Fadhila Za Hajj Na 'Umrah Na Adabu Zake

 

Fadhila Za Hajj Na ‘Umrah Na Adabu Zake

 

Imekusanywa Na: Ukht Muznah Faraj

 

Alhidaaya.com

 

Alhamdulillahi Rabbil Alaamiyn Was swalatu Wassalaamu Alaa Nabiyyinaa Waalaa Aalihi Waswahbihi Waman Tabiahum bi’ihsaani ilaa yaumid’diyn. Amma Ba’ad,

 

a).   Amesema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa): 

ۗ وَلِلَّـهِ عَلَى النَّاسِ حِجُّ الْبَيْتِ مَنِ اسْتَطَاعَ إِلَيْهِ سَبِيلًا ۚ وَمَن كَفَرَ فَإِنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ عَنِ الْعَالَمِينَ ﴿٩٧﴾ 

Na kwa ajili ya Allaah imewajibika watu watekeleze Hajj katika Nyumba hiyo kwa mwenye uwezo. Na atakayekufuru, basi hakika Allaah ni Mkwasi kwa walimwengu. [Aal-‘Imraan: 97]

 

b).   Na amesema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

“Kufanya umrah hadi umrah hufutiwa madhambi baina yake, na Hajj (Mabruur) yenye kukubaliwa haina malipo isipokuwa Jannah”. [Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim]

 

c).   Na amesema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

“Atakayehiji ikawa hakufanya maovu (kwa vitendo wala kwa maneno) na wala hakuvunja amri za Allaah (Subhaanahu Wata’ala) atasamehewa madhambi yake yote atakuwa kama siku aliyozaliwa na Mama yake.” [Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim]

 

d).   Na amesema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

“Chukueni Hajj kutoka kwangu” [Imepokewa na Muslim]

 

e).   Ni wajibu wa kila mwenye kuhiji na kufanya umrah awe mali anayofanyia ibada hizo iwe ni ya halali ili Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) aikubali, kwa kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

 

“Hakika Allaah Mtukufu ni mzuri na hakubali isipokawa kizuri”. [Imepokewa na Muslim]

 

f).   Kwa hakika hajji ni kongamano kubwa kwa waislamu linalo wakutanisha waislamu, kwa sababu kunapatikana ndani yake kujuana, kupendana, na kusaidiana katika kutatua matatizo juu ya kila hali, na pia kushuhudia manufaa yanayopatikana humo ya dini na dunia. SubhaanAllaah!! Ametukuka Aliye Mbora wa viumbe.

 

Na Amesema Allaah Mtukufu: 

 ۘ وَتَعَاوَنُوا عَلَى الْبِرِّ وَالتَّقْوَىٰ ۖ وَلَا تَعَاوَنُوا عَلَى الْإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ ۚ 

Na shirikianeni katika wema na taqwa, na wala msishirikiane katika dhambi na uadui. [Al-Maaidah: 2]

 

g).   Inajuzu kufanya umrah katika wakati wowote, lakini kufanya umrah katika mwezi wa Ramadhaan ni bora, kwa kauli aliyosema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

“Kufanya 'Umrah katika mwezi wa Ramadhaan ni kama Hajj.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

j).   Swalah katika Msikiti mtukufu wa Makkah ni bora mara laki moja kuliko Swalah katika Misikiti mingine. Kwa kauli aliyosema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

“Swalah katika Msikiti wangu huu ni bora katika Swalah elfu moja kuliko misikiti mingine iispokuwa Msikiti mtukufu wa Makkah” [Imepokewa na Muslim]

 

Swalah moja katika Msikiti wa Nabiy Madiynah ni sawa malipo yake na Swalah elfu moja (1000).

 

Na amesema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

“Swalah katika Msikiti mtukufu wa Makkah ni bora kuliko Swalah katika Msikiti wangu huu kwa Swalah mia”. [Imepokewa na Ahmad]

 

Akimaanisha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa swala moja ni sawa na swala mia, yaani 100*1000 = 100,000 .

 

Hii ni kuonyesha kuna fadhila kubwa sana na yoyote ambae amejaaliwa kufika huko basi na ajitahidi swala zake zote aziswali msikitini ili asikose thawabu hizi.

 

Kwa Ufupi:

 

Hajj ni nguzo miongoni mwa nguzo za Kiislamu na ndani yake kuna fadhila nyingi ambazo nimezitaja kwa ufupi na manufaa ya kidunia na Akhera.  Kwa mfano, unaweza kufanya biashara pindi umalizapo hajji na mengineyo ambayo tuliyataja hapo juu. Na manufaa ya akhera ambayo ni bora zaidi kuliko ya dunia.

 

Allaah Amesema:

وَالْآخِرَةُ خَيْرٌ وَأَبْقَىٰ ﴿١٧﴾

Na hali Aakhirah ni bora zaidi ya kudumu. [Al-A’laa: 17]

 

Basi ni juu ya kila muislamu ajitahidi kuendea njia hiyo pale atapo kuwa na uwezo wa kuifikia njia hiyo kabla hayajamfikia mauti hali yuko katika maaswi. Basi na ajihadhari kutokana na maovu, kuvunja amri za Allaah, mijadala isiyo ya hakki wala faida ndani yake na maaswi yote kwa ujumla.

 

Adabu Za Hajj Na Umrah:

 

1- Itakase hajji yako iwe kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu Wata’ala) na sema kama alivyosema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)

 

“Ee Mola ifanye Hajj yangu isiwe ya kujionyesha wala kusifiwa” [Swahiyh Al-Bayhaqiy]

 

Kwani kuna baadhi ya watu matendo yao wanayafanya ili waonekane na wao wamekwenda au wamefanya hajji au wamesikilikana kwa kusifiwa kama Fulani pia amekwenda iwe ni matendo ya hajji au hata ibada zozote ilihali si kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) hao matendo yao yatakuwa hayana malipo yoyote mbele ya Allaah Mtukufu.

 

2- Iwe hajji imewafikiana na hajji aliohijji Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama alivyo sema mwenyewe Bwana Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Chukueni Hajj kutoka kwangu” [Imepokewa na Muslim]

 

3- Jihadhari na kutokufanya maovu na yaliyo katazwa, na maaswi, na mijadala iliyo baatili (iliyokatazwa) mpaka hijjah yako iwe ni maqbuul (yenye kukubalika).

 

4- Jihadhari na kuomba duaa kwa asie kuwa Allaah Mtukufu. kuomba maiti mfano kwenye makaburi wakati unapo zuru makaburi ni kwa ajili ya kujikumbusha na mauti na kuwatakia rehma na maghfira sikuwaomba au kutaka msaada au kuokolewa hiyo itakuwa ni shirki ambayo itabatilisha hajji na amali zako zote. Kama alivyo sema Allaah Mtukufu: 

 

لَئِنْ أَشْرَكْتَ لَيَحْبَطَنَّ عَمَلُكَ وَلَتَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ

Ukifanya shirki bila shaka zitaporomoka ‘amali zako na bila shaka utakuwa miongoni mwa waliokhasirika. [Az-Zumar: 65]

 

5- Unatakiwa uwe mpole kwa walio karibu yako yaani walioko pembezoni mwako  wakati unapokuwa unafanya twawafu (kuizunguka al ka’abah) na unapo fanya saa’yi (kutembea kilima cha saffa na mar’wah) na wakati wa kutupa mawe katika minara ya jamaraati, wala msinyanyuwe sauti wakati wa kumtaja Allaah wala wakati wa Duaa na khasa pale mnapokuwa kwenye kundi kwani kunyanyuwa sauti kunawachanganya wengine kwakufanya hivyo hakuna dalili na hivyo kunyanyuwa sauti ni Bid’aa iliyozushwa.

 

6- Haifai kufanya zahma yaani kusukumana wakati wa kuliendea jiwe jeusi wala kusimama hapo kuwazulia wengine wakati unapo fanya tawaafu. Inavotakiwa ni kuligusa, kulibusu na huku unaomba nakuondoka si kusukumana.

 

7- Kusimama wakati wa Sa’yi kati ya Swaffa na Marwah pindi inapo nadiwa swala ya Jama'ah mpaka itapomalizika Swalah utatimiza palipobaki.

 

8- Kuhifadhi Swalah ya Jama'ah katika msikiti na khasa unapokuwa katika Msikiti wa Makkah, Kwani kuna fadhila kubwa kama tulivyotangulia kusema.

 

9- Usiwapitepite wenye kuswali ukawaudhi, kaa palipo karibu yako penye nafasi.

 

10- Jihadhari na kuwapita watu wanapo kuwa kwenye safu ya Swalah kati yako na mwenye kuswali hata kama ni katika msikiti mtukufu wa Makkah ili upite safu ya mbele ikiwa unataka kukaa mbele basi inakubidi uwahi na sio kuwakunja watu shingo ili upite mbele, kwani hayo ni matendo ya shaitwani, isipokuwa iwe kwa  dharura.

 

11- Kuzidisha kuizunguka al ka’abah kwani kufanya hivyo kuna malipo makubwa kama alivyosema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

“Mwenye kuizunguka Al-Ka’abah mara saba atakuwa kama aliyemuacha huru Mtumwa” [Imepokewa na Ibn Maajah]

 

12- Haifai kuchinja kabla ya kufikia siku ya kuchinja wala haifai kutoa sadaka kwa thamani yake.

 

13- Na katika alama za kukubaliwa hajji ni kubadilika katika hali iliyo nzuri ya aqidah yako (kutokumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) katika ibaada zako kushirikiana na Waislamu wenzio kwa wema na tabia njema na ni juu yako kumuomba Allaah wakati wote hii ni kipimo baada ya hajji kwani ikiwa hukubadilika katika 'Aqidah yako na tabia yako kwa ujumla itakuwa hajji yako ni matembezi tu na sio 'Mabruur'. 

رَبَّنَا تَقَبَّلْ مِنَّا ۖ إِنَّكَ أَنتَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ

Rabb wetu, Tutakabalie, hakika Wewe ni Mwenye kusikia yote, Mjuzi wa yote. [ Al-Baqarah: 127]

 

“Aamiyn”

 

Allaah Atuwafiqishe na Atufanyie wepesi na ajaalie manufaa na kuyafanyia kazi yote na tufaidike nayo In shaa Allaah. 

 

 

Wa Allaahu A’alam

 

Share