]

 

Jambo la kufanya ni kuwa waombe watu katika familia yako, kama unaye 'ami au mjomba au shangazi, na kila wakiwa wengi ni bora zaidi, wakutane na wazazi wako ili wawafahamishe umuhimu wako wa kufunga ndoa haraka na kijana huyo. Na ikiwezekana kuwapata viongozi wa dini wawe pamoja na watu wako na hata kama haikuwezekana kupata watu katika familia yako basi tafuta mashekhe waje kukutana na wazee wako ili wawakinaishe kuhusu jambo hilo. Na la muhimu ni kwamba uwe muwazi kabisa kuwafahamisha kuwa unapendana naye na huwezi kusubiri miaka minne na kwamba una khofu usije kuingia katika zinaa. (Huna haja ya kuwajulisha kama tayari uko katika zinaa kwani ni vizuri mtu kuficha siri yake).

Na zifuatazo ziwe ni nukta za kuwatanabahisha wazazi wako:

1-Kusoma sio tatizo kwani utaweza kuendelea kusoma huku umeolewa. 

2- Hata kama ukisoma, mume wako akitaka ukae nyumbani basi itabidi kufuata amri ya mume kukaa nyumbani na hii ni amri kutoka kwa Mola wetu kama Anavyosema:

 ((وَقَرْنَ فِي بُيُوتِكُنَّ))

((Na kaeni majumbani kwenu)) [Al-Ahzaab: 33]

3- Wafahamishwe wazazi wako hatari ya kuingia katika zinaa, na waulizwe wazazi, je, ukija kushika mimba watafurahiwa iwe hivyo au ni bora uolewe?

4- Miaka minne ni mingi sana kusubiri hadi ufunge ndoa na kutokana na hali uliyonayo ya kuwa uko katika matamanio na zinaa kwa hiyo ni vigumu kwako kusubiri.

5- Wafahamishe wajue kuwa ikiwa wao watakataa kukuozesha basi Uislamu umekuruhusu kupata Walii wengine katika familia au ikishindikana Qadhi wa kukuozesha na kukataa kwao kutakusababisha wewe kuchukua hatua hiyo. 

Na kama ukishindwa kuwakinaisha wazazi wako wakuoze, basi tafuta mwanamume aliye karibu na wewe katika familia yako kama 'ami, mjomba, kaka na kadhalika awe ndiye walii wako kwa sababu katika sharti ya ndoa ni lazima kuweko walii kama Alivyosema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kutoka kwa Abu Muusa Al-Ash'ariyyi رضي  الله عنه  

  ((لا نكاح إلا بولي))   رواه أبو داود والترمذي وابن ماجه  وصححه الألباني في صحيح الترمذي .

((Hakuna Nikaah ila kwa Walii)) [Abu Daawuud, At-Tirmidhiy, Ibn Maajah na ameisahihisha Shaykh Al-Albaaniy katika Sahihi ya At-Tirmidhiy]

Vile vile Amesema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم

  (( أيما امرأة نكحت بغير إذن وليها فنكاحها باطل ، فنكاحها باطل ، فنكاحها باطل))  رواه أحمد  وأبو داود   والترمذي  وصححه الألباني في صحيح الجامع 

 

((Mwanamke yeyote akiolewa bila ya Walii wake basi Nikaah yake ni baatil, Nikaah yake ni baatil, Nikaah yake ni baatil)) [Ahmad, Abu Daawuud, At-Tirmidhiy na kaisahihisha Shaykh Al-Albaaniy katika Sahiyhul-Jaami'i]

Shaykh Muhammad ibn Ibraahiym (Rahimahu Allaah) amesema: "Mwanamke anapotimiza umri wa kubaleghe, na anapokuja kuposwa na mtu mwenye kumridhisha kwa dini, basi Walii wake lazima akubali kumuozesha. Na ikiwa Walii wake hataki kumuozesha, basi akumbushwe wajib wake wa kumtunza mwanamke. Na akishikilia kukataa basi uwalii wake unapotea na unawakilishwa na mwanamume mwingine katika upande wa baba yake aliye karibu naye zaidi". [Fataawa Al-Shaykh Muhammad ibn Ibraahiym (Rahimahu Allaah) 10/97]

 Shaykh ibn 'Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) amesema: "Ikiwa Walii amekataa kumuozesha mwanamke kwa mume ambaye mwenye dini na tabia njema, basi uwalii unapelekwa kwa jamaa wa baba yake, aliye karibu zaidi naye, kisha mwingineo aliye karibu. Wote wakikataa kumuozesha kama inavyokuwa ni kawaida, basi uwalii unapelekwa kwa Qadhi wa Sheria Ya Kiislamu, na Qadhi huyo inampasa amuozeshe. Ikiwa Qadhi amepata kesi kama hiyo na anajua kuwa mawalii wa mwanamke wamekataa kumuozesha, basi amuozeshe yeye kwani yeye atakuwa amepata uwalii kwa ujumla madamu walii kutoka familia yake hakupatikana".

Nasaha ni kwamba fanya haraka kabisa kuwakutanisha wazazi wako kuwaelezea umuhimu wa kufunga kwako ndoa na huyo kijana, na watakapokataa basi endelea kutafuta Walii katika familia yako uanze upande wa baba yako, kisha aliye karibu zaidi. Itakaposhindikana kupata Walii katika familia ndipo uelekee kwa Qadhi wa Kiislamu ambaye Uwalii utakuwa kwake umewajibika baada ya kukosa Walii katika familia yako. 

Wakati huku unasubiri kuwakutanisha wazazi wako tafadhali jizuie na kuonana na huyo kijana na endelea kufanya tawbah kwa Mola wako, kwani Mola hupokea tawbah ya mja wake wakati wowote, ila ni vizuri zaidi kujiepusha kabisa na madhambi makubwa kama hayo, ambayo adhabu yake lau kama ingelikuwa inatimizwa ipasavyo basi bila shaka asingelithubutu Muislamu kufanya kitendo hicho. 

Njia mojawapo ya nyinyi kujiepusha na dhambi hizo ni kubakia katika Swawm kama alivyosema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم :

 ((يَا مَعْشَرَ الشَّبَابِ مَنْ اسْتَطَاعَ الْبَاءَةَ فَلْيَتَزَوَّجْ فَإِنَّهُ أَغَضُّ لِلْبَصَرِ وَأَحْصَنُ لِلْفَرْجِ وَمَنْ لَمْ يَسْتَطِعْ فَعَلَيْهِ بِالصَّوْمِ فَإِنَّهُ لَهُ وِجَاءٌ((  البخاري   ومسلم

((Enyi vijana, anayeweza kuoa  basi na aoe  kwani ni lindo la macho (na kutazama ya kutamanisha) na ni hifadhi ya tupu (kwa kufanya zinaa) Na asiyeweza basi afunge (Swawm) kwani ni kinga (ya matamanio) [Al-Bukhaariy na Muslim]

Pia jitahidi kuwa karibu na Allaah kwa kufanya ibada zaidi, kusoma Qur-aan mara kwa mara, muda mwingi kusoma vitabu vya dini na kusikiliza mawaidha; hayo yote yatakuweka karibu sana na Allaah na yatakulinda na machafu mengi.

 

Na Allah Anajua zaidi.

 

Share